Habari za siku tena ndugu zangu katika makala za wanyamapori. Leo ni siku nyingine tena tunakutana katika darasa letu huru kuhusu wanyamapori na mengi kuhusu wanyama hawa kwa ujumla. Kama ilivyo kawaida mwisho wa makala iliyopita ndo mwanzo wa makala nyingine. Nami nakualika katika makala nyingine ili ujifunze mambo fulani kuhusu wanyamapori na mazingira yao hali kadhalika uelekeo wa wanyamahawa. Leo tutamzungumzia mnyama mwingine jamii ya swala ambae kwa hakika wengi humfahamu sana hasa kwa jina tu bila kujua undani wa swala huyu na hasa tabia zake. Basi nikusihi kuwa pamoja nami katika makala hii ili kumjua swala huyu. Na moja kwa moja leo tutamzungumzia “NYUMBU”. Wanyama hawa wanapatikana Barani Afrika tu na si sehemu nyingne.

Kabla ya kuendelea na makala hii ningependa ndugu msomaji ujue kwamba kuna jamii kuu mbili za nyumbu ambao ni

1.Nyumbu wa bluu na

2.Nyumbu weusi.

Majina haya hayatokani na rangi za miili yao bali hutokana na rangi za manyoa katika maeneo ya shingoni mwa wanyama hawa. Jamii hizi mbili zina jamii nyingine ndogondogo ndani yake. Sasa leo tutamzungumzia NYUMBU WA BLUU.

UTANGULIZI

Nyumbu wa bluu ni wanyama wanao fahamika na watu wengi sana hasa kutokana na tabia yao ya kuishi kwenye makundi makubwa na tabia zao za kizembe hasa wanapo kutana na maadui zao. Mbali na kuwa wazembe katika mazingira wanayoishi wanyama hawa ni muhimu sana kwa ikolojia ya mazingira lakini pia kuweka usawa wa idadi ya wanyama wengine ambao ni tegemezi kwao.

Mfano mzuri ni kwamba simba ili waweze kuishi watahitaji nyama na maranyingi huwala nyumbu na hivyo kuendelea kuongeza idadi yao kwani uwepo wa chakula huwafanya waendelee kuzaliana. Hivyo kila kiumbe kina nafasi yake kwa wengine katika mazingira kinapoishi kiumbe hicho na hasa hapa nawazungumzia wanyamapori. Kuna wakati watu husema bora simba wafe wote ili wasiwale wenzao bila kujua kuwa kama hatutakuwa na simba au wanyama walao nyama basi idadi ya nyumbu itakuwa kubwa sana na eneo halitatosha kwa wanyama hawa.

Sasa kama kawaida twende kwa undani zaidi kumchambua mnyama huyu kwa vipengele na mwisho wa Makala hii uwe umejifunza mengi kuhusu nyumbu wa bluu.

SIFA NA TABIA ZA NYUMBU WA BLUU

1.Ni miongoni mwa wanyama jamii ya swala wenye kimo kirefu kwenye miguu ya mbele tofauti na walivyo swala wengine.

2.Wana pua lililo tanuka zaidi na pembe zao hufanana na za ng’ombe kabisa.

3.Huishi kwenye kundi kubwa lenye wanyama wengi sana na hata kufikia wanyama zaidi ya milioni 1 huku wakisafiri kutoka nchi moja mpakanchi nyingine hasa kwa ajili ya ya kutafuta chakula, maji na kuzaliana. Kundi hili huwa na nyumbu takribani milioni moja na nusu na mamia ya Pundamilia.

4.Miili yao ina rangi ya kijivu inayo fanana na rangi ya kahawia.

5.Wanyama hawa wana uwezo wa kunusa harufiu sana na kutambua anapotokea adui yao kwa njia hii kwani hawana uwezo wa kuona mbali zaidi kama walivyo swala wengine.

6.Kuanzia nyuma kidogo ya miguu ya mbele wanyama hawa wana mistari iliyo jichora kwa wima mpaka maeneo ya karibu na kichwani.

7.Sehemu ya mbele ya uso wa nyumbu wa bluu huwa na rangi nyeusi huku akiwa na manyoa marefu shingoni.

8.Wote madume na majike wana pembe zilizo jikunja kwa chini upande wa pembeni kabla ya kuelekea juu na kujikunja kwa ndani.

9.Nyumbu hawa wana miili mikubwa tofauti na nyumbu weusi lakini pia mikia yao ina rangi nyeusi tofauti na mikia ya nyumbu weusi yenyewe ina rangi nyeupe.

10.Nyumbu hawa huwasiliana kupitia sauti hasa pale wanapo hisi kuna hatari.

11.Nyumbu ni miongoni mwa wanyama kumi wenye uwezo wa kukimbia kwa kasi zaidi duniani na wana uwezo wa kukimbia umbali wa kilometa themanini kwa saa (80/saa).

12.Miili ya nyumbu ukiichunguza vizuri utagundua wamefanana na wanyama aina tatu. Yaani kichwa cha Nyumbu kinafanana na kichwa cha panzi, mwili anafanana na ng’ombe na mkia ni kama wa farasi.

13.Katika kundi kubwa ndani yake huwa na makundi madogo mdogo ambayo kila kundi huwa chini ya uongozi wa nyumbu jike na hugawa madaraka ya usimamizi hususani wakati wa kusafiri.

14.Wanapo safari, hutumia umbali wa kilometa 922km hadi 1852km, na wanapo safari huangalia sana hali ya hewa japo mara nyingi safari huanza kati ya mwezi wa tano na mwezi wa sita.

UREFU, KIMO NA UZITO WA NYUMBU WA BLUU

Urefu=Kichwa na kiwiliwili huwa na urefu wa sentimita 150sm – 240sm, huku mkia ukiwa na urefu wa sentimita 60sm – 100sm.

Kimo=Nyumbu hawa hufikia kimo hadi futi 4.2 hadi futi 4.6

Uzito=Uzito kati ya jike na dume huwa tofauti. Dume huwa na uzito mkubwa kuliko jike ambapo hufika uzito wa kilogramu 290kg huku jike hufikia uzito wa kilogramu 260kg.

Je, unajua kwanini wanyama hawa huishi pamoja na Pundamilia?

Maranyingi nyumbu huonekana wakiwa pamoja na Pundamilia katika makundi yao na hata wanapo kuwa wanasafiri. Hii ni kwasababu Nyumbu wana uwezo wa kunusa harufu zaidi kuliko Pundamilia na wanapo hisi harufu ya adui huanza kukimbia basi na Pundamilia hukimbia kufuata uelekeo wa Nyumbu.

Pundamilia ana uwezo wa kuona mbali zaidi kuliko Nyumbu, hivyo ikitokea kaanza kumuona adui kabla Nyumbu hajahisi harufu basi hukimbia na Nyumbu hufuata uelekeo wa pundamilia.

Hivyo wanyama hawa hutegemeana sana kwani mmoja ana uwezo wakunusa zaidi kuliko kuona mbali na mwingine ana uwezo wa kuona mbali kuliko kunusa zaidi.

MAZINGIRA

Nyumbu hawa wanapendelea sana maeneo yenye majani na miti miti hasa sehemu yenye miti jamii ya Michongoma sana hali kadhalika sehemu yenye vichaka. Mazingira haya pia ni mazuri kwa Nyumbu kwani wanapendelea sehemu ambayo sio kavu sana wala isio na maji maji sana.

Nchi ambazo Nyumbu wa Bluu wanapatikana sana ni Tanzania, Kenya, Zambia, Namibia, Botswana, Msumbiji, Kaskazini mwa Afrika Kusini na Angola kaskazini.

CHAKULA

Kama walivyo swala wengine Nyumbu wa bluu chakula chao tegemezi ni majani kwani ni miongoni mwa wanyama walao majani. Na wana uwezo wa kula aina mbali mbali za majani pindi wanapokuwa wana tafuta chakula.

Wana uwezo wa kuishi muda mrefu kidogo bila kunywa maji kwani maji mengi huyapata kupitia majani wanayo kula.

KUZALIANA

Huwa sio kazi rahisi kumiliki kundi la majike kwa Nyumbu dume kwani lazima apambane na madume wenzie na anaposhinda basi hutawala kundi la majike. Kundi hili anaweza kulitawala kipindi wanasafiri tu au akalitawala kwa miaka kadhaa. Mara baada ya kutawala kundi kuwapanda majike na kuwapa mimba.

Nyumbu jike hukaa na mimba kwa muda wa miezi 8 – 9 na baada ya hapo huzaa mtoto mmoja tu. Nyumbu ni miongoni mwa wanyama wenye uwezo wa kujizuia kuzaa kwa muda kama yupo kwenye mazingira ambayo sio mazuri kwa malezi ya mtoto na hujitahidi kutembea mpaka sehemu nzuri na salama. Asilimia 80% – 90% ya watoto wa Nyumu huzaliwa wiki 2 – 3 kabla ya msimu wa mvua kuanza na kwa wakati huu huzaliwa watoto wengi sana. Mara baada ya kuzaliwa ndani ya dakika 15 mtoto huanza kumfuata mama na kuingia kwenye kundi la Nyumbu wengine huku akiwa chini ya uangalizi wa mama.

Baada ya miezi minne watoto huwa wameshakuwa wakubwa japo huendelea kunyonya mpaka mwaka mmoja. Watoto wa kike hufikia kuwa tayari kwa kuzaa wafikishapo umri wa kati ya mwaka mmoja na nusu hadi miwili na nusu huku madume ni mpaka miaka mitatu hadi minne.

Baada ya mwaka mmoja watoto wa kiume hufukuzwa ndani ya himaya na wakati huu hujikusanya kwa pamoja na kuunda kundi lao la watoto wa kiume tu. Mara baada ya miaka 3 – 4 kundi hili huvunjika na kila mmoja huanza kupambana ili kuanzisha himaya yake na kupanda majike katika himaya ile. Nyumbu jike huzaa mtoto mmoja kila mwaka na ndio maana wanyama hawa wamekuwa ni wengi sana.

Umri wa Nyumbu wawapo katika mazingira asili hususani katika hifadhi za wanyamapori huwa ni miaka ishiri ni (20) japo akiwa anafugwa huenda akazidi miaka hiyo.

UHIFADHI

Nyumbu wa bluu bado wanapatikana na wametawanyika katika maeneo mengi sana hususani kwenye maeneo ya hifadhi za wanyamapori. Mfano wa kujivunia kwa upatikanaji wa Nyumbu hawa ni Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo ni Urithi wa Dunia na inasemekana ndio sehemu yenye idadi kubwa ya wanyama hawa kuliko sehemu nyingine zote.

Japo kuna taarifa zinaonyesha kuna badhi ya jamii za Nyumbu hawa wamekuwa wakipungua kwa kasi kubwa sana kwani inatakiwa tufahamu kuwa Nyumbu wa bluu wana jamii ndogo ndogo tano. Kwa kuongeza ni kwamba mbali na kuwa wanyama hawa hawajawa hatarini kutoweka lakini uwepo wao unatokana na sera imara za uhifadhi.

Ukanda wa Serengeti – Masai Mara una asilimia sabini- 70% ya idadi ya Nyumbu wa bluu wote. Hii ina maana kwamba idadi ya Nyumbu katika eneo hili ina hitaji umakini mkubwa sana hasa tunapo zungumzia suala la uhifadhi wa wanyamapori. Kwa ufupi Nyumbu wa bluu ndio wanyama watawala kati ya wanyama walao majani katika ukanda huu wa Serengeti – Masai Mara.

MAADUI NA TISHIO KWA NYUMBU WA BLUU

Maadui wakuu wa nyumbu hawa hasa katika mazingira yao asili nisimba, Mbwa mwitu wa Afrika, Chui, Duma, Mamba na Fisi madoa.

Tishio kubwa kwa wanyama hawa ni binaadamu na hasa kutokana na shughuli za kibinadamu.

Tukianza na suala la ujangili ambalo limekuwa tatizo sugu sana linalo sumbua mamlaka za uhifadhi wa wanyamapori na misitu. Watu wamekuwa waki wawinda sana wanyama hawa na kusababisha idadi kuwa inapungua. Hii inatokana na biashara haramu ya wanyamapori pamoja na malighafi zao.

Uharibifu wa mazingira unaofanya na binaadamu kwani umepelekea kupungua kwa mahitaji ya wanyama hawa hasa chakula na vyanzo vya maji. Watu wamekuwa wakivamia sana maeneo ya hifadhi za wanyamapori kwa ajili ya kuanzisha makazi hivyo kulazimika kukata miti hovyo na kuvamia vyanzo vya maji ambavyo ni muhimu sana kwa wanyama hawa.

Jamii za wafugaji pia hazijabaki nyuma kwani tumekuwa tukishuhudia sana migogoro baina ya wafugaji na mamlaka za uhifadhi. Hii ni kwasababu wafugaji waliyo wengi wamekuwa wakikiuka sheria za matumizi ya ardhi hasa kwa upande wa sheria za ardhi za hifadhi za wanyamapori. Wanaingiza mifugo katika maeneo hayo wakati sheria zipo wazi kabisa kwamba si ruhusa kuingiza mifugo katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori na adhabu yake inajulikana kabisa.

Ufungwaji wa varanda au mapitio ya Nyumbu wa bluu maeneo mbali mbali imekuwa ni tishio kubwa kwa wanyama hawa. Kama tulivyoona hapo juu wanyama hawa wanaishi kwa kusafiri kutoka eneo moja kwenda linguine sasa maeneo wanayo pitia yamekuwa yakivamiwa na watu kwa ajili ya makazi na kufanya wanyama hawa kukosa njia za kupita hivyo kuwafanya baadhi kubaki katika eneo moja. Mfano mzuri ni sehemu kama Minjingu ambayo ni muhimu sana kwani ilikuwa inaunganisha Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara kwa sasa imezibwa kabisa kutokana na uvamizi wa watu na makazi kitu ambacho kimefanya wanyama wasipite tena katika eneo lile.

MAMBO YA KUFANYA ILI KUEPUKA MATISHIO HAYA KWA NYUMBU WA BLUU

Kupitia mashirika mbali mbali yanayo jihusisha na ulinzi wa wanyamapori mfano PAMS Foundation, serikali haina budi kushirikiana na mashirika haya katika kudhamini mafunzo kwa askari wa wanyamapori ili kuongeza idadi ya askari hawa muhimu sana hasa kwenye ulinzi wa maliasili hizi muhimu sana hapa nchini kwetu. Askari hawa wana hitaji mafunzo muhimu sana ili kupambana na majangili lakini pia wapewe elimu juu ya umuhimu wa uhifadhi kwani kwa kutambua umuhimu huo watakuwa wanafanya kazi kwa umakini na uchungu sana kuwalinda wanyama hawa.

Serikali isimamie na kuhakikisha utekelezwaji wa sheria za mipango miji na makazi ili kupunguza tatizo la uvamizi wa maeneo ambao ni njia za wanyamapori kutoka hifadhi moja hadi nyingine. Mfano mzuri ni Kwakuchinja aneo ambalo ni muhimu sana linalo unganisha Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara. Eneo hili hutumiwa sana na wanyama kama mapitio, sasa linaonekana kuvamiwa sana tena na hapo baadae kama hali ikiendelea hivi linaweza likazibwa kabisa kutokana na uvamizi wa watu kwa kuanzisha makazi.

Kupambaza na uvamizi wa maeneo ya hifadhi za taifa ili kupunguza au kutokomeza kabisa suala la uharibifu wa mazingira kwani limepelekea wanyamapori kuhama baadhi ya maeneo kwa tatizo la mapungufu ya mahitaji yao ya kiikolojia. Mlunddikano wa watu katika maeneo ya Hifadhi za Taifa hupelekea hata tatizo la ujangili kuzuka kwani pale hukutana watu wenye tabia mbali mbali.

Ubunifu wa miradi mbali mbali ya maendeleo kwa jamii zinazo pakana na maeneo ya Hifadhi za wanyamapori na mapori ya akiba ili waweze kutumia muda mwingi kuwaza maendeleo ya miradi hiyo pasi na kuwaza suala la uwindaji haramu wa wanyamapori. Kwa hili napenda sana kulitolea mfano shirika binafsi linalo jishughulisha na uhifadhi wa mazingira kwa wanyamapori na maendeleo ya jamii (Environmental Conservation for Wildlife and Community Enterprise-  ECOWICE) kwa mradi wa uzalishaji uyoga kwani kuna baadhi ya vijiji hususani maeneo ya Hifadhi ya Taifa Mikumi wameanza kunufaika na mradi huu.

Kuishirikisha jami katika masuala ya uhifadhi lakini pia kuwagawia shemu ya faida itokanayo ya uhifadhi wa wanyamapori. Hii itasaidia kutengeneza mabalozi katika jamii ambao watakuwa ni chachu ya maendeleo ya uhifdhi lakini pia hata kwenye kuwafichua majangili kwani wengi wao tunaishi nao katika jamii zetu. Hivyo jamii ina mchango mkubwa sana katika suala la uhifadhi.

Serikali ifikirie kwa kina tena sana juu ya uanzishwaji wa mtaala wa somo la uhifadhi maliasili shule za msingi kwani kwa kufanya hivyo wanafunzi hawa watoto watakuwa na uelewa mkubwa juu ya umuhimu wa wanyama hawa kadri wanavyozidi kukua na hatimae kuwa mabalozi wazuri katika sualala uhifadhi wa wanyamapori. Unaweza ukaliona kama suala dogo kwa sasa kumbe lina mchango mkubwa sana katika maendeleo ya uhifadhi wa wanyamapori hapa nchini hapo baadae.

HITIMISHO

Uhifadhi wa maliasili hususani kwa upande wa idara hii ya wanyamapori ni jukumu la kila mtanzania kwani faida za uhifadhi unaweza usizione au kuzishika mkononi ila kwa maendeleo ya jamii mbali mbali. Tulio wengi hatuthamini mchango wa uhifadhi kwani tumezoea faida ya kitu ni mpaka ukipate mkononi mwako na wewe kwa uhalisia. Kumbe sio hivyo kabisa ndugu zangu, mfano nikupe ufumbuzi juu ya faida tunazo zipata kupitia uhifadhi bila sisi wenyewe kujua.

Serikali inakusanya kiasi kikubwa sana cha fedha kupitia Wizara ya maliasili na utalii, na fedha hizo hutumika kuendeleza miradi mbali mbali hapa nchini mfano ujenzi wa miundombinu kama barabara, madaraja na miradi ya maji. Hii haijalishi tunaishi karibu na hifadhi za wanyamapori au mbali bali tunafaidika kwa pamoja kupitia miradi hiyo. Wale waliopo karibu na hifadhi za taifa wanapata misaada mingi mfano kujengewa shule na vifaa vya hospitalini kupitia pato la hifadhi za taifa. TANAPA huwa wana asilimia kabisa ya pato lipatikanalo kutokana na shughuli za kitalii au shughuli zozote zile za hifadhini na kuzigawa asilimia hizo kwa vijiji husika vinavyo pakana na hifadhi.

Hivyo bila kujali umbali au faida mkononi zitokanazo na uhifadhi wa wanyamapori hatuna budi kuwaunga mkono wale wanaoonesha nia ya kuhifadhi maliasili hizi muhimu sana na adimu kwa baadhi ya nchi hpaduniani.

Endelea kutega jicho ili kujua ni makala ipi inafuata baada ya makala hii ya nyumbu wa bluu.

AHSANTENI

Kwa mengi zaidi na ushauri juu ya makala hizi wasiliana na mwandishi wa Makala hii kupitia

Sadick Omary

Simu= 0714 116963/0765 057969/0785 813286

Email= swideeq.so@gmail.com

Au tembelea= www.mtaalamu.net/wildlifetanzania

”I’M THE METALLIC LEGEND”…