Tanzania imebarikiwa kwa kuwa na bioanuai za aina mbalimbali kama vile mimea na wanyama . Miongoni mwa makundi ya wanyama ambayo nchi yetu imeweza kupewa kipaumbele cha kuwa makazi yake ni wanyama wanaokula nyama (kanivora). Fisi maji ni miongoni mwa aina 35 za wanyama wanaokula nyama ambao wanapatikana Tanzania. Fisimaji hawa wapo katika makundi kumi na tatu ulimwenginu, kati ya hayo matatu yapo Africa na mawili yanapatikana Tanzania. Aina ya fisi maji wanoapatikana Tanzania ni pamoja na  fisimaji madoa (spotted necked otter) na fisimaji mkubwa kijivu (African clawless otter). Jina hili la fisi maji limetokana na neno la kingereza “otter” ambapo  chimbuko la neno water maana yake maji kwa Kiswahili. Vile vile fisi maji wamepata jina hilo kutokana na maumbile yao kufanana na fisi na kuishi kwa kula na kutembea usiku kama fisi ila tu maisha yake kwa ujumla yanategemea maji. Chakula kikuu cha mnyama huyu ni samaki na uduvi japokuwa kuna wakati hulazimika kula vyura vyura.

Fisi maji madoa (Picha na Wozencraft, W.C. 2005)

Fisi maji wanapatikana katika maji yaliyo hai kwa maana ya maji  yenye mzunguko, masafi na pia yanasafirisha kwa urahisi hewa ya oksijeni. Vile vile maji yaliyo pekee na kuwe na umbali kidogo na mawe mawe iwe mtoni au ziwani. Kwa Tanzania Fisimaji wanapatikana kwenye maziwa mfano Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa. Mito mikubwa kama Ruaha na Kilombero, mabonde yenye ardhi oevu za kudumu kama vile Ngwazi Mufindi, pamoja na maeneo ya miinuko mikali yenye unyevu nyevu na upatikanaji wa chakula mzuri kama vile kwenye maporomoko ya Rungwe.

Fisi maji wa kijivu mkubwa  ( Picha na Wozencraft, W.C. 2005)

 Fisi maji ni viumbe tegemezi katika maeneo ya maji kwani uwepo wake katika maeneo yenye maji huashira ya kwamba maji hayo ni masafi uwepo wa viumbe hai vinavyoliwa na fisimaji pamoja na mwingiliano mdogo kutoka kwa jamii ya binadamu.

Fisimaji hutumia sana mashimo au majani makubwa pembezoni mwa chanzo cha maji kama maeneo yake ya malazi pamoja na mawe  kama maeneo yake ya kujikaushia. Fisimaji hapendi sana baridi, na ndio maana maeneo mengi ulimwenguni mabako kuna baridi kali huwezi kuwakuta wanyama hawa.

HATARI ZINAZOMKABILI FISIMAJI

Fisimaji wamekuwa wakipungua kwa kasi sana duniani licha ya kuwa viumbe vyenye kupendeza na kutegemea sana maisha yao kwenye maji. Upo mwingiliano mkubwa baina ya Fisimaji na binadamu hususani wavuvi, uliopelekea kuuwawa kwa wingi aidha kwa kuwindwa au kujinyonga na mitego ya nyavu zinazotumiwa na wavuvi kwa ajili ya kuvua samaki. Mgogoro baina ya fisimaji na wavuvi  unatokana na fisimaji kula samaki na kupelekea wavuvi kuona kama uwepo wa fisimaji utapunguza sana samaki nao kupata hasara. Changamoto nyingine ni mila potofu juu ya fisimaji, ambpo baadhi ya mila hizo ni waganga wa jadi kusema fisimaji ana mzizi ambao huutumia kujipatia samaki hivyo basi yeyote atake muua na kuupata huo mzizi atakuwa tajiri. Wengine husema ngozi ya fisimaji hutibu kifafa endapo mtoto atalala juu yake na akifungwa kama cheni kwenye mkono wake. Wapo walioenda mbali zaidi kwa kusema fisimaji anaongeza nguvu za kiume, hivyo nyama au supu ya uume wa fisimaji imekuwa hitaji la wanaume wengi maeneo wanapotakina na kupelekea msako na mawindo mkubwa ya fisimaji. Jambo jingine ni kukauka kwa vyanzo vya maji kutokana na mabdadiliko ya tabia ya nchi, kuchafuka kwa maji kwa kuvamiwa na wakulima wanaotumia sumu kuua wadudu au mbolea za kemikali kukuza mazao hususani mboga mboga na matunda.

Hivyo basi ili kupunguza hatari hizi na zingine ambazo zinawakabili wanyama hawa jamii ya fisimaji ni muhimu maboresho katika matumizi bora ya ardhi katika nchi yetu na usimamizi wa rasilimali zetu unao husisha jamii ya chini kabisa mpaka viongozi wa juu serikalini uboreshwe. Uwepo wa utoaji elimu kwa wakulima, wavuvi na na wanajii wote  kuhusu umuhimu wa viumbe hawa na madhara yakuwaua bila mpangilio itaongeza mafanikio katika kuhifadhi wanyama hawa.  Ikumbukwe wanyama hawa wapo katika ngazi ya juu kabisa ya mfumo wa chakula (top of the food chain) kwa maana ya kwamba wanaweza kuwa wa kwanza kupotea kwenye mazingiria endapo chochote kisicho sawa kitaendelea katika maeneo wanayo ishi.

Naamini umepata mambo mazuri katika makala hii kuhusu fisimaji, nawakaribisha kwa maswali, maoni na ushauri ili kubioresha Zaidi kazi zetu, pia usisite kuwashirikisha wengine maarifa haya muhimu ili kwa pamoja tushiriki katika uhifadhi wa fisimaji..

Shukrani za pekee kwa Alphonce Msigwa (alphonce84@yahoo.com ), Mwikologia hifadhi za taifa Tanzania kwa kuhariri Makala hii.

Makala hii imeandikwa na:

Mr. Martin J Bayo.

M.Sc. Wildlife Management and Conservation.

B.Sc. Wildlife Management.

SOKOINE UNIVERSITY OF AGRICULTURE

P.O BOX 3073

EMAIL; josephmartin592@gmail.com

MOBILE NO; +255762181639