Kila siku kuna vitu tunafanya ikiwa ni njia mojawapo ya kujipatia mahitaji ya kila siku kutoka kwenye mazingira yetu mfano matunda, chakula na mara nyingine hata nyama, lakini je? njia tunayotumia ni sahihi na inaweza kuyafanya mazingira kujitengeneza na kujirudusha kwenye mstari wake (ecosystem balance)?

Pia je wale viumbe pori wanaoishi kwenye hayo mazingira una uhakika hawata athirika na unachokifanya? Ikumbukwe hawana uwezo mkubwa wa kujiongeza kama wewe!

Ukiacha ujangili ambao umefanya wanyama wengi kupungua idadi mfano tembo na mbwa mwitu hadi kutoweka kama faru, mammoth na mastodon (familia moja na tembo ila hawa ni wazamani sana). Yapo mengi utajifunza leo, mwanzoni kabisa mwaka 2019 ili tuweze epuka na kuyapunguza.

1.Kutambulishwa wanyama wapya kwenye mazingira asilia (introduction of invasive/exotic species)

Viumbe Vingi asilia vinazidi kupungua na kutoweka kwa sababu ya viumbe vipya au vamizi ambavyo vimetambulishwa kwa sababu mbalimbali kwenye mazingira asilia ukiacha mbuga za wanyama, mfano;

1.Kunguru (Indian house crow) waliotambulishwa Zanzibar kipindi cha Sultani lengo ikiwa kusafisha jiji lakini imekuwa tofauti kabisa wameathiri 70% ya ndege asilia miji ya ukanda wa pwani ya Afrika mashariki hasa kunguru asilia (Pied crow).

2.Mmea (Gutenbergia cardifolia) ambao sasa umesambaa na kuvamia zaidi ya 50% eneo la Ngorongoro, bahati mbaya hauliwi na wanyama hivyo hufanya wanyama kukimbilia vijijini na kusababisha migogoro kati ya wanyamapori na wakulima (human wildlife conflicts).

3.Magugu maji (water hyacinth) yaliyoletwa barani Afrika Mwaka 1980 na sasa yanaendelea kuathiri uzazi wa viumbe wengi wa majini mfano ziwa Victoria.

Viumbe hawa vamizi vimepelekea viumbe asilia kutoweza kumudu mazingira yao na kutoweka.

  1. Mabadiliko ya tabia ya nchi(climate changes)

Mabadiliko haya yana ambatana na matukio mbalimbali kama joto kuongezeka zaidi ya kawaida(global warming), vina vya maji kuongezeka kwenye maziwa na bahari hasa ya barafu, na kubadilika kwa upatikanajinwa mvua na mara nyingi kuongezeka mabadiliko ya hali ya hewa kama mafuriko na ukame.

Unakuta mnyama kazoea mazingira yenye joto la kawaida na mvua pia (narrow range of PH) lakini inapotokea madhara ya kubadilika kwa tabia ya nchi lazima wengine watakufa tu kutokana na kushindwa kuhimili mabadiliko.

18_35% ya wanyama na mimea inakadiriwa kutoweka ifikapo mwaka 2050 kutokana na matazamio ya kubadilika kwa tabia ya nchi.

Pia mabadiliko hata kama mafuriko yanahamisha viumbe majini na kupeleka nchi kavu ambapo wanashindwa kuhimili mikikimikiki ya nchi kavu na bahati mbaya wengine wanauliwa, hivyo kutoweka(sana imetolea kwa mamba).

3.Uvunaji na matumizi kupitiliza pamoja na ujangili (over harvesting resources)

Kwa mfano uwindaji halali, vibali vinatolewa kuwindwa kwa mnyama fulani mbugani(game reserve),lakini bahati mbaya mnyama huyo akawa na uwezo mdogo wa kuzaliana mfano tembo ndio mnyama anaebeba mimba kwa muda mrefu miezi 22 na kwa uhai wake wote miaka 60_80 anazaa watoto wa NNE tu, hembu mfikirie huyu ikatokea akawindwa sana porini(hasa majangili) nini kitatokea kama sio kutoweka?

Pia fikiria mfano mzuri wa kawaida kabisa, kama mvuvi mmoja akavua samaki wengi zaidi ambazo hana matumizi nazo zote (Najua unapata wazo la mfrige na freezers) na vipi ikatokea wavuvi wote wakafanya hivo kwa lengo la kupata pesa na ushujaa wa kuvua samaki wengi ambazo zinapitiliza mahitaji, ziwa litabaki na nini kama sio kupelekea samaki kutoweka?, fikiria vizuri

NB: Pesa na madaraka ni yako lakini malighafi ni zetu sote.

4.Uharibifu na kugawanya mazingira ya wanyama (habitat loss and fragmentation)

Mfano kutengeneza barabara kubwa hasa za lami ndani ya hifadhi kama Hifadhi ya Taifa ya Mikumi,  madhara yake ni makubwa inagawa wanyama bahati mbaya kama baadhi ya wanafamilia walikuwa upande mwingine na barabara ikapita hawajarudi hivyo ndivyo inapelekea wanyama kufa baadhi yao wakijaribu kurudi kwa ndugu zao ikiwa labda ni watoto na wengine kushindwa kurudi kwa ndugu zao kabisa mwisho kukosa furaha na kupata sononeko la moyo pia hulazimika kuyazoea mazingira mapya na kupelekea kutofautiana kabisa na ndugu zao(emergence of discontinuities in species).

Pia barabara ndani ya hifadhi ina mchango mkubwa wa kupoteza wanyama pori kama madereva wasipokuwa makini inapelekea ajali nyingi za kuwagonga wanyama na kupunguza idadi yao.

5.Ukataji na uharibifu wa misitu(deforestation and forest degradation)

Miti inapokatwa sana ikiwa kwa lengo la kuongeza mashamba au moto unapotokea unamchango mkubwa wa kupoteza wadudu wengi japo wanaweza kuruka vipi mayai yao na watoto wao?

Fikiria zile faida kuu za wadudu kama kuchavusha mazao yetu n.k.

Uvunaji holela wa mbao unapelekea wanyama wengine kufa na wengine kuhama mazingira yao hapo ndio tatizo linapokuja kutafuta mazingira mapya, chakula na katika harakati zote hizi idadi ya kufa inaongezeka tu.

Pia uharibifu wa misitu ambao unapelekea kutengenezeka upya kwa umbo la msitu na pori mfano uwazi wa juu kabisa ya mikutano ya miti(creation of opening in the canopy) ambao inapelekea uoto mpya na kufanya baadhi ya wanyama kuhama.

6.Magonjwa

Wanyama baadhi hupoteza maisha kutokana na magonjwa ikiwa ni ngumu kufikiwa na wataalam mara kwa mara kutokana na uchache wao na wakati mwingine kukosekana kwa sasa mfano, Chytridiomycosis ugonjwa unaosababishwa na fangasi umesababisha madhara makubwa kwa chura wa Kihansi (Kihansi spray toad; chura anae zaa) na jamii nyingine ya amphibia

7.Kufungwa kwa ushoroba au njia za wanyama pori (Closure of wildlife corridor)

Wanyama wengi njia zao siku hizi zimekuwa zinafungwa kutokana na ongezeko la watu hivyo kupelekea wanyama hao kuzaa kwa wasiwasi na mashaka mfano chukulia zile njia wanazotumia nyumbu leo kutoka Serengeti kwenda Masai mara na wanaporudi pia, halafu zikafungwa nini kitatokea? Kama sio kutoweka kwao kwa sababu wanahama hama kwa lengo la kutafuta chakula kibichi na kuzaliana.

8.Uchafuzi wa mazingira (environmental pollution)

Kama kemikali zinazotumika kwenye kilimo, uchimbaji madini na viwanda, vyote hivyo vinachangia kuharibika na kuchafuka kwa hewa, ardhi na maji ambako kote kuna viumbe hai hivyo kuharibu makazi yao na kupelekea kutoweka kabisa.

9.Migogoro kati ya binadamu na wanyama pori(human wildlife conflict HWC)

Mfano wanyama wanapovamia mashamba ya wanakijiji jirani na mbugani wakala mazao, baadhi ya wanakijiji hawaoni thamani yao hivyo hawapeleki malalamishi kwenye mbuga stahiki badala yake hujichulukulia maamuzi mkononi ya kuwaua wanyama hao, sasa vipi wakala mashamba mia moja ya watu kama hawa wanyama si watatoweka wengi sana? Fikiria vizuri ndio maana sheria ya wanyamapori kuvamia mazao ya wanakijiji ipo na fidia ya hasara pia ipo.

Fikiria vizuri sana kwa hayo machache niliyosema hapo juu kwa yale yanayowezekana kuchukuliwa hatua yafanyike ile tuepushe uwepo wa sentensi shurutia “NINGEJUA”.

Pia vipi tukipuuzia ndani ya miaka mitano unafikiri tutakuwa wapi na uhifadhi wetu?, vipi wanyama wenyewe?, muelimishe rafiki yako nae awaelimishe rafiki zake ili tupunguze ikiwezekana tuache kabisa.

Shukrani sanaa

 Leena Lulandala

Mwanafunzi UDSM

 0755369684

  Lulandalaleena@gmail.com