Katika harakati za kuhifadhi wanyamapori na rasilimali nyingine, ili ziwe na faida kwa kizazi cha sasa na kizazi cha baadaye tunatakiwa kuwa na jamii yenye uelewa na azima ya kufanya hivyo kwa weledi na kwa uwazi mkubwa. Tunatakiwa kuhakikisha namna ambavyo jamii ya sasa inanufaika na usimamizi au uhifadhi wa maliasili hizo utakavyoweza kuwa ni shauku ya jamii ya sasa kunufaisha jamii nyingine kupitia mipango na namna ambavyo jamii husika inapata faida kutokana na uwepo wa rasilimali hizi kwenye maeneo yao.
Mfumo wa kunufaisha jamii kutokana na uwepo wa maliasili umekuwa ukiimbwa na kuandikwa vizuri sana kwenye makarataisi, na ripoti nyingi za sekta hii ya maliasili, zaidi imetamkwa kwenye sera ya uhifadhi wa wanyamapori kuwa jamii inatakiwa kunufaika na uwepo wa wanyamapori na rasilimali nyingine zinazopatikana kwenye maeneo yao.
Jambo hili ndio likapelekea kuanzishwa kwa hifadhi za jamii, yani WMAs, maeneo ambayo ni sehemu ya ardhi ya vijiji ambavyo vimeridhia kutoa ardhi yao kwa ajili ya kuunda jumuiya moja ya uhifadhi wa wanyamapori wanao patikana kwenye maeneo ya ardhi yao. Ni kweli kabisa uanzishaji wa maeneo haya ya jumuiya yalianzishwa Tanzania nzima, hivyo hadi sasa tuna maeneo yasiyopungua 38 ambayo jumuiya au asasi za kijamii zimeyatoa ili yawe ni sehemu ya hifadhi ya maliasili mbali mbali zilizomo kwenye maeneo hayo, rasilimali hizi ni wanyamapori, misitu, maji, na rasilimali nyingine muhimu ambazo zimo kwenye maeneo hayo.
Baada ya kuanzishwa kwa maeneo haya, ilibidi kuweka mfumo ambao unajumuisha uongozi, usimamizi na hata namna ambavyo mapato yatokanayo na rasilimali hizi yatakavyo kusanywa na kufika sehemu husika. Usimamizi wa jumuiya hizi huwa chini ya halmashauri za vijiji, na hata halmashauri za wilaya za eneo hilo, hivyo uangalizi wake upo pia kwa idara ya mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori Tanzania kwa sasa inajulikana kama TAWA, Tanzania wildlife authority, mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori Tanzania.
Maeneo haya ya hifadhi ya jamii, au WMAs ni muhimu sana, na lengo la kuanzasha maeneo haya ni zuri sana na ni hazina nzuri sana ambayo ikitumika vizuri na kwa usimamizi makini maeneo haya yatasaidia sana uhifadhi endelevu wa maliasili. Na pia ni sehemu muhimu kwa jamii kutambua na kuona thamani ya wanyamapori na rasilimali nyingine kwenye maeneo yao hivyo wataona umuhimu wa kuhifadhi rasilimali hizo.
Ninachotaka tufikirie na kukiweka wazi ni kwamba ili maeneo haya yawe endelevu na yanayotoa manufaa, kazi kubwa bado inahitajika kwa ajili ya uangalizi na namna ya kuyatangaza ili yaweze kutengeneza manufaa yaliyokusudiwa. Pia tunatakiwa kuangalia mfumo wa utaoji wa manufaa yatokanayo na mapato ya rasilimali za meneo haya.
Manufaa yatokanayo na uwepo wa maliasili hizi ambazo zipo kwenye maeneo ya ardhi ya vijiji ilitakiwa na inatakiwa manufaa yote kama ni fedha au faida nyingine yoyote ibaki kwenye jumuiya hizi, kwa lengo la kuhamasisha uhifadhi na pia kuitia jamii moyo kutokana na manufaa yaliyopatikana kwenye maeneo yao. Serikali kuu inatakiwa kupata kodi yake tu, inayobaki iwe wazi kwa jamii, na ielezwe wazi kwa vijiji husika, na vijiji vipange kwa pamoja namna ya kutumia fedha au mapato yaliyopatikana kwa maendeleo yao na maendeleo ya WMA.
Naamini kabisa haya yakifanyika kwa weledi na kwa uwazi, WMA zetu zingepiga hatua kubwa sana na jamii itathamini uwepo wa rasilimali zao, na watafanya kazi kwa pamoja kuhakikisha uwepo wa WMA na rasilimali zake unaendelea kuwepo kwa ajili ya kunufaisha wao na vizazi vijavyo. Hii ni kwa sababu kama kitu hakina faida kwake au mfumo wa ufanyaji kazi unapokuwa mgumu na usioeleweka kwa jamii, watu watakosa motisha na hamasa ya kufuatilia na kujua nini kinaendelea, pia watu hawatathamini uwepo wa rasilimali zao kwasabau hakuna namna nzuri ya wao kunufaika hivyo hawatakuwa na hamasa ya kuendelea kuhifadhi kitu ambacho hakina faida kwao.
Ni kazi ya mamlaka husika pamoja na serikali kupitia mara kwa mara maeneo haya, na pia kuangalia tena na tena mfumo wa uendeshaji wa maeneo haya, ili kubaina upungufu na udhaifu mapema. Pia kuangalia mambo kwa jicho la kisasa na mahitaji ya watu, mfumo wao wa kupata kipato ili waweze kuweka mipango na sera ambazo zinaenda na wakati na pia zinatekelezeka.
Ahsante sana!
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255683 862 481/+255742 092 569