Usafirishaji umerahisisha sana maisha hapa duniani, mambo mengi yamewezekana kwa sababu ya uwepo wa usafiri wa uhakika na salama. Katika zama hizi ambazo ni zama za teknolojia na taarifa kila kitu tunachotaka kukijua tunaweza kukijua ndani ya muda mfupi, hali hii ina faida yake na hasara zake kwenye kujenga maisha bora ya binadamu na kutunza mazingira yanayofaa kwa viumbe hai.
Katika karne hii usafiri sio shida kabisa, ukitaka kwenda sehemu yoyote ile duniani ni rahisi kufika unakotaka kwenda, ukitaka kutuma kitu chochote sehemu yoyote ile duniani, unaweza kutuma na kumfikia mlengwa kwa muda mfupi. Maisha yamekuwa rahisi na yamerahisishwa zaidi kutokana na uwepo wa njia nyingi za usafirishaji. Kwa sasa kuna njia za barabara, njia za baharini, njia za reli na njia za anga, zote hizo ni njia kuu za usafiri ambazo tunaweza kutumia kufika sehemu yoyote hapa duniani.
Karne za nyuma mambo hayakuwa hivi, usafirishaji ulikuwa mgumu sana, watu wengi walipoteza maisha kutokana na kukosekana kwa usafiri salama, mambo mengi yalikwama kutokana na kutokuwepo kwa usafiri. Hivyo maisha kwa kiasi fulani yalikuwa magumu kwa binadamu.
Usafirishaji wa bidhaa kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine ni muhimu kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya binadamu na pia kurahisisha maisha hapa duniani. Kwa sasa mtu anaweza kusafirisha kiasi kikubwa cha bidhaa kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine kwa usalama mkubwa kabisa.
Kwa mfano hapa Afrika, bidhaa nyingi husafirishwa kwenda nchi za nje kwa ajili ya kuzalisha bidhaa mbali mbali. Mfano usafirishaji wa magogo, majani ya chai, pamba, madini na bidhaa nyingine nyingi ambazo husafirishwa kwenye makontena makubwa kwenda nje ya nchi. Njia kuu za usafirishaji wa bidhaa hizi umekuwa ni bandari, reli na kwa kiasi usafiri wa anga.
Kwa sababu ya uwepo wa njia hizi za usafiri, kumekuwa na mambo mengi ambayo yanafanyika nyuma ya pazia kusafirisha magendo, dawa za kulevya, meno ya tembo, pembe za faru na bidhaa nyingine ambazo husafirishwa kwa njia haramu kwenda nchi za nje kwa njia ambazo ni kinyume na sheria za usafirishaji wa bidhaa na pia ni hatari kwa maisha ya watu na maisha ya viumbe hai kwa ujumla.
Kwenye ripoti mbali mbali za uchunguzi na utafiti zinaonyesha jinsi ambavyo suala la ujangili linavyozidi kuwa kubwa kutokana na urahisi wa usafirishaji wa bidhaa za wanyamapori, kiasi kikubwa cha meno ya tembo na wanyama wengine husafirishwa pamoja na bidhaa nyingine hadi kuwafikia walengwa.
Moja ya ripoti muhimu inayoelezea mambo haya ambayo yanaendelea kwenye masuala ya usafirishaji wa meno ya tembo na pembe za faru inaitwa, Species of Crime. Typologies & Risk Metrics for Wildlife Trafficking. Ripoti hiii ambayo ilitoka May 2015, inaelezea kwa kina njia mbali mbali saba ambazo hutumiwa zaidi katika usafirishaji wa wanyamapori na bidhaa nyingine haramu kinyume na sheria za nchi.
Mpaka sasa hili ni tatizo kubwa sana linalotukabili kama taifa na dunia kwa ujumla, njia nyingi za siri zimegunduliwa kwa ajili ya kusafirisha meno ya tembo, dawa za kulevya na vitu vingine haramu. Juhudi zetu kama dunia kufanya kazi kwa pamoja kutatua tatizo hili ni muhimu sana kwa ajili ya usalama wa mazingira yetu na mazingira asili ya wanyamapori na mimea.
Usimamizi na ukaguzi kwenye maeneo ya bandari na vituo vya usafirishaji bado ni dhaifu na hauwezi kukabiliana na mbinu nyingi wanazotumia majangili na watu wanaohusika na usafirishaji wa bidhaa hizo kwa njia haramu. Mfumo ambao hutumiwa na majangili kusafirisha meno ya tembo na pembe za faru ni mfumo uliojaa mambo mengi “complicated”. Ambao sio rahisi kugundulika kirahisi bila nguvu ya ziada.
Tunachoweza kukifanya ni kufanya kazi ya ziada, kubaini na kuharibu kabisa biashara haramu na mifumo yake yote. Jambo hili sio jepesi wala sio la mtu mmoja au nchi moja pekee, ni jambo ambalo dunia inahitaji kuliunga mkono na kutoa ushirikiano wa dhati kupambana na njia zote wanazotumia kusafirisha meno ya tembo na pembe za faru; kuzuia njia zote haramu za usafirishaji.
Asante sana kwa kusoma makala hii.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569