Maeneo ya Usimamizi wa Wanyamapori, au Maeneo ya Hifadhi ya Jamii, kwa kingereza, Wildlife Management Areas (WMA), ni maeneo muhimu ya uhifadhi wa wanyamapori yanayosimamiwa na jamii.
Maeneo haya yana utajiri mkubwa wa wanyamapori na bayoanuai nyingine muhimu, hivyo ni maeneo muhimu sana kwa uhifadhi na usalama wa wanyamapori.
Makala hii ni maboresho ya makala niliyoandika mwaka septmba 2017, ambapo nilichambua Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009. Nimefanya maboresho haya kwa kuzingatia mabadiliko yaliyofanyika katika sheria hiyo, na sasa tuna sheria ya Uhifadhi wa Wayamapori iliyoboreshwa ya mwaka 2022.
Katika makala hii, nitachambua Sehemu ya 5 ya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya mwaka 2022, hususani vifungu vya 31 hadi 33, vinavyoelezea uanzishwaji wa Maeneo ya Usimamizi wa Wanyamapori nchini Tanzania.
WMA huundwa kwa kujumlisha ardhi ya vijiji ambavyo vimeamua kwa hiari kutenga sehemu ya ardhi yao kwa ajili ya uhifadhi. Lengo kuu ni kuwahusisha wanajamii moja kwa moja katika uhifadhi wa wanyamapori, huku wakinufaika kupitia utalii, uwekezaji, na shughuli nyingine endelevu.
Karibu tujifunze tuone sheria inasemaje kuhusu WMA, ni nani mwenye mamlaka ya kuanzisha, ni nani anayehusika katika utungaji wa sheria na kanuni, na miongozo ya kisheria kuhusu mgawanyo wa faida zinazotokana na uwepo wa WMA.

Ramani inayoonyesha mtawanyiko wa maeneo ya WMA Tanzania, rangi ya kijani iliyokolea ndio maeneo ya WMA
Uanzishwaji Na Usimamizi Wa Maeneo Ya Hifadhi Ya Jamii (WMA)
31.-(1) Maeneo ya hifadhi ya jamii yameanzishwa kwa kusudi la kuhamasisha jamii kwenye masuala ya uhifadhi wa wanyamapori kwenye maeneo ya-
(a) nje ya maeneo muhimu ya hifadhi ya wanyamapori, mfano hifadhi za taifa, Mapori ya akiba, Maeneo tengefu na Eneo la hifadhi ya Ngorogoro;
(b) maeneo yanayotumiwa na wanajamii kama vile misitu, mashamba na mapori ya vijiji
(c) maeneo yaliyo ndani ya ardhi ya Kijiji
(2) Mgawanyo wa faida katika maeneo ya WMA utazingatia miongozo iliyotolewa na Serikali na kufuata mifumo ya usambazaji wa gharama na faida kwa usawa, kwa lengo la kuendeleza uhifadhi wa wanyamapori, kuimarisha maendeleo ya kiuchumi, na kupunguza umaskini
(3) Maeneo ya WMA yataanzishwa na kusimamiwa kulingana na kanuni na mapendekezo yaliyofanywa na Waziri mwenye dhamana na kuchapishwa kwenye Gazeti la serikali.
(4) Waziri, kwa kushauriana na Waziri anayehusika na Mamlaka za Serikali za Mitaa, ataandaa kanuni na sheria ndogo ndogo, zitakazopitishwa na mamlaka za vijiji kwa marekebisho yanayohitajika, ambazo zitatumika katika eneo husika la WMA.
(5) Waziri, katika kutunga kanuni chini ya kifungu hiki, atahakikisha kwamba jamii ya eneo husika inashirikishwa ipasavyo na kupewa taarifa juu ya jinsi itakavyonufaika na maeneo ya WMA.
(6) Shughuli zitakazotekelezwa katika maeneo ya WMA zitazingatia Sheria ya Misitu, Sheria ya Ufugaji Nyuki, Sheria ya Uvuvi, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira au sheria nyingine yoyote husika.
(7) Chama chochote kilichoidhinishwa kinachosimamia eneo la WMA, kwa mujibu wa masharti ya kifungu cha 33(1), kitakuwa na haki ya kujadiliana na kusaini makubaliano na wawekezaji watarajiwa, mradi tu wawakilishi wa Mkurugenzi na Halmashauri ya Wilaya washirikishwe katika mchakato wa majadiliano na utiaji saini wa makubaliano hayo
(8) Masuala yanayohusiana na vigezo vya ugawaji, aina, ukubwa, idadi na ubora wa vitalu vya uwindaji ndani ya maene ya WMA yanatakiwa kuanishwa katika kanuni za usimamizi wa maeneo ya WMA.
32.- Waziri baada ya kupokea maombi yaliyofanywa na Baraza la Kijiji na maoni ya Mkurugenzi na pia kwa kutoa taarifa kwenye Gazeti la serikali, anaweza kutangaza eneo la ardhi ya Kijiji husika lililotengwa kwa ajili hifadhi ya jamii kuwa Eneo la Usimamizi wa Wanyamapori (Wildlife Management Areas, WMA).
33 (1) Kila Wilaya yenye eneo la WMA lililotangazwa itaanzisha Kamati ya Ushauri wa Maliasili ya Wilaya kwa ajili ya kutoa ushauri kwa vyama vilivyoidhinishwa na mamlaka husika za serikali za mitaa kuhusu masuala yanayohusiana na uratibu na usimamizi wa eneo la Usimamizi wa Wanyamapori.
(2) Ushauri utakaotolewa chini ya kifungu kidogo (1) utakuwa sambamba na Mpango Mkuu wa Usimamizi wa eneo husika la Usimamizi wa Wanyamapori.
Mfano wa baadhi ya maeneo ya Usimamizi wa Wanyamapori au WMA ni; Burunge WMA, Enduimet WMA, Ikona WMA, Makao WMA, Makame WMA, Randilen WMA, Chingoli WMA, Kimbanda WMA, Kisungule WMA, Mbaran’gandu WMA, Nalika WMA & Liwale WMA, Juhiwangumwa WMA, Ngarambe-Tapika WMA, Illuma WMA & Ukutu WMA, Ipole WMA, Uyumba WMA, Mbomipa WMA, Waga WMA, Umemaruwa WMA.

Picha ya Tembo akiwa katika WMA ya Burunge.
Hata hivyo, licha ya malengo mazuri ya uanzishaji wa hizi WMA, bado zimekuwa na changamoto nyingi za usimamizi, mgowanyo wa mapato, na migogoro mingi inayohusu ardhi. Tafiti zinaonyesha ni WMA chache zinafanya vizuri na kukaribia kufikia malengo ya kuanzishwa kwake.
Makala ijayo nitaangazia changamoto, na kuanisha WMA zinazofanya vizuri hapa Tanzania.
Asante sana kwa kusoama makala hii, tukutane hapa kwa makala ijayo. Endelea kujifunza na kushirikisha wengine makala hii.
Hillary Mrosso |+255 683 248 681 |hmcoserve@gmail.com
Tunaandika makala hizi ili tuongeze uelewa wetu kuhusu wanyamapori, tunaamini tukipata uelewa tutachukua hatua kushiriki katika uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yake asilia.Kazi hii tunafanya kwa kujitolea na hakuna malipo yoyote, endapo umefurahia kazi zetu unaweza kutuunga mkono kwa kiasi chochote ili tupate mtandao, vifaa vyua kufanyia kazi kama kamera na komputa. Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana kwa mawasiliano haya; hmconserve@gmail.com |+255-683-862-481