Habari za siku kidogo ndugu msomaji wa makala za wanyamapori. Nikuombe radhi kwa kuwa kimya kidogo kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu lakini nimerudi tena kukujuza juu ya rasilimali zetu za wanyamapori tulizo jaaliwa. Vijana wanasema kazi juu ya kazi, basi mimi nakwambia makala juu ya makala. Leo tutahama kidogo toka upande wa mamalia na kwenda upande wa ndege tena ili kuweza kuwajua na ndege tulionao hapa nchini kwetu hususani katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori. Kuna jamii nyingi sana za ndege duniani ambao wamegawanyika katika makundi mbalimbali wakiwemo wanaoruka na wasioruka.
Sasa leo tutamuona ndege mmoja hivi ambae ndio ndege mkubwa kuliko ndege wote duniani wanaoruka. Ndege huyu anajulikana kwa jina la “TANDAWALA”
Sasa kabla sijaendelea ningependa ufahamu kuwa Tandawala hawa wamegawanyika katika jamii mbili ambazo ni Tandawala Somali ambao wanapatikana sana maeneo ya kaskazini na mashariki mwa Afrika na Tandawala ambao wana patikana maeneo ya kusini mwa Afrika. Katika makala hii tutamzungumzia Tandawala Somali japo sifa za jamii mbili hizi zina fanana sana kwa kiasi kikubwa.
SIFA NA TABIA ZA TANDAWALA SOMALI
1.Ndio ndege mzito kuliko ndege wote wanao ruka duniani.
2.Wana miili mikubwa, shingo nene na ndefu huku miguu ikiwa na rangi ya njano.
3.Uso na shingo vina rangi ya kijivu huku sehemu ya taji kichwani mwake pakiwa na rangi nyeusi.
4.Sehemu ya chini shingoni wana alama nyeusi na maeneo ya mabegani wana mchanganyiko wa rangi nyeupe na nyeusi.
5.Sehemu ya juu mgongoni wana rangi ya kahawia huku upande wa chini wakiwa na rangi nyeupe.
6.Japo jike ana manyoa yafananayo na dume lakini manyoa ya dume ni mengi zaidi kuliko jike.
7.Hawa ni ndege ambao wanaishi kwa mipaka na mara nyingi huruka pale anapo hisi kuna hatari sana. Hivyo ndege hawa hutumia muda mwingi sana wakiwa chini.
8.Hupendelea sana kufuata makundi ya wanyama kwani huweza kula wadudu ambao wanakuwa wanapatikana katika majani ambayo yameliwa na wanyama au wadudu wanaoruka. Lakini pia hupendelea maeneo yaliyo chomwa kwani sehemu hizi zinakuwa na wadudu wakutosha.
9.Wana alama nyeupe na nyeusi katika mbawa zao.
UREFU NA UZITO
Urefu= Tandawala hufikia urefu wa mita moja nukta mbili (1.2)
Uzito= Kama tulivoona hawa ni miongoni mwa ndege wazito na huwa wanafikia uzito wa 11kg-19kg.
MAZINGIRA
Tandawala hawa hupendelea sana maeneo yenye tambarare na majani ambapo kuna uwazi na uwezekano wa kuona mbali zaidi. Wakati mwingine huishi hadi maeneo ya nusu jangwa.
Maeneo ambayo wanapatikana sana tandawala hawa ni kusini mwa Ethiopia, Kenya na maeneo ya kaskazini mwa Tanzania.
CHAKULA
Ndege hawa wanakula vyakula aina mbali mbali kama panya wadogo, panzi, vyura, mizizi, mbawakawa pamoja na mbegu za mimea mbalimbali.
KUZALIANA
Kabla ya kupandana dume huanza kufanya manjonjo ya kumvutia jike kwa kusimamisha manyoa ya kichwani na kukunja ku ja shingo huku akitanua mkia wake.Wakati anamvutia jike huweza kutoa sauti ya chini ya kumvutia jike na kasha jike kukubali kupandwa.
Baada ya kupandana dume huondoka zake kwani dume huwa haridhiki na jike mmoja (kwa binaadamu tunasema mze wa wake wengi-ndoa za mitara) na dume huwa hana hata muda wakujua malezi ya watoto.
Jike hutaga yai moja au mawili sehemu ya ardhini na hutamia kwa muda wa siku 23 – 24 kisha watoto hutoka kwenye mayai. Watoto huwa chini ya uangalizi wa mama na huanza kuruka wafikishapo kuanzia miezi mitatu na kuendelea. Hata baada ya kuanza kuruka bado uangalizi huwa upo kwa mama na huanza kujitegemea mara tu mama atakapoanza kutamia mayai tena.
Tandawala watoto mara baada ya kuachana na mama huanza kujitegemea kwa kila kitu nao huanza kuzaliana wafikishapo kuanzia myaka miwili. Maisha ya ndege hawa japo bado hayaja julikana ila inasemekana wana weza kuishi myaka 26 hadi 28.
UHIFADHI
Tandawala hawa wanaonekana kwa wingi katika maeneo yaliyo hifadhiwa hususani hapa nchini wanapatikana sana katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Jambo la kushukuru nikwamba ndege hawa bado hawajawekwa kwenye kundi la viumbe walio katika hatari ya kutoweka kutokana na shirika la umoja wa mataifa
linalo shughulika na uhifadhi wa maumbile sasili (International Union for Conservation of Nature- IUCN).
Japo mkataba wa mataifa unao jihusisha na biashara za wanyama na mimea iliyo hatarini kutoweka (Convention on International Trade in Endangered Species of Wild Fauna and Flora-CITES) umewaweka ndege hawa katika nyongeza ya pili hii inamaanisha kwamba Mnyama anaweza kuuzwa kibiashara kwa mataifa mbali mbali lakini ndani ya sheria ambayo ina tambua udumisho wa wanyama hao kisheria.
CHANGAMOTO KWA NDEGE HAWA
1.Ujangili ulio kithiri kwa ndege hawa ndani na nje ya maeneo ya hifadhi za wanyamapori umepelekea idadi ya ndege hawa kupungua sana.
2.Uharibifu wa mazingira ambao unatokana na shughuli za kibinaadamu kama kilimo na uchomaji wa maeneo hovyo umepelekea sana ndege hawa kuhama baadhi ya maeneo kwani ndege hawa hawana uwezo wa kuvumilia mazingira magumu hata kwa kipindi kifupi na hivyo kulazimika kuhama.
3.Biashara haramu ya wanyamapori imepelekea ndege hawa pia kupungua sana kwani watu wamekuwa wakiwauza sana maeneo mbali mbali na hasa wale ambao wapo nje ya maeneoya hifadhi za wanyamapori.
NINI KIFANYIKE HASA HAPA KWETU TANZANIA KUNUSURU NDEGE HAWA
Kama tulivoona hapo juu ndege hawa wanapatikana maeneo ya kaskazini tu mwa nchi yetu hivyo tusipokuwa makini tutawapoteza kabisa. Hivyo inahitajika jitihada binafsi na za uhakika ili kuhakikisha tunaendelea kuwa na ndege hawa hapa nchini.
Kuimarisha ulinzi wa wanyamapori walio ndani na nje ya maeneo ya hifadhi za wanyamapori kwa kuongeza idadi ya askari ili kupambana na suala la ujangili. Ujangili umekuwa ni tatizo kubwa sana hapa nchini kwa upande wa wanyama hivyo lazma kupambana kwa hali na mali.
Kuishirikisha jamii katika masuala ya uhifadhi ili waweze kuwa mabalozi wazuri kwani jamii zitaweza kusaidia katika kufichua majangili na maeneo wanapo patikana. Hii ni kwasababu majangili wengi tunaishi nao katika jamii zetu.
Usimamizi mzuri wa biashara za maliasili hususani wanyamapori ni jambo muhimu sana kwani litasaidia kupambana na biashara haramu ya wanyama hawa. Lakini pia utasaidia kupunguza ukiukwaji wa sheria za biashara na uwindaji wa ndege hawa na hatimae kupunguza changamoto kwa upande wa uhifadhi wa wanyamapori.
Ufuatiliaji wa utekelezaji wa sheria za mazingira chini ya wizara husika ili kupunguza uharibifu wa mazingira kwani tumeona katika makala mbali mbali uharibifu wa mazingira umekuwa ni tatizo kubwa kwa wanyamapori.
HITIMISHO
Tandawala Somali ni ndege ambao wanapatikana maeneo ya kaskazini mwa Tanzania tu kwa hapa nchini na wana umuhimu mkubwa sana katika ikolojia. Hivyo sisi kama jamii hatuna budi kushirikiana na mamlaka husika kama TANAPA na TAWA ili kupambana na biashara haramu za wanyamapori lakini pia kuwafichua majangili kwani wamekuwa wakidhulumu mali zetu kwa manufaa yao binafsi.
Tusi tegemee watu kutoka nje ndo wawe wanafanya kusimamia uhifadhi wa wanyamapori na kufanya tafiti mbali mbali kwani thamani ya kitu lazima uijue mwenyewe muhusika mkuu kabla ya mtu mwingine. Kwasasa watanzania tulio wengi hatuoni thamani ya wanyamapori tulionao lakini siku wakija kutoweka ndo tutakuja kuona thamani yao.
Tuwe mstari wa mbele ili kunusuru maliasili zetu ili vizazi vyetu vya baadae vije kunufaka pia kutokana na maliasili hizi. Ni aibu kubwa sana na hata makosa mbele na Mungu kufuja mali kwa matamanio ya nafsi zetu na kuwasahau wengine ambao wana uhitaji mkubwa sana wa mali hizo, na hapa nagusia hasa vizazi vijavyo kwani nao wata hitaji kuwajua na kuwaona wanyama hawa tulonao kwa sasa.
AHSANTENI….
Kwa mengi zaidi kuhusu wanyamapori lakini pia kwa ushauri juu ya makala hizi wasiliana na mwandishi kupitia,
Sadick Omary
Simu= 0714 116963/ 0765 057969/ 0785 813286
Email= swideeq.so@gmail.com
Au tembelea = www.mtaalamu.net/wildlifetanzania
”I,M THE METALLIC LEGEND”