MBEGA
Neno Mbega ( Colubus) limetokana na neno la Kigiriki likiwa na maana mnyama jamii ya nyani mwenye vidole vinne pasipokuwa na kidole gumba.
Mbega weupe na weusi ni viumbe jamii ya nyani wanao patikana barani Afrika ambapo kuna aina kuu mbili ambazo kwa majina ya kitaalamu hujulikana kama (Colubus angolensins) na (Colubus gueleza) aina hizi mbili zinapatikana Tanzania. Lakini pia kuna makundi madogo madogo ya wanyama hawa wakuvutia , Mbega ni wazawa na wanapatikana Bara la Afrika pekee, hususani ukanda wa nchi za Afrika mashariki na kati.
Mbega aina ya (Colubus angolensis) hawana tofauti kubwa na (Colobus guereza). Mbega hawa wana rangi nyeupe na nyeusi, ambapo rangi nyeupe huonekana maeneo ya mabegani na maeneo ya usoni ndio maana tunawaita mbega weupe na weusi.
Mbega aina ya (Colobus guereza), ameunda umbo linalo fanana na herufi U ingawa sio kamili ukimuangalia kwa makini utagundua hilo, rangi hiyo nyeupe inaanzia bega moja kwenda mkiani hadi bega lingine ingawa sehemu za mkiani haija kolea sana na sehemu kubwa ya uso kwenye mashavu, na masikioni. Lakini mbega wa aina ya (Colubus angolensis) wana alama nyeupe ambazo zina bembea mabegani na sehemu chache za usoni weupe huo haupo masikioni hiyo ndio tofauti yake kubwa.
Leo nitazungumzia mbega weupe na weusi wanaopatikana ukanda wa Afrika mashariki ( Colubus guereza) ambao mengi nitakayo zungumia yatamgusa pia (Colubus angolensis) kwa uchache kwa sababu tabia zao na maisha yao kwa ujumla hufanana kwa asilimia kubwa, tofauti kubwa ni hiyo ya muonekano wa nje.
Mnyama huyu anapatikana maeneo mengi Tanzania, hasa yaliyohifadhiwa kama hifadhi za Taifa, mapori ya akiba, hifadhi za jamii, na hata maeneo yasiyo hifadhiwa nchini Tanzania
SIFA NA TABIA ZA MBEGA WENYE RANGI NYEUPE NA NYEUSI
- Kama nilivyotangulia kusema kwenye utangulizi mbega utamjua kwanza kwa kuona rangi za kuvutia nyeupe na nyeusi. Ambapo rangi nyeusi inachukua sehemu kubwa ya mwili wa mbega, rangi nyeupe kuongeza mngao ambao ndio hubeba maana halisi ya jina la Mbega weupe na weusi. Mabegani, mashavu, shingo, paji la uso na kwenye ncha za mikia wana rangi nyeupe.
- Mbega wana vidole vinne, hawana kidole gumba tofauti na jamii nyingine ya nyani.
- Mbega dume ana umbo kubwa kidogo ukilinganisha na mbega jike.
- Wana mikia mirefu yenye rangi nyeusi, ambapo mwisho una rangi nyeupe.
- Ana macho meusi na makubwa yanayoona vizuri, pia wana masikio makubwa kuwawezesha kusikia vizuri.
- Mbega hawana tabia ya wizi kama aina nyingine ya nyani kwa sababu ya tabia yao ya uchaguzi wa chakula.
- Mbega hutumia muda wa nusu siku wakiwa wamejipumzisha, na muda uliobaki huutumia kutafuta chakula na kucheza juu ya miti kwa madaha. Hivyo unaweza kuwaona muda wa asubuhi sana na jioni jua likiwa limetua.
- Wanaishi katika makundi madogo ambayo yanakua na mwanaume mmoja ambaye ndio baba wa familia na wanawake kuanzia watatu hadi wanne pamoja na kundi rika lenye vijana na mbega
- Muda wa usiku wanalala pamoja kama ilivyo kawaida ya familia, huku wakijitawanya kwenye miti ambayo hujipatia chakula kwa urahisi zaidi
- Kila kundi lina mipaka ya kifamilia inayoeleweka, huwasiliana kwa kutumia ishara na sauti mbalimbali kama kuna uvamizi umetokea, kuweka nafasi kati ya kundi moja na jingine, kuimarisha ulinzi katika kundi pia kuonyesha utawala wa kundi husika.
- Mbega hupendelea sana kukaa juu ya miti, ni nadra sana kuwaona ardhini, kwenye miti wanauwezo wa kuruka toka mti mmoja hadi mwingine kwa madaha umbali upatao Mita 15 ambazo ni sawa na futi 50 bila hofu yoyote, ina aminika manyoya yanayo ninginia mabegani na mkia ndio huwa kama mwamvuli (parachuti) kuzuia wasiweze kuanguka kwa umbali mrefu wanaoweza kuruka.
UREFU, UZITO WA MBEGA
Mbega wana uzito upatao kilogram 4 hadi 14 na urefu upatao sentimita 75,
WASTANI WA MAISHA YA MBEGA
Kwa wastani maisha ya mbega weupe na weusi ni miaka 20 wakiwa porini na miaka 25 hadi 30 wakiwa kwenye uangalizi maalumu “Captivity”. wakiwa msituni au Mazingira yake ya asili, wanakabiliana na changamoto mbalimbali kama kujilinda dhidi ya maadui, uwezo wa kukabiliana na magonjwa, na changamoto za utafutaji wa chakula na pia hutegemea sana majani machanga ya miti na baadhi ya matunda machanga hivyo hufupisha wastani wa maisha yake.
MUUNDO WA KUNDI, MAISHA KWA UJUMLA NA KUZALIANA
Mbega wana makundi maalumu na mipaka inayofahamika kutofautisha kati ya kundi moja la mbega na kundi jingine, ukubwa wa eneo yapata hekari 40 kwa kila kundi, ambapo linatengenezwa na Dume la mbega mmoja, wanawake kuanzia wa 3 hadi 4, vijana, pamoja na watoto, hivyo idadi yao hukamilika kukiwa na kundi lenye wastani wa mbega wa 5 hadi 10 katika kundi moja, Dume la mbega hao likiwa ndio kiongozi wa familia kwa kuweka mipaka na kuhakikisha ulinzi wa kundi hilo.
Kila mbega wana mipaka ya uongozi lakini ni mara chache sana kukuta wanagombana kwa ajili ya kupata mwenza, ingawa inaonyesha kuwa na idadi kubwa sana ya vifo kutokea pindi uongozi wa awali wa kundi kupinduliwa.
Hakuna kipindi sahihi cha kueleweka cha kuzaliana, ingawa kujamiina hutokea sana kipindi cha msimu wa mvua hivyo tunaweza kusema wanazaa kipindi chote cha mwaka, majike hubeba mimba hadi kujifungua kwa muda wa miezi 6 ambapo anajifungua mtoto mmoja, majike ya mbega huzaa kila baada ya miezi 20 kwa wastani.
Watoto wa mbega mara wanapozaliwa rangi yake ni ya kustaajabisha, anakua ana rangi nyeupe katika mwili wake huku uso ukiwa na rangi ya pinki, baada ya mwezi mmoja anaanza kubadilikika na kupata rangi yake ya asili, mtoto wa mbega mara anapozaliwa anakua na wastani wa urefu upatao inchi 7-8 na uzito usiozidi paundi moja, wanatunzwa na wazazi wote, katika uangalizi maalumu muda wingi akiwa tumboni mwa baba au mama, kitu kizuri ni kwamba wazazi wote wanahusika katika kulea watoto au mtoto, kwa miezi kadhaa ya mwanzo kundi lote lina wajibu wa kutunza watoto waliopo katika kundi hilo, wiki 20 mbega mdogo anaanza kuongezeka na kuweza kujitegemea bila uangalizi mkubwa kutoka kwa ndugu zake.
Mbega wa kiume waliozaliwa katika kundi hilo huondoka tu mara wanapokuwa wana uwezo wa kujitegemea, kwa hiari, au kwa kulazimishwa.
Mbega jike hubaki katika kundi alilozaliwa kwa kipindi chote cha maisha.
CHAKULA NA MAKAZI
Mbega hupendelea kuishi kwenye misitu iliyotanda, hasa misitu inayopatikana kandokando ya mito, misitu inayopatikana pwani za Afrika ya mashariki, kutokana chakula chake kinachotegemea sana majani ya miti na matunda hivyo mbega hawa weupe na weusi hupatikana katika misitu mingi ya asili.
Chakula kikubwa cha Mbega ni majani hasa machanga na matunda machanga yanayopatikana juu ya miti. Miti ya aina nyingi zaidi inaweza kutumiwa na wanyama hawa walio na aibu na kuchagua chakula, ikitokea chakula kimepungua wanakula hata majani yaliyokomaa.
Tumbo lao lina uwezo wa kula majani na matunda yenye sumu ambayo jamii nyingine ya nyani hawawezi kutumia chakula hicho, matumbo yao yanafanana na wanyama kama n’gombe kwa jina la kitaalamu ( Mult chambered stomach) na Bacteria ambao wanaweza kusaidia mmengenyo wa majani magumu.
Wanyama hawa wanaweza kupata maji katika vyakula wanavyokula, na maji yaliyotuama kwenye mashimo ya miti baada ya mvua kunyesha.
UHIFADHI
Taarifa kutoka shirika linalosimamia uhifadhi wa maumbile asili Duniani (IUCN – International Union for Conservation of nature). Wanyama hawa wamewekwa katika kundi ambalo linaonyesha kwamba “Least threatened” Wakimaanisha kwamba wanaweza kutoweka endapo Mazingira yao yakiharibiwa, hasa ukataji wa misitu kwa ajili ya maendeleo mbalimbali ya binadamu” shughuli za binadamu, ingawa bado wanapatikana katika maeneo mengi Afrika na Afrika mashariki idadi yao kamili bado haijulikani lakini uharibifu mkubwa utapelekea kutoweka kwa hawa viumbe.
Kwa Tanzania wanyama hawa wanapatikana Hifadhi ya Milima ya Udzungwa, Msitu wa Mkange uliopo kijiji cha Mkange, hifadhi ya taifa Arusha, Msitu wa Kiembe unaopatikana mkoa wa Pwani kijiji cha Mkange, hifadhi nyingi Tanzania kama Udzungwa, Arusha , na maeneo mengi yasiyohifadhiwa.
UMUHIMU WA MBEGA KWENYE IKOLOJIA NA WATANZANIA
- Wanyama hawa ni wala majani kama nilivyotangulia kusema hapo awali, hivyo kwa wanyama wala nyama huwa nichakula chao, hivyo kuweka uwiano sawa wa ki asili, pia husaidia katika usambazaji wa mbegu pindi tu wakila matunda yaliyo komaa ingawa ni nadra sana.
- Wanyama hawa huwa kama kivutio kikubwa cha utalii hii kutokana kwamba wanapatikana Barani Afrika pekee, hivyo huwavutia watu wengi wageni na hata wazawa kuja kuona uzuri wa viumbe hawa huku wakipata nafasi ya kupata historia kuhusu maisha ya wanyama hawa hivyo husaidia kuongeza pato la Taifa na kwa mtu mmoja mmoja.
- Wanyama hawa husaidia watafiti mbalimbali kufanya shughuli zao za utafiti kuhusu mambo mbalimbali ya mnyama huyu, kuzaliwa, vyakula, na mambo kadha wa kadha hivyo kuweza kutimiza ndoto zao kielimu na pia kupata taarifa nyingi ambazo zitasaidia utunzaji wa Mbega hawa weupe na weusi pamoja na misitu.
CHANGAMOTO NA MAADUI WA MBEGA WEUPE NA WEUSI
Maadui wakubwa kwa wanyama hawa ni Chui, Tai wakubwa , na Binadamu
Kwa upande wa binadamu, wamekua chanzo kikubwa sana cha uharibifu wa Mazingira hasa miti ambayo hutegemewa sana na wanyama hawa kwenye kujipatia chakula, kujilinda dhidi ya maadui na maradhi, pia binadamu huwawinda kwa ajili ya kupata ngozi yao kutengeneza ngoma, na kupata mafuvu kwa ajili ya urembo.
Hatari kubwa sana kwa Mbega weupe na weusi ni kuharibiwa kwa makazi yao, kadri maendeleo na ongezeko la binadamu, misitu mingi hukatwa kwa ajili ya kilimo, makazi na kutengeneza barabara, makazi yao yanapotea kwa haraka sana, na hupelekea kutokuwa na maendeleo endelevu kwa hawa wanyama
Kama ilivyoainishwa katika shirika la kusimamia maumbile asili wanyama hawa bado wanapatikana katika misitu mingi kutokana na uwezo wao wa kuishi hata katika misitu iliyoharibiwa lakini ukataji wa misitu hii ukiendelea kwa kasi hivyo kutaweza kupelekea kutoweka kwa viumbe hawa.
NINI KIFANYIKE ILI KUWANUSURU VIUMBE HAWA
Kama nilivyotangulia kusema awali, changamoto kubwa ni uharibifu wa misitu ( Kuharibu makazi ya hawa wanyama) hivyo kwa misitu iliyoharibiwa, nawasihi na kuwaomba wasimamizi wa Misitu Tanzania na Wizara ya maliasili na utalii kutafuta mbinu mbadala ya kugundua na kutafuta maeneo wanayopatikana hawa wanyama na kuyatenga kwa ajili ya uhifadhi wao, mara nyingine kuwahamisha pale inapobidi.
Kuhakikisha upandaji wa miti katika maeneo husika ambapo wanyama hawa wanapatikana.
Wito kwa Watanzania wenzangu viumbe hawa wana umuhimu sana kwetu, hasa wanapopatikana katika maeneo yetu huwa kama kivutio na kuongeza utalii hivyo kutuongezea kipato kwa namna moja ama nyingine, hivyo ni jukumu letu kutunza misitu ili hawa wanyama wawe na ustawi mzuri na hatimae taifa letu kuwa na vivutio vingi, ambavyo tunajivunia kwa uwepo wao.
HITIMISHO
Ukataji miti na uharibifu wa misitu kwa ujumla imekua ni changamoto kubwa sana Duniani kote, Shukrani kwa Wizara zinazozisamia misitu, Maliasili na Utalii kwa jitiada za upandaji miti katika nchi yetu kwani miti ina faida kubwa sana, ukiachana na hawa wanyama ambao nimewazungumzia leo, Miti ndio chanzo kikubwa cha vyanzo vingi vya maji katika uso wa dunia , hivyo husaidia katika kilimo, uvuvi, na Sekta nyingine nyingi ambapo Wizara ya maliasili na utalii pamoja.
Misitu pamoja na Mazingira inafanya jitihada kubwa sana hasa katika kutoa elimu kuhusu umuhimu wa misitu asili na miti kiujumla, pia nitoe shukrani kwa wizara husika kwa kutenga msitu wa Magombera kwa kajili ya kutunza na kuhifadhi rasilimali, Watanzania wenzangu tuungane kwa pamoja ili kuinusuru rasilimali hii Muhimu ambayo ni chanzo cha uhai kwa sababu tunategemeana sana kwa namna moja ama nyingine
NB: “Tafakari” Umezaliwa hapo, umelelewa hapo, umesomea hapo, nyumba yako ndio inakufanya uishi hapo, na shughuli zako unafanyia hapo, kujitafutia pesa ya kula, ya kuvaa, na kulea watoto, yani maisha yako yote umewekeza hapo hauna mahali pengine unapotegemea. Ghafla ikatokea unatakiwa usitishe shughuli zako na nyumba yako ikabomolewa nini kitatokea, utafanyaje?
Ukipata majibu waza upande wa pili wa hawa wanyama viumbe ambao wana utashi mdogo kuliko wewe mwanadamu wanapata masahibu gani hasa pale makazi yao yanapoharibiwa?
Tukutane tena kwenye makala nyingine panapo majaliwa, kwa Maswali, ushauri, na maoni usisite kuwasiliana nami.
Ahsante sana!
Naomi Mnyali +255 788 706 476
Barua pepe: naomimnyali@gmail.com