1. UTANGULIZI
Katika bara la Africa kuna nyoka wa aina nyingi sana kwa makundi yao. Lakini leo natamani tuangazie kidogo kuhusu aina hizi mbili za nyoka na utofauti wao yaani Koboko au Black Mamba pamoja na Fira au COBRA kwa lugha ya kiingereza.
Nia na madhumuni ya kuandika makala hii ni kutoa elimu kwa wafuatiliaji na wapenzi wa wanyama pori na jamii kwa ujumla wake kwa sababu ya Umaarufu wa nyoka hawa wawili duniani kote na Mkanganyiko mkubwa uliopo kwenye jamii yetu katika kuwatofautisha nyoka hawa wawili yaani Fira na Koboko.
2. MAMBO MUHIMU KUYAFAHAMU KUHUSU NYOKA HAWA WAWILI(Fira na Koboko)
Unapohitaji kuwafahamu nyoka hawa wawili kwa undani kuna taarifa muhimu zitakazokupa uelewa kuhusu nyoka hawa ili uweze kuelewa zaidi tutakapoingia kuwatofautisha.
A) Kwanza kabisa asili ya majina yao
FIRA/ SWILA (COBRA)
Hawa ni nyoka wenye sumu ambao wana wa nusufamilia Elapinae katika familia Elapidae. Kwa lugha za Ulaya huitwa “cobra” ambalo ni kifupi cha cobra de capelo, jina la Kireno lamaanishalo “nyoka mwenye ukaya”.
KOBOKO AU BLACK MAMBA
Hawa pia ni nyoka wenye sumu kutoka kwenye family ya elapidae na kisa cha kuitwa Black mamba ni kwa sababu ya weusi wa mdomo wake kama unavyoona pichani kwa kawaida nyoka hawa ngozi zao ni zenye rangi ya kijivu ila vinywa vyao ni vyeusi sana na hapa ndipo lilipotokea jina la Black mamba
B) Jambo la pili wacha tuangazie kuhusu mchanganuo wao wa kisayansi (Classification)
Jedwali no 1; Mchanganuo wa kisayansi kati ya nyoka Koboko na Swila
KOBOKO( BLACK MAMBA) | SWILA (COBRA) | |
KINGDOM | Animalia | Animalia |
PHYLUM | Chordata | Chordata |
CLASS | Reptilia | Reptilia |
ORDER | Squamata | Squamata |
SUB- ORDER | Serpentes | Serpentes |
FAMILY | Elapidae | Elapidae |
GENUS | Dendroaspis | Ophiophagus |
SPECIE | D. polylepis | O. hannah |
Kutoka kwenye jedwali namba 1 hapo juu tunaona kabisa kuwa nyoka hawa katika hatua nyingi za mchanganuo huu (classification) wamewekwa kwenye kundi moja hii inaashiria wamefanana vitu vingi sana katika namna ya tabia na maumbile yao.
B) Mambo yanayofanana kuhusu nyoka hawa wawili
i) Wote ni Reptilia, yaani mfumo wao wa uzalianaji ni wa kutaga mayai
ii) Wote ni jamii ya nyoka wenye sumu Kali kitaalamu wanaitwa Venomous snake wana sumu aina ya Neurotoxin sumu hii hulenga kuathiri sana mfumo wa fahamu (nervous system)
iii) Ishara zao za hatari pindi unapokutana nao Wote huwa wananyanyua vichwa vyao juu , wanatoa sauti ya onyo inayosikika kama tairi la baiskeli linavyotoa upepo (hissing sound)
3.Nyoka hawa wana namna wanatofautiana ki muonekano, Uwezo wao, pamoja na Ki Ikolojia (mazingira wanayopatikana)
A). KIMUONEKANO
Fira/ Swila mkubwa aliyekomaa huwa anakuwa mrefu na mzito kuliko Koboko aliyekomaa hii
Swila mkubwa wastani wa urefu wake ni mita 3.18 hadi mita 4 (futi 10.4 mpaka 13.1).
Wana uzito kuanzia kilo 5 hadi 10 inategemea na urefu na jinsia Mara nyingi madume ndo wanakuwa wakubwa na wazito zaidi
Swila mrefu zaidi aliyewahi kutokea alifika mpaka mita 5.85 yaani sawa na futi 19.2
Swila mzito zaidi kutokea alipatikana huko Royal Island Club nchini Singapore mnamo mwaka1951, aliyefikisha hadi kilo 12 mwenye urefu wa mita 4.8
Koboko mkubwa aliyekomaa ana wastani wa mita2 hadi 3 yaani sawa na futi 6 na inch 7 hadi futi 9 na inch 10
Uzito wao una wastani kati ya gramu 520 hadi kilo 1.03kg
Ukifuatilia vipimo hivi kwa makini utagundua kuwa Fira ni wakubwa kwa urefu na uzito tena kwa tofauti kubwa sana na Koboko
Katika nyoka wenye sumu (Venomous snakes) wa kwanza kwa ukubwa duniani ni Fira wa pili huwa ni Koboko halafu wengineo wanafuata hapa nazungumzia kwa upande wa nyoka wenye sumu tu.
Rangi ya ngozi zao
Koboko wao ngozi zao ni za rangi ya kijivu na huwa inakolea kuelekea kwenye kijivu yenye weusi (dark grey) kadri anavyozidi kuwa mkubwa ndivyo rangi yake inavyozidi kukolea vinywa vyao ni vyeusi sana hutakuta ana madoa wala mistari ya namna yoyote.
Fira wapo wa rangi tofauti tofauti kulingana na asili yake au inategemea na species. Unaweza kukuta ni mweusi ila ana mistari ya njano unaweza kukuta ana rangi ya kahawia au ya kaki kifupi wapo wenye rangi za aina nyingi na pichani ni baadhi tu.
B). UWEZO WAO
Mwendo kasi
Koboko anauwezo wa kukimbia kwa kasi zaidi kuliko Swila. Koboko anakimbia kwa kasi ya hadi 19 km/hr wakati Swila anaishia 12 km/ hr
Kurusha mate
Kuna makundi mawili makubwa ya Swila wanaoweza kurusha mate yao hawa wanaitwa (Spitting Cobras) na wasioweza kurusha mate hawa huitwa (Non spitting Cobras)
Swila hawa ambao ni spitting Cobras wanaweza kurusha mate tena wanalenga macho ya adui zao kwa usahihi mkubwa sana na hii unaweza kusababisha upofu kwa adui anaweza kuwa ni binadamu au ndege wakubwa wanaokula nyoka kama tai nk
Kitu ambacho koboko hawawezi
Madhara wanayoweza kusababisha
Koboko ni hatari zaidi kwa sababu anaweza kugonga Mara nyingi na kwa uharaka zaidi anaweza kugonga watu hadi 25 tena kaachilia dose ya uhakika ndani ya muda mfupi sana wasipotibiwa haraka wanaweza kupoteza maisha ndani ya dk 30 (nusu saa)
Swila ana uwezo wa kugonga hadi watu 10 na anaishiwa nguvu haraka sana ukilinganisha na Koboko japo nae sumu yake ni Kali sana kama ya koboko
Kutanua shingo
Swila na Koboko wote wakikasirika wana simama na kutanua shingo zao japo ya Swila hutanuka zaidi na hii ndio imempa kuwa tofauti yake na nyoka wengineo tazama picha hapo chini.
C). UTOFAUTI WA KI IKOLOJIA
Koboko wanapatikana Afrika pekee haswa maeneo yenye ukame yaani savana yenye nusu jangwa na yenye vichaka vichache pia maeneo haya yawe na miinuko yenye atitude si zaidi ya mita 1000 ,maeneo yenye miamba kuna wakati wanapatikana hata kwenye savanna zenye unyevu kiasi.
Hapa nyumbani Tanzania nyoka hawa wanapatikana sana mkoani Tabora, Shinyanga, Singida na Dodoma kwa sababu za kimazingira nilizozielea hapo juu.
Hawa pia wanaweza kutambaa chini kitaalamu ni (terrestrial) lakini pia unaweza kuwakuta juu ya miti kitaalamu kama (arboreal)
Swila/Fira wao hupatikana sana bara la asia haswa kusini na kusini-mashariki mwa bara hilo wao hukaa sehemu zenye miinuko yenye atitude ya mita 2000
Hawa wanatambaa chini peke yake.
Hizi ni baadhi ya tofauti ambazo Reptilia hawa wanazo najua zipo nyingi sana hata kiutamaduni wanavyotumika kiutamaduni na jamii tofauti n.k
Mwisho kabisa natamani jamii ielewe kuwa nyoka sio adui kama wengi walivyozoeshwa na mapokeo tofauti ya kidini na kimila kuwa wengine huamini nyoka ni shetani hii sio kweli nyoka ni kiumbe tena ni maliasili nzuri tu na kuna watu wanaendesha maisha yao kwa sababu ya uwepo wa nyoka hapa duniani kwa kuwafanyia tafiti, utalii, pia wana faida kubwa tu kwenye mnyororo wa ki ikolojia isipo kuwa tunapaswa kuishi nao kwa tahadhari kama tunavyoishi kwa tahadhari na wanyama wengine na sio vizuri kila unapokutana nao unawaua labda kama anataka kuleta madhara.
Vinginevyo tuwahifadhi ili kesho wanaweza kuleta faida kubwa kwenye jamii kupitia utalii n.k Ahsante
Imeandaliwa na
Amos. B. George
0765304204