Habari ndugu mtanzania, karibu kwene makala zetu za kila siku ili kupeana maarifa, ufahamu na taarifa muhimu ili tuweze kuishi vizuri sehemu yoyote ile tulipo. Kuna vitu vidgogo tunapaswa kuvifahamu hata kama havitiliwi mkazo sana kwenye sharia za mahali husika, ni bora ukafahamu kwa uchache ili usisumbuke na kusumbuliwa unapofany safari zako. Naamini umewahi kuwaona watalii wanavyo vaa, inawezekana kutoka ndani ya nchi au nje ya nchi, kuna namna ya uvaaji wao, kuna mavazi fulani hivi akivaa unamwona mtalii au mtu anayekwenda sehemu fulani, au ametoka sehemu fulani. Mavazi ni muhimu na pia hututambulisha sehemu mbali mbali tunapokuwa au tunapoenda. Makala hii imechambua kwa undani mavazi sahihi unayotakiwa kuvaa unapotembelea hifadhi yoyote au sehemu yoyote porini kwa malengo mbali mbali uliyo nayo, inawezekana utafiti, kazi au utalii. Hivyo nakukaribisha usome makala hii hadi mwisho upate ufahamu huu muhimu.

  1. Suruali

Unapotembelea hifadhi maana yake unaenda porini, hivyo lazima uvae nguo ambazo zitakusaidia  ukae, utembee na kusimama bila wasiwasi, na hapa kwenye suruali ni kwa wote, kama ni mwanamke nashauri avae tu suruali, ingawa sio lazima sana ila itamfanya ajisikie salama sana kuliko kuvaa sketi au dela, kwa wadada au wanawake wavae suruali nzuri inayowatosha isikubane sana, vaa kinadhifu suruali inatakiwa iwe ya kitambaa kigumu kidogo sio vile visuruali vilaini ambavyo mwiba ukikushika tu vinachanika hapo hapo, unaweza kuvaa suruali ya kitambaa kigumu kidogo. Hivyopia kwa wanaume tunatakiwa kuvaa suruali nzuri na yenye kitambaa kigumu kidogo, kwa mfano naona wengi sana wanapotembelea hifadhi huvaa suruali za kaki, za kadeti, au jinsi, ambayo ukivaa unapendeza na kuvutia sana. Pia ni muhimu kuepuka kuvaa nguo za kung’ara, unapokuwa porini usivae nguo za kung’ara sana kwasababu unawaumiza wanymapori, wanyama kama tembo au wengine huwa wanaathirika na kukwazika unapovaa nguo za kung’ara au vitu vinavyo ng’aa. Vaa tu kawaida kabisa nguo zilizopoa zinazoendana na mazingira ya porini.

  1. Shati/tisheti

Hapa kwenye mashati au nguo utakazo vaa juu kama blauzi kwa wanawake ziwe nadhifu pia, unapoingia porini unaingia kwenye miji ya viumbe hai wengine na viumbe hai wana namna yao ya mazingira yanayoendana na tabia na miili yao ilivyo, hivyo kwa namna yoyote ile vaa vizuri usiwakwaze wanyamapori. Kama nilivyoelezea kwenye pointi ya kwanza hata shati au tisheti unayoivaa iwe ngumu kidogo, isiwe laini au umevaa tu vesti, zingatia nguo zinazoendana na huko unakotaka kwenda. Kwa mfano sehemu nyingine huko porini kuna mbung’o wananga’ata sana, sasa kama umevaa kinguo kimeacha mabega na mongo wote nje utang’atwa sana, na utaichukia safari yako. Pia usivae mashati au blauzi ya kung’aa sana hii pia sio nzuri kwa baadhi ya wanyamapori.

  1. Koti/Jaketi/sweta

Inategemea na hifadhi unapotaka kutembelea hifadhi nyingine huwa na joto sana na sehemu nyingine ni baridi sana, hivyo unavyopanga safari yako unatakiwa kuuliza maswali ambayo yatakufanya ujiandae na kwenda kufurahiya safari yako. Uliza hali ya hewa ipoje kwa mwezi unaotaka kutembelea hifadhi. Kwa mfano kwa hapa Tanzania hifadhi Ngorongoro inabaridi sana karibia mwaka mzima hivyo unavyopanga kwenda ktembelea angalia kama unaweza kwenda na sweta, au koti au wengine wanatumia mashuka ya kimasai ambayo hujifunika na kujikinga na baridi. Hivyo angalia namna unavyoweza kuifanya safari yako kuwa nzuri na yenye furaha,pia hata sweta, koti, na jaketi visiwe vya kung’ara sana ili kuepuka kuwasumbua wanyama.

  1. Kofia

Kofia ni muhimu pia unapotembelea hifadhini au porini, kwani itakusaidia kujikinga na jua na pia hata manyasi. Kwa watalii wanaotumia magari ya wazi ambayo hayajafunikwa juu, kofia ni muhimu kwasababu ya kujikinga na jua, na hatari nyingine za porini. Hata hivyo kofia itazuia usichafuke nywele zako na vumbi la barabarani. Kuna hifadhi nyingine kuna vumbi sana hasa wakati wa mchana kipindi ambacho watalii wanakuwa wengi, na magari huwa mengi sana na kusababisha vumbi kubwa barabarani hivyo zingatia kuvaa kufia nzuri itakayofunika kichwa na nywele zako. Kofia zinaweza kuwa za mduara, au zile za kawaida wanaziita cap, zinaweza kuwa za rangi mbali mbali ila pendelea kuvaa zenye rangi ya kaki, au nyeusi , upendavyo wewe.

  1. Miwani

Miwani ni vazi jingine ambalo sio la lazima sana, ila ngoja tu nikwambie namana linavyoweza kukusaidia mkiwa porini au hifadhini,kuna miwani za aina nyingi sana, za jua, za kuendeshea bodaboda nk. Hapa miwani itakusaidia kujikinga na vumbi wakati mkiwa njiani au ukiwa mnafanya utalii ndani ya hifadhi,pia itakusaidia kupunguza jua lisikuathiri unapotaka kuona wanyamapori au vivutio vingine. Wakati mwingine kuna baridi sana na miwani huweza kukusaidia kuzuia macho yako yasitoe machozi kama kuna baridi kali.

  1. Viatu

Hapa kwenye viatu ni muhimu ukavaa viatu vinavyoendana na huko porini, usivae ndala au kandambili hifadhini, tafuta raba nzuri zinazofunika miguu yako. Kama mnavyojua porini ni mji wa viumbe wengine ambao wapo wengi sana, hivyo wanyama kama nyoka ambao hupenda kung’ata miguuni, kama umevaa viatu vizuri utajikinga na hatari hiyo, mwinginea atasema si nitakuwa kwenye gari, sitatembea kwa miguu, ngoja nikwambie mnaweza kuharibikiwa na gari yenu au ukashuka sehemu ambayo unafikiri ipo salama kumbe kuna nyoka, maana hawa wanyama hawauliwi wanapokuwa hifadhini. Miiba na hata kwenye mahali pa kutembea kwa miguu, vaa tu viatu vyako vizuri. Na hapa ni kwa wote wanaume na wanawake.

Kwa hayo machache najua umepata ufahamu kidogo kwenye suala la mavazi. Si unajua hata ukiwa mjini unataka kwenda kwenye ofisi ya mtu fulani kuna aina ya mavazi wangependa mvae, kuna baadhi ya ofisi au makampuni hata ndala huruhusiwa kabisa kuvaa katika eneo lao. Hivyo utaona kila sehemu kuna utaratibu wao wa maisha ya mavazi na taratibu nyingine zenye lengo zuri.  Ukifahamu taratibu na sharia za mahali fulani wala hutapata shida wala usumbufu, utaokoa muda na kufanya mambo yako kwa wakati. Hivyo hivyo na unapotembelea hifadhi au porini kuna taratibu zao na kanuni zao zenye makusudi kabisa ili kuepuka usumbufu kwa wengine hasa viumbe hai. Vaa vizuri usiwakwaze watu na wanyamapori.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

0742092569

hillarymrosso@rocketmail.com