Habari msomaji wa makala za wildlife Tanzania, karibu kwenye makala yetu ya leo  ambayo nimeiandaa kukusaidia kufahamu kwa kina dhamira ya nchi ya Tanzania ya tangu mwanzo katika uhifadhi wa wanyamapori. Mara baada ya nchi yetu kupata uhuru kutoka kwa wakoloni mwasisi wa Taifa la Tanzania, hayati Baba wa Taifa Mwalimu J.K. Nyerere alitamka maneno maarufu sana kakatika moja ya mikutano yake. Maneno haya yamekuwa msaada sana kwenye kujua kulinda na kuhifadha wanyamapori na maliasili za Tanzania. Maneno haya yanatumika sana sehemu mbali mbali za uhifadhi wa wanyamapori kama mwongozo na hamasa kuhusu uhifadhi na thamani kubwa iliyopo tunapochukua hatua za kuhifadhi wanyamapori na na maliasili nyingine. Maneno haya yana jina maarufu kama “AZIMIO LA ARUSHA, AU ARUSHA MANIFESTO”.

Maazimio haya yaliyosemwa tangu mwaka 1961, yamekuwa chachu na hamasa kwenye uhifadhi wa wanyamapori, ni maneno ya hekima ya hali ya juu sana kuwahi kutamkwa katika sekta yote ya wanyamapori na maliasili kwa ujumla. Kwa kiasi kikubwa maneno haya yalikuwa katika lugha ya kingereza, ambapo watu wengi wasio na uelewa wa lugha hiyo hawawezi kujua kilichodhamiriwa kwenye maneno hayo. Hivyo nimeyaweka kwenye lugha ya Kiswahili ili kila mtanzania na watu wengine wanaofahamu lugha ya Kiswahili wayaelewe vizuri, maneno hayo ni haya hapa chini.

“Uhai   wa   wanyamapori   ni   jambo   linalotuhusu   sana sote   katika   Afrika.   Viumbe   hawa   wa   porini, wakiwa   katika mapori   wanamoishi,   sio   muhimu  tu  kwa  ajili   ya  kuajabiwa   na kuvutia   lakini   pia   ni   sehemu   ya   maliasili   yetu   na   pia   ndio mustakabali wa maisha yetu ya baadaye.

Kwa   kukubali   dhamana   ya   wanyamapori   wetu tunatamka   kwa   dhati   kwamba   tutafanya   kila   tuwezalo kuhakikisha   kwamba   wajukuu   wa   watoto   wetu   wataweza kufurahia urithi huu mkubwa na wa thamani adimu.

       Uhifadhi   wa   wanyaampori     na   maeneo   yote   yenye mapori   huhitajia   maarifa   ya  kitaalamu,   wafanyakazi   waliopata mafunzo   maalumu,   na   fedha;   na   hivyo   tunaomba   mataifa mengine   yashirikiane   nasi   katika   kazi   hii   muhimu,   ambayo kufanikiwa au kutofanikiwa kwake hakuathiri tu Bara la Afrika bali ulimwengu mzima kwa ujumla”.

(Mwalimu J.K. Nyerere 1961)

Hili ndio Azimio la Arusha, kama ulivyosoma hekima ya hali ya juu sana katika uhifadhi. Ni Azimio hili la Arusha ambalo kabla ya kuwepo kwa sera ya wanyamapori sehemu hii ndio ilitumika kama muongozo kwenye uhifadhi wa wanyamapori.

Mwalimu aliona mbali sana, na maneno yake aliyoyatamka yanahitaji kufanyiwa kazi, sii na watanzania pekee bali na dunina nzima, tunahitaji kila juhudi, fursa na utalaamu katika kuhakikisha uhai wa wanyamapori unaendelea kuwepo hapa duniani.

Kwa miongo michache iliyopita tumeshuhudia uharibifu mkubwa sana kwenye maeneo ya wanyamapori, tumeshuhudia maelfu ya viumbe hai yakitoweka  na kuuwawa kwa sababu ambazo nyingi tuna uwezo wa kuzizuia. Tumeshuhudia biashara haramu ya wanyama na bidhaa za wanyamapori. Tumeshuhudia maelfu ya tembo yakiuwawa katika bara la Afrika na sehemu nyingine duniani.

Kwa jinsi ujangili wa wanyamapori kama tembo ulivyotapakaa duniani kote, juhudi za kupambana na ujangili sio tena wa nchi moja au wa Tanzania pekee bali ni jukumu la dunia nzima, kama alivyosema mwalimu, tunahitaji jitihada za kila moja wetu hapa duniani ili kuwalinda na kuwahifadhi wanyamapori wetu, tunahitaji nguvu ya kila taifa, tunahitaji wataalamu, na fedha kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori kwenye maeneo yetu. Tunahitaji kufanya kila tunaloweza kuwahifadhi wanyamapori kwa manufaa ya sasa naya  baadaye.

Naamini kwa maneno ya hekima na busara aliyoyasema hayati Mwalimu J.K. Nyerere utakuwa umepata dhamra na maono makubwa aliyokuwa nayo kwenye uhifadhi wa wanyamapori na maliasili kwa ujumla.

Kama una maswali, maoni au ushari kuhusu makala hizi, usisite kuwasiliana nami, karibu sana tuwalinde na kuwahifadhi wanyamapori wetu.

Ahsante sana!

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania