Habari msomaji wa wildlife Tanzania, karibu kwenye makala yetu ya leo ambayo pamoja na mambo mengine nitakushirikisha mambo niliyojifunza kutokana na maonyesho ya Nanenane ambayo yalifanyikia Dodoma. Nitalenga zaidi kwenye sekta ya Maliasili na utalii, kama nilivyotangaulia kukuandikia kwenye makala ya kwanza , “Neno la shukrani kwa wizara ya maliasili na utalii tanzanaia”. Kuna mambo mengi nilijifunza ambayo nataka na wewe msomaji wa makala hizi uyajue ili tujue hali ya mambo inavyokwenda kwenye malisili zetu.

Sikukuu za nanenane huwa ni sikukuu za wakulima ambapo kwa nchi ya Tanzania hufanyika kila mwaka kwenye mikoa tofauti tofauti. Ambayo watu wengi huuhudhuria kwa maonyesho mbali mbali ya bidhaa zao walizo nazo au huduma wanazotoa kwa jamii, kwa hiyo utakuta watu wakinadi na kuelezea biashara zao, na hapa inajumuisha serikali na watu binafsi. Kwa kuwa mimi mwenyewe nilikwepo kwenye maonyesho ya Nane nane, hivyo ngoja nikushirikishe mambo hayo;

Kivutio kikuu msimu wa Nanenae

Nimejionea mamia na mamia ya wakazi wa Dodoma wakifika kwenye mabanda ya maliasili na utalii wakiuliza mambo mbali mbali, lakini kikubwa nimeona wana kiu kubwa sana ya kuwaona wanyamapori walioletwa kwa ajili ya maonyesho. Nimekuwa nikiwauliza watu mbali mbali siku hiyo tulivyokuwa wote huko Dodoma, nikitu gani kimekuvutia ulivyoenda Nanenane? Wengi wao wamejibu, mimi nimevutiwa sana na  kumwoana simba na wanyamapori wengine. Kuna ndugu yangu mwingine akaniambia we unafiiri kuna kitu kingine kinachowavutia watu kwenda nanenane zaidi ya kwenda kuwaona wanyama? Kwa kweli ninakubaliana naye kwa jambo hili.

Nimeona wanafunzi na watoto wadogo wa miaka kama 5 wakiwa Nanenane, nikajiuliza mtoto kama huyu ni kitu gani ambacho atakifurahia akienda kwenye maonyesho zaidi ni kwenda kuwaona wanyamapori walioletwa. Nimeona vijana, nimeona wazee, nimeona wanawake kwa wanaume wakiwa kwenye foleni ndefu ya kuona wanyamapori. Ingawa ilikuwa ni kulipia kiasi cha shilingi 1000 kwa kila mtu bado watu walikuwa na kiu na hamu ya kuona wanyamapori.

Watu wengi walizijua hifadhi za Ruaha na Tarangire

Licha ya watu waliopata na kutumia fursa ya ofa ya kutembelea hifadhi za Ruaha na Tarangire, bado watu walipata na kuona matangazo na mabango makubwa sana ya ofa za kutembelea hifadhini. Mji wa Dodoma ulipambwa na matangazo ya kumvutia kila mtu anayeyaona matangazo na mabango ya wizara ya maliasili na utalii. Kwa jinsi hii watu wengi walijua na kupata habari kuhusu ofa ya kutembelea hifadhi za wanyamapori, na pia kuwafanya wengine kujua kuwa kuna hifadhi za wanyamapori katika nchi yetu.

Gharama na maandalizi ya kutembelea hifadhini

Licha ya kuwepo kwa muda wa tangazo kama siku 10, bado kuna watu walitamani sana kutembelea hifadhi za wanyamapori lakini walishindwa kumudu gharama za gafla namna hiyo. Wengine walisema hali ni ngumu, wengine walisema gharama ni kubwa, na wengine walisema wamechelewa kupata taarifa za ofa hiyo iliyotolewa na wizara ya maliasili na utalii kupitia shirika la hifadhi za taifa TANAPA.

Hayo ni baadhi tu ya yale nilioyaona ni muhimu nikushirikishe ili uweze kufahamu yaliyojiri huko Nanenane Dodoma. Nitoe pongezi kwa wizara husika kwa kufanikisha jambo hili kubwa na zuri kwa wakazi wa Dododma licha ya changamoto mbali mbali bado mmeendelea kutoa huduma nzuri. Pia nitoe rai kwa safari zijazo ningependa taarifa zitolewe mapema hata mwezi mmoja kabla ili watu wapate nafasi ya kujiandaa na gaharama za safari. Pia endapo ofa hizi zitaendelea kuwepo tutawajengea watanzania utamaduni mzuri wa kujipanga mapema na kujitengea bajeti ya kutembelea hifadhi za wanyamapori

Asante sana kwa kusoma makala hii;

Hillary Mrosso

+255 683  248 681/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaam.net/wildlifetanzania