Unaweza kujiuliza maswali mengi kwa nini serikali za nchi mbali mbali duniani zinatumia gharama kubwa sana katika uhifadhi wa maliasili za nchi zao. Pia unaweza kujiuliza kuna faida gani kwa mashirika na wadau kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza miradi mbali mbali ya uhifadhi wa maliasili hizi. Kuna mengi ya kufahamu ambayo msingi wake ndio inayopelekea serikali, wadau na mashirika ya uhifadhi wa maliasili kutumia gharama kubwa sana katika uhifadhi wa mazingira asilia, au maliasili.
Mfumo wa maisha ya viumbe hai hapa duniani umeuganishwa na vitu vingi ambavyo vingine tunavijua na vingine hatuvijui. Mungu alipoumba dunia alihakikisha vitu vyote vya misingi vinakuwepo ili mfumo wa maisha uweze kujiendesha wenyewe, baadaye alimuumba binadamu na kumuweka kwenye mazingira ambayo ndio yana mahitaji yake ya msingi yanayomfaa kuishi.
Fikiria mwenyewe kuna sayari nyingi sana, kuna nyota na vitu vingi sana ambavyo Mungu aliviumba, lakini katika sayari zote hizo na maeneo mengine mengi aliyoyaumba hakuna sehemu yenye mahitaji muhimu kwa maisha ya binadamu na viumbe wengine kama dunia hii. Tumepewa dunia, na dunia ndio ina mahitaji yote ya msingi kwa ajili ya maisha yetu na maisha ya viumbe hai wengine.
Hivyo basi, hakuna kitu kilichopo hapa duniani bila faida, kila kitu kina kusudi lake, wanyama, mimea, mito, hewa, mwanga, ardhi, milima, mabonde, kila kitu kina kusudi lake hapa duniani. Na kusudi kuu la uwepo wa viumbe na vitu vyote vilivyopo hapa duniani ni ili kufanya maisha kuwa bora kwa wote, wanyama na mimea. Hivyo msingi wa kila kitu na kila kiumbe kilichopo duniani ni kutegemeana, wanyama wanategemea mimea na mimea inategemea wanyama, hiyo ndio kanuni kuu ya maisha hapa duniani.
Kwa uwelewa huu kidogo, tunaweza kufahamu kwa nini tunatunza mazingira, tunatunza wanyama, ndege na samaki wa baharini. Katika mfumo huu wa utegemezi kitu kimoja kikikosekana maisha na hali ya hewa inabadilika kabisa katika dunia. Hivyo tunatakiwa kufanya kila tunachojua kufanya maisha ya viumbe hai kuzunguka katika kanuni hii ya asili.
Fikiria kama wanyamapori wote watatoweka, kitakachofuatia hapo ni watu watageuza mapori hayo kuwa mashamba, watakata miti, watachoma mioto, kitakachofuatia ni mabadiliko ya tabia nchi, mvua zinaanza kupungua na hatimaye zinakatika kabisa, kinachofuata hapo ni ukame na ujangwa, kinachofuatia hapo ni njaa kwa sababu hakuna chakula, jua ni kali, mvua na kitakachofuatia hapo ni kifo, kifo ambacho kitasababishwa na jua kali ambalo litaleta kansa ya ngozi na magonjwa mengine, pia vita vitatokea watu watauana kutafuta chakula, mwisho wote tutatoweka.
Kuna madhara mabaya sana yasiyoweza kuzuilika kirahisi pale tunaposhindwa kusimamia rasilimali zetu, kama misitu na wanyamapori, sijui hali ya hewa ingekuwaje maana kama miti au mimea itaangamizwa, maana yake kiasi cha hewa ya ukaa, au kabondiokside kingekuwa kikubwa sana duniani maana miti au mimea ambayo hunyonya au hutumia hewa hiyo imekufa, ni hatari sana kwa kweli.
Ndio maana, serikali, wadau na mashirika wameamua kujitoa kufanya kazi ya ziada kuzuia hali hiyo isitokee duniani. Ingawa kuna viashiria vya kutokea kwa hali hizi mbaya baadhi ya sehmu duniani. Hatua za makusudi zinatakiwa kuchukuliwa ili kudhibiti hali hiyo kuendelea.
Tufahamu hayo na tubadili tabia na mifumo yetu ya maisha ambayo inaweza kuleta athari kwenye mazingira yetu. Kumbuka sio wewe pekee unayepaswa kuishi hapa duniani, kuna watoto na vitukuu, kuna vizazi vingi vijavyo tunapaswa kujua hilo na kuishi kwa busara.
Tushirikiane na serikali zetu, wadau na mashirika yanayofanya kazi hii njema, tuwe wazalendo na kutunza wanyamapori, mimea na misitu yetu, uwe mwalimu kwa kuwajuza wengine wanaoharibu mazingira kwa namna yoyote ile. Tuwe sehemu bora na baraka kwa dunia.
Asante sana,
Makala hii imeandikwa na;
Hillary Mrosso
+255 683 862 481