Tunatumia mamilioni ya dola za kimarekani, na kuweka maisha yetu hatarini ili kuwatunza wanyamapori ambao tunaamini wana thamani kubwa kwa maisha yetu na maisha ya vizazi vijavyo. Gharama kubwa za uendeshaji na usimamizi, juhudi kubwa za serikali na wadau wengine katika kulinda rasilimali za nchi ambazo ni urithi kwa ajili ya kunufaisha taifa zima ni ndoto ambayo bado inaonekana kutotimia kwa sababu ya tamaa na ufisadi wa watu wachache ambao wanaonekana kuwa na nguvu kubwa na ushawishi kuliko kilio cha mamilioni ya watu masikini ambao maisha yao yapo hatarini siku zote kwa kuishi, kutunza na kusimamia na rasilimali hizi.
Uwepo wa rasilimali na maliasili kwenye nchi si kwa ajili ya kunufaisha mtu mmoja au kikundi fulani cha watu, sheria za nchi zetu zipo wazi kabisa kwamba kila mwananchi ana haki kunufaika na uwepo wa rasilimali zilizopo katika nchi yake. Lakini haki ya kunufaika na rasilimali hizi imebakia kwenye vitabu na makaratasi bila utekelezaji. Hii ikiwa na maana kuwa uwepo wa ujangili kwenye hifadhi za wanyamapori na hata kwenye maeneo ambayo yanadhaniwa kuwa na usimamizi na ulinzi mkubwa, unaonyesha jinsi ambavyo wanyamapori tunaowahifadhi kwa ajili ya kunufaisha jamii na taifa zima zinaishia kwenye mikono ya watu wachache ambao wana mtandao na watu matajiri wa nchi nyingine za Ulaya, Marekani na Asia.
Kinachoendelea kwenye hifadhi za wanyamapori wetu ni uporaji wa haki za msingi za wananchi kutonufaika na maliasili zao ambazo serikali inazilinda kwa gharama kubwa sana. Uwepo wa ujangili ni wazi kabisa kuwa haki za msingi za wanajamii zimeporwa na zinawanufaisha watu wachache wenye nguvu na kuwaacha mamilioni ya watu wakiwa hawana maelezo mazuri kwanini rasilimali zao haziwanufaishi, na uwepo wa wanyamapori wenye thamani hauonekani kuongeza thamani kwenye maisha yao.
Maswali tunayopaswa kujiuliza siku zote, serikali na wadau wa sekta hii, gharama zote zinazotumika kwenye uhifadhi nini hasa dhamira ya dhati ya kuhifdhi maliasili hizi? Je, jamii yetu na sisi wenyewe tunaona matokeo chanya yanayoendana na gharama za uhifadhi? Nini hasa kinaturudisha nyuma kwenye suala la uhifadhi wa wanyamapori? Nani hasa anastahili kunufaika na rasilimali za wanyamapori? Je, mipango na mikakati tuliyonayo inaweza kukabiliana na changamoto iliyopo sasa kwenye uhifadhi wa wanyamapori? Maswali haya na mengine mengi tunaweza kujiuliza ili kujikagua ni kiasi gani tumedhamiria kutokomeza ujangili kwenye maeneo ya wanyamapori na kwenye jamii yetu.
Moja ya ripoti niliyosoma iliyoandikwa na shirika la kimataifa la linalojihusisha na uhifadhi wa wanyamapori na misitu kwenye bara la Afrika, na pia kusaidia juhudi za uhifadhi na kupinga ujangili wa wanyamapori kama vile tembo na faru katika bara la Afrika. Shirika hili linaitwa African Wildlife Foundation (AWF), sio shirika jipya hapa Afrika, lipo zaidi ya miaka 60 iliyopita na linafanya kazi na nchi mbali mbali za Afrika ikiwemo Tanzania. Kwenye ripoti hiyo inayojulikana kwa jina la AWF’s Response to Illegal Wildlife Trafficking, wanaeleza mambo mengi kuhusiana na ujangili, biashara haramu za usafirishaji wa wanyamapori na pia wanaeleza juhudi kubwa wanazofanya ili kuokoa na kutoa elimu kwa watumiaji wa bidhaa za wanyamapori kama vile meno ya tembo na pembe za faru, ili waelimike na kuachana na kutumia na kutegemea bidhaa hizo ambazo zinatoka kwa wanyama ambao wapo hatarini kutoweka kwenye uso wa dunia.
Pamoja na mambo mengine, kwenye ripoti hii wameandika hali ambayo inaikabili bara la Arika na kuainisha kuwa ujangili wa wanyamapori ni tishio na umekuwa ni moja kati ya biashara haramu kubwa sana ikiwa inaingiza kiasi cha zaidi ya dola za kimarekani bilioni 10 kwa mwaka. Kwa mujibu wa ripoti hii inaonyesha biashara hii ya wanyamapori inaingiza fedha nyingi sana huku ikiwa inazikaribia kwa karibu sana biashara nyingine haramu kama vile biashara ya dawa za kulevya, biashara ya binadamu, biashara ya silaha.
Aidha, kwa hali ilivyo ni dhahiri kuwa kuna uhitaji mkubwa sana wa meno ya tembo na pembe za faru kutoka katika bara la Afrika kwenda kwenye nchi zenye uhitaji huo. Hivyo jambo ambalo limechangia kukua na kushamiri kwa ujangili kwenye bara la Afrika. Kwa mujibu wa taarifa ya ripoti hii inaonyesha kuwa kila siku tembo 100 wanauwawa kwa ujangili, na pia inaonyesha kwa tangu mwaka 2007 hadi 2012 idadi ya faru wanaouwawa kwa ujangili imeongezeka kutoka 13 hadi 668 kwa nchi ya Afrika ya Kusini pekee, nchi ambayo ni sehemu pekee katika bara la Afrika yenye idadi kubwa ya faru.
Kutokana na kasi ya ujangili wa wanyamapori hasa tembo na faru kwenye bara la Afrika, wanyamapori hawa ambao walikuwa na idadi nzuri sasa wameporomoka na kuwa kwenye hatari kubwa sana ya wanyamapori wanaoelekea kutoweka duniani. Kwa mfano katika bara la Afrika inakadiriwa kuwa kiasi cha tembo waliobaki ni 450,000 na idadi ya faru waliobaki katika bara hili ni 25,000. Hii ni dalili mbaya sana kwenye uhifadhi wa wanyamapori hawa adimu na wenye thamani kubwa. Kwa kasi hii ya ujangili dhidi ya wanyamapori hawa kama juhudi za makusudi hazitachukuliwa tunaweza tusiwe na tembo na faru miaka 20 ijayo.
Sasa jiulize kila siku tembo 100 wanauwawa kwa ujangili, je unanufaika au ulishawahi kunufaika na ujangili huo? Kwa wengi ni hapana, na jamii inaendelea kuwa masikini huku ikishikilia na kuaminishwa kuwa wanyamapori hawa wanafaida na wataleta faida kwao. Utanishawishije nielewe kuwa kuna manufaa ya kuwahifadhi wanyamapori hawa ikiwa kuna udhaifu mkubwa kwenye usimamizi na milango mingi inafunguliwa kwa siri ili watu wabaya wawaue wanyama wetu? Tunasikia kila siku kwenye vyombo vya habari na kupitia ripoti mbali mbali kuwa watu wanakamatwa kwa ujangili na wengine wengi wanahusishwa na ujangili ikiwemo viongozi wetu tuliowapa dhamana ya kusimamia rasilimali hizo.
Serikali zetu na wadau wengine waliopewa dhamana ya usimamizi wa rasilimali hizi, wanatakiwa waonyeshe bila shaka yoyote na bila kumuonea haya mtu yeyote anayejihusisha na ujangili wa wanyamapori, kwa kumchukulia hatua kali za kisheria. Waonyeshe dhamira iliyo wazi kwa maneno na kwa vitendo kupambana na ujangili ili kulinda haki za watu wake na wanyamapori.
Hivyo hivyo, serikali na mamlaka zake zinatakiwa kuangalia mara kwa mara jinsi jamii inavyonufaika na inanufaika kwa kiasi gani na uwepo wa rasilimali hizi kwenye maeneo yao. Uwazi na uwajibikaji vinatakiwa viende pamoja kwenye uhifadhi wa wanyamapori na rasilimali hizi ili kujenga matumaini na hari ya jamii kushiriki katika uhifadhi wa maliasili.
Tunatakiwa kuzuia hisia zetu linapokuja suala la uhifadhi wa wanyamapori hasa tembo na faru ambao wanatafutwa sana. Tunatakiwa kujua kuwa fedha nyingi tunazopata kwa kushiriki kwa namna yoyote ile kwenye ujangili haziwezi kuwarudisha wanyamapori waliouwawa. Hivyo tunatakiwa tuishi kwa kufuata sheria na misingi ya haki; mtu au kikundi cha watu kisiwe ndio chanzo cha kupotea na kuuwawa kwa wanyamapori wetu. Uwezo tunao, nguvu tunazo kuwalinda na kuwahifadhi wanyamapori hawa ili wawafikie vizazi vingi vijavyo.
Karibu kwa maoni, maswali, ushauri na hata mapendekezao. Yote ni muhimu ili kwa pamoja na kwa namna yoyote njema tushiriki katika uhifadhi wa rasilimali zetu muhimu za wanyamapori.
Ahsante sana!
Hillary Thomas Mrosso
Wildlife Conservationist
+255683 862 481/+255742 092 569
www.mtalaam.net/wildlifetanzania