vulture

Habari ndugu msomaji na mfuatiliaji wa blogu hii ya wildlife Tanzania. Leo nimekuandalia mambo mazuri niliyojifunza hivi karibuni kuhusu Tumbusi, tumbusi kama wengi wanavyo mfahamu, huyu ni ndege jamii ya tai, au ndege wala mizoga. Hawa ni ndege wa kipekee sana na wapo aina zaidi ya 22 duniani kote, lakini kwa tafiti za hivi karibuni zimebaini na aina 15 tu. Katika mafunzo tuliyoyapata hivi karibuni kuhusu ndege hawa kwa undani wake, nimeona ni mafunzo na masomo ambayo mtanzania yeyote hapaswi kuyakosa kuyafahamu. Hivo basi baada ya kujifunza vizuri ndege hawa nimekaa chini na kuandika ili nikushirikishe na wewe ndugu yangu upate ufahamu ambao najua utakuwa na matokeo mazuri yenye tija kwa kuendelea kuwepo kwa ndege hawa.

Haya ninayokushirikisha hapa ni machache kati ya mengi tuliyojifunza, ila nitakupa yale ya muhimu zaidi na ya msingi kuyaelewa kwa urahisi. Kwa historia tumbusi ni ndege wenye historia ya pekee nay a ajabu sana kuliko ndege wengine, wana historia na mahusiano mazuri kati ya watu na Wanyama wa kufugwa na pia wanyamapori. Katika mafunzo yaliyotolewa na Shirika la Uhifadhi wa wanyamapori duniani ( Wildlife Conservation Society, WCS) jinsi ya kuwatambua tambusi, umuhimu wa kuwahifadhi na changamoto wanazokutana nazo.

Ndege hawa kwa asilimia kubwa wanaishi ndani ya hifadhi za taifa na sehemu nyingine zenye mapori yaliyohifadhiwa kwa ajili ya viumbe hai na maliasili nyingine. Ndege hawa kama wanavyojulikana na watu wengi hasa wafugaji ambao kwa asilimia kubwa huishi karibu na hifadhi za wanymapori na kwenye mapori yaliyohifadhiwa wanajulikana kama ndege wala mizoga. Ni kweli ndege hawa hula mizoga sana. Kama nilivyokwambia hapo juu kwamba ndege hawa wanaishi sana hifadhini, na baadhi yao hupenda kuishi kwenye makundi yanayofikia hadi 60 kwa mara moja. Asili ndio inayosema chakula wanachokula, kwa kuwa wapo hifadhini basi hawawi mbali na mizoga au sehemu ambazo simba au uwindaji napotokea.

Ndege hawa wanafaida nyingi sana kwa hifadhi na kwa jamii pia, kwa Tanzania tafiti nyingi za ndege hawa bado hazijafanyika hasa maeneo ya hifadhi za kusini, hivyo kuna taarifa chache tu za hifadhi za kusini mwa Tanzania na taarifa nyingine ni kutoka hifadhi ya taifa ya Serengeti na Masaimara. Hivyo basi hii ni fursa pekee kwa watalaamu wengine na watafiti wa sekta hii kugeuzia macho yao kwenye utafiti wa ndege hawa. Kwa nchi nyingine kama Rusia na India kuna tafiti nyingi zimefanywa kuhusu ndege hawa lakini kwa hapa kwetu ndio tunaanza. Mara zote tunapojifunza masuala ya ikologia ya Wanyama na mazingira, unakuta kunakuwa na muunganiko wa moja kwa moja na wa muhimu kwa ndege kama tumbusi na simba, mbwa mwitu, duma, chui,na wanyama wengine nk.  Pamoja na hayo tumbusi wanafaida nyingi sana kwa baadhi tu nitaziweka hapa;

Sabuni ya savanna

Utashangaa kama nilivyoshangaa mimi, ndege hawa wanasababu ya kuitwa ni sabauni ya savanna, yani ni sabuni ya hifadhini. Hii ikiwa na maana kwamba endapo kuna mzoga wa mnyama yeyote amekufa hifadhini ndege hawa huenda na kula mzoga wote na kubakiza mifupa ikiwa haina nyama hata kidogo, hivyo husafisha hifadhi dhidi ya wanyama wanaokufa au kuuliwa na wanyama wengine au majangili. Kizuri zaidi ni kwamba endapo mnyama amekufa kwa ugojwa kama kimeta, kichaa cha mbwa au magonjwa mengine, ndege huyu anapokuja kula ule mzoga wa  mnyama huyo hapati madhara yoyote, kwa sababu ndani ya ndege huyu kwenye mfumo wa umeng’enyaji wa chakula na maji umetengenezwa kwa namna ambayo vijidudu vyote vya magojwa ya kuambukiza vinafia ndani ya tumbo la ndege hawa hivyo kupunguza magonjwa ya kuambukizwa kwa wanyama na ndege wengine. Hii ndio faida ya tambusi kwenye hifadhi.  Kwa wanyama wengine wanaokula nyama au mizoga wendapo watakula mzoga wenye vijidudu vya magonjwa kama ya kichaa cha mbwa nakimeta hawana mfumo wa kuua vijidudu hivi vikiwa ndani ya matumbo yao hivyo wanapojisaidia huacha kinyesi chenye asilimia kubwa ya vijidudu hivi ambavyo husambaa na kwenda kuambukiza wanyama wengine wa kufugwa na waporini. Ndege hawa wana uwezo wa kula asilimia 70 ya mzoga wote ulioachwa na fisi na bweha.

Faida ya kitamaduni

Hapa tumbusi walikuwa wakitumika na hadi sasa kuna baadhi ya nchi na jamii duniani zina Imani na ndege hawa kwenye mambo ya maziko. Mfano nchi ya Misri na baadhi ya nchi nyingine duniani mtu anapokufa wanamuweka nje ya mji juu ya kichanja au kwenye jiwe, au sehemu yoyote juu kabisa kwenye milima na kumuacha hapo, hivyo tumbusi wanakuja na kuona miili ya watu waliokufa imewekwa juu wanaila yote, bila kubakisha chochote, hivyo watu hufikiri kuwa mtu huyo amekwenda mbinguni wanapokuja na kukosa maiti au mzoga wa mtu huyo aliyekufa. Hi ndio jinsi watu wanavyohusianisha tumbusi na maswala ya Imani na tamaduni.

Rafiki mkubwa wa askari wa wanyamapori

Kwa wale askari na watu wengine wanaofanya utafiti porini au katika hifadhi, huwa njia ya uhakika sana kujua endapo kuna mahali kuna mzoga ndani ya hifadhi huangalia tambusi wapo sehemu gani, endapo wataonekana kukusanyana na kuruka sehemu moja ujue hapo lazima pana mzoga hivyo husaidia askari wa wanymapori kufika kwa urahisi eneo la tukio. Hivyo husaidia sana kuonyesha maeneo yenye mizoga na hivyo kurahisisha kazi yao na kujua endpo mzoga huo umesababishwa na majangili au umeuliwa na simba. Hii yote husaidia kufuatilia maeneo yote  yenye changamoto za ujangili ndani ya hifadhi. Hata kwa watafiti wanapotaka kufanya utafiti wa wanyama hawa huwa sehemu nzuri kuwaona ni sehemu yenye mzoga. Hivyo wanaweza kutumia mbinu mbali mbali kuwashika na kufanyai utafiti

Mwisho, kuna mengi sana ya kuandika kuhusu tumbusi, lakini kwa haya machache unaweza kuona umuhimu wa tumbusi kwenye hifadhi zetu. Licha ya kwamba tumbusi wanafaida ndini ya hifadhi lakini pia hata nje ya hifadhi, wafugaji hutumia sana ndege hawa kutafuta mifugo iliyopotea na hata mfugo unapokufa ndege hawa huja na kula mzoga wote hivyo kufanya mazingira kuwa safi na huweza kuzuia sana magojwa hasa ya kuambukizaa. Hivyo ndege hawa ni afya ya watu na Wanyama pai.

Wito wangu kwa watanzania wote, tumewajua ndege hawa angalau kwa uchache, havyo basi popote ale tulipo na tunapoishi tusiwauwe ndege hawa wenye kazi kuu ndani na nje hii ya hifadhi. Tuwtunze tuwaache wanafaida sana, kumbuka ndege hawa hula mizoga hivyo unapoweka sumu kwenye mzoga kwa bahati mbaya au bahati nzuri, unawaua ndege hawa, unapoona mzoga wa ngombe au mnyama yeyote, usiwashauri watu kuweka sumu, kwani inamadhara makubwa sana hata kwa afya zetu pia.

Makala hii imeandikwa na;

Hillary Mrosso

hillarymrosso@rocketmail.com