Habari ndugu wasomaji wa makala hizi za wanyamapori na pole kwa majukumu mazito ya kulijenga taifa. Katika kuadhimisha wiki ya NENDA KWA USALAMA BARABARANI natamani wote kwa pamoja tuadhimishe wiki hii kwa kujuzana machache kuhusu ajali mbali mbali ambazo zinahusisha vyombo vyetu vya usafiri na wanyamapori. Wiki hii ya nenda kwa usalama barabarani ni muhimu sana ndugu zangu kwani mbali na wanyamapori hata binadamu pia huwa kuna changamoto nyingi  tunakutananazo barabarani.

Utangulizi

Ajali zinazo husisha vyombo vya usafiri na wanyamapori hapa nchini zimekuwa mwiba mkali  katika shughuli za uhifadhi wa wanyamapori. Kwa  miaka mingi  kumekuwa na vifo vya wanyamapori vinavyotokana na ajali za barabarani hasa katika maeneo ya hifadhi za taifa, mapori ya akiba na shoroba ambazo zimekuwa zikitumiwa na wanyamapori kutoka eneo moja kwenda jingine. Ajali hizi zimekuwa zikisababishwa na madereva ama kwa kukusudia au bahati mbaya japo bado haibadilishi hija kuwa tunapoteza rasilimali zetu kwa njia rahisi sana.

Kuna barabara nyingi zimepita au kupakana na hifadhi za taifa na maeneo ya mapori ya akiba ambayo kwa mwaka hushuhudiwa ajali nyingi za vifo vya wanyamapori. Miongoni mwa maeneo ni pamoja na Hifadhi ya taifa ya Mikumi kwani ndani ya hifadhi hii inapita Barabara  kubwa ambayo inatumiwa na magari yaendayo mikoa na nchi mbalimbali. Sehemu nyingine ni barabara ya kwenda Ifakara ambapyo inapita kando kando ya Hifadhi ya taifa Milima  Udzungwa, barabara ya kwenda Arusha kutokea Babati ambayo inapita katika ushoroba wa  Kwakuchinja, barabara ya kuelekea Eneo la hifadhi ya Ngorongoro hasa kuanzia hifadhi ya taifa ya Ziwa Manyara, barabara ya kuelekea Musoma hasa maeneo ya Hifadhi ya taifa ya Serengeti na baadhi ya maeneo mengi.  Lakini pia hifadhi zingine ambazo zinapitiwa na barabara kuu ni Katavi, Burigi-Chato, Mkomazi, Saadani n.k

Pamoja na kuwa na barabara hizo, tunafahamu kuwa serikali inatumia gharama kubwa  katika kuendesha shughuli za uhifadhi chini ya mashirika yake kama vile Mamlaka ya Ngorongoro (NCAA) Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania, (TANAPA) na Mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori (TAWA). Hivyo sisi kama wananchi na wadau tunapaswa kuunga mkono jitihada hizi kwani  mapato yatokanayo na  shughuli za uhifadhi hususani  utalii hutunufaisha sote bila kujali maeneo tunayoishi ama yanapakana na hifadhi za wanyamapori au yako mbali zaidi na hifadhi hizo. Soma zaidi hapa Kilio Kisichoisha Ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi

Vyanzo vya ajali za Barabarani

Matendo yetu ndio mwiba mkali kwenye maisha ya wanyamapori ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakiishi katika maeneo yao ya asilia. Hivyo binadamu amekuwa ndio sababu kubwa za ajali za barabarani na kuleta madhara kwa wanyamapori. Baadhi ya vyanzo vikuu vya ajali hizo ni Pamoja na;

1.Mwendo Kasi;  Mwendokasi ni chanzo kikubwa cha ajali za wanyamapori ukilinganisha na vyanzo vingine. Baadhi ya madereva huwa hawajali kabisa au kufuata vibao vinavyo elekeza mwendo wa kutembea hasa kwenye maeneo yenye wanyamapori. Mfano  katika hifadhi ya taifa Mikumi kwa mwaka huwa wanagongwa zaidi ya wanyamapori 100 na miongoni mwao ni wanyama walio hatarini kutoweka duniani kama tembo na twiga.

2.Ulevi; Kuna baadhi ya madereva huwa wanaendesha vyombo vya moto wakiwa wamelewa na hivyo huwapelekea kushindwa kuzingatia sheria za barabarani. Kuendesha gari ukiwa umelewa hupelekea ama kuendesha gari kwa kasi au kuendesha nje ya eneo la barabara hasa kutokana na kuyumba kitu ambacho husababisha kuwagonga wanyamapori ambao wanapenda kutafuta chakula maeneo ya kando kando ya barabara lakini hata kwa wale wanao pumzika katika maeneo hayo. Kuna baadhi ya wanyamapori hasa walao majani hupenda maeneo kama hayo kwani huamini pia wanakuwa salama zaidi kwasababu wanyama wanaokula nyama huwa ni nadra sana kuonekana maeneo ya kando kando ya barabara. Hivyo kitendo cha kulewa na kuendesha gari husababisha ufanisi wa akili ya dereva kupungua na kwa asilimia kubwa matokeo yake ni ajali.

3.Kutozingatia Sheria za Barabarani; Kushindwa kuzingatia kwa sheria za barabarani kuna athari kubwa hususanani katika maeneo ambayo hutumiwa na wanyamapori.  Kuna baadhi ya madereva husimama na kupisha wanyamapori wavuke barabara lakini mwingine anakuja na kuamua kumpita mwenzie bila kujiuliza ni kwanini mwenzake kasimama na hatimae kugonga wanyamapori.

4.Usingizi; Hii hutokea kwa bahati mbaya na hata hivyo kutokana na tafiti ajali za wanyamapori zitokanazo na kusinzia kwa dereva huwa ni chache. Kuna baadhi ya madereva huwa wanachoka  na kulazimika kuendelea kuendesha gari hali ambayo huwapelekea kugonga wanyamapori katika hifadhi za taifa na maeneo mengine ya mapori ya akiba. Kuna wakati unapita hata mwaka husikii kuna ajali ya wanyamapori ilotokana na dereva kusinzia. Hii inatupa jibu kuwa sababu hii inachangia sehemu ndogo ya ajali za wanyamapori ukilinganisha na sababu ambazo nimezielezea hapo juu kama mwendokasi, ulevi na kutozingatia sheria za barabarani.

Baada ya kujua kuhusu visababishi vya ajali zinazotokea kati ya vyombo vya moto na wanyamapori, sasa tujifunze namna ajali hizo zinvyoleta athari katika uhifadhi;

1.Kupungua kwa idadi ya Wanyamapori; Kupungua huku ni changamoto kwa ikolojia ya wanyamapori  kwani hakutokani na maumbileasili ambayo huwa ni lazima itokee ili kuweka usawa katika mazingira. Kitendo cha mnyama kupoteza maisha kutokana na shughuli za kibinaadamu au ajali ya gari moja kwa moja huingilia asili ya mazingira.

2.Tishio kwa wanyamapori walio hatarini kutoweka duniani; Hii ni miongoni mwa athari kubwa  ya ajali za wanyamapori na sio hapa Tanzania tu bali duniani kote. Mfano katika hifadhi ya taifa Mikumi huwa kuna ajali nyingi  zinazo wahusisha tembo. Tukumbuke tembo ni miongoni mwa wanyama waliyopo hatarini kutoweka duniani. Hivyo kitendo cha kumgonga tembo kinazidi kuwaweka wanyama hawa katika hatari zaidi ya kutoweka hasa kutokana na kuzaliana kwa wanyama hawa ambao huchukua miaka mingi sana mpaka familia ya tembo kuwa kubwa. Hawana tofauti kubwa  na binaadamu katika kukuza idadi yao kwenye familia hivyo akifa mmoja kwa ajali basi inakuwa ni pigo kubwa kwa familia ya tembo.

3.Mabadiliko Hasi ya Kiikolojia; Ajali za wanyamapori zinapo ongezeka huathiri moja kwa moja ufanisi wa ikolojia ya eneo hilo. Mfano kwa mwaka tukipoteza  wanyama wanaokula nyama mfano Simba katika eneo moja hali hii inaweza kusababisha idadi ya wanyama wanaokula majani kuongezeka kwa wingi  na kusababisha eneo hilo kuwa dogo kutokana na wingi wao. Eneo linapokuwa dogo huwa kuna changamoto nyingine zinatokea hasa upungufu wa chakula, maeneo ya kunywa maji, maeneo ya kupumzika na vurugu kubwa linapokuja suala la kuzaliana.mwisho. Wanyama hao wanaweza kuanza kwenda katika maeneo ya nje ya hifadhi na hvyo kuanza kusababisha migongano na binadamu.  Lakini uwepo wa wanyama walao nyama katika eneo hilo husaidia kuweka usawa wa kiikolojkia kwani huwapunguza wanyama walao majani kwa kuwala kitu ambacho tunaita ni asili katika wanyamapori na mazingira yao.

4.Kupungua kwa Shughuli za Utalii; Utalii siku zote huwa imara kutokana na uwepo wa vivutio eneo fulani. Kuna baadhi ya wageni wanakuja kutoka sehemu mbali mbali duniani ili kuwaona wanyamapori. Endapo idadi ya wanyama hawa itapungua kutokana na kugongwa na magari na kupelekea kuonekana kwa shida  basi itapelekea idadi ya wageni pia kupungua  kwani hawatokuwa na sababu ya kutembelea maeneo ambayo wanajua kabisa kuwaona baadhi ya wanyama ni kazi. Hali hii hupelekea hata kupungua kwa mapato yatokanayo na shughuli za utalii.

5.Kupungua kwa Fedha za Kigeni; Kupungua kwa idadi ya wageni nchini hupelekea kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi kwani shughuli za kitalii huchangia kwa kiasi kikubwa. Hali kadhalika upatikanaji wa fedha za kigeni hususani dola ya Marekani pia utapungua  kutokana na kupungua kwa idadi ya wageni ambao kwa kiasi kikubwa huchochea upatikanaji wa fedha za kigeni hapa nchini kutokana na shughuli za kitalii ambazo zinaendelea.

Nini Kifanyike Kupunguza ajali kwa Wanyamapori

  • Mamlaka husika za usalama barabarani hasa Jeshi la Polisi lihakikishe linatoa elimu kwa madereva tena kwa kushirikiana na mamlaka za uhifadhi wa wanyamapori. Elimu hii ijikite katika umuhimu wa kuwalinda wanyamapori na faida zake, matumizi sahihi ya barabara lakini pia kupunguza mwendo katika maeneo yenye wanyamapori.
  • Madereva wahakikishe wanaepuka kutumia vilevi hasa pombe, bangi au mirungi pale wanapokuwa wanaendesha magari. Hali ya ulevi hupunguza ufanisi wa dereva katika kuendesha gari kitu ambacho hupelekea kutokea kwa ajali nyingi  na kusababisha kupungua kwa idadi ya wanyamapori. Si wanyamapori tu bali hata kwa binaadamu pia kwani kumekuwa na ongezeko la watu kupata ajali kutokana na madereva kuendesha magari wakiwa wamelewa au kutumia bangi.
  • Dereva anapohisi usingizi basi ahakikishe anasimamishe gari na apumzike kwanza. Hii sio kwa waliyopo nje tu bali hata kwa usalama wake mwenyewe na ambao yukonao kwenye gari kwani usingizi unaweza kusababisha akapata ajali hata kama sio kugonga mnyama au binaadamu, anaweza kujikuta kaingia kwenye mtaro au kuporomoka kwenye makorongo kisa tu alikuwa anasinzia.
  • Serikali ijitahidi  kupitia mamlaka husika za usimamizi na uhifadhi wa wanyamappori kuweka kamera kwenye hifadhi za taifa na maeneio mengine ya hifadhi za wanyamapori. Hii itapunguza ajali kwa kiasi kikubwa  kwani kuna baadhi ya madereva huwa wanakimbia baada ya kugonga mnyama kwasababu wanakuwa hawaonekani. Lakini kama kutakuwa na kamera katika maeneo mbali mbali basi ni rahisi kutambua gari lililo sababisha ajali na hata kumpata dereva husika. Hii pia itasaidia kujua madereva ambao wanakiuka au hawafuati sheria za barabarani mfano mwendokasi.
  • Faini za ajali zote zinazo husisha wanyamapori zisimamiwe kwa ufasaha zaidi ili iwe fundisho kwa madereva wazembe wanao sababisha ajali kwa wanyamapori. Tuepuke kuingia katika wimbi la rushwa ili kuhakikisha mtu anapata adhabu kutokana na kosa alilotenda bila kumuonea au kuchukua rushwa na kutohukumiwa kama wengine. Faini zote ziorodheshwa kwenye tovuti nahata kwenye vipeperushi mbali ili kila dereva awe na ufahamu na kujua endapo atatenda kosa la kumgonga mnyamapori basi ajue adhabuyake.

Hitimisho

Tunapo adhimisha wiki ya nenda kwa usalama barabarani hatuna budu kuwa mabalozi kwa kila mmoja wetu ili kuhakikisha usalama wa  wanyamapori wetu. Wapo watu ambao ni wabinafsi hawaoni thamani ya uwepo wa wanyamapori katika nchi yetu kwasababu tu hawaoni faida ya moja kwa moja ambayo inawagusa wao binafsi. Endapo tutakuwa mabalozi wazuri wa kutoa elimu kwa madereva haw abasi tutasaidia kwa kiasi kikubwa  kupunguza matukio ya wanyamapori kugongwa.

Hii si kwa upande wa wanyamapori tu bali hata kwa usalama wetu pia. Kumekuwepo na ajali nyingi  ambazo zimepelekea familia nyingi  kubaki na huzuni kwa kuwapoteza wapendwa.

Asante sana kwa kusoma makala hii, naamini utaenda kuyafanyia kazi yote uliyojifunza hapa,

Makala hii imeandikwa na Sadick Omary Hamisi na kuhaririwa na Alphonce Msigwa.

Kwa mengi zaidi kuhusu wanyamapori basi wasiliana nami kupitia;

 

Sadick Omary Hamisi

Simu; 0714116963

Email; swideeq.so@gmail.com

Instagram; wildlife_articles_tanzania

Facebook; Sadicq Omary Kashushu/Envirocare and wildlife conservation

Tovuti; www.wildlifetanzania.co.tz