HERI YA MWAKA MPYA, 2020
Awali ya yote nina kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kuuona mwaka mpya tukiwa na afya njema, pia kwa kuiwezesha makala hii hatimaye imekufikia mpendwa msomaji wetu wa makala za wanyamapori na maliasili kiujumla ilitujifunze sote zaidi kuhusu mambo madogo madogo ya msingi katika uhifadhi na utalii, kwanini nimeita madogo modogo ya msingi? Kwa nini nimeiandika mwanzoni mwa mwaka? Na yatakujenga na kubadilisha vipi mtazamo wako katika uhifadhi na utalii?, Karibu.
Utangulizi mfupi; Makala hii imeainisha mambo ambayo mara nyingi tunayaona mdogo madogo lakini ukiyafikiria na kuyatambua mapema yana mchango mkubwa sana katika kubadilisha mitazamo ya wasomi, wasio wasomi na watu wa rika zote ili kuendesha na kufanikisha uhifadhi, utalii na hata kupunguza umaskini kwa kubadilisha matumizi ya maliasili tulizo nazo, mambo hayo ni pamoja na ngazi ya Tanzania kwa utajiri wa bioanuwai, Hifadhi ya Taifa Nyerere kuibadili Hifadhi ya Taifa Ruaha kwa ukubwa, “Big five” kupisha wanyama wengine kuwa vivutio vikubwa vya kitalii, kufungwa kwa biashara ya wanyamapori Tanzania pia madhara ya uhifadhi uliopitiliza.
Niimani yangu utatoka na kitu kipya chenye kukubadilisha mtazamo, kukufungua na kukuongezea uwezo wako wa kufikiria zaidi juu ya maliasili pia kukupa mawazo mapya yatakayo wasaidia wafanya maamuzi juu ya bioanuwai tulizo nazo nchini kwetu, “nchi yanguTanzania nakupenda kwa moyo wote”…
- Tanzania kidunia inashika namba ya 19 kwa utajiri wa bioanuwai ikijumuisha 10.6% spishi za ndege, 2.7% spishi za Amfibia, 6.5% spishi za Mammalia, 3.5% spishi za Reptilia, 5.3% spishi za Samaki, na 3.7% spishi za mimea mikubwa ( Vascular plants), kwa bara la Afrika inashika namba ya 3 ikoongozwa na Afrika kusini na Congo na kwa Afrika Mashariki inashika nafasi ya kwanza ikifatiwa na Kenya, kitu cha muhimu ni kuzijua hizo bioanuwai zote na kujiuliuza umeshaowa viumbe wangapi wa kipekee wanaopatikana Tanzania? Na kila siku unaimba “nchi yangu Tanzania na kupenda kwa moyo wote”, ipende kwa matendo na sio myimbo tuu.
- Mambo yanaenda kasi na kubadilika sana, ikiwa miezi michache nyuma Ruaha ndio ilikuwa hifadhi kubwa Tanzania na ya pili barani Afrika baada ya hifadhi ya Kruger ya Afrika Kusini, yenye eneo la mraba sawa na nchi ya Denmark lakini sasa imepisha ukubwa wa Hifadhi ya Taifa mpya ya Nyerere ambayo siku za nyumba ilitambulika kama pori la akiba Selous. Ushawahi tembelea Hifadhi yoyote ya Taifa? Au unasubiri ziongezeke nyingine tena? Utaweza kutembelea au ndo subiri subiri kwanza?Tenga muda tembelea yoyote iliyokaribu nawe, usisubiri wazungu waje wakuandikie vitabu vya vivutio vya watalii vilivyopo nchini ikiwa wewe pia unaweza kuandika na kwa gharama ndogo zaidi.
- Makampuni ya kitalii, kila siku yanabadilisha utangazaji wa vivutio vya kitalii kulingana na ushindani uliopo miongoni mwa matakwa ya wa wateja wao wengi wenye pesa na pia kuwa wa kitofauti ili kuwapa thamani na wanyama wengine pia, mfano mkubwa uliopo sasa na wenye kushamili sana mbugani wanyama wote wa “Big Five” wapisha utalii wa wanyama wadogo, ndege na wadudu; Kuwa makini tenga muda andaa pesa ya kutosha tembelea eneo lolote lenye wanyama pori, jitahidi uendane na muda kwa faida yako….mambo hayakawii huwezi jua kesho ikawa kutalii ndani ya eneo la wanyama ni kwa anga tu ilikupisha uhifadhi uendelee utaweza gharama za kupanda na kukodi ndege?.
Picha 1: ikiwaonyesha ndege (blacksmith lapwings) kama miongoni mwa vivutio vikubwa vya watalii wengi wanaoenda na muda.
Picha 2; Inamuonyesha kibongo mongoose (dwarf mongoose) miongoni mwa wanyama wadogo wanaokula nyama.
- Biashara ya wanyama pori Tanzania kufungiwa mwaka 2015 ni kitu kuzuri ukiangalia upande wa kusaidia wanyama kurudi katika uwingi wao wa zamani (population restoration) na kupunguza biashara haramu za wanyama ambao kisheria hawaingizwi kwenye biashara hiyo mfano faru wa aina zote weusi na weupe, lakini je? Upande wa pili, ambao baada ya wanyama hao kurudi kwenye uwingi wao wa zamani inapelekea kuwa wengi zaidi kiasi ambacho eneo lao tengevu kushindwa kuwamudu na badala yake kuongeza usumbufu kwa jamii jirani hivyo kushushwa thamani na madhara yake ni makubwa hasa pale ardhi itakapo simamiwa kidedea ihamie matumizi mengine ya ardhi kama kilimo kikubwa cha biashara hivyo wanyama kutanga tanga na kupotea; Jipe muda wa kusoma vitu vipya na venye faida si kwako na kwa wanyama pia.
- Uhifadhi ni mzuri na wenye faida nyingi lakini unapozidi madhara yake ni makubwa na ya muda mrefu, jifunze kitu, Australia ni miongoni mwa sehemu ambazo zimefanikiwa sana kwa utunzaji wa misitu lakini mnamo mwezi wa nane (August, 2019) msitu ulishika moto mpaka sasa naandika Makala hii (tarehe 05/01/2020) bado unawaka moto takribani ekari milioni 6.3 (sawa na kilomita za mraba 63000) zimeshaungua na kuharibu majengo 2500, kuua watu 25 na wengine 6 kutojulikana waliko; Tafakari zaidi jua unahifadhi kwa njia gani na kwa sababu gani na ukiwa unatarajia nini haijalishi matokeo yatakuwa mazuri au mabaya.
- Usisahau hiki, kisayansi inasemekana kila spishi ina muda wake wa kutamba duniani takribani miaka milioni kumi kwa kila spishi hasa kwa mazingira yasiyo na uharibifu na usumbufu wowote, lakini jifunze kitu kwa mamba ambaye walikuwa pamoja na mijusi wakubwa (dinosaurs) miaka yapata milioni 200 iliyopita na mijusi hao walishatoweka duniani, lakini mamba hana dalili zozote za kutoweka; Tenga muda jifunze mambo yote yanayochangia kutoweka kwa viumbe hai na jitahidi usiwe miongoni mwa visababishi.
- Nchi nyingi zenye bioanuwai kubwa zaidi duniani ndizo nchi maskini zaidi kidunia vile vile, mfano hai nchi nyingi za kiafrika kama Botswana, Namibia, Tanzania na Zimbabwe ndio nchi tano za juu kidunia zinazojitahidi kuhifadhi bioanuwai zikifwatiwa na nchi ya Norway inayoshika nafasi ya sita, nafasi ya nane Canada na ya kumi na tisa ni United States; Fikiri njia sahihi za matumizi bora ya mali asili tulizo nazo kujikwamua na umaskini na wakati huo huo tukifanya uhifadhi.
“Tazama ramani utaona nchi nzuri yenye mito na mabonde mengi ya nafaka, nasema kwa kichwa halafu kwa kufikiri, nchi hiyo mashuhuri huitwa Tanzania majira yetu haya, yangekuwaje sasa Utumwa wa nchi, Nyerere ameukomesha × 2……”
Mungu ibariki Afrika, Mungu ibarikiTanzania,
Ni matumaini yangu umepata kitu kipya na kubadilika mtazamo mapema kabisa mwanzoni mwa mwaka 2020, hivyo naamini utayatendea kazi vyema.
Asanteni sanaa
Imeandikwa: Leena Lulandala
Mawasiliano; 0755369684
Mwanafunzi-UDSM.