Sote katika hatua moja ya kukua tumewahi kujiuliza na kuwastaajabia viumbe ambao wanawaka taa Usiku.

Kimulimuli ni jina la kiswahili la mdudu mdogo mwenye ukubwa wa inch 1 ambaye anawaka taa usiku ,ambapo kwa lugha ya kiingereza anajulikana kama Firefly. Jina la kisayansi huitwa Lampyridae ,kuna aina 2000 za Kimulimuli.

Kimulimuli anapatikana katika mabara yote isipokuwa Antarctica, hali ya hewa inayomfaa ni Joto na Kitropiki na hii ndio sababu nchi zingine zenye hali ya hewa ya baridi Kimulimuli huonekana sana katika mwezi Mei na Julai ambapo ni msimu wa joto .

Pichani ni Kimulimuli akiwaka taa sehemu za kuanzia tumboni hadi mkiani

Kimulimuli huonekana vyema katika siku iliyopata mvua mchana na jioni isiyo na joto wala baridi sana pasipo mbalamwezi basi maajabu huanza kutokea utaanza kuona viumbe wenye kumetameta wakiruka ,Kimulimuli anaweza kuwa na rangi ya kijani, njano au machungwa.

Kwanini Kimulimuli anawaka taa usiku.

Kimulimuli anawaka taa ili kuwasiliana ,hii ni muhimu kwa kimuli dume kumvutia jike ili aweze kurutubisha mayai ambayo jike atatagaa baadae . Kuna aina nyingine ya Kimulimuli wao hawawaki taa na huwasiliana kwa harufu zilizo kwenye miili yao.

Kimulimuli anawaka taa ili kuwaonya ama kuwatisha maadui zake kama Popo ambao wanakula wadudu, akiwaka taa huwapa ujumbe wa kaa mbali mimi si mtamu.

Sababu za Kimulimuli kuwa mdudu wa kustaajabisha.

♤Kimulimuli ni mdudu anayetengeneza mwanga wake bila kuhitaji msaada wa betri au chaji hivyo kisayansi huitwa Bioluminescent. Hii ni kutokana na uwepo wa kiungo katika tumbo chenye uwezo wa kuzalisha mwanga .

♤Jambo jingine la ajabu ni kuwa mwanga anaozalisha kimuli ni wa baridi yani hamna joto ,mvuke wa majivu tofauti na vyanzo vingine vya mwanga kama jua ,chemli.

kimulimuli wakati wa usiku.

♤Kimulimuli anauwezo wa kuratibu muda ambao atawaka taa ,mfano kama ni saa moja usiku basi atawaka taa kila saa moja usiku.

Visababishi vya Kimulimuli kuweza kutoweka katika siku zijazo.

Matumizi ya sumu za kuulia wadudu mashambani ambazo mara nyingi hazichagui aina ya wadudu.

Kimulimuli huathirika na uchafuzi wa mwanga hii ni kutokana na taa ambazo binadamu ameziweka nje ya nyumba na barabarani

Mabadiliko ya tabia ya nchi ,hii imeharibu mfumo mzima wa maisha ya Kimulimuli.

Kukosa makazi na chakula uvamizi wa binadamu katika misitu na kuanzishwa makazi ,kilimo na ufugaji imepelekea Kimulimuli kukosa mahali pakutaga, Mabuu yake kufa kwa kukanyagwa vilevile chakula chake kama konokono ambao huliwa na mabuu na chavua inayoliwa na Kimulimuli mkubwa.

Kuvunwa kwa ajili ya kemikali (Luciferase) iliyoko kwenye miili yao kwa ajili ya kutumika viwandani.

HITIMISHO

¤Kimulimuli ni mdudu muhimu katika ikolojia kwa kuwa huleta uiano haswa pale mabuu yake yanapokula viumbe wengine wadogo.

¤Kimulimuli pia ni mdudu ambaye amewahi kukustaajabisha na anawastaajabisha wengi huko Mashariki na kati ya Mexico katika mji wa Tiaxcala ,ambapo ni chanzo cha utalii.

¤Pia Kimulimuli amekuwa msaada katika tafiti, vipimo vya usalama wa chakula na vipimo vya forensiki.

Kwa wema huu wa Kimulimuli ni dhahiri anastahili kutunzwa na kufikiriwa kuwa ni muhimu.

Asanteni sana kwa kusoma makala hii hadi mwisho, usisite kuwashirikisha wengine Makala hii, pia jiandae na makala nyingine bora kabisa.

Maureen FN Daffa

maureen.nick08@gmail.com  

+255 626 331 871.