Nukuu: “Mikoko ni hazina isiyothaminiwa, yenye uwezo wa kufyonza kaboni mara nne zaidi ya miti ya nchi kavu.”

Mazingira ya bahari yanahusisha maeneo yote yanayozunguka bahari ikijumuisha fukwe za bahari, misitu ya mikoko, majani bahari(seagrasses) na matumbawe.

Wengi hudhani kuwa mazingira ya bahari ni eneo tu la uso wa maji linaloonekana kwa macho huku wakisahau hayo maeneo mengine muhimu.

Mandhari safi ya bahari hususani maeneo ya fukwe hutumiwa sana na watalii wa ndani na nje nchi kupumzika na kufurahia upepo mwanana unaosindikizwa na sauti za mawimbi ya maji kutoka baharini.

Watu wengi wanaobahatika kutembelea maeneo haya huweza kupata nafasi ya kuona viumbe wengi wa baharini wakitambaa katika fukwe hizo mfano kasa, konokono,yavuyavu, samaki nyota n.k.

Licha ya umuhimu huo bado utunzaji wa mazingira mengine ya bahari umesahaulika na hata juhudi zinazochukuliwa kutunza maeneo haya bado hazitoshelezi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Raisi Muungano na Mazingira, Mh. Dr. Selemani Jafo akishiriki kupanda miti aina ya mikoko.

Licha ya maeneo haya kuwa na umuhimu mkubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kama vile uwezo mkubwa wa kufyonza hewa ukaa au hewa ya kaboni.

Mabadiliko ya tabianchi yanayoshuhudiwa katika kona mbalimbali za dunia yamekuwa yakichangiwa na mkusanyiko wa hewa ukaa angani jambo linaloathiri ustawi wa dunia kimazingira hivyo kuathiri pia sekta nyeti hasa za kilimo na ufugaji.

Hewa ukaa imekuwa ikizalishwa kwa wingi duniani kutokana na maendeleo katika sekta ya viwanda,usafirishaji,uchimabaji madini na kilimo. Makala inayoelezea biashara ya hewa ukaa kwa ujumla, unaweza kuisoma hapa

Hivyo basi, mazingira ya bahari yanamchango mkubwa katika kupunguza hewa ukaa na kuiweka dunia katika hali nzuri.

Elimu ya utunzaji wa mazingira ya bahari imekuwa ikitolewa kwa uchache, ikiwa ni pamoja na miradi ya kaboni ukilinganisha na elimu ya utunzaji wa uoto wa nchi kavu; hivyo watu wengi hawana elimu ya kutosha juu ya uhusiano uliopo kati ya hewa ukaa na mazingira ya bahari.

Picha ya msitu wa mikoko, picha kutoka mtandaoni.

Kipi kinapunguza hewa ukaa Kwa kiasi kikubwa kati ya Mazingira ya bahari na mimea ya nchi kavu?

Hili ni swali muhimu ambalo majibu yake yanaleta changamoto kwa watu wengi. Miradi mingi ya kaboni inayolenga kupunguza hewa ukaa katika kanda za bahari ni michache.

Tunaona nguvu kubwa ikielekezwa katika uoto wa nchi kavu, jambo ambalo limepelekea watu kuamini kuwa pengine uoto wa asili unaopatikana nchi kavu ndio mwarobaini wa kufyonza kiasi kikubwa cha hewa ukaa.

Ukweli ni kwamba mazingira ya bahari yanauwezo wa kupunguza kiasi kikubwa cha hewa ukaa mara nne zaidi, ukilinganisha na kiasi cha hewa ukaa ambacho kinaweza kufyonzwa na uoto wa mimea ya nchi kavu.

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine wakiwa katika mafunzo ya vitendo katika mazingira ya bahari yenye misitu ya mikoko, Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Picha na Victor Wilson

Hii inaonyesha wazi kuwa mazingira ya bahari ni miongoni mwa tunu pekee zilizobaki zenye uwezo mkubwa wa kuinusuru dunia dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Tafiti zinaonyesha kuwa kiasi cha hewa ukaa kinachofyonzwa na misitu ya mikoko ni kikubwa zaidi kuliko miti ya kawaida.

Lakini pia udongo unaopatikana katika misitu ya Mikoko inauwezo mkubwa wa kutunza kiasi kikubwa cha hewa ukaa(Soil-carbon sequestration);

Hii ni kutokana na asili ya udongo huu kushikamana sana na kutengeneza tope zito ambalo haliwezi kuruhusu tena kaboni/hewa ukaa iliyohifadhiwa kurudi angani.

Lakini pia, uozo wa asili unaopatikana Baharini husaidia kutunza kiasi kikubwa cha hewa ukaa, kama alivyoandika mwandishi Benner na wenzake mwaka 1984.

Mazingira ya nchi kavu na bahari yameleta taswira mtambuka kiuchumi hasa kwa kuhusianisha rangi ya kijani na bluu.

Uchumi wa bluu umechukua dhana hii ikimaanisha uchumi unaotokana na rasilimali zitokanazo na bahari. Soma hapa kufahamu zaidi

Aina hii ya uchumi inahusisha shughuli mbalimbali kama uvuvi, utalii, ufugaji wa samaki na usafiri. Shughuli zote hizo zinafanyika kwa misingi ya uhifadhi wa ikolojia ya bahari pamoja na mazingira yake.

Falsafa ya uchumi wa bluu imesaidia Kwa kiasi kikubwa kuhifadhi mazingira ya bahari na kuinua watu kiuchumi huku wakiacha mazingira ya bahari yakiwa salama.

Kutoka kushoto ni mwandishi wa makala hii Victor Wilslon, Prof. RPC Temu, Mhadhiri Chuo Kikuu Cha Sokoine Cha kilimo,  na Mtaalamu wa Sayansi ya misitu wakiwa katika misitu ya mikoko Hifadhi ya Taifa ya Saadani.

Je? Unajua maana ya kaboni ya kijani na kaboni ya bluu??

Kutokana na muktadha wa nchi kavu na Bahari zimesababisha uwepo wa aina mbili za kaboni/hewa ukaa ambazo ni kaboni ya kijani na kaboni ya bluu.

Licha ya hayo, rangi ya kijani na bluu hazimaanishi rangi halisi za viwango vya kaboni vinavyopatikana katika maeneo hayo.

Kaboni ya kijani ni aina ya kaboni ambayo mchanganuo wake uko kama ifuatavyo;

  • Hii ni aina ya kaboni ambayo inafyonzwa na mimea ya nchi kavu ikihusisha misitu, nyasi na kilimo. Misitu hufyonza kaboni inayopatikana angani kupitia majani yake.Rangi ya kijani ya uoto wa misitu na majani umesababisha kaboni inayopatikana katika maeneo hata kupewa rangi ya kijani.
  • Kaboni ya kijani huhifadhiwa katika miti, mizizi,na udongo. Sehemu hizo hufanya kazi ya kutunza gesi ya kaboni inayofyonzwa na majani kupitia usanisi nuru. Udongo imara huweza kutunza kiasi kikubwa cha kaboni na ukubwa wa mti huweza kubainisha kiasi cha kaboni iliyohifadhiwa. Uhai na uwepo wa misitu mikubwa huashiria wingi wa kaboni unaoweza kuhifadhiwa.

Lakini pia, kaboni ya bluu ni aina ya pili ya kaboni ambayo inaelezewa na mchanganuo ufuatao;

  • Kaboni ya bluu hutokana na gesi ya kaboni inayofyonzwa kutokana na mimea ya pwani na Baharini. Miti ya mikoko, majani bahari, matumbawe n.k huhifadhi kaboni inayobeba rangi ya bluu.
  • Uimara wa misitu ya mikoko na aina ya udongo,kupwa na kujaa kwa maji katika mazingira ya bahari hufanya mazingira haya kuwa kinara katika kuhifadhi viwango vikubwa vya kaboni ukilinganisha na uoto wa nchi kavu.
  • Licha ya kuhifadhi viwango vikubwa vya kaboni pia huhifadhi bayoanuai muhimu ambazo zisipohifadhiwa zinaweza kutoweka hasa jamii ya amfibia, Reptilia n.k. Wanasayansi na watafiti wamejaribu kutumia rangi ya vitu halisi katika kuwasilisha matokeo ya tafiti zao kiurahisi.
  • Mwandishi Nellemann (2009), aliapendekeza kutumia jina la kaboni ya bluu litumike kuwakilisha kaboni inayopatikana katika maeneo ya bahari kutokana na kuwa tafiti zake zilijikita katika maeneo hayo.

Kwa dhana hiyo Mazingira ya bahari yanamchango mkubwa katika kukabiliana na madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi.

Utafiti uliofanywa na Mpango wa Ikweta kupitia Shirika la Mikoko la nchini Kenya lilibainisha kuwa mikoko inayopatikana pwani ya Kitropiki na chini ya Kitropiki inakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Kuna nchi 15 duniani zenye zaidi ya 75% ya misitu ya mikoko. Nchi hizo zinakabiliwa na changamoto ambazo zinatishia uhai wa muda mrefu wa misitu hii duniani.

Nchi kama Indonesia, Brazil, Nigeria na Mexico huchukua zaidi ya 40% ya mikoko duniani zenye hekta milioni 6.5.

Nchi nyingine zenye utajiri wa mikoko ni India, Malaysia, Australia na nchi za kusini mashariki mwa bara la Asia ambazo ni Thailand, Vietnam, Myanmar na ufilipino.

Na tafiti hiyo ilibainisha kuwa kuna 7% ya misitu ya mikoko ambayo imehifadhiwa. Hii inaonesha ni jinsi gani ambavyo kuna pengo kubwa katika uhifadhi wa mikoko licha ya ubora wake katika soko la hewa ukaa.

Tanzania, Madagascar na Msumbiji ni miongoni mwa nchi zinazopatikana katika bara la Afrika zenye utajiri wa Mikoko.

Misitu hii ya ukanda wa bahari imekuwa ni hazina kubwa kutokana na umuhimu wake mkubwa katika kufyonza hewa ukaa, lakini pia bado inamchango mkubwa kiuchumi,ki-ikolojia, kisayansi na kijamii.

Jamii Rufiji, ikishiriki katika kupanda miti aina ya mikoko katik, picha na Kizito Makoye

Matumizi ya nishati ya kuni inayotokana na miti ya mikoko, upasuaji wa mbao, uanzishwaji wa miundombinu mbalimbali ya ujenzi ni vitendo ambavyo vinaathiri ustawi wa misitu hii.

Mazingira ya bahari husaidia kukuza uchumi wa nchi kutokana na uwezo wake wa kutunza mazalia ya samaki.

Samaki huzaliana kwa wingi katika maeneo tulivu hasa maeneo ya mikoko ambayo haiathiriwi na mawimbi makali ya bahari na kuweka ikolojia ya bahari katika ustawi wake.

Sekta ya uvuvi imekuwa na mchango mkubwa kiuchumi katika nchi mbalimbali duniani hivyo kukuza pato la taifa, mfano nchi ya Norway huweza kukusanya zaidi ya Trilioni 40 kutokana na makusanyo katika sekta ya uvuvi.

Licha ya hayo, maeneo ya bahari ni makazi ya Ndege na viumbe wengine ambao  huweza kuweka viota vyao na kuendeleza maisha Yao katika misitu hii.

Napenda kutoa rai kwa serikali, sekta binafsi na wananchi kuzidi kuweka mkazo juu ya uhifadhi wa mazingira ya bahari, ili kuweza kufikia misingi mizuri ya uchumi wa bluu na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Mchango wako msomaji ni muhimu sana katika kujenga uchumi na uhifadhi endelevu, kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya bahari na rasilimali zake.

Makala hii imeandaliwa na Mhifadhi, Victor Wilson na kuhaririwa na Hillary Mrosso. Kama utakuwa na maswali, maoni, ushauri usisite kuwasiliana na mwandishi wa makala hii kwa mawasiliano hapo chini.

Victor Wilson

Barua pepe: wilsonvictor712@gmail.com

Simu: +255620861002

Whatsapp: +255743880175