Habari msomaji wa makala za Wildlife Tanzania, karibu kwenye makala yetu ya leo ambapo tunaendelea na uchambuzi wa sheria namba 5 ya mwaka 2009 ya Uhifadhi wa Wanyamapori, ambapo tulikuwa tunajifunza sehemu ya Saba ya sheria hii ambayo inaelezea matumizi ya wanyamapori yaani (consumptive and non-consumptive). Hapa tumejifunza kwa ujumla wake jinsi sheria inavyoelekeza dhana nzima ya matumiza ya maliasili, utoaji wa vibali vya uwindaji, masharti ya uwindaji na masharti ya kumiliki silaha za uwindaji kama vile bunduki, mchakato mzima wa kuendesha shughuli zote za uwindaji kwenye vitalu vya uwindaji, masharti ya kuzingatia wakati wa kutekeleza masula mbali mbali kwa mujibu wa sheria.

Pia kwa kuwa nimepanga kuchambua kila kilichomo kwenye sheria hii ili kila mmoja wetu apate ufahamu na kujifunza mambo mbali mbali yaliyomo kwenye sheria hii kwa lugha rahisi. Hivyo Rafiki karibu sana kwenye mwendelezo wa makala hii inayochambua sehemu ya saba ya sheria hii ya uhifadhi wa wanyamapori Tanzania. Tutaendelea kuchambua kifungu cha 44.

  1. –(1) Nyara na uwindaji kwa ajili ya matumizi ya kujikimu unatakiwa kufanyika kwa namna ambayo imeelezwa kwenye kanuni ambazo zimetungwa na Waziri na kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali. Hivyo uwindaji wote kwa ajili ya nyama au chakula unatakiwa kkufanyika kwa mujibu wa sheria hii, na pia unatakiwa mchakato mzima wa kufanya uwindaji huu uchapishwe kwenye Gazeti la serikali ili kila mtu apate kujua kinachoendelea.

(2) Waziri ataanzisha kamati ambayo inajumuisha watu wenye weledi na utalaamu unaotakiwa kwenye masuala yanayohusiana na usimamizi wa wanyamapori, kwa kusudi la kumshauri Mkurugenzi kuhusu kutenga maeneo maalumu au kutoa idadi ya maeneo yatakayotumika kwa ajili ya uwindaji, na pia atakuwa anayapitia maeneo hayo. Hapa anaeleza kwamba Waziri ataunda kamati ambayo itakuwa inamshauri Mkurugenzi wa wanyamapori kwenye masula ya uwindaji wa kienyeji, na kamati hii itajumuisha watu wenye utalaamu wa masula ya uhifadhi wa wanyamapori na pia mwenye uzoefu kwenye sekta hii.

Upatikanaji wa wanyamapori kwa Jamii za Kimila

(Access to wildlife by traditional community)

Katika kifungu hiki cha sheria kinaeleza namna jamii za kimila zinavyoweza kupata maeneo maalumu kwa ajili ya wanyamapori.

45.- (1) Waziri anaweza, baada ya kutoa taarifa kwenye Gazeti la Serikali, anaweza kutangza jamii yoyote kuwa jamii ya kimila kwa kusudi la sheria hii na kuamuru masharti na kanuni zinazosimamia matumizi ya wanyamapori. Hivyo waziri ana nguvu ya kuitangaza jamii yoyote ile kuwa jamii ya kimila ili kutoa fursa kwa jamii husika kushiriki kwenye matumizi ya wanyamapori kwa mujibu wa sheria na mapendekezo mengine muhimu.

(2) Mkurugenzi anaweza kutoa kwa jamii za kimila lesseni ya kuwinda wanyamapori kwa kiasi fulani cha wanyama kama inavyotakiwa kwa vigezo vya kanuni na vigezo vilivyoanishwa kwenye lesseni.

(3) Waziri anaweza, baada ya kutoa taarifa kwenye Gazeti la serikali, kuandaa eneo la ardhi kwa ajili ya kuwa eneo la wanajamii kwa ajili ya uwindji na masharti na namna nzuri za kufanya uwindaji wa wanyama kwa maeneo kwa wazawa.

(4) Kila uwindaji kwa ajili ya kujikimu, baada ya siku thelethini za uwindaji wa wanyama, watazitunza vizuri Ngozi na nyara nyingine za mnyama huyo au nyara nyingine na kuhakikisha kwamba Ngozi na nyara zinakabidhiwa kwa wahusika au ofisa wa lesseni na pia wahusika wanaochukua nyara au ofisa wa lesseni atahakikisha nyara hizo zinasajiliwa kwa mujibu wa sheria. Katika kuhakikisha usimamizi wa nyara za serikali, baada ya uwindaji kufanyika na wazawa au wakazi walioruhusiwa kuwinda kwenye maeneo husika, kitawasilishwa kwa mamlaka husika kwa ajili ya serikali.

  1. Bila kuathiri mapendekezo yaliyotolewa na sehemu hii, kila lesseni ya uwindaji inatakiwa kuonyesha aina ya spishi na idadi iliyoonyweshwa au wanyama waliopo kwenye jedwali, ambao kisheria wanatakiwa kuwindwa na muhusika na inatakiwa kuwa halali kwa kipindi chote kama itakavyoamururiwa. Hapa sheria inaelezea kuwa lesseni zote ambazo zitatolewa kwa wawindaji wa aina hii zinatakiwa kuonyesha aina ya mnyama ambaye atawindwa na pia idadi ya wanyama watakao windwa kwa mujibu wa sehemu hii ya sheria.
  2. Mtu yeyote ambaye-

(a) sio mmiliki wa lesseni ya uwindaji, akawinda, kuua au kujeruhi mnyama yeyote aliyeainishwa au mnyama aliyetajwa kwenye jedwali; au

(b) akawa mmiliki wa lesseni ya uwindaji, kuwinda, kuua, au kujeruhi-

(i) mnyama aliyeainishwa au aliye kwenye jedwali la spishi, aina,au maelezo mengine ambayo yameelezwa kwenye lesseni;

(ii) idadi ya wanyama walioainishwa waliopo kwenye jedwali kuwa kubwa kuliko ya idadi iliyoidhinishwa na mamlaka kwenye lesseni ya uwindaji;

(iii) mnyama aliyeainishwa au aliyetengwa kwenye jedwali sehemu nyingine tofauti na jinsi ilivyoelezwa kwenye lesseni anafanya kosa na atakuwa na hatia kwa kufanya hivyo-

(aa) kwa kesi ambayo muhusika atahusishwa na uwindaji au uuaji wa mnyama ambaye ametajwa kwenye Sehemu I ya Jedwali la Kwanza ya Sheria hii, atahukumiwa kifungo jela kwa muda usiopungua miaka mitatu lakini isizidi miaka kumi na mahakama inaweza kumwongezea adhabu ya kulipa faini isiyopungua mara mbili ya thamani ya mnyama aliyemuwinda;

(bb) kwa kesi ambayo inahusisha uwindaji au uuaji wa mnyama ambaye ametajwa kwenye Sehemu II ya Jedwali la Kwanza la Sheria hii, atahukumiwa kifungo jela kisichopungua miaka miwili lakini kisichozidi miaka mitano na mahakama inaweza kumwongezea adhabu nyingine ya kulipa faini isiyopungua mara mbili ya thamani ya mnyama aliyewindwa au kuuwawa.

(cc) kwa kesi inayohusisha uwindaji au uuaji wa wanyama ambao wametajwa kwenye Sehemu III ya Jedwali la Kwanza la Sheria hii, atahukumiwa kifungo jela kisichopungua miezi kumi na mbili lakini isizidi miaka mitatu, na pia mahakama inaweza kuongeza adhabu ya kulipa faini isiyopungua mara mbili ya thamanai ya mnyama aliyewindwa au kuuwawa; au

(dd) kwa kosa au hatia inayohusisha kujeruhiwa kwa mnyama, atahukumiwa kutoa faini isiyopungua mara mbili ya thamani ya mnyama au kwenda jela kwa kifungo kisichopungua miezi kumi na mbili.

Lesseni ya utalaamu au ubobezi kwenye masuala ya uwindaji (Professional hunter Licence)

Katika kipengele hiki sheria inaelezea watalamu wa kuwinda ambao wanajulikana na kutambuliwa na sheria hii kama watalaamu au wabobezi kwenye maswala ya kuwinda, kulenga shabaha kwa kimombo au kingereza wanajulikana kama “Professional Hunters” ambao wana cheti na lesseni ya ubobezi kwenye masuala ya uwindaji.

  1. –(1) Mtu yeyote hatafanya kazi kama mtalaamu mwindaji (professional hunter) kama hana lesseni ya utalaamu wa kuwinda ambayo inatolewa kwa mujibu wa sheria hii.

(2) Mkurugenzi hatatoa lesseni ya ubobezi au utalaamu katika maswala ya uwindaji (professional hunter) kwa mwombaji isipokuwa amejiridhisha kwamba mwombaji-

(a) ana umri zaidi ya miaka ishirini na tatu;

(b) ametunukiwa cheti cha ubobezi au utalaamu kwenye maswala ya uwindaji (professional hunter) kutoka katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori au kwenye taasisi nyingine ya wanyamapori inayojulikana na ana uelewa wa kutosha kuhusu Sheria hii,sheria nyingine na makubaliano ya kimataifa kuhusu uthibiti na usimamizi wa viwanda vya uwindaji au biashara ya uwindaji;

(c ) awe amepitia mafunzo ya miaka mitatu ya uangalizi na katika kampuni ya utaii wa uwindaji inayojulikana; na

(d) awe amefaulu kila zoezi na mitihani aliyokuwa anafanya na kupewa kama inavyohitajika.

(3) Lesseni ya utalaamu katika maswala ya uwindaji inatakiwa kugawanyika katika sehemu mbili kama ifuatavyo;

(a) sehemu A ambayo itamruhusu mwenye lesseni kuwa msimamizi wa uwindaji wa wanyama wowote; na

(b) sehemu B ambayo itaruhusu mwenye lesseni ya uwindaji kusimamia uwindaji wa wanyama ambao sio hatari.

(4) Mtaalamu wa uwindaji mwenye lesseni atahusika pia kusimamia uwindaji wa mnyama yoyote aliyeruhusiwa na sheria hii na kuongoza kwenye uwindaji wowote wa nyara kulingana na Sheria hii au sheria nyingine zinazohusika.

(5) Kampuni yoyote ya uwindaji inatakiwa kuhakikisha kwamba kiasi cha chini cha wazawa ambao ni wataalamu wa masuala ya uwindaji isiwe chini ya asilimia kumi na tano kwa muda wowote ule.

(6) Sehemu hii ya kifungu cha sheria haitahusisha kipindi maalumu cha miaka mitatu  kabla ya kufanya malipo ambacho makampuni ya uwindaji yatakuwa yanatoa mafunzo kwa wanafunzi. Hapa inamaana kuwa katika kipindi hiki ambacho makampuni ya uwindaji yanatoa mafunzo na kwa wataalamu kwenye masuala ya uwindaji. Kipindi hiki cha miaka mitatu ambacho kifungu hiki cha sheria kinazungumzia kinaitwa kwa kimombo au kingereza “grace period”.

Lesseni kwa wataalamu wa uwindaji wasio wazawa (Professional Hunter licence for non-citizen)

Kwenye kipengele hiki cha sheria kinaelezea umiliki wa lesseni ya uwindaji kwa watalaamu ambao sio watanzania au wasio wazawa, sheria hii inaeleza masharti ya kufuata kwa watalaamu wasio wazawa.

49.-(1) Lesseni ya uwindaji kwa watalaamu ambao sio wazawa inatakiwa kuidhinishwa na mwajiri wa mwindaji, ambaye ndiye aliyeidhinishwa kwenye kibali cha kufanya kazi, sawa na masharti yaliyotamkwa kwenye kifungu cha 47. Kwa hiyo hapa wataalamu wa masuala ya uwindaji ambao sio wazawa wanatakiwa kuelewa mfumo huu wa ufanyaji kazi kwenye kampuni ya uwindaji sawa sawa na masharti na mapendekezo ya sheria hii.

(2) Pale ambapo mabadiliko yoyote ya mwajiri wa mtaalamu kwenye masuala ya uwindaji kwa ambao sio wazawa itakapotokea, lesseni ya mtalaamu wa uwindaji itakuwa sio halali na inatakiwa kuikabidhiwa kwa Mkurugenzi ndani ya siku kumi na nne ya mabadiliko hayo. Hapa sheria inaeleza namna ambavyo mabadiliko ya mwajiri yanaweza kuathiri lesseni ya mtaalamu wa uwindaji aliyemwajiri. Hivyo mabadiliko yoyote yale yatapelekea lesseni hiyo kukosa uhalali wa kufanya kazi kisheria.

(3) Pale ambapo lesseni ya utalaamu wa uwindaji itakapokuwa sio halali au itakapokosa uhalali, lesseni nyingine ya utalaamu wa uwindaji inaweza kuombwa, kwa kusudi la kuidhinisha jina la mwajiri mpya, na pia lesseni hii inaweza kutolewa bila kuhitajika kwa majaribio, au bila kuwepo kwa majaribio. Hivyo kama mabadiliko ya mwajiri yatakapotokea na kusababisha lesseni ya uwindaji kukosa uhalali kisheria, sheria hii inatoa nafasi kwa maombi mapya ya lesseni nyingine kwa kutumia jina la mwajiri mwingine ambaye atafanya naye kazi.

(5) Mkurugenzi anaweza kuambatanisha masharti au mapendekezo yoyote kwenye lesseni kama atakavyoamua. Hii inampa uwezo na fursa Mkurugenzi kuambatanisha masharti mbali mbali kwenye lesseni za uwindaji, kwa kadri anavyoona mambo yanavyokwenda kwenye uwindaji katika maeneo mbali mbali.

Naamini hadi kufikia hapa umepata mwanga mzuri kuhusu masuala ya uwindaji, vibali, vitalu na masharti au mapendekezo mbali mbali yaliyopo kwenye sehemu hii ya sheria. Kwenye uchambuzi wa sehemu hii ya Saba ya sheria kuna vipengele viwili, cha kwanza kinahusu “Uwindaji wa Wanyama” (Hanting of Animals) ambacho ndio tumechambua tangu tulipoanza kuichambua sehemu ya Saba hadi mwisho wa makala hii ya leo, amapo tumechambua na kujifunza mambo mengi kuhusu uwindaji wa wanyama kwa mujibu wa sheria hii, lakini kipengele cha pili kinahusu Wanyama wa kukamatwa au Ukamataji wa Wanyama (Captured of Animal) ambacho kipo ndani ya sehemu hii ya Saba ya sheria hii, kipengele hiki bado hatujakichambua, tutakichambu katika makala zijazo hapa hapa kwenye mtandao wako wa Wildlife Tanzania.

Hii ni sehemu muhimu sana ya sheria hii ambayo inahitaji kueleweka kwa viongozi, wataalamu na watu wote wanaojihusisha na masuala mbali mbali ya uhifadhi wa wanyamapori pamoja na uwindaji. Pia ni sehemu muhimu kwa watanzania kuifahamu vizuri ili waelewe jinsi ambavyo maliasili zao hasa wanyamapori na biashara hii inavyoendeshwa kisheria, pia ni muhimu kwa watu wanaofikiria kuwekeza kwenye sekta hii, kwani kupitia makala hii utapata mahali pa kuanzia.

Ahsante sana kwa kusoma makala hii, mshirikishe na mwenzako maarifa haya, nakutakia kila la kheri kwenye kazi na shughuli zako, karibu hapa tushirikiane kuhifadhi wanyamapori wetu.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 248 681/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania