Bundi ni ndege wanaopatikana kwenye oda ya Strigifomi, ambayo inajumuisha Zaidi ya spishi 200 za bundi duniani. Ndege hawa huonekana zaidi wakati wa usiku, na ni kati ya jamii za ndege wawindaji ambapo ndege wengine kama mwewe na tai hufanya shughuli zao mchana zaidi. Kuna jamii za bundi ambao hufanya shughuli zao kwa ustadi wakati wa mchana, ambazo ni bundi wa kaskazi (northern hawk-owl), bundi masikio mafupi (short-eared owl) na bundi wa mapangoni (burrowing owl). Jamii ya bundi wadogo zaidi huitwa elf owl (wanapatikana bara la Amerika), wanaokadiriwa kuwa na uzito wa gramu 31. Jamii mbili za bundi wakubwa zaidi duniani huitwa bundi-tai wa Ulaya (Eurasian eagle owls) na bundi mvuvi wa Blakistoni (Blakiston’s fish owl) wenye kufikia uzito wa kilo 4.6.
Bundi wana faida nyingi katika uhifadhi na ikolojia ya dunia, ikiwamo kupunguza kuenea kwa magonjwa yanayoenezwa na wanyama jamii ya panya, ndege wengine na wadudu. Bundi huwinda viumbe hao waharibifu kupunguza magonjwa hayo, husaidia pia kuhakikisha idadi ya viumbe hao waharibifu haizidi kiwango na kuleta madhara. Bundi pia husaidia binadamu kupunguza wanyama waharibifu wa maghala na mazao kama panya, ambao ni chakula chao kikubwa.
Kumekuwa na hadithi nyingi kuhusu bundi hali inayopelekea watu wengi kuvutiwa au kuwaogopa na kuwahusisha bundi na Imani za kishirikina. Hii inaweza pia kusababishwa na hali ya bundi wengi kufanya shughuli za maisha yao wakati wa usiku ikiwemo kutoa sauti kali. Kiuhalisia, bundi hawana madhara kwa binadamu na hawaingiliani sana na binadamu huku wakileta faida ya kupunguza wanyama na wadudu waharibifu kama panya na viwavi. Bundi pia ni miongoni mwa ndege wanaovutia kuwatazama wakiwa wamepambwa na manyoya yenye nakshi mbalimbali pamoja na macho makubwa yanayowawezesha kuona vyema hata gizani.
Spishi za Bundi Nchini Tanzania
Miongoni mwa spishi za bundi zinazopatikana Tanzania, spishi 14 ni maarufu zaidi nchini Tanzania, zikipatikana katika maeneo tofauti tofauti ya milima, misitu, mapori, majangwa na karibu na makazi ya watu. Spishi hizo ni kama ifuatavyo,
- Kungwi (African Spotted Eagle-owl)
Kungwi au bundi-tai wa Afrika ni miongoni mwa spishi za bundi wenye ukubwa wa kati, kufikia uzani wa hadi gramu 900. Licha ya kuwa nchini Tanzania, spishi ya bundi hawa hupatikana kwa wingi pia katika nchi nyingi za kusini mwa Afrika. Huweza kutambulika kwa urahisi kutokana na kuwa na manyoya yaliyochomoza mithili ya masikio juu ya vichwa vyao, huku nyuso zao zikiwa na manyoya meupe pamoja na macho ya njano yenye kiini cheusi. Sehemu kubwa za manyoya ya miili yao huwa na mabaka ya rangi ya nyeupe, kahawia pamoja na nyeusi. Bundi hawa pia wamepewa jina la bundi wa mjini kutokana na uwezo wao mkubwa wa kuishi karibu na makazi ya watu.
Kungwi hufanya shughuli zao wakati wa usiku ambapo huwinda wadudu, wanyama jamii ya panya, ndege na reptilian wengine. Huweza kuwinda wanyama wasioweza kuwala mara moja, hivyo kutumia midomo na kucha zao kuwararua vipande na kuvihifadhi kwenye viota vyao. Kungwi huweza kuanza kuzaliana wakifika umri wa mwaka mmoja, ambapo jike huandaa kiota chini, juu ya mti, kwenye pango au kwenye nyumba za watu. Jike hutaga mayai kati ya 2-4 na kuyaatamia kwa siku 32, ambapo dume humletea chakula kipindi hicho.
Vifaranga vyao huweza kuanza kuruka baada ya wiki saba, japo wazazi wao huendelea kuwatunza kwa wiki kadhaa zaidi. Wakiwa porini huwa na wastani wa kuishi wa kati ya miaka 10 hadi 15, huku wakiweza kuishi zaidi ya miaka 20 wakitunzwa na binadamu. Bado kwa wastani idadi ya spishi ya bundi hawa inaridhisha na wanapatikana kwa wingi kwenye maeneo wanayoishi.
Bundi anina Kungwi
2. Bundi wa Sokoke (Sokoke Scops Owl)
Spishi hii ya bundi hupatikana Afrika ya Mashariki pekee, hususani nchini Kenya na Tanzania. Wanapatikana kwenye milima ya tao la mashariki (Eastern Arc Mountains) inayoanzia nchini Kenya kisha kuungana na milima ya Pare, Usambara, Uluguru na Udzungwa nchini Tanzania. Takwimu zinaonyesha bundi hawa nchini Tanzania wameonekana katika milima ya Usambara pekee. Ni bundi wadogo wasiofikia uzito wa gramu 70. Huwa na manyoya yenye rangi ya kijivu na madoa meusi, au kahawia iliyochanganyika na nyekundu na madoa meusi.
Spishi hii ya bundi huishi kwenye misitu iliyo kwenye muinuko kidogo ambayo haijasumbuliwa kwa shughuli za kibinadamu. Misitu hii pia huwasaidia kupata vyakula wanavyohitaji kwa wingi. Sokoke huwinda na kula wadudu kama chakula chao kikuu, jambo linaloweza pia kusababishwa na udogo wa miili yao ambapo hawawezi kuwinda hata wanyama wadogo.
Tafiti zaidi juu ya idadi na maisha ya spishi hii ya bundi zinahitajika. Shirika la IUCN limewaweka bundi hawa miongoni mwa viumbe vilivyo katika hatari ya kutoweka (endangered) kutokana na kuzidi kupungua kwa idadi yao. Shughuli za kibinadamu za kukata miti na kuzidi kuvamia maeneo ya misitu pamoja na mabadiliko ya hali ya nchi yanaweka bundi hawa kwenye hatari kubwa ya kutoweka. Wanyama kama tembo pia huchangia kuharibu makazi ya bundi wa Sokoke kutokana na kuangusha miti mara kwa mara.
Bundi wa Sokoke
3. Kitaumande Madoa (Pearl spotted owlet)
Hii ni kati ya spishi ya bundi wadogo kabisa barani Afrika, ambapo majike hufikia uzito wa gramu 100 huku madume yakifikia gramu 70. Wana manyoya yenye rangi ya kahawia na nyeupe na madoa doa ya rangi ya lulu. Wana macho na midomo ya njano, pia nyuma ya vichwa vyao wana madoa mawili yanayofanana na macho, ili kuwachanganya adui zake. Huishi zaidi maeneo ya uwanda wa miti huku wakiepuka maeneo ya wazi sana au yenye misitu minene.
Spishi hii hufanya shughuli zake zaidi wakati wa mchana, ikiwemo kutengeneza viota na kuwinda, ambapo huwinda wadudu, nyoka wadogo, ndege, mijusi na popo. Huweka viota vyao kwenye mashimo ya miti ambapo kiota kinaweza kudumu kwa miaka hadi minne. Hutaga mayai kati ya 2-4 na kuyaatamia kwa takribani siku 29. Hawa ni miongoni mwa spishi za bundi ambao hawako kwenye hatari ya kutoweka duniani (least concern).
Kitaumande Madoa
4.Bundi maji (Marsh owl)
Hawa ni bundi wakubwa kwa wastani (gramu 230 – 480), wenye rangi ya kahawia iliyokolea huku wakiwa na kichwa chenye umbo la boga. Wana macho yenye rangi nyeusi na kahawia iliyokolea sana, pia huwa na manyoya mafupi yaliyochomoza juu mithili ya masikio. Bundi hawa huishi maeneo ya tambarare zenye nyasi au vichaka, karibu na vyanzo vya maji ambapo huweka viota vyao ardhini. Kiota huandaliwa kama shimo dogo lililowekwa nyasi kavu, ambapo jike hutaga kati ya mayai 2 hadi 6 na kuyaatamia kwa siku 28.
Makinda yakianguliwa hukaa kwenye kiota kwa karibu wiki tatu huku wazazi wao wakiyahudumia kabla ya kuruka kuanza kujitegemea. Ni wawindaji hodari wa wanyama jamii ya panya lakini pia wadudu na ndege wadogo wakati wa usiku. Spishi hii ya bundi inaweza kuonekana katika hifadhi mbalimbali za taifa nchini Tanzania ikiwemo Serengeti. Bundi hawa wanapatikana pia nchi nyingine za kusini mwa Afrika hususani nchi ya Afrika Kusini, Namibia, Madagascar, Zimbabwe lakini pia hupatikana kaskazini kwenye nchi ya Morocco. Bado spishi hii ya bundi haimo miongoni mwa spishi zilizo kwenye hatari ya kutoweka (least concern).
Bundi Maji (chanzo: eBird)
5. Bundi misitu (African wood owl)
Hii ni spishi ya bundi inayopatikana maeneo mengi kusini mwa jangwa la Sahara, na Tanzania ikiwa moja ya nchi hizo. Ni bundi wakubwa kiasi (gramu 250-350) wenye macho makubwa meusi huku juu ya macho wakiwa na mistari mfano wa kope yenye rangi nyeusi au kahawia. Huwa na manyoya yenye rangi ya kahawia iliyokolea sana mgongooni huku tumboni wakiwa na rangi nyeupe zaidi ikichanganyika na madoa ya kahawia. Spishi hii ya bundi huishi kwenye misitu au uwanda wa miti na wakati mwingine huweza kukaa kwenye mashamba makubwa. Hufanya shughuli zao wakati usiku tu na ni nadra kuonekana wakati wa mchana.
Bundi misitu huwinda wadudu, reptilian, ndege na wanyama wadogo. Huweka viota vyao kwenye mapando ya miti ambapo jike huatamia hadi mayai matatu kwa mwezi mmoja. Makinda wa ndege hawa huweza kuruka baada ya wiki tano, lakini hukaa chini ya uangalizi wa wazazi wao kwa angalau miezi mine. Ndege hawa hupumzika kwenye viota au mapango yao wakati wa mchana, na jua likikuchwa huweza kusikika wakiitana kwa sauti kubwa. Bundi hawa pia hawako kwenye hatari ya kutoweka duniani.
Bundi misitu
6 Bundi mbuga (African grass owl)
Spishi hii ya bundi kwa muonekano wana sura bapa yenye umbo la moyo, ikiwa na manyoya yenye rangi nyeupe na mdomo uliochongoka. Kwa upande wa nyuma ya vichwa vyao hadi mgongoni huwa na manyoya ya rangi nyeusi iliyochanganyika na kahawia, pamoja na madoa machache meupe au ya kijivu. Majike huwa wakubwa zaidi ya madume na hutaga mayai kati ya 2-5 na kuyaatamia kwa mwezi mmoja au zaidi kwenye kiota kinachotenhenezwa chini kwenye nyasi.
Makinda yakianguliwa huanza kujifunza kuruka yakiwa na umri wa wiki 5 na kuweza kuruka yakifika wiki 7. Wazazi wao huendelea kuyaatunza hadi kufikia wiki 10 ambapo hujitegemea yenyewe kabisa. Bundi hawa hufanya shughuli zao wakati wa jioni, kisha kuendelea tena alfajiri. Huwinda panya, sungura, popo, vyura, karunguyeye na ndege wadogo wasiozidi uzito wa gramu 100. Jumuiya ya kimataifa ya uhifadhi wa mazingira (IUCN) inawataja spishi hii kuwa hawako kwenye hatari ya kutoweka (Least concern).
Bundi Mbuga
7. Bundi ghalani (Common barn owl)
Spishi hii ya bundi imesambaa sana maeneo mengi duniani, na ni miongoni pia mwa ndege waliosambaa zaidi duniani isipokuwa maeneo ya majangwa, safu za milima mirefu na kwenye ncha za dunia na kaskazini mwa bara la Asia. Wanakaribia kufanana na bundi mbuga, lakini nyuma ya vichwa vyao hadi shingoni huwa na rangi ya kahawia iliyokolea ikichanganyikana na kijivu. Manyoya ya migongo yao huwa na rangi ya kahawia ikichanganyika na kijivu au nyeusi iliyopauka, huku upande wa tumbo ukiwa na manyoya meupe.
Bundi hawa hufanya shughuli za kuwinda usiku na wana uwezo mkubwa sana wa kunasa mawimbi ya sauti, hali inayopelekea kuweza kunasa mawindo yao kwa urahisi hata kama yamejificha penye giza totoro. Huwinda wanyama jamii ya panya zaidi, lakini huwinda pia mijusi, ndege, popo na wadudu. Bundi hawa hupevuka wakifika miezi 10 au 11 na hujenga viota kwenye miti au miamba ambapo jike hutaga mayai hadi kati ya 3-5. Mayai huatamiwa kwa mwezi mmoja, ambapo 75% ya mayai huweza kutoa makinda. Makinda hukaa chini ya uangalizi wa wazazi kwa wiki 13 hadi waweze kujitegemea. Spishi hii ya bundi huishi kati ya miaka 18 na 35, lakini kwa nchini Tanzania mara nyingi huishi kwa pungufu ya miaka 5. Spishi hii haipo kwenye hatari ya kutoweka duniani kulingana na takwimu za IUCN.
Bundi ghalani
8. Mtiti wa Afrika (African Scops Owl)
Spishi hii inaundwa na bundi wadogo kutoka kusini mwa jangwa la Sahara, wenye uzito wa wastani wa gramu 65. Spishi hii ya bundi pia wana manyoya yaliyochomoza toka kwenye vishwa vyao mithili ya masikio. Kwa ujumla, spishi hii ya bundi huwa na manyoya yenye rangi ya kijivu na madoa meusi na nyeupe katika miili yao. Wana midomo meusi na miguu yenye rangi ya kahawia. Huwa na macho yenye kubwa karibu sawa na ya binadamu, yenye rangi ya njano na kiini cheusi.
Bundi hawa hufanya makazi kwenye mapango ya miti na mara nyingine huweka viota vyao chini, ambapo jike hutaga mayai 4-6. Huyaatamia mayai hayo kwa siku 28, ambapo makinda hutunzwa kwa angalau miezi miwili kabla hawajaanza kujitegemea. Kulingania na ukubwa wao, bundi hawa hupendelea kula wadudu zaidi lakini pia huwinda panya wadogo na ndege. Bado idadi ya bundi hawa inaridhisha na hawako kwenye hatari ya kutoweka duniani.
Mtiti wa Afrika
9. Bundi wa Pemba (Pemba scops owl)
Kama lilivyo jina lao, bundi hawa wanapatikana kwenye kisiwa cha Pemba pekee. Ni bundi wenye maumbo madogo kiasi, wanaopendelea kuishi kwenye maeneo yenye miti mingi, misitu au kwenye mashamba makubwa ya karafuu na miembe. Rangi za manyoya ya miili yao yana rangi ya kahawia iliyochanganyika na nyekundu pamoja na kijivu na macho makubwa yenye rangi ya njano na kiini cheusi. Hupendelea kuwinda wadudu zaidi kuliko kuwinda wanyama wadogo wadogo kama wafanyavyo bundi wengine. Bado tafiti zinahitajika ili kuweza kupata taarifa zaidi kuhusu maisha yao na uzao wao. Shirika la uhifadhi wa mazingira (IUCN) linataja idadi ya bundi hawa kuwa katika hali isiyo salama (vulnerable).
Bundi wa Pemba
10. Bundi-Tai wa Usambara (Usambara eagle owl)
Hii ni spishi ya bundi inayopatikana nchini Tanzania pekee kwenye milima ya tao la mashariki. Bundi hawa walizoeleka kuonekana milima ya Usambara mkoani Tanga pekee, lakini tafiti za hivi karibuni zimegundua bundi hawa wameonekana pia katika milima ya Uluguru na Udzungwa mkoani Morogoro. Ni bundi wakubwa (uzito hadi gramu 875) wenye rangi ya machungwa na kahawia upande wa mgongoni, na mabaka meupe, meusi na kahawia kwa upande wa tumboni. Bundi hawa huishi kwenye misitu ya milima kati ya usawa wa mita 900 hadi 1500 kutoka usawa wa bahari.
Hufanya shughuli zao wakati wa usiku na huwinda wanyama jamii ya panya, ndege, vyura na wadudu. Hutengeneza viota vyao kwenye mapango ya miti au majabali, na jike hutaga mayai mawili ambayo huyaatamia kwa mwezi mmoja. Bado kuna uhitaji wa tafiti zaidi juu ya maisha ya bundi hawa ili kuwa na taarifa za kutosha. Bundi hawa pia wako kwenye tishio la kupotea kutokana na kuzidi kupungua kwa maeneo rafiki ya wao kuishi, hali inayotokana na shughuli za kibinadamu kwenye misitu ya milima hii.
Bundi-Tai wa Usambara
11. Mtiti Uso-mweupe Kusi (African Southern White-faced Owl)
Spishi hii ya bundi kwa kawaida huwa ni wadogo kiasi (gramu hadi 220) na wana rangi ya kahawia au kijivu pamoja na madoadoa ambayo yanafanana na gome la miti. Nyuso zao huwa na manyoya meupe yakizungukwa na miraba ya manyoya meusi kwenye kingo za nyuso zao. Huwa na manyoya mafupi yaliyochomoza kama masikio yenye ncha nyeusi juu ya vichwa vyao. Wana macho makubwa ya rangi ya machungwa yenye kiini mviringo kikubwa cheusi. Kwa kawaida jike huwa mkubwa kuliko dume.
Mititi huishi kwenye tambarare ya nyasi au uwanda mkavu wa miti na huonekana wakiwa wawili au mmoja. Kwa kawaida huwinda usiku na hula wadudu wakubwa, wanyama na ndege wadogo pia na amfibia. Jike huyataga mayai 2-6 katika shimo lililoachwa na ndege au mnyama mwingine, lakini mara nyingi kinda mmoja tu anakua kufikia kufikia bundi mkubwa. Kinda huondoka kwenye kiota baada ya mwezi mmoja au zaidi. Tafiti zinaonyesha spishi hii ya bundi huwa na mfumo wa umeng’enyaji unaoenda taratibu kiasi kwamba hawahitaji kula mara kwa mara, hali inayowawezesha kuweza kuishi hata kwenye mazingira magumu. Bado idadi ya spishi hii ya bundi inaridhisha na hawako kwenye hatari ya kutoweka.
Mtiti Uso-mweupe Kusi
12. Bundi Madoa (African Barred Owlet)
Spishi hii ya bundi Madoa inaundwa na bundi wadogo wenye vichwa na migongo yenye manyoya ya rangi ya kahawia na madoa meupe, huku sehemu ya tumbo ikiwa na manyoya meupe na madoa ya kahawia. Hupendelea kuishi katika maeneo yenye uoto wa wazi kama vile uwanda wa vichaka, tambarare, kingo za misitu na uwanda wa wazi wa miti.
Kwa kiasi kikubwa bundi hawa hufanya shughuli zao wakati wa mchana ikiwemo kuwinda, na pia huendela na shughuli zao kwenye usiku wenye mbalamwezi inayoangaza. Huwinda wanyama na ndege wadogo, wadudu, reptilia na amfibia. Huweka makazi yao kwenye mapango ya miti na mara nyingi huvamiwa na ndege wengine pindi wanapoonekana kutokana na uadui waliojijengea. Hutaga kati ya mayai 3 hadi 5 na kuyaatamia kwa mwezi mmoja, ambapo makinda hutunzwa na wazazi hadi kujitegemea kabisa baada ya miezi saba. Spishi hii nayo pia bado haiko kwenye hatari ya kutoweka duniani kulingana na IUCN.
Bundi Madoa
13.Kokoko (Verreaux’s eagle-owl)
Kokoko ni spishi ya bundi iliyo miongoni mwa tai-bundi, na ndio bundi mkubwa zaidi katika bara la Afrika. Majike huwa wakubwa zaidi kuliko madume wakifikia uzito wa kilogramu mbili na nusu huku madume yakiwa pungufu ya kilogramu mbili. Huwa na urefu wa mabawa (wingspan) wa wastani wa futi tano, ambapo huweza kuzidi ikiwa watafugwa na binadamu. Sehemu kubwa ya miili yao huwa na rangi ya kijivu pamoja na kahawia iliyopauka, lakini huwa na kope za rangi ya waridi kuzunguka macho yao ikiwa ndio sifa ya kipekee tofauti na bundi wengine wote.
Spishi hii ya bundi huishi zaidi kwenye tambarare yenye nyasi na miti isiyo na mvua nyingi katika ukanda wa Afrika, ikiwemo Tanzania. Hufanya shughuli zao usiku, huku mchana wakionekana wamejipumzisha kwenye matawi ya miti mikubwa iliyo na kivuli kizuri. Kama bundi hawa hawana makinda au jike hana kiota chenye mayai basi mara nyingi hujipumisha kwenye miti ambapo asubuhi imewakutia huko kutokana na uoni wao hafifu wakati wa mchana.
Kokoko hujenga kiota juu ya mti mrefu na jike hutaga wastani wa mayai mawili, na kuyaatamia hadi siku 38. Makinda yakianguliwa, huweza kupaa baada ya takribani wiki saba na huruka karibu na wazazi wao na kukaa pamoja kwa angalau miezi mitano. Kokoko ni wawindaji hodari sana miongoni mwa jamii za ndege, na huweza kuwinda sungura, panya buku, kalunguyeye, nyoka, ndege wengine na mara chache wadudu. Kokoko pia huweza kuwinda ndege wakubwa kama kanga, kware na jamii za bundi wengine kama bundi mbuga. Kwa takwimu za pamoja inaonyesha bado idadi ya Kokoko inaridhisha japo kwenye baadhi ya mataifa ya kusini mwa Afrika idadi yao inapungua kwa kasi.
Kokoko (Chanzo: eBird)
14.Bundi mvuvi wa Pel (Pel’s fishing owl)
Hii ni jamii ya pili kwa ukubwa Afrika baada ya kokoko, na hufahamika zaidi kama bundi wavuvi. Bundi majike huweza kufikia uzito wa kilogramu 2.3, huku madume wakiwa pungufu ya kilogramu 1.8 na huishi kwenye maeneo yenye vyanzo vya maji kama mito, mabwawa na maziwa. Huwa na manyoya yenye rangi mchanganyiko wa kahawia na nyekundu au kama chuma kilichopata kutu. Wanapatikana kwa uchache kabisa katika nchi ya Tanzania, na wameweza kuonekana Mikoa ya kusini Mashariki mwa nchi.
Huwinda usiku kwenye maeneo yenye maji yasioenda kwa kasi, na huwinda samaki au vyura kwa kuwakamata kutoka kwenye uso wa maji au kwenye kingo za mto/ziwa. Huweka pia viota vyao kwenye miti karibu na maeneo hayo ya vyanzo vya maji ambamo huwinda. Jike hutaga mayai mawili na kuyaatamia kwa siku 32, ambapo mara nyingi kinda moja tu huanguliwa na kukua. Kinda hilo hukuwa na wazazi wake kwa miezi mitatu au zaidi kabla ya kujitegemea. Bundi hawa hupendelea kukaa wawili (dume na jike) wakati wa mchana, na wakati mwingine hulazimika kuwinda mchana endapo chakula ni haba. Idadi kamili ya spishi hii ya bundi bado haijafahamika lakini bado hawajawekwa miongoni mwa viumbe wanaokaribia kutoweka.
Bundi aina ya Pel’s fishing owl
Sifa za pamoja
Spishi zote za bundi zina manyoya mepesi sana na yaliyopangana kwa mfumo ambao hayakinzani na upepo. Hii huwawezesha bundi kuweza kuruka kwa ukimya mkubwa na kuwashtukiza mawindo yao. Ukimya huu hufanya baadhi ya binadamu kudhani kuwa bundi hutokea kwa mazingira yasiyo ya kawaida katika maeneo yao kwani hawawasikii wakiruka au kutua. Bundi pia hawana huwezo wa kugeuza macho yao, lakini wanaweza kuzungusha shingo zao hadi nyuzi 270 (2700), na kutazama nyuma au pembeni bila kugeuza mwili mzima.
Bundi wote wana macho ya duara yanayoelekea mbele, na spishi nyingi za bundi huwa na uwezo mdogo wa kuona kitu kilicho karibu sana na macho yao, lakini huona vyema sana kitu kilicho mbali. Uwezo wao wa kuona penye mwanga mdogo au giza totoro ni mkubwa sana ukilinganisha na ndege wengine. Miongoni mwa sababu zinazowafanya bundi kupendelea kufanya shughuli zao usiku ni kuepuka ushindani na ndege wengine wawindaji kama tai na mwewe. Bundi pia hukumbana na maadui wengi mchana wakiwemo jamii tofauti za ndege ambao huwazonga na kuwafukuza bundi pindi wanapowaona.
Bundi humeza mawindo yao kama wadudu, panya au mijusi yakiwa mazima, lakini mfumo wao wa umeng’enyaji hauwezi kumeng’enya manyoya na mifupa. Mabaki ya vyakula yasiyoweza kumeng’enywa tumboni mwao hukusanywa mfano wa matonge madogo ambayo huyatapika. Bundi wengi pia hawajengi viota vyao bali huchukua viota vya ndege wengine au mapango yaliyo kwenye miti au majabali. Bundi hukaa na mwenzi mmoja maisha yao yote ambapo atamchukua mwenza mwingine endapo tu mwenza wake amefariki. Makala nyingine nzuri kuhusu Bundi unaweza kusoma hapa Mfahamu Ndege Bundi, Tabia Zake Na Uhalisia Kuhusu Bundi
Changamoto Zinazowakabili.
Sumu za mashambani na majumbani – Tafiti zinaonyesha kwamba bundi wengi wengi wanaathirika kutokana na kula wanyama au wadudu waliothiriwa au kufa kutokana na sumu za mashambani au majumbani. Hii huchangia kupoteza idadi kubwa ya bundi maeneo ya vijiji hata miji pia
Imani za Kishirikina – Zipo baadhi ya jamii za watu nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla waowahusisha bundi na Imani za kishirikina kutokana na aina yao ya maisha. Hii hupelekea kuwaua au hata kuharibu viota vyao na mayai yao ili kuwaondoa. Wengine huenda mbali zaidi na kutega sumu ili waweze kuwaangamiza bundi hao wasiendelee kukaribia makazi yao.
Kupotea kwa makazi rafiki – Shughuli za kibinadamu zinazoambatana na ukataji wa miti na uchomaji wa misitu husababisha bundi wengi kulazimika kuhama na kupunguza kuzaliana. Hali ya mabadiliko ya tabia ya nchi pia husababisha baadhi ya bundi wanaopendelea kuishi kwenye misitu minene nao kuathirika.
Imeandaliwa na kuandikwa na Ezra Peter Mremi na kuhaririwa na Hillary Mrosso. Kwa maoni, ushauri, maswali au mapendekezo kuhusu makala hii unaweza kuwasiliana na mwandishi.
Ezra Peter Mremi
Phone No: 0786078728/0756438692
Email: mremiezra@gmail.com