Heloo Tanzania, habari za siku kidogo ndugu wasomaji wa makala hizi za wanyamapori. Ni matumaini yangu muwazimna wa afya na mnaendelea vyema katika utekelezaji wa majukumu yenu ya kitaifa na hata yale binafsi lengo tu ni kuyafanya maisha yaendelee kuwa sawia. Katika mfululizo wa Makala hizi za wanyamapori leo tutaingia tena darasani kujuzana machache kuhusu rasilimali za wanyamnapori tulizojaaliwa na Mwenyezi Mungu hapa nchini kwetu Tanzania kitu ambacho kimekuwa ni cha kujivunia mbele ya mataifa mengfine duniani kote.
Katika makala ya leo nakuletea mnyama mwingine jamii ya swala baada ya makala iliyopita kukujuza machache kuhusu ndege ajulikanae kama Karani tamba. Hivyo nikusihi uwe pamoja nami katika makala hii mwanzo mpaka mwisho ili uweze kujua mengi na kemkem kuhusu mnyama swala ambae siku ya leo ndio atabeba kiini cha makala hii na kwahakika utajifunza na kujua mengi kuhusu swala huyu.
Na bila kupoteza muda leo tutamjua swala ajulikanae kwa jina la “TOHE” ambae kwa lugha ya kingereza hujulikana kama “REEDBUCK”. Tohe wapo wa jamii tatu tofautu ambao ni
1.Tohe kusini (Tohe wa kawaida),
2.Tohe wa milima na
3.Tohe bohor.
Sasa kwa ufafanuzi zaidi leo tutamzungumzia TOHE WA KUSINI.
UTANGULIZI
Kama nilivyo tangulia kudokeza hapo juu, tohe ni wanyama wapatikanao katika kundi la wanyama jamii ya swala. Kundi hili lina wanyama jamii ya swala lina wanyama aina nyingi sana na kama usipoweza kupata elimu kuhusu wanyama hawa basi ni vigumu kuweza kuwatofautisha pale unapowaona kutananao kutokana na kufanana kwa ukaribu zaidi kwa aina mbalimbali za swala. Tohe ni swala wapatikanao bara la Afrika tu na si kwingineko kokote duniani hivyo kama watanzania hatunabudi kujivunia kuwa na mnyama huyu hapa nchini.
Tohe ni wanyama wanao vutia sana kuwaangalia hasa katika mazingira yao asilia kwani huwa wana vitu mbalimbali vya kujifunza lakini pia vya kufurahisha. Wanyama hawa wamekuwa wakikumbwa na matatizo mbalimbali katika mazingira yao asilia hali ambayo inapelekea kupungua kwa idadi yao siku baada ya siku mbali na jitihada kubwa zinazofanywa na mamlaka mbalimbali za usimamizi na uhifadhi wa wanyamapori.
Sasa tuanze kutiririka na makala hii ili kumuelezea mnyama tohe kwa kina zaidi hasa kwa kuelezea sifa na tabia zake, makazi, idadi ya wanyama hawa, changamoto wanazo kumbananazo hali kadhalika njia mbalimbali ambazo zitasaidia kutatua changamoto hizo kwa wanyama hawa.
SIFA NA TABIA ZA TOHE WA KUSINI
- Tohe hawa wana miili yenye rangi ya kahawia huku sehemu za chini maeneo ya tumboni wakiwa na rangi nyeupe.
- Miguu yao yote minne ina alama za mistari myeusi sehemu ya chini kwa upande wa mbele.
- Sehemu za kwenye macho wana alama ya miduara yenye rangi nyeupe iliyo zunguka macho yao.
- Wana mikia iliyo chanua sehemu ya nchani ya yenye manyoa yenye rangi nyeupe.
- Katika mashina ya maskio yao wanyama hawa wana matezi ambayo pale wanapohisi hatari matezi haya huwa na rangi nyeusi mfano wa ngozi isiyo na manyoa.
- Madume pekee ndio wenye pembe, pembe hizo zimejikunja kama upinde kuelekea mbele kuanzia sehemu ya chini mpaka nchani. Pembe zao hutengeneza umbo la herufi “V” ukiwatazama kwa mbele na hurefuka mpaka kufikia urefu wa kati sentimita 25 mpaka 45.
- Tohe dume mkubwa huwa anamiliki himaya akisaidiwa na jike na himaya hii huwa ni yakudumu huku wengine huishi kwa kujitenga na wakati mwingine unaweza kuwakuta wakiwa kwenye makundi hadi kufikia wanyama 20 kwenye kundi moja.
- Tofauti na wanyama wengi jamii ya swala, tohe hawa uwa hawaweki alama kwenye himaya wanazo miliki kwa kutumia matezi, kinyesi au mkoji bali huwa na jukumu la kufanya doria ya kuzungukia maeneo yao mara kwa mara ili maadui wasivamie.
- Ni wanyama wenye kasi ndogo ya hukimbia kwa mkimbio wa mtitio huku wakipeana ishara kwa sauti ndogo hasa pale wanapo mkimbia adui yao. Lakini mikimbio yao hii husaidia kuwapa taarifa wanyama wengine ambao hawajajua kama kuna adui anawanyemelea.
- Tohe hawa niwanyama wenye uwezo wa kufanya shughuli zao katika vipindi vyote vya siku yaani mchana na usiku pia japo hupendelea sana muda wa jioni. Kipindi wanapo pumzika hutumia muda huo kucheuwa majani na kuyatafuna upya.
- Kutokana na wanyama hawa kupendelea sehemu zenye majani marefu ambayo ni vigumu kuona mbali, njia kuu ya kuwasiliana kwa wanyama hawa huwa ni sauti ndigo yenye mithili ya filimbi na kwa kutumia matezi mbalimbali.
KIMO, UREFU NA UZITO WA TOHE WA KUSINI
Kimo: Wanyama hawa hufikia kimo cha sentimita 80-105 kwa madume na sentimita 65-95 kwa majike.
Urefu: Kuanzia kichwani mpaka mwisho wa kiwiliwili madume hufikia urefu wa sentimita 130-160 na majike wakiwa na urefu wa sentimita 120-140, huku mikia yao kwa pamoja madume na majike hurefuka na kufikia urefu wa sentimita 18-30.
Uzito: Dume mkubwa hufikia uzito wa kilogramu 60-95 huku jike akifikia uzito wa kilogramu 50-85.
MAZINGIRA
Wanyama hawa hupendelea maeneo ya savana yenye majani marefu lakini kipindi cha kiangazi hupendelea kwenye maeneo yenye miti mingi na sehemu yenye maji yakutosha. Jamii hii ya tohe hupatikana kwa sana katika maeneo mengi ya nchi za upande wa kusini mwa Afrika.
CHAKULA
Hawa ni miongoni mwa wanyama walao majani na aina yao ya ulaji nikama nyati, hii ikimaanisha ni wanyama walao majani ya chini kutokana na maumbile ya midomo yao japo kipindi cha kiangazi hulazimika kula majani ya juu kutokana na uhaba wa chakula.
KUZALIANA
Tohe hawa huzaliana majira yoyote ya mwaka hivo hakuna muda maalumu kwa ajili ya kuzaliana japo kwa nchi kama Afrika kusini kuzaliana huwa sana kipindi cha joto au kiangazi kuanzia mwezi wa 11 mpaka mwezi wa 4 kutokana na maeneo ya nchi hiyo.
Mara tu baada ya dume kupanda majike, jike hubeba mimba kwa muda wa siku 233 (wastani wa miezi 7) na baada ya hapo jike huzaa mototo mmoja tu. Mtoto wa tohe anapo zaliwa hulazimika kuachwa mafichoni na mama kwa takribani wiki sita na muda wote huu mama hulazimika kurudi mafichoni ili kumnyonyesha mototo na kuondoa viashiria vyote ambavyo vinaweza kusababisha maadui kugundua alipo mtoto. Mtoto anapo fikisha miezi mitatu huanza kuongozana na mama kwaajili ya malisho na atimizapo mwaka mmoja basi huanza kujitegemea kimaisha. Majike hufikia umri wakuzaliana mapema kuliko madume. Wafikishapo umri wa mwaka mmoja tu majike huwa tayari kuzaliana wakati madume huchukua takribani miezi 18 (sawa na mwaka mmoja na nusu).
Umri wa tohe hawa ni takribani myaka 10 wawapo katika mazingira asilia japo tafiti zinaionyesha kuwa kama watakuwa wanafugwa kwenye mabustani ya wanyama basi huweza kuishi hadi myana 16.
UHIFADHI
Katika vipengele vyote kwenye makala hizi, basi hiki ndio kipengele chenye thamani kubwa sana kuliko vyote katika makala za wanyamapori. Hii ni kutokana na changamoto zinazo wakumba wanyamapori na kupelekea kupungua idadi yao siku baaada ya siku. Hivyo huwa nasisitiza kila ufikapo katika kipengele hiki basi kisome kwa umakini zaidi ili uweze kujua idadi na uelekeo wa wanyama hawa kwa sasa.
Ni jambo la kumshukuru Mungu kutokana na takwimu na tafiti zilizofanyika kuhusu wanyama hawa ambazo zinaionyesha bado hawajawa hatarini kutoweka duniani. Hii ni kutokana ta utafiti uliofanywa mwaka 2008 na shirika laumoja wa mataifa linalo shughulikia uhifadhi wa maumbile asili (IUCN – International Union for Conservation of Nature). Idadi kubwa ya wanyama hawa ambayo inakadiriwa kuwa ni 73,000 imeenea takribani nchi 14 zipatikanazo kusini mwa jangwa la Sahara huku na Tanzania ikijivunia kuwa miongoni mwa nchiu zenye idadi kubwa ya wanyama hawa.
Mbili ya tatu ya idadi ya wanyama hawa wanapatikana katika maeneo tengefu yaliyo hifadhiwa kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori na maliasili nyingine mfano mzuri Hifadhi ya taifa ya Serengeti. Miongoni mwa sababu zinazofanya wanyama hawa kuendelea kuwepo kwa idadi ya kuridhisha ni uwezo wa wanyama hawa kuishi katika muinuko mkubwa kutoka usawa wa bahari. Wanakadiriwa kuishi muinuko wa mita 1800-2000 kutoka usawa wa bahari hali ambayo inawafanya waepukane sana na baadhi ya shughuli za kibinaadamu mfano uanzilishi wa makazi.
CHANGAMOTO NA TISHIO KWA TOHE WAKUSINI
Kwa kawaida wanyamapori hasa wale walao majanii wawapo katika mazingira yao asilia basi huwa na maadui katika mazingira hayo. Na hapa nazungumzia maadui asilia wa tohe hawa ambao wana mchango mkubwa sana katika ikolojia ya maeneo husika. Maadui asilia wa wanyama hawa ni samba, chui, fisi, mbwa mwitu wa Afrika na mamba hasa mamba wa mto Nile.
Mbali na maadui hawa asilia wapo maadui wavamizi ambao ndio kwa kiasi kikubwa wana hatarisha maisha ya wanyamapori, adui huyu ni binaadamu ambae kwa kiasi kikubwa husababisha yafuatayo kwa wanyama hawa.
Ujangili; hali ya uwindaji wa wanyama bila kuwa na kibali imekuwa ni tatizo kubwa sana kwenye maeneo tengefu ya hifadhi za wanyamapori kitu ambacho kinapelekea idadi ya wanyama hawa kupungua baadhi ya maeneo. Watu wamekuwa waki wawinda wanyama hawa kwa matumizi mbalimbali kama kitoweo majumbani na wengine kwa ajili ya biashara. Mbaya zaidi wengine huwinda bila hata kujali ni tohe mdogo au jike mwenye mimba au kunyonyesha hali ambayo inasababisha kizazi cha jike huyo kisiweze kuendelea.
Kilimo na ufugaji; shughuli za kilimo na ufugaji pia ni changamoto kwa wanyama hawa kwani idadi kubwa ya mifugo imekuwa ikiingizwa kwenye maeneo ya wanyamapori hali ambayo inapelekea kupungua kwa chakula kwasababu ya kugombania chakula kilichopo kati ya wanyamapopri na mifugo. Hali kadhalika upanuzi wa mashamba kwaajili ya shughuli za kilimo pia ni changamoto inayo pelekea wanyama hawa kuhama baadhi ya maeneo.
Makazi na maendeleo ya kibiashara; uvamizi wa maeneo ya hifadhi za wanyamapori kwaajili ya kuanzisha makazi umepelekea kupungua na kuhama kabisa kwa tohe hawa katika maeneo yao asilia. Maendeleo ya miji pia hasa kutokana na shughuli za biashara pia ni mwiba wenye sumu katika baadhi ya maeneo.
Uharibifu wa mazingira; ukataji miti hovyo na uchomaji moto katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori umekuwa ni tatizo kubwa sana linalo pelelekea kutoweka kwa wanyama hawa. Tatizo la utupaji wa taka hovyo karibu na hifadhi za wanyamapori kunapelekea wanyama kufa sana hasa pale wanapokula plastiki kama mifuko.
NINI KIFANYIKE ANGALAU KUNUSURU WANYAMA HAWA HUSUSANI HATA TANZANIA
Kupambana na tatizo la ujangili ambalo limekuwa likiumikza sana vichwa vya watu hasa kwenye mamlaka za hifadhi za wanyamapori. Ni jambo la kushukuru kwamba kutokana na taarifa iliyo tolewa na waziri wa maliasili na utalii Dr. Hamisi Kigwangalla kwamba kiwango cha ujangili kimepungua kwa asilimia kubwa sana na bado jitihada zinafanyika ili kuutokomeza kabisa. Mamlaka za usimamizi wa wanyamapori hazinabudi kuongeza askari wa doria tena wenye maadili na uaminifu ili kuendelea kupambana na majangili wachache walio salia na hatimae suala la ujangili libaki kuwa historia hapa nchini.
Serikali kupitia wizara ya ardhi, makazi na mipango miji ijitahidi kupambana na uanzishwaji wa makazi holela hasa karibu na hifadhi za wanyamapori. Nikweli watu wanahitaji maeneo ya kuishi lakini pia kupanua miji kwaajili ya maendeleo lakini yapo maeneo mengi sana ambayo yana nafasi kubwa sana kwaajili ya makazi tena mbali na hifadhi za wanyamapori. Kwa kufanya hivyo maeneo yetu tengefu ya hifadhi za wanyamapori yabaki kuwa salama.
Kudhibiti upanuzi holela wa mashamba kwaajili ya kilimo hasa karibu na hifadhi za wanyamapori kwani ili kupunguza tatizo la uharibifu wa mazingira. Watu huanza kidogo kidogo na hatimae wanajikuta wameingia mpaka kwenye maeneo ya hifadhi na kuzua migogoro baina ya jamii na mamlaka za hifadhi au baina ya jamii na wanyamapori kutokana na suala la wanyamapori kula mazao ya wakulima au wanyamapori walao nyama kuvamia mifugo.
Wafugaji wote wanaoishi kando kando ya hifadhi za wanyamapori hawana budi kuhamishwa na kutafutiwa maeneo maalumu kwa ajili ya malisho ya mifugo yao. Tanzania bado tuna maeneo mengi na makubwa sana yenye majani ya kutosha na maji mengi tu kwaajili ya mifugo. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tumepunguza ugombaniaji wa chakula kati ya wanyamapori na mifugo.
Wizara ya mazingira chini ya Mh. January Makamba pia ina jukumu kubwa sana la kusimamia sheria za uharibifu wa mazingira ili kudhibiti utupaji wa taka hovyo. Kama nilisema hapo juu kuna wanyama wengi wanakufa kwasababu ya kula uchafu wa plastiki kitu ambacho hakiwezi kumeng’enywa tumboni kwa mnyama. Mfano mzuri ni ndege jamii ya tumbusi hukutwa wakiwa wamekufa na baada ya uchunguzi wanakutwa na uchafu wa plastiki mwingi sana katika matumbo yao.
Jamii ipewe elimu ya uhifadhi na faida zake; jamii ni muhimu sana kupewa elimu kuhusu uhifadhi na faida zitokanazo na uhifadhi wa wanyamapori ili watu waweze kuthamini uwepo wa wanyama hawa. Hili ni suala ambalo nimekuwa nikilisisitiza sana kwamba elimu ya uhifadhi hasa wanyamapori na mazingira lianzie ngazi ya elimu ya msingi mpaka sekondari. Serikali kupitia wizara ya elimu sayansi na teknolojia nilazime ifanye mpango wa kuandaa mitaala kupitia wasomi mbalimbali hasa wenye taaluma za uhifadhi wa wanyamapori na mazingira ili kuweza kuwapatia vijana wetu elimu hii muhimu.
Kama mwanafunzi atapata elimu ya uhifadhi kuanzia ngazi ya shule ya msingi ni dhahiri kwamba atakuja kuwa balozi mzuri sana hapo baadae na mwanaharakati wa kusimamia rasilimali hizi za wanyamaporikwani anajua thamani yake kwa jamii na hata katika kuliingizia pato taifa kupitia sekta mbalimbali kama utalii na uwindaji kwa wenye vibali.
HITIMISHO
Tohe wa kusini ni wanyama ambao wanastahili kuendelea kuwepo katika hifadhi zetu hapa nchini Tanzania kwani kupitia wanyama hawa taifa linajiingizia pesa nyingi za kigeni kutoka nchi mbalimbali. Lakini pia uwepo wa wanyama hawa ni faida kwa wanyama walao nyama kwani endapo wanyama hawa wata toweka basi ni dhahiri kwamba wanyama hawa watakuja mitaani na kuvamia mifugo au hata watu lakini pia wanaweza kutoweka kabisa nchini na taifa likakosa fedha nyingi toka nchi za nje kwani kuna watu wanakuja hapa nchini kwa lengo la kuwaona samba tu au chui.
Uhifadhi wa wanyamapori una changamoto kubwa sana ambazo zinahitaji weledi wa hali ya juu katika kukabiliana nazo. Kwa sasa idadi ya tohe inaridhisha katika maeneo mengi wapatikanao wanyama hawa lakini bado sio jambo la kulinyamanzia au kulifumbia macho. Katika nchi ya Kongo wanyama hawa wana sadikika kuwa tayari wamesha toweka kabisa hasa kutokana na ujangili na uharibifu wa mazingira kitu ambacho kinalinyima taifa la Kongo fedha za kigeni ambazo zingeweza kupatikana kupitia uwepo wa wanyama hawa.
Napenda kutumia fursa hii kuipongeza wizara ya maliasili na utalii hasa kupitia mamlaka mbalimbali zinazo simamia uhifadhi wa wanyamapori kama TANAPA, TAWA na NCAA kwa kazi kubwa sana na yenye kutumia busara na weledi mkubwa katika kuhakikisha wanyamapori wetu wanaendelea kuwepo tena katika mazingira yao asili na tulivu. Kiukweli ni jukumu zito sana kuweza kuhifadhi na kusimamia sheria za wanyamapori kwani kuna migogoro mingi sana wanakutana nayo lakini pamoja na hayo hawajakata tamaa na bado shughuli ya uhifadhi inaendelea kama kawaida. PONGEZI SANA KWENU.
MWISHO
Mwisho wa makala hii ndio mwanzo wa makala nyingine. Hivyo nikusihi kuendelea kufuatilia makala hizi muhimu za wanyamapori na hata kama una ushauri, maswali au mchango wowote basi usisite kuwasiliana nami kupitia
Sadick Omary Hamisi
Simu: 0714116963/0765057969
Email: swideeq.so@gmail.com
Facebook: Sadicq Omary Kashushu
Instagram: @sadicqlegendary
Website: www.mtaalamu.net/wildlifetanzania
” I’M THE METALLIC LEGEND”