Faida za kiuchumi, kiikolojia na za kimazingira tunzaopata kutokana na uwepo wa wanyamapori zimekuwa ndio zinatufanya kukaa chini kila wakati na kubuni mbunu bora za wanyama hawa kuendelea kuwepo kwenye uso wa dunia. Licha ya utambuzi wa manufaa hayo tunayopata kutokana na uhifadhi wa wanyamapori bado inatuwia vigumu kuunganisha nguvu pande zote kuwatetea wanyamapori wasiendelee kutoweka katika uso dunia hii.

Licha ya serikali zetu kutenga maeneo mengi na makubwa kwa ajili ya uhifadhi wa wanyama hawa, bado kuna hatari ambayo inawakabili wanyamapori kila kona ya dunia. Sasa kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya dunia wanyamapori wamekuwa na matumizi mengi sana, ambayo kimsingi sio matumizi ya msingi kwa maisha ya binadamu.

Kila siku tunapoteza maelfu ya wanyamapori, ambao hutumika na watu matajiri na masikini kwa sababu mbali mbali, kama vile chakula, vinywaji, mavazi, urembo, madawa ya kienyeji, na sababu nyingine nyingi za kibiashara.

Mazingira na makazi asilia ya wanyamapori kila siku yanazidi kupungua, kuharibiwa na kutoweka, hii inasababishwa na ongezeko la watu kwenye maeneo karibu na hifadhi za wanyamapori. Watu wanapoingia kwenye maeneo haya, wanaanza kutafuta namna ya kuendesha maisha yao, namna ya kupata chakula, namna ya kujenga nyumba za kuishi, namna ya kulisha mifugo yao, shughuli zote hizo zenye lengo la kukidhi mahitaji muhimu ya maisha zina athari kubwa sana kwenye mazingira na makazi asilia ya wanyamapori na viumbe hai wengine.

Hali za namna hii zinasababisha kukithiri kwa vitendo vya kijangili kwa wanyamapori. Kwa mfano wanyamapori kama faru, tembo, simba, mbwa mwitu wanazidi kupungua sana kwenye maeneo yao ya kuishi kwa sababu ya ujangili na uharibifu wa makazi asili ya wanyama hawa.

Aidha, katika hali za namna hii kitu kikubwa tunachoshughudia watu kuishi karibu na maeneo ya wanyamapori ni migogoro isiyoisha na isiyo na ufumbuzi wa haraka. Kwasababu watu wanawinda wanyama wanaoliwa na wanyama wanaokula nyama, wanyama wanaokula nyama wanakosa chakula hivyo kuvamia mifugo ya wafugaji walio maeneo karibu na hifadhi, hali kadhalika uharibifu wa misitu, upanuzi wa mashamba na kilimo ambacho hufanyika karibu na maeneo ya hifadhi imesababisha wanyamapori wasumbufu wanaokula nyasi, kama vile tembo, tandala kula mazao ya wakulima walio lima maeneo hayo.

Leo katika uhifadhi, kwa changamoto hii unafikiri nini kinatakiwa kufanyika ili kusuluhisha hali hii? Naamini tunaweza kufikiri na kuja na suluhisho la kudumu ili kumaliza tatizo hili.

Naamini wasomaji wa makala hizi mnaweza kutushirikisha maoni yenu, kwasababu maoni yenu ni muhimu sana katika kujenga na kuimarisha misingi mizuri katika uifadhi wa maliasili zetu, lakini pia kuhakikisha uhifadhi unaleta manufaa yanayotarajiwa kwa jamii.

Nakushukuru sana Rafiki yangu katika uhifadhi wa maliasili zetu. Soma na washirikishe wengine maarifa haya muhimu.

Ahsante sana!

Hillary Mrosso

+255 683 862 481

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaamu.net/wildlifetanzania