Hakika kuna wanyama wengi waliopambwa kwa rangi nzuri katika ngozi zao ambazo huvutia  kuwatazama wakati wa utalii mfano twiga, chui, duma, na ndegewenye rangi nzuri . Katika hao wote, pundamilia amewazidi wanyama wengine kwa rangi zake mbili yaani nyeupe na nyeusi Pundamilia ni wanyama jamii ya farasi wanaoishi mwituni, na wanakwato moja ngumu na miguu  mifupi kiasi. Zipo jamii tatu za Pundamilia ambao wanatofautiana kwa mpangilio wa mistari yao. Jamii hizo ni Pundamilia changarawe (grevy’s zebra), Pundamilia wa milimani  (mountain zebra), na Pundamilia wa kawaida ( plain zebra.)

 Kataka makala hii tutajifunza kuhusu Pundamilia wanaoishi maeneo ya wazi yasiyo na nyasi ndefu , miti mirefu na hawapendi miinuko mikubwa. Pundamilia ni mnyama rahisi sana kuonekana  mbugani kwani hupendelea maeneo yasiyo na nyasi ndefu au miti mirefu,  pia ni mnyama ambae asili yake ni Afrika. Pundamilia (plain zebra) wanapatikana sana nchini Tanzania na Kenya katika hifadhi mbali mbali. Mfano hifadhi ya Taifa Serengeri. Pundamilia wanaipa maajabu hifadhi hii wakati wanapohama pamoja na nyumbu (wilderbeast) kwenda hifadhi ya Maasai Mara  nchini kenya.

Pichani: Pundamilia changarawe (grevy zebra). Wanapatikana Nchini Ethiopia, kenya na somalia.( Wapo hatarini kutoweka).

Pichani: Pundamilia wa milimani (mountain zebra), wanauwezo mkubwa wa kuhimili joto na wanapatikana  nchini Afrika Kusini ( mountain zebra national park).

 

Pichani: Pundamilia anaeishi maeneo ya wazi (plain zebra)  wanapatikananchini Tanzania na kenya.

MATUMIZI YA RANGI YA PUNDAMILIA AKIWA MWITUNI

Pundamilia (plain zebra), ni mnyama mwenye rangi nyeupe iliyopambwa kwa mistari ya rangi nyeusi. Akiwa mchanga pundamila huanza na rangi nyeupe na badae vichocheo katika vinasaba ndani ya mwili hupendezesha kwa rangi nyeusi. Ajabu ya wanyama hawa ni kwamba kila pundamilia ana mpangilio wa kipekee katika rangi zake, yaani kama ilivo alama za vidole kwa binadamu. Namna michoro ya mistari haifanani kati ya Pundamilia mmoja na mwingine hata kama ni wa kundi moja na hii huwasaidia katika kutambua wakiwa kundini. Matokeo ya rangi hii inayopendeza ni kwasababu ya vichocheo katika vinasaba vyao na kutengeneza ngozi yenye rangi nyeupe huku ikipambwa kwa rangi nyeusi.

1. Rangi ya Pundamilia husaidia kuwachanganya maadui mwituni.

 Kundi la pundamilia wakiwa pamoja mwituni linatengeza sifa inayofahamika kama dazzle (rangi ya kung’aa kutokana na upekee wa rangi zao). Hivyo wanapotembea au wakiwa katika kuchunga pundamilia huwachanganya maadui zao kwa kutojua wapo wangapi, pia rangi hii hupekelea adui kama simba ambae mwenye shida ya kuona vizuri hasa wakati wa mchana kushindwa kuchagua yupi aweze kumkamata kwa urahisi. Pia wakati wa hatari Pundamilia hujikusanya pamoja, kutokana na rangi zao huwachanganya adui kwa kutojua wanaelekea upande gani  na kupata urahisi wa kumkwepa adui.

Pundamilia wanapohisi hatari wanakimbia kwa kujikusanya (motion blur) na sio kutawanyika kama ilivyo kwa nyumbu. Tabia hiyo hupelekea ugumu wa adui kushindwa kuchagua yupi amuweke katika windo lake.

Pichani: Pundamilia wakiwa wanakunywa maji  huku wakijipanga kwa ajili ya ulinzi.

Pia maadui hawa yaani simba, chui, duma na fisi huwinda kwa mahesabu kwa huangalia umbali, wingi  na ukubwa wa Pundamilia na wanyama wengine ili waweze kuwakamata kwa urahisi.

2. Husaidia  kurekebisha kiwango cha joto mwilini.

Rangi nyeupe katika mwili wa Pundamilia husaidia kuakisi mwanga na kufanya  kiwango kidogo cha joto kuingia mwilini na rangi nyeusi hufyonza joto na kuongeza joto mwilini. Hali hii humsadia kurekebisha kiwango cha joto hasa pale jua linapokuwa kali sana .

TABIA NYINGINE ZA MNYAMA PUNDAMILIA

Tofauti  na rangi , tabia nyingine za pundamilia ni kama ifuatavyo

  • Pundamilia anauwezo wa kutembea umbali mrefu hadi  kilomita 800. Pundamilia wanahama pia katika hifadhi zingine Mfano hifadhi ya Taifa Tarangiree na kwenda katika maeneo mbali mbali  karibu na hifadhi kupitia shoroba( corridor) mbalimbali hasa kipindi cha mvua kubwa kuepuka kwato zao kuoza na nyasi ndefu kwao sio rafiki sana Baada ya pundamilia hao kuhama katika hifadhi hiyo msimu wa masika huweza kurejea kipindi cha kiangazi.
  • Kundi la Pundamilia huongozwa na dume mkubwa (stallion). Wakati wa hatari yeye ndio hutoa taarifa kwa wengine  mfano masikio akiyalaza kwa upande wa nyuma, hii huonesha hatari hivyo wanakimbia.  Pundamilia akikamatwa na adui mfano kama simba, kiongozi huwaongoza wengine waje kupambana na adui ( wanaumoja).
  • Pundamilia ni mnyama ambae hafugiki hii inashangaza kwa kiasi fulani, vipi watu hawajawahi kufuga pundamilia, je ni mkorofi sana. Kwa hali iliyo ya kawaida Pundamilia ni mnyama jamii ya farasi, lakini hajawahi tumika na watu kwenye kusafirisha mizigo kama alivyo farasi (horse), na punda(donkey). Kwa sababu ya mabadiliko mbalimbali Pundamilia wamezoea kuishi katika makundi porini hivyo amekosa tabia za kujifunza kama ilivyo kwa farasi na punda wanaotumika kusafirisha mizigo au katika shughuli zingine.

Nakushukuru sana kwa kusoma Makala hii, endelea kujifunza kila siku kupitia makala hizi, pia usiache kumshirikisha na rafiki zako kuhusu Makala hizi. Makala hii pia imefanyiwa uhariri na Alphonce Msigwa, ambaye ni Mwikolojia Hifadhi za Taifa Tanzania.

Makala hii imeandikwa na ;

Shadrack Kamanga Andrea

Simu: +255 678 577 786

Email: bigstarshadrack@gmail.com.