Kwa miaka saba iliyopita tumeshuhudia kupungua sana kwa idadi ya tembo wa Afrika kutokana na ujangili hasa katika eneo la Kusini mwa bara hili. Kwa miaka ya 2011 na 2012 tumeshughudia kiwango kikubwa sana cha uuaji wa tembo kwa njia haramu, yaani ujangili kuliko kipindi cha miongo mingine iliyopita. Inasemekana pia asilimia 7.4 ya tembo wote wa Afrika wameuwawa na majangili kwa sababu ya biashara ya meno yao.

Rafiki yangu karibu katika mfululizo wa makala hizi za uchambuzi kutoka katika ripoti inayojulikana kama ELEPHANT IN THE DUST, THE AFRICAN ELEPHANT CRISIS. Ripoti ilichapishwa mwaka 2013, ripoti hii imesheeni visa na matukio ya kutisha kuhusu unyama wanaofanyiwa tembo wetu. Ingawa ripoti hii ilitoka zamani, kuna mambo mengi yanayofaa sana kujifunza na kuyajua ili tuboreshe mikakati na mbinu zetu tunazotumia katika uhifadhi wa wanyamapori hasa tembo. Hivyo nikukaribishe tuendelee kujifunza yale muhimu niliyochambua.

Katika kazi hii ya kukusanya taarifa za tembo waliouwawa na majangili, taarifa hizi kwa mujibu wa ripoti hii zilikusanywa na askari wa wanyamapori kwenye maeneo na vituo vyao vya kazi, hasa kipindi wanafanya doria huwa wakiona mizoga ya tembo huandika sehemu alikofia, umri wa tembo huyo, jinsia yake, nk. Taarifa hizi ndio hutumika kaundaa ripoti hizi na pia hufanyiwa uchunguzi wa kitalaamu ili kujiridhisha na kuweka makadirio yanayoendana na idadi ya tembo katika eneo husika.

Katika ukusanyaji wa taarifa hizi za mizoga ya tembo kwenye maeneo yao, kuna maeneo ambayo yameonyesha kukithiri kwa mizoga ya tembo katika bara hili, taarifa za kitafiti zinataja maeneo ya Okapi Wildlife Reserve iliyopo Afika ya Kati, hifadhi ya taifa ya Salonga na Virunga iliyopo katika nchi ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, taarifa hizi zinaonyesha mizoga yote iliyokutwa katika mapori hayo ilikuwa imeuliwa na majangili. Pia kuna maeneo mengine ya Urithi wa Dunia katika nchi ya Kongo zinasema idadi ya tembo katika hifadhi hii ya Kuhuzi-Beiga, tembo katika eneo hili wamepungua sana na kubakia tembo 20 tu, hii ni kutokana na mapigano na vita katika eneo la mashariki mwa Kongo.

Kama tulivyokwisha kuona kwenye makala zilizopita kuwa sehemu ya Afrika ya Kati na Afrika ya Magharibi ndio sehemu ambayo imerekodiwa kuwa na mauaji mabaya sana ya tembo katika kipindi kinachoishia mwaka 2012. Mapigano ya vita, vikundi vya kigaidi na vya uasi ndio hupelekea mauaji mabaya ya kutisha katika eneo hili la Afrika. Kuna taarifa za kuuwawa kwa tembo 200- 300 katika kipindi kifupi sana, hii ni kutokana na migogoro mingi ya kisiasa katika eneo hili la Afrika.

Nini kinachopelekea kushamiri kwa ujangili?

Kuelewa sababu zilizo nyuma ya ujangili sio kazi rahisi hata kidogo, mambo mengi sana yanahusishwa, vitu vingi vinahusishwa, watu wengi wanahusishwa kuna mlolongo mrefu sana wa kujua ujangili wa meno ya tembo umeanzia wapi na umesababishwa na nani? Hii ndio sababu inayopelekea ukusanyaji wa taarifa kama hizi unakuwa mgumu sana, kwa sababu hujui uanzie wapi, na sehemu nyingine ni hatari sana hata namna ya kupata taarifa hizi unakuwa mgumu.

Katika mataifa makubwa yaliyoendelea ambayo yanahitaji meno ya tembo kwa gharama kubwa ni kutokana na hali nzuri walizo nazo kiuchumi, maana meno ya tembo hutumiwa tu kama sehemu ya anasa na ufahari kwenye jamii hizo. Katika karne ya 20 sehemu kubwa ya nchi za Ulaya, Marekani na Japani ndio waliokuwa wahitaji wakuu wa meno ya tembo, hali ambayo ilipelekea mataifa hayo kuwa na masoko makubwa sana ya biashara ya meno ya tembo, hata hivyo kushamiri kwa biashara ya meno ya tembo katika mataifa hayo kulipelekea mahitaji makubwa zaidi ya meno ya tembo kutoka sehemu nyingi duniani na hapa ndipo maelfu kwa maelfu ya tembo wa Afrika walipokatishwa maisha yao kwa ajili ya kupata meno yao ambayo ilikuwa ni bidhaa yenye faida katika biashara zao.

Hata hivyo taarifa zinasema kipindi hicho nchi ya China haikutajwa sana kwani haikuwa na masoko yanayotishia kama mataifa hayo mengine. Lakini cha ajabu sana baada ya miongo michache nchi ya China imeibuka kuwa ndio nchi yenye masoko na viwanda vingi kwa ajili ya biashara hii haramu ya meneo ya tembo. China sasa inanyooshewa kidole kila kona ya dunia hii ni kwa mujibu wa taarifa za kitafiti na hali ya mambo inavyokwenda huko.

Aidha, baada ya biashara hii haramu kushika kasi nchi nyingi zenye wanyama hawa zilijihusisha na biashara hii zilikwa pia ni kichocheo cha kushamiri kwa baishara hii katika bara ili la Afrika, taarifa zinasema upatikanaji rahisi wa maeno ya tembo tena yakiwa yanauzwa tu kwa uwazi kama nyanya sokoni ndio ilisababisha kushamiri kwa ujangili katika bara hili. Hata hivyo katika ripoti hii imetaja miji ambayo biashara hizi za meno ya tembo zilifanyika kama kuuza nyanya sokoni, mfano ni Khartoum, Kinshasa Logosi na Luanda na sehemu nyingine za miji ya Asia.

Kufanyika kwa biashara hii kwa uwazi katika sehemu hizi ni kutokana na udhaifu wa sharia za usimamizi wa wanyamapori, hata hivyo migogoro mingi ya kisiasa nayo imechangia sana udhaifu wa sharia katika maeneo haya. Pia biashara hizi zilisimamiwa na watu matajiri na wenye nguvu katika serikali za nchi, hivyo zilifanyika kwa umakini.

Kwasababu hiyo, kumekuwa na ongezeko la kandarasi nyingi kutoka China na nchi nyingine duniani, wengi wakiwa na miradi ya ujenzi, uchimbaji madini na rasilimali nyingine, hali hii imetajwa kuwa wengi wa wageni hawa hujihusisha na biashara ya meno ya tembo kwenye maeneo yao ya kazi. Wengi husafirisha na kununua meno ya tembo ambayo hupatikana katika nchi walizokuwa na miradi ya ujenzi. Katika hali kama hii, tunatakiwa kuwa makini na wawekezaji wanaoingia katika nchi zetu ili wasije wakatorosha rasilimali zetu na kupeleka kwenye nchi zao kwa ajili ya manufaa yao.

Katika ngazi ya taifa au nchi, ripoti hii imeeleza kwa undani kuwa kushamiri kwa ujangili na biashara ya meno ya tembo kunachangiwa sana na hali ya siasa za nchi zetu, mfano kama kuna vita, migogoro ya ndani ya nchi, vita vya wenyewe kwa wenyewe, vikundi vya kigaidi, au vikundi vya waasi, imetajwa sana kuwa ndio milango mikubwa sana inayochochea kushamiri kwa ujangili na biashara za meno ya tembo. Pamoja na hali kama hizi kuwepo, pia kuna kuwa na mianya mingi ya rushwa, ufisadi, uingizaji wa silaha kinyume na sheria, katika kipindi cha mvurugano kama hiki sheria inalegea sana, umakini kwenye usimamizi wa rasilimali za nchi unapungua sana na hapo ndipo ujanili unapopata nafasi.

Ujangili katika ngazi ya chini kabisa umetajwa kuhusishwa na sababu nyingi sana, lakini kubwa likiwa ni umasikini wa katika jamii za watu wanaoishi kwenye maeneo hayo. Kuna sababu za kiuchumi, kitamaduni nk. Lakini utafiti unaonyesha uwindaji kwa ajili ya nyamapori umeshamiri sana kwenye maeneo haya duni, hata hivyo kuna wanaotiliwa shaka kuwa siku zijazo watu wanaowinda kwa ajili ya chakula na kitoweo wanaweza kuja kuwinda na kuwauwa tembo kwa sababu hizo.

Katika hali hiyo ya umasikini ni rahisi sana watu kushawishika pale wanapopewa fedha ili wakawinde au waue tembo, kwa kuwa watu hawa ni wazoefu na wanajua maeneo yenye tembo wengi, basi wafanyabiashara ya meno ya tembo huwatumia watu hao kufanikisha malengo yao. Pamoja na hayo kufanyika majangili wa meno ya tembo huwatumia sana baadhi ya maaskari wa wanyamapori ili kufanya ujangili wa tembo, na kwa kuwa maaskari hawa wanalipwa mishahara na posho kidogo sana ambazo hazikidhi mahitaji yao,wamekuwa wakishawishiwa na kupokea rushwa ili kufanya ujangili.

Halikadhalika, migogoro kati ya watu na tembo imekuwa ikihusishwa sana na kupungua au kuuwawa kwa watu au tembo, pale mkulima anapopata hasara ya mazao yake ni rahisi sana kulipiza kisasi. Ingawa sababu hii haionyeshi kuwa ndio sababu kuu ya kupungua kwa tembo, tafiti zinasema endapo hatua za makusudi hazitachukuliwa watu watazidi kuvamia maeneo ya hifadhi za wanyamapori na hapo ndipo idadi ya tembo itakapozidi kupungua, na pia ujangili utafanyika kwenye maeneo hayo.

Kufikia hapa sina la ziada, naamini umefahamu mambo machache kati ya mengi yaliyopo kwenye ripoti hii muhimu. Naamini utashirikiana na mamlaka husika katika ulinzi, na uhifadhi wa maliasili za nchi yetu. Washirikishe wengine makala hii ili kwa pamoja tupate maarifa na ujumbe huu muhimu.

Ahsante sana kwa kusoma makala hii hadi mwisho!

Uchambuzi huu umeandaliwa na;

Hillary Mrosso

+255 683 862 481/255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaamu.net/wildlifetanzania