Kama baada ya moja inayofuata ni mbili, basi nami baada ya makala iliyo pita inafuata makala nyingine katika mtiririko wetu wa darasa huru la wanyamapori. Huwa sikuachi hivihivi bila kukupa angalau kitu kipya kutokana kwenye darasa hili huru na nimatumaini yangu huwa unajifunza kupitia mapya upatayo toka kwenye makala hizi.

Leo tena tuingie darasani ili kuendeleza mfululizo wa darasa letu huru kuhusu wanyamapori na kujua uelekeo wa wanyama hawa na mazingira yao hali kadhalika ni changamoto zipi zinawakumba wanyama hawa na njia za kutatua changamoto hizo kwa ujumla. Nakusihi ndugu msomaji kuwa nami kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa makala hii kwani utajifunza mengi sana kutoka kwa mnyama ambae atakuwa mezani kwa siku ya leo.

Na leo moja kwa moja tutamwangalia mnyama “KIBOKO” ambae anapatikana bara la Afrika tu.

UTANGULIZI

Kiboko ni miongoni mwa jamii ya wanyama ambao wana ishi muda mrefu sana kwenye maji ukilinganisha na mamalia wengine wote. Kiboko hutafsirika kama farasi wa mtoni na hii imetokana na asili ya jina la kingereza la mnyama huyu kwani unaposema hippopptamus kwa kigiriki basi unamaanisha “river horse” farasi wa mtoni. Kiboko ni mnyama mkubwa kimaumbile na ana sifa nyingi sana hata baadhi kuandikwa kwenye historia ya maisha ya binaadamu.

Sasa tuingie ndani zaidi ili kujua sifa za mnyama huyu na historia aliyo jiandikia mnyama huyu hata kuwa hatari sana kwenye maisha ya binaadamu.

SIFA NA TABIA ZA KIBOKO

1.Macho na matundu ya pua ya kiboko yapo kwa upande wa juu ya kichwa na hii inamsaidia kuona na kupumua hasa pale anapokuwa kiwili wili kimezama ndani ya maji na kutoa kichwa juu ya maji.

2.Ana vidole vine kwenye kila mguu ambavyo kidole kimoja na kingine vimeshikana kupitia ngozi katikati kama vilivyo vidole vya bata na hii humsaidia kuupa mwili usawa kwenye kusimama.

3.Macho ya kiboko yana utandu wenye kuonesha ambao humuwezesha mnyama huyu kufumbua macho na kuona hata awapo ndani ya maji.

4.Wana miili mikubwa, vichwa vikubwa na miguu mifupi yenye misuli yenye nguvu.

5.Kiboko ana mdomo mkubwa na taya zenye nguvu sana .

6.Ni wanyama ambao wanaishi kwa mipaka na hii hutokea tu wawapo ndani ya maji kwani huweka mipaka yao kupitia kemikali lakini kinyesi ili kuzuiya viboko wengine wasivmie eneo lao.
7.Viboko ni wanyama ambao wanaishi kwa makundi, na kundi huwa na viboko 10-30 au zaidi. Kundi hili huongozwa na dume mtawala kwa kipindi hicho na ndio mwenye uhuru wakupanda majike wote wapatikanao kwenye kundi.

8.Viboko ni wanyama ambao hutumia muda wa usiku kutafuta chakula na wanaweza kutembea hadi kilometa 10 wakiwa wanakula tu.

9.Hutoa maji maji yenye rangi nyekundu na watu huchanganya nakusema hii ni damu laaghasha, haya ni maji maji maalumu ambayo wanyama hawa huyatoa ili kuulainisha mwili kutokana na athari zitikanazo na mionzi ya jua.

10.Mbali na kuwa na maumbile makubwa ya mwili, kiboko ana uwezo wa kukimbia kwa umbali wa kilometa 23km kwa saa ( 23km/saa)

11.Viboko hukaa kwenye maji kwa takribani masaa 16 kwa siku.

JE, UNAJUA KUWA…

1.Kiboko mnyama mwenye hasira sana na ndio mnyama mwenye historia ya kuuwa binaadamu wengi kuliko wanyama wengine wote?. Takwimu zinaonyesha kuwa viboko wanauwa watu 3,000 kwa mwaka.

2.Mdomo wa kiboko ni mkubwa kiasi kwamba anaweza kuufunua hadi kufikia upana wa futi 14?

3.Kiboko ni mnyma wa tatu kwa ukubwa katika wanyama waishio nchi kavu baada ya Tembo na Faru mweupe.

UZITO,UREFU NA KIMO

Uzito=hufikia uzito wa kilogramu 2,268 hadi 3,629 ( sawa na tani 2 – 3 au zaidi)

Urefu=hufikia urefu wa mita 2.8 – 4.2m na mkia huwa na urefu wa cm 35sm mpaka 50sm

Kimo=kiboko huenda juu hadi kufikia kimo cha mita 1.6m

MAZINGIRA

Viboko wanaishi au kupatikana maeneo ya Sahara Afrika na maeneo haya huwa yana maji ya kutosha na ndiyo maana wanyama hawa hutuimia masaa 16 wakiwa ndani ya maji kwa siku. Hutumia muda wa mchana kupumzika ndani ya maji na kutoka usiku kwa ajili ya kutafuta chakula.

Mawiza au mito wapatikanayo viboko huwa ni yale ambayo yamezungukwa na majani au vichaka ambavyo huwa pia hutumiwa na wanyama hawa kama chakula.

CHAKULA

Viboko ni wanyama jamii wanyama walao majani kama kina nyati,wanyama jamii ya swala na wengineo. Kama tulivoona hapo juu mnyama huyu hutafuta chakula usiku na ana uwezo wakutembea kilometa sita mpaka kumi akiwa anakula kwa nyakati za usiku. Kiboko ni mnyama ambae ana uwezo wa kula kilogramu 40kg – 60kg kwa mlo mmoja.

Kutokana na umbo la mdomo wake, kiboko ni mnyama alae majani ya chini kama walivyo nyati kwani midomo yao ina umbo la bapa. Kiboko pia anaweza kuhifadhi chakula na kukaa takribani wiki hadi tatu bila kula.

KUZALIANA

Dume mwenye nguvu ndio huwa mtawala na mwenye ruhusa yakupanda majike wote waliyopo chini ya himaya yake. Kabla ya hatua ya kupandana dume huyu anaopo miliki himaya hii huweka mipaka kwa kutumia kemikali azalishazo ndani mwili wake lakini pia hutumia mkia wake ulio bapa kusambaza kinyesi ili kuweka alama ya mipaka ya himaya yake na kuzuiya madume wengine wasije kuvamiaeneo hilo.

Viboko hupandana wakiwa ndani ya maji. Mara baada ya kupandana kiboko jike hukaa na mimba kwa muda wa miezi minane (8) na baada ya hapo kuzaa mtoto mmoja. Halika kadhila hata kuzaa pia kiboko huzalia ndani ya maji. Mtoto wa kiboko huzaliwa akiwa natakribaki kilogramu 25kg – 50k na anaweza kunyonya akiwa nchi kavu au kwenye maji.

Awapo kwenye maji mtoto wa kiboko huziba matundu ya pua na masikio pia ili kuepuka maji kuingia puani wakati wa kunyonya. Kiboko jike huzaa kila baada ya miaka miwili na mara tu baada ya kuzaa hujiunga na kundi la kina mama na watoto ambalo linakuwa chini ya utawala wa dume mmoja. Mtoto wa kiboko huwa chini ya uangalizi wa mama kwa takribani miezi 18 ( sawa na mwaka mmoja na nusu). Baada ya miaka mitano hadi saba ( 5-7) watoto wa viboko huwa wamekwisha kuwa wakubwa na huwa tayari wana uwezo wa kuzaliana.

Umri wa kiboko una kadiriwa kuwa miaka 35 – 40 wakati mwingine anaweza fikisha hata miaka 50.

UHIFADHI

Viboko ni wanyama ambao bado hawajawa hatarini katika kutoweka duniani na hii ni kutokana na tafiti zilizo fanywa na shirika la umoja wa mataifa linalo hisika na masuala uhifadhi maumbileasili ( International Union for Conservation of Nature – IUCN). Lakini shirika hili limedai kuwa hapo baadae wanyama hawa nao wanaweza kuingizwa kwenye kundi la wanyama ambao wapo hatarini kutoweka duniani na hii ni kutokana na kupungua kwa wanyama hawa.

Idadi ya viboko inaonekana kupungua kwa asilimia 7% mpaka 20% kwa miaka kumi iliyopita na inasemekana bado wanazidi kupungua na watazidi kupungua hadi zaidi ya asilimia 30%. Hivyo pale takwimu za sasa zitakapotoka tutazidi kujuzana uelekeo wa wanyama hawa.

Viboko wamesalia nchi 29 tu barani Afrika na kila nchi imeripoti kuwa idadi ya wanyama hawa imepungua zaidi ya nusu huku nchini Kongo wakiongoza kwa kupungua zaidi. Kwasasa idadi ya wanyama hawa inakadiriwa kuwa 125,000 – 148,000 dunia nzima.

CHANGAMOTO ZINAZO WAKUMBA VIBOKO

1.Changamoto kubwa inayo wakumba viboko ni ujangili hasa kutokana na mahitaji ya meno pamoja na nyama ya wanyama hawa. Mahitaji haya yamepelekea wanyama hawa kuwindwa sana na kufikia hali ya kuelekea kutoweka baadhi ya maeneo hapa barani Afrika na mfano mzuri ni nchini Kongo huku wakiwa wametoweka kabisa nchi kama Algeria, Misri na Mauritania.

2.Uharibifu wa mazingira utokanao na shughuli za binaadamu mfano kilimo cha umwagiliaji na uchafuaji wa vyanzo vya maji hali kadhalika ukataji miti na uchomaji wa vichaka kando kando ya mito na maziwa. Viboko ni wanyama ambao wanahitaji maji sana tena maji safi, hivyo shughuli za umwagiliaji zimekuwa zikipelekea sana upungufu wa maji kwenye mito nakusababisha mito hii hata kukauka na kuwafanya viboko kuhangaika sana. Pia matumizi ya mbolea za viwandani zimekuwa zikichafua sana maji nakusababisha matatizo kwa wanyama hawa. Mfano mzuri ni Mto Ruaha Mkuu jinsi unavyo pungua maji na hata kutoweka kwa baadhi ya matawi yake umefanya sifa nyingi za Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kupungua ambapo pia ni tegemezi kubwa sana kwa viboko.

3.Utekelezaji hafifu na ufuatiliaji duni wa sheria zinazo simamia masuala ya uhifdhi na hasa kutokana na msukumo mdogo wa serikali katika masuala ya uhifdhi wa wanyamapori.

NINI KIFANYIKE KUWANUSURU VIBOKO HAPA KWETU TANZANIA

1.Kuongeza idadi ya askari wa wanyamapori katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori ili kupunguza suala la ujangili, lakini pia askari wanao ajiriwa wawe wazalendo katika shughuli zao za ulinzi ili kutokomeza masuala ya ujangili katika maeneo hayo. Kwa wale viboko waliyo nje ya hifadhi za wanyamapori basi jitihada za dhati zifanyike katika kuwalinda.

2.Matumizi mazuri ya kilimo cha umwagiliaji na kupunguza ukataji wa miti kando kando ya mito na maziwa. Hii itasaidia kupunguza adha ya upungufu na uchafuzi wa maji ambayo yanaonekana kuwa tegemezi kubwa sana kwa viboko.

  1. Jamii katika uhifadhi wa wanyamapori na faida zake ili hizi jamii ziwe ni mabalozi wazuri katika kufichua makazi ya majangili na wahusika pia wa ujangili katika maeneo tengefu ya wanyamapori.

4.Serikali kupitia wizara husika hususani wizara ya maliasili na utalii ikishirikianana wizara ya mazingira kuanzisha sera au sheria madhubuti zitakazolenga kutokomeza uharibifu wa mazingira lakini pia kuhamasisha jamii kuthamini uwepo wa wanyama hawa hapa nchini.

HITIMISHO

Napenda kuwapongeza sana mamlaka zinazo simamia masuala ya uhifadhi wa wanyamapori hapa nchini mfano TANAPA kwa kazi kubwa sana wanayo ifanya wakati mwingine hata kutofautiana na baadhi ya jamii ili tu kunusuru wanyama hawa, pongezi sana kwenu TANAPA. Lakini pia bila kuzisahau mamlaka kama TAWA na matawi yake yote kwa shughuli pevu inayo endelea katika uhifadhi.

Pongezi sana kwa Muheshimiwa January Makamba kwa kazi aliyo ifanya ya kunusuru uharibifu wa vyanzo vya maji vya mto mkuu Ruaha kule Songwe kwani mto huu ni moja kati ya mahitaji makubwa sana ya wanyama hawa voboko katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na angalau leo matunda ya upambanaji kutokana na uharibifu wa mto huu tuna yaona.

Kilio changu kikubwa sana kitabaki upande wa serikali pia kwani serikali inasimamia sana maeneo machache na kusahau suala la uhifadhi wa wanyamapori pamoja na mazingira yao. Sekta hii ya wanyamapori chini ya wizara ya maliasili na utalii inaliingizia Taifa fedha nyingi sana za kigeni kwani wageni wanaokuja hapa nchini kwa dhumuni la kutembelea hifadhi za Taifa na maeneo mengine ya uhifadhi wa wanyamapori ni wengi sana.

Hata ukiangalia pato la Taifa mwaka jana utaona ni dhahiri kwamba sekta ya uhifadhi au hifadhi za Taifa zimechangia pesa nyingi sana kwenye pato la nchi.

Ahsante sana!

Kwa mengi zaidi kuhusu wanyamapori na ushauri juu ya makala au darasa hili huru wasiliana na mwandishi wa makala hii kwa namba zifuatazo;

Sadick Omary

SIMU= 0714116963 / 0765057969 / 0785813286

Email= swideeq.so@gmail.com

”I’M THE METALLIC LEGEND”