Kwa hakika ni matumaini yangu una mapumziko mazuri na siku nyingi za kupumzika za mwisho wa juma huku zikiongezeka na nyingine za sikukuu ya Eid. Basi nami nikusihi tumia muda huu japo kujua machache kuhusu rasilimali zetutulizo jaaliwa na Mwenyezimungu hapa nchini kwetu. Somo la leo lipo madhubuti kwa kukuelimisha juu ya NDEGE ambao kwa hakika anapewa heshima kubwa sana na nchi fulani hapa Afrika Mashariki, si hivyo tu bali pia ni ndege ambae anavutia sana hata tu kwa kumuangalia.Na moja kwa moja tutamjua vizuri “KORONGO-TAJI KIJIVU”
UTANGULIZI
Korongo-taji kijivu kwa hakika ni ndege ambae anavutia sana kumwangalia hasa anapokua katika maeneo huru hususani maeneo ya Hifadhi za Taifa kwani huwa huru na kuweza kuonesha makeke na sifa zake zote alizonazo ndege huyu.
Kama walivyo ndege wengine, Korongo-taji kijivu hupendelea maeneo yalio tulia sana kwani usumbufu wowote kwa ndege husababisha ndege kuhama eneo hilo.
SIFA ZA KORONGO-TAJI KIJIVU
- Manyoa yake yana rangi ya kijivu huku akiwa na na rangi nyeupe sehemu ya mbawa zake.
- Ndege huyu hukua hadi kufikia urefu wa sentimita mia moja kumi na sita (sm116), ana uzito wa kilogramu tatu hadi tatu na nusu (3-3.5kg).
- Asili ya mbawa za ndege huyu ni rangi nyeupe, ila utakapo mchunguza vizuri na kwa utulivu utagundua ana rangi mbalimbali kwenye mbawa zake.
- Kichwani ana manyoa marefu yaliyo tengeneza umbo la taji yenye rangi ya dhahabu.
- Upande wa kulia na kushoto mwa uso ana rangi nyeupe ambazo kwa juu ya weupe huu kuna vifuko vyenye rangi nyekundu ya kung’aa.
- Ana mdomo mfupi wenye rangi ya kijivu na miguu yenye rangi nyeusi.
- Nivigumu kumtofautisha dume na jike, japo dume huonekana mkubwa kidogo kuliko jike.
- Korongo-taji kijivu wadogo huwa na rangi ya kijivu iliyo kolea zaaidi kuliko wakubwa.
MUHIMU KUJUA
- Jamii ya ndege hawa ina heshima ya kuwa ndege wa Taifa wa nchi ya Uganda na pia ni moja ya alama katika bendera ya Taifa la Uganda.
- Ndege hawa husemekana kuwa hawana usaliti katika mahusiano. Yaani dume hawezi kuwa na jike zaidi ya mmoja hali kadhalika kwa jike pia hawezi kuwa na dume zaidi ya mmoja. Kamwe hawasalitiani na hakuna michepuko. Woowwww “MAPENZI MUBASHARA”
MAENEO WAPATIKANAYO KORONGO-TAJI KIJIVU
Ndege hawa wana patikana sana maeneo ya Savana kavu kusini mwa jangwa ka Sahara na hutengeneza viota maeneo yenye maji maji kidogo na aridhi oevu. Mfano wa nchi ambazo ndege hawa huonekana sana tena kwa urahisi ni Uganda, Kenya, Tanzania, Namibia, Rwanda, Msumbiji na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Hapa nchini Tanzania Koongo-taji kijivu huonekana zaidi maeneo ya Kaskazini mwa nchi hususani katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro.
CHAKULA
Chakula kikubwa cha ndege hawa ni wadudu na wanyama jamii ya tambaaji. Japo kuna wakati hula mpaka mamalia wadogo wadogo kama panya.
KUZALIANA
Kabla ya kupandana ndege hawa huanza kucheza na kurukaruka huku kila mmoja akionesha kumvutia mwenzake. Michezo hii huambatana na au kwenda sawia na sauti nzuuri ambazo husababisha muonekano wa kutanuka na kusinyaa kwa fuko la hewa lenye rangi nyekundu linalo onekana maeneo ya shingoni.
Mara tu baada ya kupandana ndege hawa hujenga kiota kwenye maeneo yenye majani marefu au miti mirefu sana iliyo karibu na maeneo yenye aridhi oevu.
Jike hutaga mayai mawili mpaka matano (2-5). Jukumu la kutamia mayai huwa ni la wote kwa pamoja kati ya dume na jike na mayai hutotolewa baada ya siku ishirini na nane mpaka thelathini na moja (28-31) yaani takribani mwezi mmoja.
Watoto wa Korongo-taji kijivu huanza kuruka baada ya siku 56-100 japo bado kwa wakati huu huwa wapo chini ya uangalizi wa baba na mama. Kongoro-taji kijivu huishi kwa takribani miaka ishirini au na zaidi.
UHIFADHI
Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya ndege hawa kwa sasa ni kati ya 26,500-33,500. Na kati ya hao idadi ya Korongo-taji kijivu wakubwa ni kati ya 17,700-22,300 na walio salia ni watoto.
Utafiti uliofanywa na shirika la umoja wa mataifa linalo shughulika na uhifadhi wa maumbileasili duniani (International Union fo Conservation of Nature-IUCN) umebaini kuwa idadi ya ndege hawa imepungua kwa asilimia kubwa sana kutoka 100,000 hadi kati ya 50,000-64,000 toka mwaka 1985-2004. Hii inaonesha kuwa kuanzia mwaka 1985-2004 ndege hawa walipungua kwa asilimia 50% ndani ya myaka 19.
Kama hali itaendelea kubaki hivi hawa ndege wanaweza kutoweka kabisa duniani ukizingatia ni ndege ambao wanapatikana barani Afrika tu. Hivyo kutokana na wasiwasi huu ndege hawa wamewekwa katika kundi la wanyama walio kwenye tishio.
CHANGAMOTO ZINAZO WAKUMBA KORONGO-TAJI KIJIVU
Japokuwa ndege hawa bado wanaonekana baadhi ya maeneo mengi ila wamekua wakikumbwa na changamoto mbalimbali kama zifuatazo hapa chini.
- Upungufu au kuongezeka kwa mikondo ya maji hasa kwenye maeneo ya mazalia ya ndege hawa hivyo kusababisha kupungua kwa kasi ya kuzaliana.
- Kiwango kikubwa cha mifugo na baadhi ya wanyama walao majani kwani huaribu sana maeneo ya mazalia ya Korongo-taji kijivu.
- Watoto wa Korongo-taji kijivu kuna wakati huwa wanaliwa na ndege walao nyama kama mwewe na tai lakini hata pia nyoka wakubwa wakubwa.
- Matumizi ya sumu hasa kwa upande wa wakulima wamekuwa wakiweka sumu yakuwauwa ndege hawa kwani wanadai wamekuwa wakiharibu mazao yao. Mfano mzuri ni hapa kwa majirani zetu wa Kenya ndege hawa wamekuwa wakiuwawa sana kwa sumu mashambani.
- Uharibifu wa mazingira unaosababishwa na shughuli za kibinadamu katika maeneo ya hifadhi. Mfano mzuri ni uchimbaji wa makaa ya mawe nchini Afrika Kusini umeharibu sana makazi ya ndege hawa.
- Ujangili ulio kithiri katika maeneo ya hifadhi na nje ya maeneo ya hifadhi kumesababisha kupungua kwa ndege hawa.
NINI KIFANYIKE KUWANUSURU KORONGO-TAJI KIJIVU HUSUSANI HAPA KWETU TANZANIA
- Kupambana na uharibifu wa mifereji au mito inayo tiririsha maji katika maeneo oevu wanapoishi ndege hawa.
- Kupambana na uharibibu wa mazingira hususani ukataji miti hovyo na nyasi hasa maeneo yanayo zunguka hifadhi zetu.
- Itafutwe njia nyingine kuwasaidia wakulima wasitumie sumu kuwauwa ndge hawa kwa ajili ya kuharibu mazao yao kwani limekuwa tatizo kubwa sana kwa ndege hawa.
- Kuhakikisha askari wa wanyamapori wanafanya doria kila mara ili kupunguza au kutokomeza tatizo la ujangili.
HITIMISHO
Ni matumaini yangu sasa utakuwa umeelewa japo machache kuhusu Korongo-taji kijivu ndugu msomaji na mfuatiliaji wa makala zangu za wanyamapoi. Napenda pia kukusihi ndugu msomaji wa makala hizi kuwa unaweza pia kufuatilia ukurasa wangu wa facebook na kusoma makala nyingine lakini pia kupata taarifa za makala mpya ninazo andika.
Kwa moyo wa dhati napenda kulipongeza shirika linalo simamia wanyamapori hapa nchini TANAPA na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kwa kazi kubwa wanayo ifanya kusimamia ulinzi wa wanyamapori ili wasitoweke.
Nasi kama wananchi wenye haki na rasilimali za Taifa letu tusisite kutoa msaada wa dhati na kuyaunga mkono mashirika na mamlaka mbalimbali katika jukumu la uhifadhi wa wanyamapori.
Ahsante kwa kuwa na mimi pamoja mwanzo mpaka mwisho wa makala hii.
Kwa mengi zaidi kuhusu wanyamapori wasiliana na mimi kupitia
Sadick Omary Hamisi
SIMU=0717-116963, 0765-057969, 0785-813286
Email= swideeq.so@gmail.com
“I’M THE METALLIC LEGEND”