Sehemu yoyote yenye vita, migogoro ya mara kwa mara husababisha hali duni ya maisha kwa wanajamii wanaoishi kwenye maeneo hayo. Kuna migogoro mingi sana katika nchi yetu na nchi nyingine duniani, migogoro mikubwa ni migogoro ya ardhi, mipaka ya maeneo, migogoro kati ya wakulima na wafugaji, migogoro kati ya wafugaji na mamlaka za uhifadhi wa maliasili nk.
Migogoro mingi inasababishwa na kutokuwepo au kutokueleweka kwa mipaka na maeneo maalumu ya kufanyia shuhuli za uzalishaji. Yani kutokuwepo kwa mipango bora ya matumuza ya ardhi pia kumesababisha watu kuingilia na kutumia maeneo ambayo hawajapangiwa kwa mujibu wa sheria zilizopo.
Kwa kiasi kikubwa migogoro hii imekuwa haina tija yoyote kwa jamii hata kwa nchi. Migogoro hii inaleta hali duni ya maisha kwa jamii. Hii ni kwa sababu watu wanatumia muda mwingi kutatua migogoro iliyopo na kushindwa kuzalisha, hivyo kupelekea hali mbaya ya uchumi kwa jamii hizi, hasa jamii ambazo zinaishi karibu na maeneo yaliyo na migogoro hii.
Mfano mzuri unaweza kuangalia hali ya mambo ilivyo kwenye maeneo mengi yenye migogoro ya ardhi, migogoro ya wafugaji na wakulima, migogoro kati ya mamlaka za hifadhi na wafugaji pia migogoro kati ya wanyamapori na wanajamii kwa ujumla. Ukiangalia maeneo haya utagundua kuwa licha ya kuwa na rasilimali muhimu kwa ajili ya kusaidia maisha yao kuwa bora, hali ya mambo haipo hivyo kwa sasa kutokana na migogoro iliyopo.
Migogoro hii isipotatuliwa mapema, tutakuwa kwenye hali mbaya hasa kwa siku za baadaye. Kwa sababu migogoro hii inachangia sana kukua kwa umasikini na pia hali ya uchumi kwa jamii hizi inazidi kuwa chini. Hivyo kusababisha umasikini uliokithiri licha ya rasilimali zilizopo kama vile maji, ardhi yenye rutuba, nk.
Changamoto zinazotokea kutokana na migogoro hii zinaacha alama ambayo sio nzuri katika jamii, kwa mfano fikiria mfugaji ameingiza ngombe katika hifadhi, au wanyamapori walao nyama wameua mifugo ya mfugaji, vilevile fikiria wakulima wanapoharibiwa mazao yao na wanyamapori kama vile tembo, nyani, tandala, kima, ng’uruwe nk. Kwa hali ya kawaida uhusiano na ushirikiano kwa matabaka haya mara nyingi sio mzuri.
Hali hii ndio hupelekea kukosa ushrikiano kwenye masuala mengi ya usimamizi na utunzaji wa mazingira. Chuki dhidi ya wanyamapori, kuongezeka kwa vitendo vya kijangili. Na pia ukizingatia jamii hizi zinapata manufaa kidogo sana kutokana na uwepo wa rasililamali hizi kwenye maeneo yao, hivyo jamii hizi huona kama zinakosa usawa katika haki na manufaa wanayotakiwa kupata.
Wizara ya maliasili na utalii, wizara ya kilimo, wizara ya ardhi na nyumba, wizara ya maji na umwagiliaji, wizara ya mazingira na wizara zote zinazohusiana kwenye matumizi ya ardhi zinatakiwa kufanya kazi kwa pamoja ili kutatua tatizo la migogoro inayowasumbua wananchi.
Napongeza juhudi zinazochukuliwa na serikali kupitia wizara ya ardhi, wizara hii ina mambo mengi sana ya kuyaweka sawa, hivyo naamini kwa kushirikana na wizara na mamlaka nyingine za kiserikali na za binafsi wanaweza kutatua tatizo migogoro isiyoisha ya ardhi.
Tukitatua migogoro hii mapema tutaisaidia sana jamii yetu kuwa na muda wa kuzalisha kwa wingi na pia mazingira mazuri ya kufanya kazi zao kwa usalama na amani.
Ahsante sana!
Hillary Mrosso
+255 683 862 481