Papa Potwe ni samaki mkubwa baharini ingawa wengi wetu hupinga na kusema kuwa Nyangumi ndiye samaki mkubwa lakini Nyangumi ni Mamalia na sababu hii inamuacha Papa Potwe bila mpinzani.

Papa Potwe hujulikana kama ‘Whale shark’ kwa lugha ya kiingereza na jina lake la kisayansi ni RHINCODON TYPHUS.

Samaki huyu mkubwa anaurefu wa futi 18-32.8 na anauzito wa wastani, ton 20.6; kiuhalisia Papa Potwe analingana na Daladala!

Papa Potwe anauwezo wakuishi miaka 70 akiwa chini ya uangaliz wa binadamu. 

Papa Potwe tofauti na samaki wengine wakubwa yeye hula dagaa na vimelea ambao huingia mdomoni mwake na kuchujwa.

Picha hii inaonyesha Papa potwe akila samaki wadogo; picha hiiimepigwa na info@tanzaniaodyssey.com

Tabia hii ya ulaji wa Potwe huwezesha ikolojia ya baharini kuwa katika uiano mzuri. kwani kama si hivyo potwe angemaliza samaki wote na yeye mwenyewe kufa kwa njaa na vilevile binadamu asingepata kitoweo.

Papa potwe hupatikana katika nchi zenye hali ya hewa ya kitropiki kama vile Australia, Ufilipino ,Msumbiji, Eucador ,Indonesia na Tanzania.

Kwa Tanzania papa potwe hupatikana katika kisiwa cha Mafia, katika Pwani ya Magharibi kati ya Kilindini na rasi Mbisi.

Uwepo wa papa potwe katika  kisiwa cha Mafia umeleta umaarufu mkubwa kwa nchi yetu pamoja na faida kemkem kama Ajira , kuongezeka kwa pato la Taifa ,kukua kwa sekta ya uvuvi na utalii,kuwepo kwa miundombinu bora katika kisiwa cha Mafia haya yote yamechangia maendeleo ya Tanzania kwa ujumla.

Pichani ni waogeleaji wakiogelea karibu na papa potwe;picha hii imepigwa na Simon Pierce

Papa Potwe huonekana kwa urahisi kati ya mwezi Oktoba na Machi katika kipindi hiki watali hufurika ili kumuona samaki huyu mkubwa.

Papa Potwe huitwa Papa Mwema na wakazi wa Mafia hii ni kutokana na tabia yake ya upole ukilinganisha na papa wengine ambao wamekua wakidhuru na kula watu.

Lakini Mambo yamekuwa tofauti kwa Papa Potwe kwani yeye ni mkarimu kiasi kwamba binadamu anauwezo wa kuogelea nae kwa karibu sana bila kupatwa na dhara lolote.

Wema wa Papa Potwe umekua ukisimuliwa sana na wavuvi ambao wao hujipatia samaki wengi kutokana na tabia ya Potwe kuzuru pwani akiwa na makundi ya samaki wengi wadogo.

Papa Potwe anauwezo wa kusafiri hadi kilomita 10,000. Hii inamuweka samaki Potwe katika changamoto mbalimbali na kumfanya kuwa miongoni mwa viumbe vilivyopo hatarini kutoweka .

Hitimisho

Juhudi za makusudi zimekuwa zikifanyika na Hifadhi ya Bahari ya Mafia pamoja na wavuvi katika kisiwa cha Mafia ili kuhakikisha vizazi vijavyo vinapata fursa ya kumshudia na kupata kheri za samaki huyu mkubwa.

Pamoja na hayo ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha anatunza mazingira haswa ya baharini na kuwa chachu kwa wengine ili sote tuweze kujivunia uwepo wa Papa Potwe katika kisiwa cha Mafia.

Ahsante sana kwa kusoma Makala hii, jiandae kwa Makala nyingine bora kabisa.

Makala hii imeandikwa na

Maureen FN Daffa

+255 626 331 871

maureen.nic08@gmail.com