Tangu karne nyingi zilizopita watu wamekuwa wakitumia nyamapori kwa matumizi mbali mbali kama vile kitoweo, dawa, na kufanyia mila na na desturi zao. Katika zama hizo wanyamapori walikuwa wengi na idadi ya watu ilikuwa ndogo. Idadi ya wanyamapori ilikuwa kubwa kwasababu hakukua na madhara makubwa kwa wanyamapori na mazingira yake. Lakini pia kipindi hicho shughuli za binadamu hazikuwa na athari makubwa kwa wanyamapori kama ilivyo sasa.
Picha hii imepigwa na Dr. Ali; Ikionyesha ujangili wa nyamapori ya Twiga.
Makala iliyopita niliandika kuhusu changamoto mbalimbali ambazo wanyamapori wanakabiliana nazo ikiwepo ujangili na biashara za mazao ya wanyamapori. Katika makala ile nilieleza jinsi matumizi yaliyopitiliza yanavyo weza kusababisha kukosekana kwa uhifadhi endelevu wa misitu na maeneo ya hifadhi za wanyamapori. Makala hiyo inapatikana katika tovuti yetuTishio Kubwa Kwa Wanyamapori Na Mazingira Tanzania
Leo nataka tuangazie kwa upana matumizi ya nyamapori yanavyochangia kutoweka kwa kwa aina mbalimbali za wanayamapori ambapo kitaalamu huitwa spishi. Nyamapori ninayoelezea katika makala hii ni ile iliyopatikana kwa uwindaji haramu yaani uwindaji usiokuwa na kibali kutoka kwa mamlaka husika. Kila mnyamapori ana umuhimu wake katika mifumo ya ikolojia, na sio rahisi kuona umuhimu huo kwa haraka kwasabau wengi hatuna uelewa wa kutosha kuhusu maisha na mifumo ya kiikolojia.
Mifumo hii ya kiikolojia imekuwa haiku imara kutokana na idadi kubwa ya wanayamapori kuendelea kuteketea kila siku. Upotevu wa Wanyama hao umekosa taarifa sahihihi juu ya idadi yao. Chanzo kikuu cha kupotea kwa wanyampori hao kinatajwa kuwa ni ujangili ambao unafanywa wanadamu wasiokuwa na mapenzi mema na shughuliza uhifadhi.
Tafiti nyingi kwenye eneo hili zimekuwa na upendeleo, mfano taarifa nyingi zinaelezea baadhi tu ya wanyamapori wachache kama vile tembo, faru, simba nk. Ukisoma machapisho mengi yaliyofanywa kuhusu matumizi ya wanyamapori utaona wengi wamejikita zaidi kuelezea wanyama hawa pekee na kuacha wanyamapori wengine bila kuwa na taarifa za kutosha.
Upendeleo huu unasababisha kukoasekana kwa uwiano mzuri wa uwekezaji kwenye uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori. Nguvu kubwa inawekwa kwenye kuhifadhi wanyama hao wachache na kutowapa kipaumbele wanyamapori wengine muhimu kama swala, nyoka, twiga, nyati, pundamilia, fisi, nyumbu, kakakuona, ndege, vipepeo, kobe, mijusi, sungura, panya, nk.
Shirika la Umoja wa mataifa linalosimamia uhifadhi linalojulikana kama International Union for Conservation of Nature (IUCN) limeorodhesha baadhi ya wanyamapori ambao wapo hatarini kutoweka kwasababu mbali mbali ikiwepo ujangili kwa ajili ya kupata nyamapori. Lengo ni kutaka mamlaka za usimamizi kuongeza juhudi katika uhifadhi wa wanyama hao waliotajwa na shirika hilo. Licha ya hayo, utafiti wa Varun Swamy na Miguel Pinedo-Vasquez (2014) umebaini kuwa kuna idadi kubwa sana ya wanyamapori wasioainishwa na IUCN wanawindwa kila siku kwa ajili ya nyamapori.
IUCN imeendelea kubainisha kwamba 85% ya wanyama jamii ya nyani na swala wapo hatarini kutoweka. Uwindaji haramu kwa ajili ya nyamapori umetajwa kuwa ndio kichocheo kikubwa cha kuendelea kutoweka kwa wanyamapori hawa muhimu. Kama wewe unashangaa nyani wanaishaje basi nikujuze tu kuwa kuna watu wanapenda sana kula nyama ya nyani, na wanaripoti kuwa ni nyama tamu kuliko nyama nyingine. Mfano nchi nyingi za Magharibi mwa Afrika kama Kongo DRC, wanawawinda nyani kwa ajili ya kitoweo.
Takwimu nyingine kutoka kwenye utafiti wa Varun Swamy na Miguel Pinedo-Vasquez unaonyesha kuwa zaidi ya 93% ya wanyama wenye miili mikubwa kama nyati, tembo, twiga, pofu na ndege kama kanga na mbuni wameripotiwa kuwa katika hatari ya kutowena kutokana na uwindaji haramu.
Matumizi ya nyamapori yamekuwa sehemu muhimu ya mlo wa jamii nyingi zinazoishi kando ya hifadhi za wanyamapori. Jamii zinazoishi kando ya hifadhi za wanyamapori zinakabiliwa na changamoto nyingi hasa ukosefu wa chakula kwenye baadhi ya misimu, hivyo uwindaji haramu umekuwa ukiwasaidia sana kukabiliana na majanga ya njaa na ukosefu wa kipato.
Mfano, kwenye misitu ya Amazon nchini Brazili ambako kuna idadi kubwa ya aina nyingi za wanyamapori, taarifa zinaonyesha mtu mmoja anakadiriwa kutumia zaidi ya kilogram 63 za nyamapori kwa mwaka. Kwa upande mwingine inaripotiwa kuwa wakazi wanaoishi katika misitu ya bonde la Kongo, mtu mmoja anatumia zaidi ya kilogramu 51 za nyamapori kwa mwaka.
Matumizi ya nyamapori yamekuwa makubwa na yanaendelea kuwa makubwa kila siku, mfano zaidi ya asilimia 88 ya nyumba zilizohojiwa mwaka 2006, zilikiri kuwa wanakula nyamapori kama kitoweo. Kuna taarifa nyingi za matumizi ya nyamapori nchini Tanzania, mfano utafiti wa Jambiya wa mwaka 2007, unaonyesha matumizi makubwa ya nyamapori kama chakula muhimu kwenye makambi ya wakimbizi yaliyoko Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.
Hata hivyo, matumizi ya nyamapori yamekuwa sio tu sehemu ya chakula muhimu kwa jamii zilizopo karibu na maeneo ya hifadhi hizi za wanyamapori; bali kumekuwa na uhitaji mkubwa sana wa nyamapori kwenye vijiji, miji, majiji na nchi jirani. Mfano, utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na mwandishi wa makala hii ndugu Hillary Mrosso kwa upande wa Ruaha nchini Tanzania, unaonyesha mzunguko na mtiririko wa biashara ya mazao ya wanyamapori, nyamapori ikiwa ndio bidhaa inayosafirishwa na kutumiwa zaidi (60%) kwenye eneo hilo.
Maendeleo ya sayansi na teknolojia yamerahisisha mambo mengi ikiwemo suala la kufanya ujangili. Kwa sasa majangili wanaweza kupata silaha za kisasa ambazo zinaweza kuua wanyama wengi kwa mara moja. Vile vile kuna miundombinu mizuri ya barabara zinazoweza kufika hadi maeneo ya hifadhi za wanyamapori kwa kutumia baiskeli, pikipiki (bodaboda), magari, ndege, meli nk. Uwepo wa njia za usafirishaji umerahisisha ujangili kufanyika kwa ufanisi maeneo mengi. Mfano, taarifa kutoka katika hifadhi za Kaskazini mwa Tanzania zinaonyesha jinsi uwepo wa silaha na njia za usafirishaji unavyosaidia kusambaza na kusafirisha nyamapori kwenye miji ya Arusha, Moshi, na kwenye nchi jirani kama vile Kenya.
Ndugu msomaji wa makala hii, nimejaribu kutoa mifano hai ya sehemu mbali mbali ili wote tuone ukubwa wa janga hili. Wanyamapori ni hazina muhimu kwa vizazi vya sasa na vya baadaye. Tusipozingatia matumizi endelevu ya rasilimali hizi muhimu tutazipoteza muda sio mrefu. Yote niliyoeleza kwenye makala hii sio hadithi za kufikirika, bali ni tafiti zilizofanywa na kuhakikiwa na watu mahiri wenye weledi kwenye fani hii. Hivyo endelea kujifunza na kuchukua hatua kupambana na vitendo vya uwindaji haramu kwenye hifadhi zetu.
Sheria ya Tanzania ya Wanyamapori namba 5, ya mwaka 2009 inakataza kabisa watu au mtu kujihusisha na vitendo vya ujangili. Kifungu cha 18 na 19 vimeweka wazi jambo hili pamoja na adhabu imetolewa kwa wanaovunja sheria hii ikiwemo kifungo cha miaka 5 hadi 10 au kulipa faini isiyopungua shilingi 500,000 hadi 2,000,000 au vyote kwa pamoja.
Asante kwa kusoma makala hii; Makala hii pia imehaririwa na ndugu Alphonce Msigwa, ambaye ni Mwikolojia Hifadhi za taifa Tanzania (TANAPA). Kwa maoni, ushauri, maswali kuhusu makala hii usiache kuwasiliana nami kwa mawasiliano hapo chini.
Washirikishe wengine makala hii,
Imeandikwa na
Hillary Mrosso (BSc, MSc. Wildlife Management and Conservation)
Simu: +255 683 863 481, Email; hmconserve@gmail.com