Habari msomaji wa makala za wildlife Tanzania, karibu tena kwenye mfululizo wa makala za uchambuzi wa sheria ya wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009. Baada ya kujifunza na kuchambua sehemu nne za sheria hii, leo tunaingia sehemu ya Tano, ya sheria hii muhimu. Lengo letu kubwa ni kufanya yote ili watanzania waelewe kwa urahisi mambo yaliyopo kwenye sheria hii. Hata wale wenye ndoto za kufanya kazi au kusomea wanyamapori na maliasili basi wanaweza kupata msingi mzuri wa sheria kupitia blog hii.

Kichwa cha sehemu ya sheria hii ni Wildlife Management Areas, WMAs au kwa Kiswahili wanaita maeneo ya hifadhi ya jamii, au maeneo ya asasi za jamii, au maeneo ya usimamizi wa wanyamapori. Lakini yote katika yote tutajifunza hapa sheria inayatambuaje maeneo haya muhimu kwa hifadhi ya wanyamapori. Haya ni maeneo muhimu sana kwa  kuwa ndio maeneo ambayo yanasimamiwa na jamii au vijiji moja kwa moja na pia mapato yatokanayo na uwepo wa asasi hizi huenda moja kwa moja kwa jamii na kufanyia shughuli za maendeleo. Ngoja tuende kwenye sheria tuone inavyoyamulika maeneo haya, kuanzia kifungu cha 31 cha sheria hii ya wanayamapori kinaelezea mambo yote ya kisheria kuhusu maeneo haya ya hifadhi ya jamii.

UANZISHWAJI NA USIMAMIZI WA MAENEO YA HIFADHI YA JAMII (WMA)

31.-(1) Maeneo ya hifadhi ya jamii yameanzishwa kwa kusudi la kuhamasisha jamii kwenye masuala ya uhifadhi wa wanyamapori kwenye maeneo ya-

(a) nje ya maeneo muhimu ya hifadhi ya wanyamapori;

(b) yanayotumiwa na wanajamii

(c) ndani ya ardhi ya Kijiji

(2) faida zinazopatikana kutokana na uwepo wa maeneo haya ya hifadhi ya jamii zinatakiwa ziendane na maelekezo yanayotolewa na serikali mara kwa mara na inatakiwa iwe inaendana na mpango wa mgawanyo sawa wa faida na hasara ikiwa na lengo la kuhamasisha uhifadhi wa wanyamapori, kuinua maendeleo kiuchumi na kupunguza umasikini.

(3) Maeneo ya hifadhi ya wanyamapori yataanzishwa na kusimamiwa kulingana na kanuni na mapendekezo yaliyofanywa na Waziri na kuchapishwa kwenye Gazeti la serikali.

(4) Waziri atashauriana na Waziri anayehusika na masuala ya mamalaka ya  serikali za mitaa kuandaa mpango wa sheria ndogo ndogo na kanuni ambazo zitaendana na mabadiliko muhimu ya mamlaka za vijiji na zitatumika kwa maeneo ya hifadhi ya wanyamapori.

(5) Waziri atahakikisha wakati wa kutengeneza kanuni kwa mujibu wa sehemu hii, ameshauriana na jamii na kutoa taarifa jinsi jamii itapata faida kutokana na uwepo wa asasi hii ya hifadhi ya maeneo wanyamapori.

(6) Shughuli ambazo zitafanyika kwenye maeneo haya ya hifadhi ya jamii zinatakiwa ziendane na sheria na kanuni za  Sheria za Misitu, Sheria ya Uhifadhi wa nyuki, Sheria ya Uvuvi,  Sheria ya Usimamizi wa Mazingira na sheria nyingine zinazoendana nazo.

(7) Jumuiya yoyote yenye mamlaka ya kusimamia maeneo ya hifadhi ya jamii kulingana na kifungu cha 32(1), wana haki ya kushauriana na kusaini makubaliano na wawekezaji muhimu, kwa kuhakikisha kwamba kuna wawakilishi wa Mkurugenzi na Baraza la Wilaya wanatakiwa kuwepo katika mchakato wa mashauriano na kusaini makubaliano hayo. Hapa inaanisha kwamba endapo kutatokea mwekezaji kwenye maeneo ya Asasi hizi za hifadhi ya jamii, wajumbe na wawakilishi wanatakiwa kuwepo kwenye mchakato mzima wa kuhakikisha wote wanakubaliana na uwekezaji unaotaka kufanyika kwenye asasi husika, anatakiwa kuwepo mwakilishi wa Mkurugenzi wa wanyamapori na Baraza la Wilaya.

(8) Mambo yanayohusu  vigezo vya ugawaji, aina, kiasi, na idadi ya ubora wa vitalu vya uwindaji ndani ya Maeneo ya Hifadhi Jamii yanatakiwa kuelezwa kwenye kanuni. Kuna kanuni nzuri  zilizotoka mwaka 2012 ambazo zineleza vizuri kuhusu ugawaji wa vitalu na vigezo vyote vya ugawaji wa vitalu kwenye Maeneo haya ya Hifadhi ya Jamii.

32.-  Waziri baada ya kupokea maombi yaliyofanywa na Baraza la Kijiji na maoni ya Mkurugenzi na pia kwa kutoa taarifa kwenye Gazeti la serikali, anaweza kutangaza eneo la ardhi ya Kijiji husika lililotengwa kwa ajili  hifadhi ya jamii kuwa Eneo la Usimamizi wa Wanyamapori (Wildlife Management Areas, WMA).

33.- (1) Kila Wilaya ambayo ina eneo lililotangazwa kuwa ni Eneo la Usimamizi wa Wanyamapori au Eneo la Hifadhi ya Jamii wanatakiwa kuanzisha Bodi ya Ushauri wa Maliasili ya Wilaya kwa kusudi la kushauri jumuiya zilizopewa mamlaka  na mamlaka za serikali za vijiji katika mambo yanayohusu uratibu, uongozi na usimamizi wa Maeneo haya ya Hifadhi ya Jamii.

(2) Ushauri utakaotolewa kulingana na kifungu kidogo cha (1) unatakiwa uwe sawa na uendane na Mpango wa Jumla wa Usimamizi wa Eneo (General Management Plan) husika la Hifadhi ya Wanyamapori.

Hivyo ushauri ambao unatolewa na bodi unatakiwa kuwa wa kitaalamu zaidi ili uwe na nia ya kuendeleza uhifadhi wa wanyamapori kwenye asasi hizi na pia ushauri huo ulenge kwenye dhima kuu ya uanzishwaji wa maeneo haya ya hifadhi ya jamii ambayo ni kuchochea maendeleo ya kuichumi na kupunguza umasikini kwenye maeneo haya ya jamii. Hivyo kwa vyovyote vile bodi hii inatakiwa kufanya kazi kwa weledi mkubwa sana, ili jamii hizi zinufaike na uwepo wa wanyamapori na maliasili zilizopo kwenye maeneo ya vijiji vyao.

Naamini kufikia hapa umepata mwanga mzuri kuhusu uchambuzi wa sehemu hii ya Tano ya sheria ya hifadhi ya wanyamapori. Sehemu hii ya sheria imeelezea vizuri maeneo haya ya hifadhi ya jamii. Pia ikumbukwe kuwa Tanzania ina maeneo mengi sana ya hifadhi ya jamii. Ingawa maeneo haya yapo mengi ni maeneo machache yanayofanya vizuri mengi ya hayo yanashindwa kujiendesha na kuleta faida inayotegemewa kwa jamii. Hivyo maeneo haya yanakubwa na changamoto kubwa sana kwenye kutengeneza faida, masuala ya usimamizi na utawala, pia uwekezaji kwenye maeneo haya bado hauridhishi kwanai kuna sehemu nyingine ya maeneo haya hakuna uwekezaji wowote unaotengeneza fedha au faida kwa jamii hizi. Hivyo ni juhudi za makusudi zinahitajika kunusuru maeneo haya muhimu.

Asante sana kwa kusoama makala hii, tukutane kesho hapa kwa makala ijayo. Endelea kujifunza na kupata maarifa muhimu yatakayokusaidia katika kufanya maamuzi mbali mbali na pia katika uongozi endapo unafanya kazi kweneye asasi hizi, na pia endapo utafuatilia na kusoma makala hizi utagundua haya ni maeneo yaliyotupu na kama unataka kufanya uwekezaji kwenye maeneo haya fursa ni kubwa na ipo wazi jipange kwani hata sheria inaruhusu kufanya hivyo.

Ahsante sana!

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 248 681/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania