Salamu sana ndugu zangu katika sekta yetu hii ya wanyamapori. Kwanza kabisa niombe radhi kwa kuwa kimya kwa muda mrefu kutokana na pirika pirika za maisha na misukosuko pia ya hapa na pale lakini yote hayo huja bila kutegemea. Ila kama ilivo ada ninapo pata wasaa basi sinabudi kuutumia muda vizuri angalau tukumbushane machache kuhusu wanyamapori na mazingira yao hali kadhalika uelekeo juu ya wanyama hawa.
Leo tutamuangalia mnyama mwingine ambae ni maarufu na kwa hakika hujulikana hata kwa watoto wadogo na mpaka kupewa jina la akiba kwa uhifadhi wa fedha za watoto. Je unataka kumjua mnyama huyu maarufu?, basi nikusihi uwe pamoja nami mwanzo mpaka mwisho wa makala hii au darasa hili huru la wnyamapori.
Na moja kwa moja leo tutamuona mnyama “TEMBO”
Kabla yakuanza kumzungumzia mnyama tembo basi ni vyema tukajua kwanza kuna aina ngapi za tembo. Hapa diniani kuna tembo wa aina mbili ambao ni
- Tembo wa Afrika na
- Tembo wa Asia.
Lakini hawa tembo wa Afrika pia wamegawanyika katika makundi mawili ambayo ni
- Tembo wa Savana na
- Tembo wa msituni.
Kwa ufahari na upendeleo hapa tutawazungumzia tembo wa barani Afrika ili watu wajue thamani na umuhimu wake kwa uchumi lakini pia umuhimu wa uwepo wa tembo kwa wanyama wengine.
UTANGULIZI
Tembo ni wanyama maarufu sana na kwa hakika huwa wana vutia sana kuwaangalia katika mazingira yao asilia hasa wanapokua kwenye kundi kubwa. Ni wanyama ambao ni rahisi sana kuwaona hasa unapokuwa katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori. Hii ni kwasababu wanyama hawa huwa wana tembea sehemu nyingi hasa wanapokuwa wanatafuta chakula. Umoja na mshikamano uliopo katika kundi la tembo hufanya wanyama hawa kuonekana hatari sana hasa pale mmoja wao anapopata matatizo au mtoto anapo shambuliwa na adui. Ni wanyama wenye thamani kubwa sana na ndiyo maana wamekuwa wakiwindwa sana kutokana na malighafi zilizopo katika miili yao.
SIFA NA TABIA ZA TEMBO WA AFRIKA
1.Tembo ndio wanyama wakubwa kuliko wanyama wote waishio nchi kavu
2.Tembo hawana uwezo wakuona mbali ila wana uwezo mkubwa sana wakunusa na kusikia.
3.Ni wanyama wenye hasira sana hasa wanapokuwa wanaumwa au pale wanapokua wanalea watoto.
4.Mkonga wa tembo una misuli zaidi ya 40,000 na hutumika kwa kazi mbali mbali kama kupumua,kukusanyia chakula,kunusa pia kunywea maji.
5.Tembo anapokuwa na hasira na kumkimbiza adui basi masikio yake huenda mbele na nyuma na hii inasemekana huwa anafanya hivyo ili kupunguza joto mwilini pale anapo kimbia.
6.Mawasiliano kwa tembo hufanyika kutumia sauti maalumu na utafiti unaonyesha kuwa sauti hii ina uwezo wa kusafiri mpaka kilometa 7 (sawa na maili 4.3)
7.Mbali na via vya uzazi, tembo dume na jike wana fanana sana kimaumbile lakini kuna utofauti mdogo kati ya kichwa cha dume na jike. Kichwa cha dume kinaumbo la duara kidogo wakati kichwa cha jike kina umbo la mraba kwa mbali.
8.Tembo wanapenda sana kuogelea kwenye maji lakini piakugalagala kwenye matope, hii huwasaidia kupunguza joto katika miili yao.
9.Tembo huwa wanaishi kwa makundi na kundi huwa linaongozwa na kina mama na kundi huwa na wanyama 20 mpaka 100.
10.Tembo ni wanyama ambao huishi kwa demokrasia sana kwani kabla yakuondoka husimama na kila kila mmoja kugeuka upande anaotaka kwenda, upande ambao utakuwa na idadi kubwa basi wengine wote hufata huko kwani wanakuwa wameshinda.
11.Tembo wana rangi ya kijivu ambayo kwa haraka haraka inaonekana kama nyeusi pale unao muangalia kwa mbali.
12.Tembo wana meno manne tu ndani ya mdomo (magego) ambayo ukubwa wake ni kama matofali madogo ya kuchoma kwa kila jino moja. Ikumbukwe pia tembo hana pembe mana walio wengi hudhani yale yalio tokeza nje ni mapembe, yale ni meno ambayo hukua kadri umri wa tembo unavyo ongezeka huwa haya simami kukua nayo. Na meno hayo yana weza mpaka kufikia urefu wa futi sita na zaidi.
13.Tembo ni wanyama ambao hutengeneza mazingira ya wanyama wengine hasa pale wanapo pita sehemu huacha wamevunja miti na vichaka hivyo kufanya eneo hilo kuwa makazi ya wanyama wengine wapatikanao katika eneo hilo.
14.Mbali na umbo lake kubwa na uzito mkubwa tembo huweza kukimbia umbali wa kilometa 49 kwa saa(40km/saa)
KIMO NA UZITO
Kimo=Tembo jike anaweza kufikia urefu wa futi kumi (futi 10) na tembo dume hurefuka hadi kufikia futi kumi na nne (futi 14)
Uzito= Tembo jike hufikia uzito wa kilogramu 7,000-10,000 ( sawa na tani 7-10) na tembo dume hufikia mpaka uzito wa kilogramu 9,000-14,000 ( sawa na tani 9-14)
CHAKULA
Tembo ni jamii ya wanyama walao majani na wana uwezo wakula aina mbali mbali za mimea na sehemu zake mfano majani, mizizi, magome ya miti, matawi na hata matunda pia. Kinacho wasaidia kutafuna magome ya miti ni magego yao makubwa na yenye nguvu sana.
Tembo ni wanyama wenye mfumo dhaifu sana wa mmeng’enye wa chakula. Hii hupelekea asilimia sitini (60%) ya chakula wanacho kula kuto meng’enywa na kutolewa nje kama kinyesi.
Sehemu yenye chakula cha kutosha tembo hula kilogramu 200-300 ambapo tafiti zinasema huwa anakula 5% ya uzito wa mwili wake na hutumia takribani masaa 16 hadi 17 kula ndani ya siku moja.
Tembo pia ana uwezo wa kunywa lita 200-250 za maji kwa siku.
UZALIANA
Baada ya kupandana tembo jike hukaa na mimba kwa takribani miezi 22 ( sawa na mwaka mmoja na miezi minane) na hapo huzaa mtoto mmoja ambae huwa na uzito wa kiligramu 68-135kg huku akiwa na urefu wa hadi futi tatu. Mtoto mara tu anapo zaliwa huwa hana nguvu na pia huwa hawezi hata kutumia mkonga wake lakini baada ya muda mfupi hupata nguvu na kuweza kuutumia mkonga wake. Wanapokuwa kwenye kundi mara nyingi watoto huwa wanawekwa katikati ili kuwakinga na maadui.
Moja kati ya shughuli na majukumu muhimu ya tembo jike katika kundi ni kuwatunza watoto mpaka pale watakapo kuwa wakubwa na kuweza kujitegemea.
Watoto wa kiume hufikia umri wa kupevuka wafikishapo myala 13 lakini katika umri huu huwa bado hawawezi kupanda majike mpaka pale wanapo fikia umri wa mwishoni wa miaka 20 ambapo wanakua na nguvu na kupambana na madume wakubwa.Endapo mtoto hato kufa basi tembo huzaa kila baada ya miaka 5.
Mara tu wanapo fikia umri wa kupevuka watoto wa kiume huondolewa kwenye kundi na kwenda kujiunga na kundi la madume ili kufundishwa kuwa majasiri lakini pia kupambana na maadui zao pia. Tembo dume hujiunga na kundi la kina mama mara tu unapofika msimu wa kuzaliana.
Maisha au umri wa tembo huenda sawia na umri wa binaadamu hivyo huweza kuishi kwa miaka mingi zaidi.
UHIFADHI
Tembo ni wanyama ambao wanakumbwa na misukosuko sana na kupelekea idadi kupungua sana kwa takribani miaka michache iliyo pita. Lakini kutokana na usimamizi mzuri na juhudi mbadala zimesaidia sana kuongeza idadi ya wanyama hawa. Kutokana na takwimu zilizo zungumziwa na shirika la umoja wa mataifa linalo shughulika na uhifadhi wa maumbileasili (International Union for Nature Conservation-IUCN) za mwaka 2005 zinasema kuwa angalau idadi ya wanyama hawa inaongezeka kwa asilimia 4% kwa mwaka.
Nchi kama Burundi, Gambia na Mauritania tembo ni wanyama ambao wametoweka kabisa huku nchini Swaziland wanyama hawa walikuwa wametoweka na sasa wamerudishwa tena ili kuwafanya wazaliane tena.
TISHIO KWA TEMBO WA AFRIKA HUSUSANI WA HAPA KWETU TANZANIA
1.Tishio kubwa sana kwa tembo wa Afrika ni ujangili uliyo kithiri kwenye maeneo ya uhifadhi wa wanyamapori. Tembo wanawindwa sana kutokana ma mahitaji ya meno yao pamoja na nyama kwani biashara haramu ya meno ya tembo na nyama inapelekea sana kuongezeka kwa ujangili.
2.Kwasasa kuna tishio lingine kubwa limeibuka ambalo ni uharibifu wa mazingira na ugawanyaji wa makazi kutokana na upanuzi wa aridhi kwa ajili ya makazi ya binaadamu.
3.Uwindaji haramu japo hii inazungumziwa sana hasa maeneo ya Afrika ya Kati.
4.Migogoro kati ya binaadamu na wanyamapori inapelekea sana kuuwawa kwa tembo kwani watu wamekuwa wakilima karibu na maeneo ya hifadhi za wanyamapori hivyo tembo wanapokula mazao hulazimika kuwauwa kwa kutumia bunduki au hata sumu pia.
5.Siasa ambazo hazina tija hasa kwa upande wa uhifadhi wa wanyamapori kwani wanasiasa waliyo wengi hawathamini kabisa shughuli hii ya uhifadhi na hii hupelekea jamii kutoona umuhimu wa wanyama hawa wakati wanaliingizia taifa fedha nyingi sana za kigeni.
NINI KIFANYIKE KUWANUSURU TEMBO WA AFRIKA HUSUSANI HAPA KWETU TANZANIA
1.Serikali ni lazima ipambane kuongeza idadi ya askari wanyamapori ili kuongeza ufanisi wa doria katika maeneo ya hifadhi. Serikali inunue vifaa au kamera maalumu ambavyo vitasaidia kuonesha matukio mengi yanayo jiri ndani ya hifadhi. Pia lazima ijitahidi kuongeza wataalamu wa uhifadhi wa wanyamapori ili kuongeza juhudi za kupambana na athari za upungufu wa tembo.
2.Waziri mwenye dhamana kupambana na uharibifu wa mazingira lakini pia uvamizi wa watu katika maeneo tengefu ya uhifadhi wa wanyamapori.
3.Migogoro baina ya wananchi na wanyamapori itafutiwe ufumbuzi mapema sana ili angalau kupunguza kuuwawa kwa tembo kwani wanyama hawa wamekuwa wakikumbwa na adha zakuuwawa kutokana na migogoro hii iliyo kithiri.
4.Wana siasa waache kabisa kuingiza siasa katika sekta ya uhifadhi wa wanyamapori kwani wao pia wamekuwa chanzo cha kuwafanya watu kuvamia maeneo ya uhifadhi wakidai maeneo haya ni ya watanzania hivyo wana uhuru wakuishi popote. Hii ni kwasababu tu wanataka kupata kura kwa wananchi huku wanasahau kwamba ipo siku watastaafu na kuachia madaraka wakati huo kama ni tembo wetu tayari wamekwisha toweka.
5.Serikali kupitia wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi iandae mtaala mahususi wa somo la uhifadhi wanyamapori mashuleni ili kuwafanya wanafunzi hawa watoto waweze kukuwa huku wakiwa na na upeo mzuri na kutambua thamani ya wanyamapori kwani msingi mzuri huanzia chini.
HITIMISHO
Suala la uhifadhi limekuwa halitiliwi maanani sana na viongozi walio wengi sana serikalini na kwa sisi wahifadhi kuona kama serikali haithamini kabisa umuhimu wa uhifadhi wakati ni dhahiri kwamba serikali kupitia Hifadhi za Taifa inaingiza pesa nyingi sana. Lakini swali la kujiuliza ni kwanini sekta hii haitiliwi maanani sana wakati ina mchango mkubwa sana kwenye pato la Taifa?
Hata ukichunguza bajeti ya mwaka 2017/2018 wizara ya maliasili na utalii ambayo ndiyo mlezi wa mamlaka za uhifadhi wa wanyamapori na misitu pia imepewa kiasi kidogo sana cha fedha za kuendeshea shughuli zake. Kweli sidhani kama hii itaweza kuendeleza chachu ya ufanyaji kazi kwenye mamlaka hizi japo watu wanajitolea sana angalau kunusuru wanyama wetu.
Kwa jicho la 3 hebu angalia mradi wa umeme unaohitajika kufanyika katika pori la akiba la SELUU (SELOUS GAME RESERVE) utakuwa na athari gani kwa tembo wa Seluu bali pia na wanyama wengine katika eneo lile. Hivi kweli wataalamu wa mazingira wameshakaa wakaona ni jinsi gani wanyama na mazingira yatakavyo athirika? wanajua mazingira yale ni mazalia ya viumbe wangapi?wanajua mazingira yale ni wanyama wangapi humia kama sehemu ya kupumzikia? Ngoja nikuache na maswali hayo machache.
Napenda sana kulipongeza shirika la hifadhi za taifa Tanzania (TANAPA) kwa kazi kubwa sana wanayo fanya kusimamia uhifadhi wa wanyamapori na kujitolea kwa hali na mali mbali na kukumbana na migogoro mingi sana toka kwa jamii zinazo zunguka hifadhi za taifa na wanasiasa pia.
Nisi isahau mamlaka ya hifadhi ya eneo la Ngorongoro pia kwa kazikubwa pia na mnavyo pambana kutunza wanyama hawa wasipotee lakini pia wasimamizi wote wa mapori ya akiba na maeneo mengine tengefu ya uhifadhi chini ya Tanzania Wildlife Authority (TAWA) kwa mchango wenu mkubwa na wakizalendo katika uhifadhi.
Na sisi watu binafsi kwa namna moja au nyingine tunao jitolea katika uhifadhi pia tuwe tayari kutoa msaada pale tutakapo hitajika kutoa msada huo au kufichua yale yaliyo jificha ili kuendeleza uwepo wa wanyamapori wetu.
Ahsanteni sana! Kwa mengi zaidi kuhusu wanyamapori ama ushauri juu ya makala hizi kuhusu wanyamapori wasiliana na mwandishi wa makala hii kwa namba zifuatazo
Sadick Omary
Simu – 0714116963/ 0765057969/ 0785813286
”I’M THE METALLIC LEGEND”