Habarini wanandugu katika sekta yetu ya wanyamapori. Kama ilivyo ada tunaingia tena kwenye mtiririko wetu wakujua japo machache kuhusu wanyamapori na uelekeo wa wanyama hawa. Leo nakuja na mnyama mwingine ambae watu wana mfahamu sema kwa uchache zaidi. Sasa kama tujuavyo hapa utapata kuongeza asilimia 85% zaidi katika kumjua zaidi ya ulivyokuwa unamjua. Na moja kwa moja namzungumzia “NYATI (MBOGO)” Tega akili kisawasawa na twende pamoja katika mtiririko huu ndugu yangu.
UTANGULIZI
NYATI ni wanyama jamii ya ng’ombe ambao wanaishi misituni au maporini japo kuna wengine hufugwa na binaadamu. Ikumbukwe kuna aina mbili za nyati ambazo ni (1) Nyati wa Afrika na (2) Nyati maji wa bara la Asia. Nyati wote hawa wana rangi za kufanana ambayo ni kijivu inayoelekea kuwa kama nyeusi. Nyati ni wanyama walio tawanyika sana hususani barani Afrika na wanaonekana kirahisi sana hasa katika hifadhi za taifa na mapori ya akiba katika nchi mbalimbali barani Afrika.
Kama kawaida tunajivuna na kile tulichonacho barani kwetu Afrika na hasa pia nchini kwetu Tanzania. Hapa bila kupoteza muda moja kwa moja tunakwenda kumuangalia nyati wa Afrika. Nyati wa barani Afrika wamegawanyika katika makundi mawili ambayo ni Nyati wa msituni na Nyati wa savanna.
Hapa nchini Tanzania nyati ni mnyama mwenye sifa kubwa sana na hasa mpaka kuingizwa katika wanyama watano ambao ni kama nguzo yakuonesha ubora na thamani ya wanyamapori tulionao katika hifadhi zetu. Wanyama hawa watano kwa lugha ya kigeni wanaitwa “BIG FIVE” ambao ni Tembo, Faru, Nyati, Simba na Chui. Sasa hapa ndo tunaona nikwajinsi gani nyati ni mnyama muhimu sana hasa katika kulitangaza taifa pia kwa upande wa maliasili.
SIFA ZA NYATI WA AFRIKA
1.Wana rangi ya kijivu ambayo inaelekea kuwa kama nyeusi au kahawia hasa kutokana na maeneo na jamii mbalimbali za nyati wa Afrika.
2.Wana miili iliyo jaa, mizito na miguu yenye nguvu zaidi.
3.Nyati wa Afrika wana vichwa vikubwa na mashing mafupi.
4.Wana pembe kubwa zilizo jikunja kuelekea ndani mithili ya ndoano…Dume ana pembe kubwa zaidi ya jike na zimekaribiana sana hasa maeneo ya chini. Na hii ni moja ya njia yakutofautisha kati ya jinsia ya kike nay a kiume. Lakini nyati wa msituni ana pembe zilizo taka kunyooka kidogo tofauti na wengine.
5.Wana masikio makubwa kidigo na yalio lala…Maranyingi masikio husimama wanapohisi hatari.
- Wana uwezo wakunusa na kutambua kitu kwa harufu hata kikiwa mbali kutokana na uelekeo wa upepo.
7.Dume huwa na mwili mkubwa ukilinganisha na nyati jike.
8.Nyati wana uwezo wakutembea kilometa 5.4 kwa saa. Lakini kwa kukimbia nyati wana uwezo wakukimbia mpaka kilimeta 57 kwa saa.
UZITO WA NYATI
Nyati wa msituni 265kg-320kg
Nyati wa savanna 300kg-900kg
UREFU
Kichwa na mwili sentimita 170cm-sentimita 340cm
Mkia sentimita 70cm-sentimita110cm
KIMO
Sentimita 100cm-sentimita 170cm
UMRI
Nyati anapiokuwa katika hifadhi ya taifa au eneo lolote lile lenye kuhifadhiwa huweza kuishi mpaka myaka ishirini (20). Lakini anapokuwa anafugwa hufikisha mpaka myaka 29.
TABIA ZA NYATI
Hapa kuna mambo mengi sana utajifunza kuhusu mnyama huyu na ndipo utaipata ile asilimia 85% niliyo isema hapo mwanzoni.
1.Nyati wa savanna huwa wanaishi kwenye kundi kubwa kuanzia wanyama 50-500. Na katika kundi hili ndani yake kunakuwa na vikundi vidogo vidogo vya familia ambavyo huundwa na kina mama na watoto.
2.Ushirikiano wa kina mama ni mkubwa sana na hasa pale wanapo sikia mwenzao katoa sauti yakulalamika au hatari basi huwa tayari kuja kumsaidia. Hii husaidia hata kuwalinda wale wasio na nguvu katika hatari kutoka kwa maadui zao.
- Ndani ya makundi hayo pia huwa kuna kundi la madume ambao wanakuwa na hawajapata majike wakuzaa nao na kundi hili la madume huweza kufikia mpaka wanyama 12.
4.Nyati wa msitu mara nyingi hupatikana kwa makundi madogo ambapo huwa na wanyama 8-20 na kundi hili huwa na kina mama ambao wana ukaribu sana hasa wa kindugu pamoja na watoto.
5.Nyati ni wanyama ambao wanaweza kufanya shughuli zao mchana na hata usiku pia kwasababu wanakuwa na uwezo wakuona angalau umbali mdogo usiku.
6.Nyati hutumia masaa 18 kwa siku akiwa anakula na wakati huo kundi likiwa lina tembea kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.
7.Nyati huitaji kunya maji kila siku na mara nyingi wanyama hawa hupatikana maeneo ambayo upatikanaji wa maji unakuwa ni warahisi sana. Hunywa maji mara nyingi wakati wa asubuhi.
8.Panapo kuwa na shida ya maji, nyati hujikusanya pamoja maeneo ambao umbali wa maji ni mfupi kutoka juu ya aridhi kasha huanza kupiga miguu yao chini kwa kushirikiana na hatimae kutengeneza shimo mpaka maji hutokea juu kasha wanaanza kunywa.
9.Hupendelea sana kuoga kwenye matope nah ii ni kwasababu wanaondoa wadudu mwilini lakini pia kupunguza joto hasa kipindi cha jua kali.
10.Kipindi cha majira ya joto kuanzia saa sita mchana mpaka saa kumi jioni nyati hupenda kupumzika na wakati huu huwa wana cheua chakukula kasha kuanza kukitafuna upya. Mara nyingi hupumzika maeneo yenye jua na sio kivulini.
11.Katika maeneo ambayo yamevamiwa sana na binaadamu nyati hupenda sana kula wakati wa usiku nah ii ni kuepusha hatari ya kutosumbuliwa na binaadamu wanapokuwa wanakula.
12.Nyati wa Afrika huishikwa demokrasia na inapofika kipindi cha kusafiri basi husimama na kilammoja kuelekea upande wake anaotaka kwenda. Baada ya hapo upande utakaokuwa na idadi kubwa basi huonekana washindi na nyati jike kiongozi hutangulia kasha wengine wote hufuata uelekeo ule.
MUHIMU KUJUA….
*Nyati ni mnyama mwenye uwezo wa kumkariri mtu alie mjeruhi mfano jangili au askari wanyamapori kama alikuwa anajitetea ili asiuwawe na kumpiga nyati. Hivo kumbuka nyati huyu endapo atapona na akuona sehemu ana uwezo wa kukumbuka na atakufata kulipiza kisasi tu.
*Nyati ni miongo mwa wanyama hatari katika historia yakumuuwa binaada baada ya kiboko.
CHAKULA
Nyati ni wanyama jamii yaw ala majani. Hivyo chakula chao kikubwa zaidi ni majani lakini wakati mwingine panapokuwa na shida ya majani basi nyati hula hata kwenye miti midgo midogo. Na kama tulivyoona hapo juu nyati hutumia mpaka masaa 18 katika kula kwa siku. Haya ni masaa mengi sana ndomana mnyama huyu ana nguvu sana ukimuangalia.
MAZINGIRA
Nyati ni wanyama wenye uwezo wakuishi kkatika mazingira ya aina tofauti tofauti sana kuanzia maeneo ya savanna, maeneo yenye majani, maeneo ya vichaka na misituni pia. Na wana uwezo wakuishi sehemu ambayo ipo wazi isiyo na kivulu kwa muda mrefu sana.
Na sili zote nyati wa afrika uwa hawakai zaidi ya kilometa ishirini (20) kutoka kwenye eneo la maji kwasababu wanahitaji maji kila siku.
KUZALIANA
Kama hali ya hewa ni nzuri na mvua zinanyesha vizuri nyati huweza kuzaliana kipindi chochote katika majira ya mwaka. Lakini maranyini huwa wanapandana kuanzia mwezi wa tatu hadi mwezi wa tano. Lakini kama maji yanakuwa ni ya shida basi nyati huzaliana kipindi cha majira ya unyevunyevu. Nyati jike huingia kwenye mzunguko wa hedhi kila baada ya siku 23 na hudumu hapo kwa muda wa siku tano mpana sita.
Anapo pata mimba nyati jike hukaa na mimba kwa muda wa siku 340 na huzaa mtoto mmoja . Ni mara chache sana kwa nyati kuzaa watoto wawili.Nyati wa savanna huzaliwa akiwa na rangi ya weusi inayofanana na kahawia au wekundu na kahawia kwa mbali wakati nyati wa msitu huzaliwa na rangi kama nyekundu iliyo pauka. Wastani wa uzito kwa watoto wa nyati hawa wanapo zaliwa uwa ni kilogramu 40kg lakini nyati wa savanna kuna wakati hufikia mpaka kilogramu 55-60 anapozaliwa. Mama hukaa na kumlinda mtoto kwa muda wa miezi sita chini ya uangalizi mkubwa sana hasa kutokana na maadui. Mtoto wa nyati hufikia umri wakuzaa akiwa na myaka kuanzia mitatu na nusu mpaka myaka mitano.Baada ya umri huo watoto wa kike hubaki nakujiunga na kundi la kina mama wakati madume hujiunga na kundi la kina baba. Ikumbukwe kua kama mazingira ni mazuri nyati huzaa kila mwaka.
UMUHIMU WA NYATI
1.Nyati ni kivutio kikubwa cha utalii hasa pale mtu anaposikia kuwa nyati ni miongoni mwa wanyama waliopo katika kundi la wanyama wakubwa watano na muhimu hapa nchini. Mtu hupata shauku kubwa sana na kutamani kumjua hasa huyu nyati ni nani bali na kumuona pia.
2.Serikali inaingiza pesa nyingi sana kupitia sekta za utalii hususani wizara ya maliasili na utalii kwani kuna watalii hutoka nchi mbalimbali kwa ajili yakuja kumuona mnyama kama nyati tu.
3.Pia katika vitalu vya uwindaji serikali inaingiza pesa nyingi tu na ukitaka kuamini hili fatilia maeneo ambayo kuna mapori ya akiba yanayo milikiwa na wanajamii au vijiji utapata takwimu nikiasi gani wanaingiza kwa mwaka kwakutoa vibali vya uwindaji wa nyati.
4.Nyati hutumika kama kitoweo kwa wananchi nahivyo kujiongezea afya nzuri kwa kula protini itokanayo na nyama ya nyati.
5.Pia malighafi kama ngozi, kwato na pembe za nyati hutumika kutengenezea vitu kama viatu, nguo na mapambo mengi sana ya nyumbani na hata yakuvaa mwilini pia.
UHIFADHI HAPA NCHUNI KWETU TANZANIA
Ni jambo kidogo lakujivunia kuwa hadi sasa nyati bado hawajaingizwa katika kundi la wanyama wanaoelekea kutoweka duniani. Lakini hii haitoshi kujiridhisha na kuamini kwamba wataendelea kubaki idadi kama hii iliyopo kwa sasa kwasababu nyati wetu wanakumbwa na matatizo mengi sana huko hifadini. Matatizo na changamoto hizo tunakwenda kuziona hapa chini sasa.
CHANGAMOTO/MATATIZO YANAYO WAKUMBA NYATI HAPA KWETU TANZANIA
1.Ujangili ulio kithiri hasa katika hifadhi zetu za taifa. Nyati huwindwa sana na majangingili kwa dhumuni la nyama,
ngozi na malighafi zake nyingine. Hii hupelekea sana kupungua kwa kiasi kikubwa kwa wanyama hawa hifadhini.
2.Uharibifu wa mazingira hasa unaosababishwa na binaadamu katika maeneo tengefu ya wanyamapori. Mazingira yamekuwa yakiharibiwa sana na hatimae nyati pamoja na wanyama wengine kukosa chakula na kulazimika kuhama maeneo yale. Yote hii husababishwa na uvamizi wa maeneo ya uhifadhi kutokana na kuongezeka kwa shughuli za binaadamu.
3.Magonjwa mbali mbali kama kimeta na homa ya bonde la ufa, Japo magonjwa sio tatizo kubwa sana lakusema kwamba nilakutilia mkazo sana kwasababu wanyamapori wamezaliwa poroni wakiwa na vinasaba vya kuwasaidia kupambana na magonjwa mbalimbali tofauti na wanyama wafugwao. Wanyamapori wana uwezo mkubwa wa kustahimili magonjwa hasa ukulinganisha na wanyama tunaowafuga majumbani kwetu.
4.SIASA katika uhifadhi, nadiriki kusema kuwa siasa ni sumu kubwa kama lilivyo tatizo la ujangingili katika wanyamapori. Viongozi wengi wamekuwa wakiingiza suala la siasa katika uhifdhi na hatimae kufanya shughuli za kihifadhi kuwa nguimu sana. Na yote hii hutokana na maslahi yakutaka kura toka kwa wananchi nakusahau kuwa kuna vizazi vinakuja ambavyo vitahitaji kuona uwepo wa nyati na wanyamapori wengine katika hifadhi zetu za taifa. Nitoe mfano mzuri tu kwa kile kinacho endelea huko Loliondo baina ya pori la akiba na viongozi wanao husika. Ukweli ni kwamba wana vijiji wanavamia maeneo ya wanyamapori lakini kila linapokuja suala lakuwakataza nakuwaondoa maeneo hayo viongozi wao wanaingilia kati kutetea wakiamini kwamba endapo wanakijiji watatolewa eneo hilo kwa kusema ukweli basi uchaguzi ujao hawatompa kura.
5.Uwindaji dhaifu, kuna tofauti kubwa sana tunaposema ujangili na uwindaji dhaifu. Uwindaji dhaifu ni kwamba mtu tayari anakuwa na kibali cha uwindaji na anapewa ruhusa yakuwinda nyati mmoja au wawili kutokana na kibali chake. Lakini anapokuwa kule anakiuka taratibu nakuzidisha idadi ya nyati aliotakiwa kuwinda. Pia maranyingi hutolewa vibali vya kuwinda nyati madume lakini mtu huwinda mpaka majike na watoto hii hupelekea sana kupungua kwa wanaya hawa hasa tu kutokana na uwindaji dhaifu.
6.Migogoro iliyopo baina ya wanyamapori na binaadamu, nyati niwanyama ambao huishi kwa kuhama na pale wanapohama kuna wakati hupita mashambani kwa watu nakula mazao yao, Hii hupelekea wanavijiji kuwauwa kwa sumu au hata kwa kuwachoma mishale. Lakini tukirudi nyuma hii husababishwa na watu kuvamia maeneo ya uhifadhi nakuanza shughuli za kibinaadamu maeneo hayo.
NINI KIFANYIKE KUWANUSURU NYATI WETU
1.Kupambana na ujangili kwa hali na mali kwa kuongeza askari wanyamapori katika maeneo tengefu ya uhifadhi wanyamapori na hifadhi za taifa. Hii pia inafatana na kuongeza doria za mara kwa mara katika maeneo husika ili kupunguza adha ya ujangili hapa nchini.
2.Kuwepo kwa sera ambazo zitasaidia kupambana na uharibifu wa mazingira hasa karibu na hata ndani ya maeneo ya uhifadhi ili ili kupunguza kuhama hama kwa wanyama hawa kwa ajili yakutafuta chakula.
3.Kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wakuwatunza wanyamapori na utunzaji wa mazingira kwasababu watakuwa mabalozi wazuri hata kuweza kuwafichua majangili ambao wanaishi katika maeneo yao.
4.Kuwaanzishia wana vijiji miradi mbali mbali ili wawe wanatumia muda mwingi kuwaza maendeleo ya miradi yao na si kuwinda wanyama pori. Shukrani sana kwa shirika la Uhifadhi wa mazingira kwa wanyamapori na maendeleo ya jamii (ECOWICE-Environmental Conservation for Wildlife and Community Enterprise) kwa miradi yao wanayo iendesha kama uoteshaji wa uyoga unasaidia sana kwa kiasi kikubwa katika utunzaji wa mazingira na uhifadhi wanyamapori.
5.Ufatiliaji mzuri na uhakiki wa vibali vya uwindaji vinavyo tolewa kwa wawindaji ili kuepuka changamoto ya kuwindwa kwa wanyama zaidi ya idadi ya waliotakiwa kuwindwa. Bali pia kuwafatilia wahusika pale wanapokuwa wanatekeleza shughuli ya uwindaji ili pasiwepo na utofauti wowote kati ya kibali kisemavyo na kile kinacho fanyika eneo la uwindaji.
6.Migogoro baina ya binadamu na wanyamapori itafutiwe ufumbuzi haraka kwasababu hii pia inazidi kukua siku baada ya siku. Mfano kupaka pilipili maeneo ya mazao au pembezoni mwa mashamba hii husaidia sana kuzuiya nyati na wanyama wengine walao mazao wasisogee karibu kutokana na kuwasha kwa pilipili.
7.Kupambana sana na kuitokomeza SIASA katika suala zima la uhifadhi wnyamapori mana ni sumu inayoenea polepole na mwisho wake kusababisha upotevu wa wanyamapori. Panapo hitajika ukweli basi pasemwe nah ii hasa wanayo WABUNGE kwani wamekuwa waleta porojo sana linapokuja suala lakkuwataka watu kuhama maeneo ya uhifadhi. Wamekuwa wakitetea sana suala hili kwa maslahi yakutaka kupigiwa kura msimu wa uchaguzi unaofuata bila kujali maslahi na thamani ya wanyamapori kwa watanania wote.
8.Kutekelezwa kwa shera zilizowekwa ambazo zinasimamia masuala ya maliasili bali pia na usimamizi wa wanyamapori. Sheria hizi zifanye kazi bila kuangalia alieye kiuka shria ni nani na ana wadhifa gani. Kwani tukumbuke ukimuangalia mtu cheo alichonacho na kuharibu mali ya uma anaumiza wananchi walio wengi sana.Hivyo mamlaka husika ziwe macho na kufatilia utekelezaji wa sheria hizi.
9.Yafanyike matangazo ambayo yatakuwa yanaonesha thamani ya wanyamapori lakini pia kuhamasisha watu kufanya utalii wa ndani kwa kupunguza gharama au kuweka wazi gharama husika kama inavyofanyika kwa baadhi ya maeneo. Gharama za sasa haziwafikii wananchi waliyo wengi na hatimae wachache ndio huweza kutembelea hifadhi zetu za taifa.
HITIMISHO
Ni matumaini yangu umejifunza mambo mengi sana kuhusu nyati na kama umesoma vizuri basi umejinyakulia zile 85% nilizo zisema hapo juu. Lakini pia hata kama ulikuwa unamjua nyati kwa undani naamini pia umepata japo kitu kipya katika, aelezo hayo mafupi kuhusu mnyama huyo.
Napenda kutoa pongezi zangu za dhati kwa shirika linalo simamia hifadhi zetu za taifa (TANAPA) kwa kazi kubwa sana mnayo ifanya ili kuhakikisha tunaendelea kuwa na wanyamapori nchini kwetu. Pia shukrani sana kwa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA-Tanzania Wildlife Authority) kwa mchango wenu mkubwa katika uhifadhi wa wanyamapori.
Sisi kama wananchi tunalo jukumu pia lakuhakikisha tunasaidia mamlaka hizi kwani uwepo wa wanyamapori ni fahari kubwa sana kwa nchi yetu. Tuwe na tabia yakutembelea hifadhi zetu za taifa na maeneo ya uhifadhi kwani kwa mtanzania gharama zake huwa ni ndogo sana kwa kima cha shilingi za kitanzania 5000 tu. Hii itakuza sana ufahari na imani ya mtu juu ya uhifadhi wa wanyamapori bali pia kuhamasisha na wengine kutembelea hifadhi zetu za taifa na kujionea mengine mengi sana katika hifadhi zetu za taifa 16.
*************MWISHO***********
Kwa mengi kuhusu wanyamapori, ushauri juu ya kazi matoleo ninayo yafanya na maoni zaidi tuwasiliane kupitia: 0714116963/0765057969 na 0785813286
Email : swideeq.so@gmail.com
Bachelor of Science in Wildlife Management-Sokoine University of Agriculture (SUA) 2016
………………. I’M THE METALLIC LEGEND……….