More

    Maendeleo Yoyote Ya Kweli Yanatakiwa Yasaidie Maisha Ya Viumbe Hai Wote Yaendelee Kuwepo

    “Progress is measured by the speed at which we destroy the conditions that sustain life”.

                                            George Manbiot

    Maisha tuliyo nayo hayapo tu kwasababu yapo, maisha tuliyonayo yapo kwa sababu ya uwepo wa vitu vingine. Uwepo wa vitu vingine vingi ndio unaopelekea maisha yaendelee kuwepo hapa duniani, uharibifu wa vitu vinvyoshikilia maisha na kufanya maisha yaendelee kuwepo imetokana na ujinga wetu wenyewe kwa kiasi kikubwa. Ujinga wa kutojua kitu kipo kwa sababu gani umepelekea uharibifu mkubwa sana kwenye vitu vingi ikianzia kwetu sisi wenyewe binadamu mpaka kwa wanyama mimea. Ujinga wetu sisi wanadamu umeleta uharibifu mkubwa sana kwenye maisha yetu na mazingira yetu.

    Wakati naisoma nukuu ya George Manbiot, nilifikiria sana  na kuona ni ukweli mtupu kwenye nukuu hii. Hivyo ngoja tushirikishane haya niliyojifunza hapa ili wote tuelewe sentensi hii ilivyo na ujumbe mkubwa na mzito sana. Kwa kweli maisha yetu kama wanadamu yametawaliwa sana na hisia na kwa kiasi kikibwa ushawishi wa watu wengine walofanikiwa na kuwa na vitu vyote walivyokuwa wanavihitaji kwenye maisha yao. Mafanikio na maendeleo ni jambo linalotafutwa sana kwa bidi na watu, na kama jambo hili lisipo dhibitiwa vizuri litasababisha watu kutafuta mafanikio kwa njia ambazo sio salama kwao wenyewe na pia sio salama kwa viumbe hai wengine na sio salama kwa mazingira.

    Tumekuwa kwenye mashindano ya kutaka kuendelea kiuchumi, kwa na viwanda, na teknologia zinazoenda na wakati. Tunaangalia majirani zetu na nchi nyingine zilivyopiga hatua kwenye uchumi na kuwa mbali kwenye teknologia na kutamani kufanya kama wao bila kuangalia matokeo ya muda mrefu ya maendeleo hayo. Nchi zilizofanikiwa sana kuwa na maendeleo na kuwa na teknologia za kisasa kwa kiasi kikubwa waliharibu  mazingira yao ya asili ya wanyama na mimea. Waliharibu mazingira ili wawe na maendeleo, waliharibu misitu na makazi ya wanyamapori ili wawe na maendeleo. Sasa ukiangalia kwa jicho la mbali hayo sio maendeleo mazuri na ya kudumu kwasababu wanaharibu vile vitu vinavyofanya maisha hapa duniani yaende kwa kutimiza matakwa ya muda mfupi.

    Sikatai kupiga hatua kiuchumi na kuwa na viwanda na teknolojia nzuri za kisasa, bali tunatakiwa kufanya mambo kwa busara na hekema sana ili mafanikio na maendeleo yoyote tunayoyatafuta yawe rafiki kwa viumbe na mazingira kwa ujumla. Hatutakiwi kukosa akili kwenye mambo ya namna hii, tunatakiwa kuona mbali zaidi. Hatutakiwi kufyeka misitu ya asili na kuchoma moto hovyo au kuruhusu majengo na miundombinu kwenye makazi na mazalia ya viumbe hali. Tunatakiwa kujifunza kwa wenzetu ambao wanahaha kurudisha mazingira waliyoyaharibu, tena wanayarudisha kwa gharama kubwa sana ambayo kama wangelijua mapema gharama zake wasingeruhusu kuharibu mazingira hayo.

    Kama tunataka kufanya jambo la maendeleo lenye kuleta madhara kwa mazingira, hatupaswi kuwa na haraka kwenye kufanya jambo hili, tunatakiwa kufanyike uchunguzi wa kutosha na utafiti, wa kimazingira wa muda mfupi na muda mrefu, wataalamu na watu wenye nia nzuri wanatakiwa kufanya kazi hii kwa weledi ili waweze kuishauri serikali kuchukua hatua stahiki. Hata kama mradi na kitu ambacho kinataka kufanyika hapo kitakuwa na fedha nyingi kiasi gani, kama kikipimwa na watalaamu na kuonekana kuwa hakina tija na maslahi mapana kwa jamii nan chi kwa ujumla jambo hilo lisitekelezwe, liachwe na waendelee na mambo mengine.

    Mwisho wa siku watoto wetu, wajukuu wetu na vitukuu wetu wataikuta dunia nan chi tuloishi ikiwa na ubora wa hali ya juu, mazingira yote muhimu yametunzwa na kuhifadhiwa vizuri kabisa. Tuiachie dunia urithi bora kabisa kuliko tulivyoikuta, hatutakiwi kuwaachia watoto na vizazi vijavyo dunia iliyochoka, mazingira yameharibika,  na hakuna matumaini kwenye maisha kwa sababu wanaona tumewaachia jangwa badala ya nchi nzuri ya kijani, misitu minene, yenye maua na ndege na wanyama wakifurahia mazingira yao ya asili. Ifanya dunia kuwa edeni sehemu nzuri na salama kuishi.

    Ahsante sana

     Hillary Mrosso

    Wildlife Conservationist

    +255 683 862 481/+255 742 092 569

    hillarymrosso@rocketmail.com

    www.mtaalamu.net/wildlifetanzania

     

     

     

     

    Latest articles

    Related articles

    Leave a reply

    Please enter your comment!
    Please enter your name here