Habarini tena ndugu katika uhifadhi wa wanyamapori

Kama ilivo kawaida yeu leo tena tunaingia katika darasa letu na kuendelea na mtiririko wa kujuzana machache na yenye manufaa kuhusu wanyamapori wetu hapa nchini. Hapautpata kuwatambua wanyama hawa vizuri na kwa undani zaidi ya ulivokuwa unawajua.

Kama utakuwa mfuatiliaje mzuri wa makala yangu kuna siku nilisema kuwa kuna aina nyingi sana za wanyama jamii ya swala na nikawataja baadhi yao. Sasa leo tunamuangalia swala mwingine tena anaejulikana kwa jina la “TANDALA”

UTANGULIZI

Kama nilivo tangulia kusema hapo juu tandala ni wanyama jamii ya swala ambao wanaishi pia misituni hususani katika hifadhi zetu za taifa. Tandala wamegawanyika katika makundi mawili ambayo ni (1) Tandala wakubwa na (2) Tandala wadogo. Japo wana fanana kwa kiasi kikubwa lakini pia kuna utofauti mkubwa pia kati ya tandala wakubwa na tandala wadogo.

Hivyo basi ili kuepuka kuchanganya mambo nivyema moja kwa moja tukachagua aina mojawapo ya tandala kasha kuanza kumuelezea vizuri na kwa ufasaha. Na moja kwa moja tunamuangalia “TANDALA MDOGO”

MUHIMU

Naposema tandala mdogo simaanishi mtoto wa tandala laghasha, jina hili ni kwaajili ya kuwatofautisha swala hawa wa aina mbili.

SIFA ZA TANDALA MDOGO

1.Ni aina ya swala anaependa kuishi maeneo ya misitu na hupenda kujificha kwenye miti inayo fanana na rangi ya ngozi zao ili kuepuka maadui zao na hii huwasaidia sana.

2.Wana mistari myeupe iliyo anzia mgongoni nakuelekea chini maeneo ya tumboni na sehemu ndogo ya miguu hususani miguu ya nyuma. Mistari hii huwa ni kati ya kumi na moja mpaka kumi na nne (11-14)

3.Dume huwa na rangi ya kijivu mchanganyiko na kahawia wakati jike huwa na rangi inayo fanana na matunda ya muarobaini yalioiva.

4.Dume huwa ana manyoya yalio jiokeza kidogo shingoni ila jika hana manyoya haya.

5.Dume ana pembe zilizo jikunja  zenye kuweza kufikia urefu wa sentimita sabini (sm70) lakini jike uwa hana pembe kabisa.

6.Tandala wadogo wote dume na jike wana mistari minene ya rangi nyeupe sehemu ya chini ya shingo.

7.Tandala hawa wana uwezo wa kuruka umbali wa zaidi ya mita 9 (sawa na futi 30) na pia kuruka zaidi ya kimo cha mita 2.5 (sawa na futi 8.2).

8.Tandala wadogo wanapokuwa hatarini wa uwezo wakukimbia kilomita mia moja kwa saa (100km/saa).

UZITO WA TANDALA WADOGO

Wanyama hawa huwa na wastani wa kilogramu 50-108 japo huwa kuna tofauti kati ya uzito wa dume na jike.

Dume=60kg-108kg

Jike=50kg-70kg

UREFU

Kiwiliwili=1.1m-1.7m (sawa na futi 3.6-5.6)

Mkia=sm25-40 (sawa na nchi 10-16)

KIMO

Sentimita 90-105sm

TABIA ZA TANDALA WADOGO

1.Huwa wapo vizuri wakati wa usiku na alfajiri tofauti na mchana.

2.Mara tu jua linapoanza kuchomoa hutafuta maeneo yalio tulia ili kupumzika na kujificha kutokana na maadui.

3.Tandala hawa ni wanyama wenye aibu na muda wote wanakuwa na wasiwasi.

4.Wanapohisi hatari hukimbia huku mkia ukiwa juu kiasi kwamba rangi nyeupe iliopo kwa ndani ya mkia huonekana.

5.Hupenda kuishi kwa kundi lakini kundi haliwi na wanyama wengi sana ambapo maranyingi huwa na wanyama 10 mpana 12.

MAZINGIRA

Tandala wadogo hupendelea sana maeneo makavu ambayo yana miti mingi na hasa kwa maeneo yenye miinuko. Ni ngumu sana kuwaona tandala wadogo kwenye maeneo ya wazi na hata ukiwaona ni mara chache sana hasa wanapokuwa wanakimbizwa na maadui zao katika kujiokoa.

CHAKULA

Hawa ni jamii ya wanyama walao majani na maranyingi hula majani machanga juu ya matawi ya miti. Wakati wa kiangazi tandala hula mpaka matikitimaji ya porini na baadhi ya matunda mengine. Ni wanyama wnye uwezo wakuishi muda mrefu bila kunywa maji tofauti na walivyo tandala wakubwa.

KUZALIANA

Inapofika msimu wa kuzaliana madume hupigana ili kupata majike na maranyingi anaeshinda ndo huwa na nafasi yakupanda majike. Dume maranyingi hujiunga na kundi la kina mama kipindi ambacho wanahitaji kuzaliana na baada ya kupandana dume huondoka ndani ya kundi hilo na kujiunga na madume wenzake. Jike hukaa na mimba kwa muda wa miezi saba na nusu mpaka minane na baada ya hapo huzaa mtoto mmoja tu. Mara tu baada yakuzaa mama hujitenga kwa muda kutoka kwenye kundi kwa muda wa wiki 4-5 ili kumtunza mwanae aweze kukua vizuri. Mtoto wa tandala mdogo huzaliwa akiwa na uzito wa wastani wa kilogramu 4kg-75kg.

Asilimia hamsini (50%) ya watoto wanaozaliwa maranyingi hufa ndani ya miezi sita kwa magonjwa au kuliwa na maadui. Na takwimu zinaonesha ni asilimia 25% t undo huwa wanafikisha umri wa myaka 3 nakuendelea. Mara tu baada ya mwaka mmoja tandala madume hufukuzwa kwenye kundi la kina mama. Tandala jike huanza kuzaa mara tu afikishapo mwaka mmoja wakati tandala dume huanza kupanda afikishapo myaka kuanzia 3 nakuendelea.

UMRI WA TANDALA WADOGO

Tandala wadogo wana uwezo wakuishi myaka 7-8 wanapokuwa hifadhini au katika mapori ya akiba. Ila wanapokuwa wamefugwa huweza kufikia mpaka myaka 23.

MAADUI WA TANDALA WADOGO

Maadui wakubwa wa tandala wadogo ni binaadamu, simba, chui, mbwa mwitu, fisi na chatu.

UHIFADHI

Tandala wadogo wanapatikana barani Afrika tu na kwenye nchi ambazo zipo upande wa mashariki mwa Afrika. Nchi hizi zipo sita tu ambazo ni Tanzania,Kenya, Uganda, Somalia, Ethiopia na Djibouti. Lakini kwa data za IUCNza mwaka 2008 inasemekana kuwa wanyama hawa tayari wamesha toweka nchini Djibouti.

Hapo zamani ilisemekana wanyama hawa wanapatikana mpaka nchi ya Saud Arabia. Lakini kwa utafiti ulio fanyika inaonekana nakutoa ripoti inaonekana kuwa wanyama hawa walipelekwa nchini humo myaka ya 1960 kwa ajili ya mawindi hasa kwa familia za kifalme.

Sensa iliyo fanyika mwaka 1999 inaonesha kuwa idadi ya wanyama hawa ni 118,000 kwa ujumla katika nchi zote na kwa sasa inazidi kupungua. Hii pia inapelekea wanyama hawa kufikia kuingizwa katika kundi la wanyama waliyo katika tishio kubwa na IUCN katika orodha ya mwaka 2016.

TISHIO KWA TANDALA WADOGO NCHINI TANZANIA

  1. Uwindaji holela wa wanyama hasa kwa makampuni ya uwindaji. Hii hupelekea wanyama hawa kutoweka hasa ukizingatia kutokana na aibu zao na adha wapatazo kutoka na uwindaji usio fatiliwa.

2.Ujangili ulio kithiri katika hifadhi zetu za taifa na mapori ya akiba.

3.Uharibifu wa mazingira na uvamizi wa maeneo ya uhifadhi wanyamapori.

4.Magonjwa hasa ukizingatia wanyama hawa kuna baadhi ya magonjwa kama rinderpest ni ugonjwa unao wauwa sana.

5.Migogoro ya kisiasa inayo endelea na udhaifu pamoja na maamuzi yasiyo na tija ya serikali hasa katika kuwapa wawekezaji maeneo bila kujali uwepo wa wanyamapori. Mfano mzuri ni kile kilicho amuliwa huko Loliondo katika pori lile la akiba.

  1. Idadi ndogo ya askari wanyamapori ambao wanashindwa kumudu doria na ufuatiliaji mzuri wa majangili hifadhini.

7.Uhaba wa elimu ya uhifadhikwa jamii hasa kupelekea wananchi hawa kujiingiza katika vitendo vya ujanginili.

NINI KIFANYIKE KUWANUSURU TANDALA WADOGO WA TANZANIA

1.Kuwepo na ufuatiliaji mzuri wa vibali vya uwindaji hasa kwa makampuni husika kwani wamekuwa wakienda kinyume sana na mikataba ya vibali hivyo.

2.Uandaaji wa sera na sheria zitakazo pambana na uvamizi wa hifadhi za taifa na mapori ya akiba ili kutokomeza tabia hii hasa ambayo hupelekea uharibifu wa mazingira na ujangili.

  1. Kuongeza idadi ya askari wanyamapori ili kuongeza msukumo wa ufuatiliaji na doria katika maeneo ya mipaka ya hifadhi za wanyamapori na mapori na mapori ya akiba.

4.Kutoa elimu kwa wananchi hasa wale wanaoishi pembezoni mwa mapori ya akiba na hifadhi za taifa. Hii napenda sana kulipongeza shirika lisilo la kiserikali la ECOWICE kwa elimu nzuri pia wanayotoa na miradi mbali mbali.

5.Tuepuke kuingiza siasa na maamuzi mabovu katika masuala ya uhifadhi wanyamapori mana inasababisha upoteaji mkubwa sana wa rasilimali hizi za wanyamapori ambazo ni mali ya watanzania wote.

 

HITIMISHO

Tandala ni wanyama wanaosemekana ndo swala wazuri zaidi na wanao vutia hasa ukiangalia rangi yao. Tuwe na utamaduni wakuwa tunajivunia wanyama wetu hapa nchini kwa kutembelea hifadhi zetu kwa wingi kwasababu tutajifunza mambo mengi  kwakufanya hivyo.

Narudia tena kulipongeza shirika na ECOWICE kwa msaada wa elimu na miradui linayo ifanya kwa wananchi ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuepukana na suala la ujangili au kutemea misaada toka kwa watu. Bila kuwasahau TANAPA kwa msaada mkubwa wanao ufanya katika kusimamia hifadhi zetu ili kuwanusuru wanyamapori na mazingira yao.Halikadhalika TAWA pia kwa kushirikiana na wizara ya maliasili na utalii wanamchango mkubwa sana katika kulinda wanyamapori wetu.

Tusiwe kama nchi ya Djibouti ambayo kwa sasa tandala wamepotea na imebaki kuwa kama historia kwao na kujutia hapo baadae.

……………MWISHO……………

 

Kwa mengi kuhusu wanyamapori tuwasiliane kupitia

Email=swideeq.so@gmail.com

Simu=0714116963/0765057969/0785813286

Wildlife Manager, Sokoine University of Agriculture.

 

……..I’M THE METALLIC LEGEND…….