Ardhi oevu ni eneo lenye uwazi mkubwa wenye maji mengi yatokayo katika vyanzo mbalimbali kama vile mito, vijito, mifereji na mitaro ambayo huweza kuwa ya msimu au ya kipindi chote cha mwaka. Maeneo haya ya ardhi oevu kama ya Usangu yamejaliwa kuwa na aina mbali mbali za mimea ya majini na nchi kavu yasiyopoteza maji kiurahisi.  Pia maeneo haya yana utajiri mkubwa wa virutubisho vingi kama majani yaliyooza na wadudu wa jamii tofauti ambao hutumika kama chakula kwa ndege na wanyama.

Ardhi oevu hii ya Usangu hupatikana katika uwanda wa chini wa tambarale ya bonde la Usangu ambalo lipo katika wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya. Hii imepelekea kuwa na mwonekano kama kitako cha bakuli iliyozungukwa na milima pande zote kama vile vilima vya Udzungwa kwa upande wa kaskazini mashariki, Mpanga – Kipengere upande wa kusini magharibi na uwanda wa juu wa vilima vya Lupa ambavyo hupatikana upande wa mashariki.

Picha; mwonekano wa tambarale wa bonde la Usangu kipindi cha mvua na milima kwa mbali

Tambarale hii ya bonde la Usangu ina ukubwa unaokadiliwa kuwa kilomita za mraba 15500 ambazo kati ya hizo, 1800 ni ardhi oevu tu. Na mnamo mwaka 2008, upande wa mashariki wa tambarale na ardhi oevu wenye ukubwa wa kilomita za mraba 6000 ulichukuliwa na kuwa chini ya hifadhi ya taifa ya Ruaha. Eneo hili lilipandishwa hadhi na serikali kutokana na mchango wake mkubwa katika mfumo wa ikolojia ya hifadhi ya Ruaha na maendeleo ya taifa kwa ujumla.  

Ardhi oevu na tambarale iliopo ndani ya hifadhi imezungukwa na uoto mbalimbali wa asili ikiwemo uoto wa miombo, uoto wa misitu kando ya mto mkuu wa Ruaha, nyasi ndefu na uoto upatikanao kwenye ardhi oevu ya muda mfupi (msimu) na ile ya kipindi chote cha mwaka. Ardhi oevu hii imegawanyika katika sehemu kuu mbili, ile ya upande wa magharibi ambayo ipo upande wa juu na ile ya mashariki/Ihefu ambayo ipo upande wa chini.

Ardhi oevu inayopatikana upande wa juu ndio hupokea maji mengi kutoka milima ya nyanda za juu kusini kupitia mito mikubwa kama vile Ndembera, Mbarali, Lunwa, Gwiri, Kimani, Chimala na mito midogo kama vile Mambi, Kioga, Mjenge, Kimbi, Itambo na Mswiswi. Kisha maji haya humwagwa kwenye ardhi oevu ile ya Ihefu. Sehemu hii ya Ihefu ipo hatarini kutoweka kutokana na uvamizi wa shughuli za binadamu. Maji haya yote kutoka aina hizo mbili za mito hukutana na kutengeneza mto mkuu wa Ruaha. Na sehemu hiyo ya makutano ya mito hii, kuna kivutio cha utallii wa kimila ambapo kuna ghofu la nyumba aliyoishi kiongozi/chifu wa kabila la wasangu aliyeitwa Ng’iriama.

Hivyo, maji ya ardhi oevu zote mbili kupitia mto mkubwa Ruaha ndio huwezesha maisha ya viumbe vipatikanavyo ndani ya hifadhi ya taifa ya Ruaha kwa kujipatia chakula, maji na sehemu ya mazalia hasa kwa samaki na reptilia pamoja na matumizi mbalimbali ya wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi.

Maji haya huchangia kwa asilimia kubwa maendeleo ya nchi kupitia mto mkuu Ruaha ambao husafirisha maji umbali wa kilomita 500 na kumwaga maji yake kwenye mabwawa mawili ya umeme. Bwawa la kwanza la umeme ni stesheni ya Mtera yenye uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 80. Bwawa la pili ni kidatu, ambalo lipo mkoa wa Morogoro na lina uwezo wa kuzalisha megawati 200. Baada ya kuzalisha umeme katika mabwawa tajwa hapo juu, mto huu huunganika na mito mingine midogo na kisha kumwaga maji yake mto kilombelo ambao maji yake huingia katika bwawa kubwa zaidi la kuzalisha umeme la Mwal Nyerere. Umeme utakao kuwa unazalishwa na bwawa hili, ndio mkubwa zaidi Afrika mashariki yote.

Hivyo, ardhi oevu hii ya bonde la Usangu ina faida nyingi kwa wanyamapori, maendeleo ya nchi kwa kuwezesha shughuli za kijamii na kiuchumi. Upande wa kijamii maji haya yamekuwa na matumizi makubwa katika kilimo cha mpunga ambao ni chanzo kikubwa cha fedha kwa wananchi wengi kuanzia Usangu hadi bonde la kilombero. Vile vile shughuli za uvuvi zimekuwa zinafanyika katika eneo kubwa ambalo maji haya yanapita.  Pia, ardhi oevu zina faida nyingine kama vile ufugaji, upandaji wa miti ya mbao na zina sehemu nzuri kwa utalii, tafiti za kisanyansi kwa wanyama, mimea, wadudu na ndege.

Kwa ujumla, maeneo yote duniani yenye ardhi oevu yanakadiriwa kuchukua eneo la ardhi lenye ukubwa wa asilimia 9% ambayo ni nafasi ndogo sana japokuwa faida zake ni kubwa. Hata hivyo yanakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zisipotatuliwa kwa uharaka tunaweza yapoteza na kusahaulika kabisa. Changamoto hizo hasa kwa bonde la Usangu ni uelewa mdogo wa wananchi juu ya umuhimu wa ardhi oevu unaopelekea uvamizi wa shughuli za kibinadamu kama vile uvuvi na ufugaji (hutumia sehemu ya ardhi oevu kwa malisho ya mifugo). Changamoto nyingine katika maeneo haya ni mabadiliko ya tabia nchi pamoja na misukumo ya kisiasa.

Kutatuliwa kwa changamoto hizi kutawezesha upatikanaji wa malisho na maji kwa wanyamapori wanaotegemea mto huu, upatikanaji wa maji salama kwa wananchi wakaao pembezoni mwa mto, uzalishaji mkubwa wa umeme ambao utawezesha uzalishaji mwingi wa bidhaa viwandani pia kutafanya eneo lote kuwa la kijani na la kuvutia zaidi kwa utalii.

Makala hii imehaririwa na Alphonce Msigwa, Mwikolojia wa hifadhi za Taifa Tanzania.

Kwa ushauri au maswali kuhusu makala hii, usisite kuwasiliana na mwandishi,

Leena lulandala

lulandalaleena@gmail.com

0755369684