Umoja wa Ulaya una sheria kwamba bidhaa ambazo zimetengenezwa na meno ya tembo au meno ya tembo yaliyochakatwa ambayo yalipatikana kabla ya mwaka 1947 yanaweza kufanyiwa biashara ndani ya umoja wa Ulaya bila mazuio ya aina yoyote. Na pia kuna sheria kuwa, meno ya tembo ambayo yamezalishwa kati ya mwaka 1947 hadi 1990 yanaweza kufanyiwa biashara katika umoja wa Ulaya kwa kibali maalumu au cheti kilichotolewa na serikali. Na meno ya tembo ambayo yamepatikana baada ya mwaka 1990, yalifungiwa kabisa na hakuana ruhusa ya kuuza wala kununua meno hayo.

SOMA: Mambo Usiyoyajua Kuhusu Nchi Za Umoja Wa Ulaya Zilivyochangia Kushamiri Kwa Ujangili Wa Tembo Barani Afrika

Kwa mantiki hii ni kwamba bidhaa zilizotengenezwa na meno ya tembo zinaweza kuuzwa popote katika Umoja wa Ulaya ili mradi tu muuzaji aseme hizi bidhaa zake zimetengenezwa na meno ya tembo ambayo yalipatikana kabla ya mwaka 1947. Hakuna udhibitisho mwingine wa kisheria unaoeleza kwamba bidhaa hizo zimetengnezwa na meno ya tembo yenye umri wa miaka mingapi, yani hakuna kipimo cha kubaini bidhaa za meno ya tembo zinazouzwa zina umri gani, ingawa mwaka 2017 Ufaransa ilipendekeza kuwa bidhaa zote zenye uzani wa gramu 200 zilizotengenezwa na meno ya tembo ziuzwe kwa cheti maalumu.

Taarifa za Tume ya Ulaya zinaonyesha kuwa kiasi cha tani kadhaa za meno ya tembo yakiwa ghafi na yakiwa yemechakatwa huuzwa ndani ya umoja huo kihalali kabisa kila mwaka. Mamlaka za usimamizi wa sheria na polisi wanasema wanashindwa kukamata watu wanaohusika na biashara hii kwa sababu hakuna namna ya kubaini bidhaa hiyo ina umri gani, yani imetengenezwa na meno ya tembo kabla ya 1947 au baada ya mwaka huo, hakuna kifaa cha kupimia umri wa meno ya tembo.

Njia ya uhakika ya kubaini miaka ya meno ya tembo ni kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya Radiocarbon, ambayo ni njia rahisi ya kujua biashara haramu ya meno ya tembo ambayo yamepatikana kipindi cha hivi karibuni. Meno hayo yanayouzwa kwa uwazi kabisa kwa watu binafsi na kwenye mitandao na hata kwa wanaojihusisha na biashara hii ya bidhaa za mapambo.

SOMA: Teknolojia Ya Kutumia RADIOCARBON Ilivyosaidia Katika Vita Dhidhi Ya Ujangili Na Biashara Haramu Katika Nchi Za Umoja wa Ulaya

Nchi nyingi za Ulaya zina shehena kubwa sana ya meno ya tembo ghafi ambayo yapo tangu kipindi cha ukoloni. Kwa sheria za sasa wanaruhusiwa kuziuza au kununua kwenye masoko ya ndani tu, lakini mwaka 2017 tume ya nchi za Ulaya ilishauri kusitishwa kwa usafirishaji wa meno ghafi ya tembo, na kwa taarifa za mwaka 2018 zinasema wanachama wa umoja huo wameridhia makubaliano hayo ya kusitisha biashara za uagizaji meno ya tembo.

Ulaya inabakia kuwa msafirishaji halali wa meno ya tembo yaliyochakatwa kwa nchi za Asia ambako masoko ya meno ya tembo yanachochea janga la ujangili katika bara la Afrika. Uchambuzi wa ripoti hii utaangalia biashara za meno ya tembo ndani ya umoja wa Ulaya ukiachilia mbali biashara ya usafirishaji kwenye nchi zingine.

Ripoti hii tunayoichambua ni moja ya ripoti zilizotoka mwezi May 2018. Hivyo ni ripoti ya hivi karibuni na imesheheni habari na taarifa nzito kuhusu nchi za Umoja wa Ulaya zinavyoendesha biashara ya meno ya tembo ambayo kwa asilimia 90, sio biashara halali. Hii ni kwa mujibu wa ripoti tunayoichambua yenye jina la “EUROPE DEADLY IVORY TRADE”.

Msomaji wa makala hii, endelea kufuatilia uchambuzi unaofuata ili kujua hali ya mambo ilivyo, nimeamua kuchambua kidogo kidogo ili iwe rahisi kwako kusoma ripoti hii.

Asante sana!

Mchambuzi wa ripoti hii ni;

Hillary Mrosso

+255 683 862 481

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaamu.net/wildlifetanzania