Habari za siku kidogo ndugu wasomaji wa makala za wanyamapori. Leo ni siku nyingine tena tunakutana katika darasa letu hili huru ili kuwajua wanyamapori na mazingira wanayoishi hali kadhalika kujua uelekeo wa wanyama hawa katika mazingira yao asilia. Kuna mambo mengi sana yamejificha hususani kwa wanyama hawa ambao wanaishi misituni na hivyo nimatumaini yangu utahihataji kujua mengi kuhusu viumbe hawa wa porini.
Basi kama ilivo kawaida leo tutaingia darasani tena kumchambua mnyama ambae ni maarufu kwa watu japo hujulikana kwa jina tu bila kujua sifa zake kwa undani zaidi. Basi kama ilivyo siku zote darasa letu litakufanya ujue mengi zaidi juu ya wanyama hawa na kujifunza mambo mengi sana na hatimae uweze kuwa balozi mzuri katika kuhamasisha suala zima la uhifadhi wa wanyamapori hapa nchini.
Leo mezani tutamuweka mnyama ajulikanae kwa jina la “PONGO” ambae kwa lugha ya kigeni anaitwa “BUSHBUCK”
Na sasa twende moja kwa moja kumjua mnyama pongo kwa undani zaidi ili hata siku ukikutana nae porini uweze kumtambua kupitia maelezo ya makala hii.
SIFA NA TABIA ZA PONGO
Pongo ni wanyama wenye rangi ya kipekee na inayo vutia sana. Rangi ya wanyama hawa huwa inaonekana kutokana na mazingira anayoishi pongo na mara nyingi huwa na rangi ya wekundi unao shabihiyana na kahawia au uzurungi inayo elekea kuwa kama nyeusi. Japo majike huwa wana rangi ya kahawia inayo ng’aa kidogo tofauti a madume.
Pongo wengi ukiwachunguza vizuri huwa wana alama ya mistari kwa upande wa ubavuni pamoja na madoa madoaya rangi nyeupe ambayo huonekana maeneo ya miguuni, masikioni, shingoni ya sehemu ya mkiani.
Madoa madoa haya yenye rangi nyeupe huwa yanasaidia sana kwa wanyama hawa kuweza kutambuana. Kwa ufupi ni kwamba madoa madoa haya huwa yapo tofauti kwa kila pongo kama vile ilivyo mistari ya pundamilia. Wakati mwingine madoa haya hutumika kama ishara ya tahadhari wakati wanapohisi kuna hatari.
Ni dume pekee tu ndo huwa na pembe katika wanyama hawa na pembe zake huwa ndefu na mikunjo mikunjo ambazo hufikia hadi urefu wa sentimeta 55sm. Majike huwa hawana pembe kabisa.
Pongo ni miongoni mwa wanyama ambao huishi kwa kujitenga sana. Huwa hawapendi kabisa kuishi kwa makundi na ni marachache sana hata kukuta kundi la kina mama wakiwa pamoja. Hata mama anapokuwa na mtoto ambae tayari kashachangamka huwa ni vigumu sana kumuona akiongozana na mwanae na kwa bahati ikitokea hivho basi ukaribu huo hudumu kwa masaa au siku chache sana.
Pongo ni wanyama ambao wanaishi kwenye eneo dogo sana na kuna wakati inatokea himaya kuingiliana lakini huwezi wakuta wakiwa pamoja sehemu moja hata kama tayari mmoja kashaingia kwenye eneo la mwingine. Pongo hasa wakubwa hupenda sana kujitenga na kuishi wakiwa peke yao.
Pongo ni baadhi ya wanyama jamii ya swala wenye uwezo mdogo sana wa kukimbia. Japo wana uwezo mdogo wa kukimbia lakini wanyama hawa wana uwezo mkubwa sana wa kuogelea na wa kuruka. Pongo wana uwezo wa kuruka uzio wenye urefu wa futi sita.
Pongo ni wanyama hatari na wenye hasira sana miongini mwa swala. Pongo aliye jeruhiwa au kutishiwa zaidi huwa anaamua kusimama na kisha kumfukuza adui yake bila uoga kabisa. Imewahi kuripotiwa kuwa pongo amewahi kuwafukuza wawindaji baada ya kumjeruhi na mishale katika maeneo ya uwindaji.
Pongo ni wanyama ambao hufanya shughuli zao hasa utafutaji wa chakula majira ya alfajiri na baadhi ya masaa machache ya usiku. Hii imefanya wanyama hawa kutaka kuwekwa kuwa ni miongoni mwa wanyama wenye uwezo wa kuona zaidi wakati wa usiku kwasababu mazingira wanayoishi huwa hawapendi kusumbuliwa sana hasa kipindi cha mchana wanapokuwa wamepumzika.
Wanapo shituliwa ghafla huwa na maamuzi tofauti tofauti ili kuepukana na hatari. Kama yupo kwenye msitu au vichaka vikubwa basi pongo hutulia kimya na kubakia katika eneo hilo bila hata kujongea. Rangi za miili yao huwa ni msada mkubwa sana kwani hufanana na mazingira
wanayoishi nakufanya kuwa ni vigumu kuonekana. Kama yupo karubu ya shimo basi huingia ndani ya shimo hilo na kulala akiwa amenyooka.
KIMO, UREFU NA UZITO WA PONGO
Kimo= Pongo hufikia kimo cha sentimita 80 – 90sm
Urefu= Pongo hufika urefu wa sentimita 110 – 150sm
Uzito= Uzito wa wanyama hawa huwa ni kati ya kilogramu 40 – 80kg
MAZINGIRA
Pongo ni wanyama ambao wanaishi mazingira yenye misitu. Wana uwezo wa kuishi katika misitu aina mbali mbali kama misitu ya mvua, misitu ya milimani, misitu ya savanna na maeneo yenye ardhi ynye miti miti.
CHAKULA
Hawa ni miongoni mwa wanyama walao majani japo pongo hawapendelei sana majani. Wanyama hawa wanapendelea sana kula vitu kama matumba, mitishamba na mara chache sana matunda.
Kutokana na maumbile ya midomo ya pongo, wanyma hawa huwa wanakula vyakula ambavyo hupatikana kwa juu yam mea kama walivyo mbuzi.
KUZALIANA
Pongo huzaa majira yoyote ya mwaka japo kwa pongo ambao hupatikana sana maeneo ya ukame huzaliana kipindi cha mvua. Pongo hubeba mimba kwa muda wa siku takribani 180, hii humfanya mnyama huyu kuwa na uwezo wa kuzaa mtoto zaidi ya mmoja kwa mwaka. Yani ana uwezo wa kuzaa mara 2 kwa mwaka mmoja.
Huzaa mtoto mmoja na mtoto huwa na uzito wa kilogramu 4kg. Mara tu baada ya kuzaa mama humsafisha mtoto kisha anakula fuko la uzazi. Mtoto huwa hana uwezo wa kumfuata mama na hivyo hufichwa katika sehemu sala hatimae baadaa ya miezi 4 ndo huwa na uwezo wa kuongozana na mama kwenda kula. Ndama anapokuwa mafichoni mama hurudi mara kwa mara kwa ajili ya kumnyonyesha na wakati huu anaporudi kumnyonyesha ndama basi mama hulazimika kula kinyesi cha mtoto ili maadui wasiweze kuhisi harufu na kuja kumla au kumjeruhi mtoto. Mama na mtoto huwa wanacheza mchezo wa kukimbia mfano wakutengeneza duara huku wakikimbizana kila mmoja.
Pongo huanza kuzaa pale afikishapo umri wa mwaka mmoja. Japo pembe za dume huwa bado zinaendelea kukuwa na hufikia urefu wa kima cha juu pale afikishapo miaka mitatu. Maisha ya pongo huwa ni miaka 12 – 15 awpo katika mazingira asili japokama anafugwa huweza kuzidi umri huo.
UHIFADHI
Jambo la kushukuru ni kwamba wanyama hawa bado wanapatikana kwa wingi katika maeneo tengefu ya uhifadhi wa wanyamapori na hii ni kutokana na taarifa ya shirika la umoja wa mataifa linalo shughulika na uhifadhi wa maumbile asili duniani (IUCN- International Union for Conservation of Nature). Kuna tafiti zilifanyika mwaka 1999 zilionesha kwamba idadi ya wanyama hawa katika maeneo ya uhifadhi ni 1,340,000 kitu ambacho kina ridhisha na hadi kufikia sasa bado wanasema idadi ya wanyama hawa ipo vizuri.
Japo kuna baadhi ya maeneo wanyama hawa wanapungua kwa kasi kubwa sana na wameanza kutoweka kabisa kwenye maeneo mbalimbali.
MAADUI NA TISHIO KWA PONGO
Napo zungumzia maaadui hapa namaanisha maadu asilia kwa wanyama hawa ambao ni lazima wawepo ili kuweza kufanya usawa wa kiikolojia kwa viumbe wote ambao wanaishi katika eneo hilo. Adui mkuu wa pongo ni chui, japo kuna maadu mbwa mwitu, mamba huwa wana washambulia pongo na mara chache sana simba.
Tukija kwa upande wa tishio hapa tunaangalia vitu ambavyo havihusiani kabia na asilia au ikolojia kwa wanyama hawa ambapo tutaona matishio kama haya;
Uharibifu wa mazingira/makazi ya wanyama hawa na kuongezeka kwa ukame. Haya mambo hupelekea sana kupungua kwa mahitaji ya kiikolojia kwa pongo na hivyo kusababisha wanyama hawa kutoweka baadhi ya maeneo. Kama tulivoona hapo juu kuwa wanyama hawa wanapendelea maeneo ya msituni sasa kama mazingira yam situ yanaharibiwa basi huwa ni hatari sana kwa wanyama hawa.
Shughuli za kibinaadamu zimekuwa zikiharibu sana mazingira nakufanya uharibifu wa kiiklojia kwa pongo. Mfano ni ukataji miti hovyo na holela hali kadhalika upanuzi wa maeneo ya kuishi umesababisha misitu mingi sana kuharibiwa na hivyo kuwa na athari kubwa sana kwa wanyama hawa.
Janga linguine kubwa ni ujangili ambao umeshamiri sana kwa wanyamapori kitu ambacho kinasababisha shughuli ya uhifadhi wa wanyamapori kuwa mgumu sana. Mahitaji ya malighafi za wanyamapori yamekuwa makubwa sana hapa nchini na hata nchi za nje, hii imepelekea kuku asana kwa biashara haramu ya wanyamapori na hatimae kuwindwa kwa kasi kubwa sana.
TUJITAHIDI KUFANYA HAYA ILI KUPUNGUZA CHANGAMOTO KWA PONGO
Kupambana na uharibifu wa mazingira hasa katika maeneo tengefu ya uhifadhi wa wanyamapori ili kusaidia upatikanaji wa mahitaji ya kiikolojia kwa wanyama hawa ambao wanahitaji utulivu tena sana. Shughuli za upanuzi wa makazi na uvamizi wa maeneo ya misitu zifuatiliwe kwa ukaribu zaidi ili kunusuru wayama hawa ambao wana mchango mkubwa sana kwenye pato la taifa.
Serikali kupitia mamlaka mbalimbali ambazo zina husika na uhifadhi wa wanyamapori, wajitahidi kuongeza idadi ya askari wa wanyamapori wenye uzoefu na moyo wa kujitolea ili kusaidia kupunguza suala la ujangili kwa wanyamapori kwani limekuwa hatari sana.
Ushirikishwaji wa jamii katika uhifadhi kwani kwa kuzishikisha jamii itasaidia sana kupunguza tatizo la ujangili. Wananchi watakuwa ni mabalozi wazuri sana katika kuwafichua majangili kwani ukweli ni kwamba majangili tunaishiao katika nyumba zetu. Sasa kama jamii itakuwa inanufaika moja kwa moja kutokana na suala la uhifadhi basi hawatokuwa tayari kuona watu wachache wanajivunia mali kwa ubinafsi.
Kuutangaza utalii wa ndani kwani hili pia litasaidia watu kuthamini kile tulichonacho kabla yakuwasubiria wageni kutoka nje ambao kwa hakika huwa wana thamini sana uwepo wa wanyamapori kuliko hata sisi wahusika wakuu. Utamaduni wa kutembelea vivutio au hifadhi za wanyamapori humfanya mtu kujua thamani ya uwepo wa wanyama hawa na hivyo kuwa muhamasishaji mzuri kwa jamii inayo mzunguka.
HITIMISHO
Napenda kuwapongeza TANAPA kwa kazi kubwa sana wanayofanya na hasa katika kupambana na ujangili hali kadhalika uhamasishaji utalii wa ndani bilakusahau ushirikishaji jamii katika uhifadhi. Mamlaka nyingine kama TAWA , TAWIRI na NCAA pia sijawasahau kwani mna mchango mkubwa sana katikauhifadhi wa wanyamapori hapa nchini.
Kunamashirika yasiyo ya kiserikali ( NGOs) mengi sana mfano Serengeti Presevation Foundation-SPF, Wildlife Conservation Society-WCS na EnvironmentalConservation for Wildlife and Community Enterprise-ECOWICE yana jitahidi sana kuendeleza uhifadhi wa wanyamapori hapa nchini. Wito wangu ni kwa serikali kuyapa ruzuku mashirika haya ili kuweza kutimiza ndoto zao katika uhifadhi kwani mashirika haya yana uhaba sana wa fedha za kujiendesha na kusababusha kutumia wahisani mbalimballi kwa michango ya uendeshaji wa shughuli za kihifadhi.
Kwa mfumo wa sasa wa serikali yetu ambayo insimamia uadiliu na utendaji kazi bora basi ndugu waziri wa maliasili na utalii Dr. Hamisi Kingwangalla tunaomba usaidie uwezeshwaji wa mashirika haya ili angalau kuendeleza chachu ya uhifadhi wa wanyamapori pamoja na mazingira kwa ujumla kwani faida yake kwa sasa hatuwezi kuiona lakini baada ya myaka 5 mbele ndo tutakuja kuona umuhimu wa kuyadhamini mashirika haya ya uhifadhi wa wanyamapori.
Pia siwezi kuwasahau watu binafsi ambao kwakweli wamekuwa na mchango mkubwa sana katikakuhamasisha suala zima la uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yao kwa ujumla lakini pia hata uchambuzi wa sheria mbali mbali za wanyamapori angalau tu jamii iweze kutambua nini kinaendelea katika sekta ya uhifadhi au malasili kwa ujumla. Shukrani sana ziende kwa ndugu yangu Hillary Mrosso na Mr. Eliyah Tarimo (Bushman) kwa kazi kubwa sana wanayo ifanya ya kuhamasisha uhifadhi wa wanyamapori kupitia mitandao ya kijamii.
Ahsanteni sana.
Kwa mengi zaidi kuhusu makala hizi na ushauri wasiliana na mwandishi wa makala hii kupitia
Sadick Omary
Simu= 0714 116963 / 0765 057969 / 0785 813286
Email= swideeq.so@gmail.com
Au tembelea= www.mtaalamu.net/wildlifetanzania
…..”I’M THE METALLIC LEGEND”….