Habari zenu tena ndugu katika makala hizi za wanyamapori lakini pia tunaliita darasa huru katika kujua wanyamapori na sifa zao kwa undani kidogo. Katika mfululizo huu leo tunaingia tena kuona machache kuhusu mnyama fulani machachari sana hasa awapo katika mazingira yake asilia.
Na bila kupoteza wakati leo tutamjua mnyama ajulikanae kama “MUHANGA” au “KUKUKIFUKU” (Aardvark).
Muhanga ni mnyama ambae kwakweli anavutia sana hasa ukimuona wakati ana pata chakula kwenye vichuguu kwani shughuli anayo kuwa anafanya ni hatari kwakweli na tunaweza sema huyu ndo komesha ya wadudu.
SIFA NA TABIA ZA MUHANGA
1.Ni mnyama ambae anafanana sana na nguruwe kwa kumtazama.
2.Ana kichwa kirefu, masikio marefu yaliyo simama na pua ndefu sana hasa hii humfananisha mnyama huyu na nguruwe.
3.Miguu ya nyuma ni mirefu kuliko miguu ya mbele.
4.Ana miguu na kucha vyenye nguvu sana na hii humsaidia kwenye kuchimba.
5.Ana rangi ya njano inayoelekea kuwa kama kijivu huku akiwa na manyoa mafupi kichwani, mkiani hali kadhalika kwenye miguu japo huwa marefu kidogo.
6.Muhanga kwa jina lingine hujulikana kama mla wadudu au nguruwe dunia au Kukukifuku
7.Ni mnyama ambae huishi kwa kujitenga na hukutana pamoja wakati wa kuzaliana tu.
8.Ni mnyama mwenye uwezo wa kuona sana usiku na hutumia muda huu kutafuta chakula. Hii pia humsaidia kuepukana na joto katika mashimo yao ya kujificha wakati wa usiku.
9.Hupendelea kuishi kwenye mashimo yenye urefu wa futi 6.5 hadi futi 42.
10.Ana vidole vinne katika kila mguu mmoja wa mbele huku miguu ya nyuma ikiwa na vidole vitano kila mmoja.
UZITO, KIMO UREFU WA MUHANGA
Uzito= Muhanga mkubwa hufikia uzito wa kilogramu 40kg – 65kg
Kimo= Hufikia kimo sentimita 60 – 65
Urefu= Muhanga mkubwa hufikia urefu wa inchi 43 -53 toka kichwani hadi mkiani.
MAZINGIRA
Muhanga ni mnyama ambaye anapatikana katika mazingira mbalimbali kuanzia maeneo yenye majani, misitu minene, misitu ya kawaida, savanna na hata misitu ya mvua katika maeneo yote ya Sahara.
Wanyama hawa hawapendelei sana maeneo yenye mawe kwasababu maeneo haya huwasumbua sana hasa wakati wa kuchimba kwani wanyama hawa huishi kwa kuchimba mashimo kama tulivyoona hapo juu, hawa ni wanyama ambao wanapenda sana kukaa kwenye mashimbo.
CHAKULA
Hawa ni wanyama ambao wanapendelea sana kula wadudu hasa mchwa kwenye vichuguu. Muhanga kwa mlo wa usiku mmoja anaweza kula wadudu hadi hamsini elfu ( 50,00). Ngozi yake nene humsaidia kuepuka maumivu ya kung’atwa na wadudu wakati wanakula hasa kwenye vichuguu.
Lakini wakati mwingine wamekuwa wakila baadhi ya mimea na hasa hupendelea pia kula matango na hasa kupelekea matango hayo kuitwa matango muhanga. Inasemekana hapa kuna mahusiano mazuri sana na kwa pamoja mimea hufaidika na muhanga pia hufaidika kwani muhanga hushiba kupitia matango lakini pia wakati anakula matango husaidia katika usambazaji wa mbegu za matango hivyo matango kuota maeneo mbalimbali.
Vitu vinavo msaidia muhanga ni miguu na kucha vyenye nguvu huku akiwa na ulimi wenye ute kama gundi na mrefu wenye kufika urefu wa hadi sentimita 30. Puani ana manyoa marefu ambayo humsaidia kuchuja vumbi hasa wakati anakula maeneo yenye vumbi.
Anakunywa maji kwa nadra sana na kwa asilimia kubwa maji huyapata toka kwa wadudu anao kula.
KUZALIANA
Kama tulivoona hapo juu wanyama hawa huishi kwa kujitenga kila mmoja na hukutana tu wakati wanataka kuzaliana. Mara tu baada ya kupandana jike na dume huendelea kila mmoja na maisha yake na jike hukaa na mimba kwa muda wa miezi saba na baada ya hapo huzaa mtoto mmoja tu.
Mtoto wa muhanga huzaliwa akiwa na uzito wa takribani kilogramu 2kg. Mtoto hukaa na kina mama kwenye mashimo bila kutoka nje kwa muda wa wiki 2. Mtoto wa muhanga hukuwa haraka sana na mara tu baada ya miezi sita mtoto huweza kuanza maisha yake mwenyewe. Baada ya miaka miwili kwa pamoja watoto majike na madume huweza kuanza kuzaliana pia.
UHIFADHI
Kwasasa wanyama hawa bado hawajawa tishio kutoweka dunuani kwani idadi yao bado haijajulikana rasmi. Japo tafiti zinaonyesha kuwa wanyama hawa wamepungua sana baadhi ya maeneo ya Afrika hususani maeneo ya Sahara.
MAADUI NA TISHIO KWA MUHANGA
Muhanga ni mnyama ambae ana maadui wengi sana msituni. Baadhi ya maadui hawa ni kama simba, chui, mbwa mwitu, fisi na chatu.
Binaadamu amekuwa akiripotiwa kuwa adui mkubwa kwa wanyama hawa kutokana na mahitaji ya nyama. Ujangili pia umekuwa ni tatizo kubwa sana hususani kwa maeneo ambayo hayana ulinzi wa kutosha ili kunusuru wanyama hawa.
Uharibifu wa mazingira pia unasababisha wanyama hawa kuhama baadhi ya maeneo na kutoweka kama tulivyoona hapo juu kuna baadhi ya maeneo wanyama hawa wamepungua kwa kiasi kikubwa sana.
NINI KIFANYIKE KUPAMBANA NA UPUNGUFU WA WANYAMA HAWA
Mpaka sasa hakuna hatua zozote za kihifadhi zilizo chukuliwa na mamlaka mbalimbali. Nadhani hii ni kutokana na kwamba wanyhama hawa bado hawajawa hatarini kutoweka ndio maana hawatiliwi maanani sana.
Hapa nadhani suluhisho kubwa hapa ni kupambana na ujangili pamoja na shughuli za kibinaadamu kwani mambo mengine yanayo pelekea kupungua kwa wanyama hawa ni ya kiasilia ambayo ni lazima yatokee. Maadui kama simba na chui hali kadhalika wengine huwala wanyama hawa kwani hii pia ni njia moja wapo ya kuweka sawa idadi ya wanyama hawa kutokana na mazingira kama ilivo muhimu kwa ikologia ya wanyama.
HITIMISHO
Wahenga wanasema ni muhimu kutunza kile ulichonacho wakati kikiwa na hali nzuri kabla hakijaanza kuingia hitilafu. Yaani kwa lugha rahisi ni sawa na kusema kinga ni bora kuliko tiba. Tujitahidi kuwanusuru au kuwatunza wanyama hawa kabla haijafikia hatua mbaya kama tunavyo pata shida kupambana na ujangili dhidi ya tembo.
Mashirika mbalimbali ya uhifadhi yasaidiane kufanya utafiti ili kugundua idadi halisi ya wanyama hawa kwani tunawza kusema tu wanapungua lakini hatujui wanapungua kwa kiasi gani. Endapo tutajua idadi halisi ya wanyama hawa basi itakuwa rahisi kutengeneza mikakati thabiti ya kupambana na upunguaji wa wanyama hawa.
AHSANTENI SANA
Kwa mengi na ushauri kuhusu wanyamapori lakini pia makala hizi wasiliana na mwandishi kupitia
Sadick Omary
Simu= 0714 116963 / 0765 057969 / 0785 813286
Email=swideeq.so@gmail.com
Au tembelea= www.mtaalamu.net/wildlifeta