Siku zote maisha yataendelea kuwa magumu sio kwa sababu maisha yamepangwa kuwa magumu kwa mwanadamu la hasha, bali ni kwa sababu binadamu ndiye anayeyafanya maisha kuwa magumu. Hali ngumu tulizo nazo, umasikini, njaa, vita, ukame na uharibifu wa mazingira, mabadiliko ya tabia nchi, mauaji na visasi haya yote yanatokana na ujinga wetu wa kutokufahamu mambo. Kutokujua nini kinatakiwa kufanika na kwanini kifanyike imesababisha watu kuishi kwa majaribio na kwa hisia badala ya ufahamu. Kila kitu kama kilivyo na kinavyoonekean ni matokeo ya uwepo wa binadamu katika uso wa dunia. Binadamu alikabidhiwa dunia ikiwa nzuri na yenye ubora ili aitunze na kuhakikisha kila kitu kinakuwa bora na kusitawi kwenye usimamizi wake.

Hali ikisha kuwa mbaya haitakiwi kuendelea kuifanya kuwa mbaya zaidi, maisha yetu yanakuwa magumu na changamoto zinaendelea kuwepo kila wakati hata kama kutatokea suluhisho la muda mfupi bado kutendelea na tatizo la msingi. Masuala ya uhifadhi wa wanyamapori na maliasili kwa ujumla sio wa kutolea maamuzi ya kisiasa ya miaka mitano mitano, au miaka kumi kumi. Ni maswala yanayohitaji maamuzi ya milele. Maamuzi ya kuzuia njaa na kupata umaarufu hayafai kwenye maliasili zetu

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kunukuliwa akisema suala la uhifadhi wa maliasili ni jambo ambalo linahitaji weledi hasa kwenye upande wa maamuzi ya kuchukua na kuamua kuhusu kuendelea na kusimamia kitaalamu rasilimali hizi. Hii inamaanisha watafiti na wataalamu wa mambo haya ya wanyamapori na misitu wanapotoa ripoti ya kitafiti na kitalaamu kuhusu mwenendo wa maisha ya mwituni au kuhusu hali ya mazingira au makazi ya wanyamapori hawa tunapaswa kuwaamini na kuthamini kazi zao na mawazo yao yaliyo na nia njema ya kutunza maliasili zetu.

Hivyo linapokuja suala la uhifadhi wa mazingira asilia na mazingira ya wanyamapori linatakiwa kuangaliwa na kupimwa kwa faida ambazo zitaendelea kunufaisha jamii kwa karne nyingi. Inasema haya kwa sababu ya miradi mingi inaanza kushika kasi sana na kibaya zaidi miradi hii ya maendeleo ili iwepo lazima mazingira asilia yaharibiwe sana, tumeona miradi mingi ikiendelezwa kwenye hifadhi za wanyama kama vile uchimbaji wa madini ya uranium huko Selous, kuna miradi ya ujenzi wa barabara itakayopita katikati ya hifadhi ya Serengeti, kuna mashamba ya mpunga yaliyopo kwenye vyanzo vya maji ya mto Ruaha Mkuu. Miradi yote hii inapigiwa kelele sana na watalaamu n ahata mashirika ya umoja wa mataifa kwasababu uwepo wa miradi hii unatishia kwa kiasi kikubwa kuendelea kuwepo kwa uwiano wa kiikologia na pia kupotea kwa baadhi ya spishi za viumbe hai.

Kuanzishwa ka miradi hii ilikuwa ni kutatua matatizo ya kiuchumi kwenye jamii na nchi kwa ujumla, lakini tukipima kwa jicho la faida za miaka mingi ijayo utaona kuwa kuna faida za kudumu endapo mradi hii haitaanzishwa kwenye maeneo haya lakini pia kuna faida za muda mfupi endapo miradi hii ya maendeleo itaanzishwa kwenye meneo haya ambayo ni nyeti kwa uwepo wa wanyamapori. Tupime kwa miaka mia ijayo faida za miradi hii itakuwa kubwa kuliko faida za malisili hizi? Tukae chini tukubaliane kufanya maamuzi muhimu hata kama yana faida kidogo kidogo lakini inayodumu kwa vizazi vingi hii itakuwa boora zaidi.

Asante sana kwa kusoma makala hii, karibu kwa makala nyingine.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania