Habari za siku kidogo ndugu zangu kwani tumepotezana kidogo katika kujuzana machache kuhusu wanyamapori. Hii ni kutokana na changamoto zilizo nje ya uwezo wangu lakini panapo patikana wasaa au nafasi kama hivi basi sitosita kuendelea na uandishi wa makala ili kukujuza machache kuhusu wanyamapori bila kusahau uelekeo wa wanyama hawa katika mazingira yao asilia. Nimepokea maombi mengi kutoka kwa watu mbalimbali na lawama nyingi tu kwanini siandiki makala sasahivi ila ukweli nikwamba sio kwamba siandiki kwa kufanya makusudi ila ni changamoto tu za hapa na pale ila kwa sasa angalau zitakua zinawajia makala za kutosha.
Katika makala ya leo nimetamani sana kuelezea viumbe jamii ya ndege kwani viumbe hawa wapo wa aina nyingi sana na tulio wengi ni wazi hatuwajui ndege kwa kina. Basi nikuombe tu kwa muda wako mchache ambao hautozidi hata dakika kumi uendelee kuwa nami katika makala hii ili uweze kumfahamu ndege ambae nitamuelezea katika makala hii.
Kama nilivyo kwisha tangulizankusema hapo juu makala hii nitamuelezea ndege, na bila kupoteza wakati ndege ambae atabeba maudhui ya makala ya leo ni ndege ajulikanae kwa jina la KARANI TAMBA ambae kwa lugha ya kingereza hujulikana kama SECRETARY BIRD.
UTANGULIZI
Karani tamba ni miongoni mwa ndege ambao wanapatikana kwa wingi hapa nchini Tanzania hasa huonekana kiurahgisi katika maeneo tengefu ya hifadhi za wanyamapori. Ndege huyu mwenye umbo kubwa ambae ni mla nyama kama jamii ya ndege kipanga na mwewe anapatikana barani Afrika tu. Kutokana na uzuri wa ndege huyu imepelekea baadhi ya mataifa barani Afrika kumuweka ndege huyu katika nembo zao za taifa na mataifa hayo ni Sudani na Afrika ya Kusini. Hii inadhihirisha ni kwa jinsi gani tunapaswa kumtunza ndege huyu hususani hapa nchini kwetu Tanzania ambapo bado tunajivunia uwepo wa ndege huyu katika maeneo mbali mbali.
Kabla sijaendelea na kipengele cha sifa na tabia za karani ningependa kukujulisha ndugu msomaji wa makala hii uweze kujua jina karani limetokana na nini mpaka kufikia ndege huyu kuitwa karani. Ndege huyu ameitwa karani kutokana na manyoya yaliyo simama sehemu ya nyuma ya kichwa chake mfano wa karani ya karne ya 18 na alama ya kalamu katika kona ya mbawa zake na hatimae jina karani likatokea kwa ndege huyu.
SIFA NA TABIA ZA KARANI TAMBA
- Karani tamba wana muonekano wa kufanana zaidi na ndege kama kongoti au korongo na tofauti na ngede wenzie jamii ya walao nyama.
- Ana kichwa kidogo na mwili mkubwa kama tai huku mdomo wake hasa mdomo wa juu ukiwa umejikunja kuelekea chini.
- Karani tamba ana miguu mirefu mfano wa korongo na mabawa yenye umbo la duara.
- Sehemu kubwa ya mwili wana manyoa yenye rangi ya kijivu na meupe kidogo, huku sehemu ya nchani katika mbawa zake na miguuni wakiwa na manyoa yenye rangi nyeusi na mkia wenye manyoa mawili marefu yaliyo chongoka.
- Sehemu ya nyuma ya kichwa karani tamba ana shungi yenye manyoa ambayo yana rangi nyeusi nchani. Ndege huyu usoni ana rangi ya machungwa ambayo inaelekea kuwa kama wekundu.
- Karani tamba ndio ndege mwenye miguu mirefu kuliko ndege wote katika jamii ya ndege walao nyama. Wana magamba magumu sana kwenye miguu yao na hii huwasaidia wasi dhurike hasa pale wanapo pambana au kugongwa na nyoka.
- Karani tamba hana vidole vyenye uwezo wa kukwarua kama walivyo ndege wengine walao nyama bali ana vidole vinene na bapa vyenye kucha fupi zilizo jikunja.
- Ndege hawa wanapendelea sana kutembea kuliko kuruka na wanakadiriwa kuwa na uwezo wa kutembea kilometa 20-30 kwa siku. Japo hupendelea kutembea ila ni warukaji wazuri sana na wana uwezo wa kuruka kimo kirefu sana kwenda angani na wanapo ruka miguu yao mirefu huonekana kuzidi sehemu ya mwili na kuchomoza upande wa nyuma.
- Dume na jike wana fanana sana ni ni vigumu kuwatofautisha japo jike huwa na mwili mdogo kidogo kuliko dume.
- Karani tamba ni ndege ambae anaishi kwa kujitenga lakini kuna wakati huonekana katika kundi au familia na wanaweza kufikia hadi wa tano. Ndege hawa pia kuishi kwa mipaka na himaya ambapo karani tamba mmoja anaweza kuwa na himaya yenye ukubwa wa kilometa za mraba 50.
- Ndege hawa ni wakimya sana na mara nyingi wanapotoa sauti basi huwa ni ya chini na husikika marachache sana watoapo sauti.
KIMO, UREFU WA MABAWA NA UZITO WA KARANI TAMBA
Kimo- hufikia kimo cha mita 1.3-1.4 wastani wa futi 4.5.
Upana wa mabawa hufikia mita mbili ambao ni sawa na futi 6.6.
Uzito-ndege hawa hufikia uziti wa kilogramu 2.3-5
MAZINGIRA
Kama nilivo tangulia kusema hapo juu ndege hawa wanapatikana barani Afrika tu na hasa maeneo ya kusini mwa jangwa la Sahara. Hupatikana zaidi maeneo ya muinuko wa takribani mita 3,000 kutoka usawa wa bahari.
Wanapendelea sana maeneo ya wazi yenye majani mafupi na savana japo wana uwezo wa kuishi maeneo ya nusu jangwa na sehemu zenye miti na vichaka. Mara tu jua linapo zama ndege hawa hupendelea kupumzika katika miti jamii ya michongoma na huamka mapema sana kasha kushuka ardhini kwa ajili ya kutafuta chakula.
CHAKULA
Karini tamba ni miongoni mwa ndege walao nyama na hupendelea sana kula nyoka, mijusi, vyura, wanyama jamii ya panya, ndege wadogo na mayai ya ndege wengine. Muda mzuri wa mawindo kwa ndege hawa huwa ni mchana kwani wana uwezo wa kuona mchana zaidi kuliko usiku. Japo wakati mwingine hula mizoga ya wanyama ambao wameuwawa katika mazingira yao.
KUZALIANA
Karani tamba huishi wawili katika maisha yao, hii ina maana kwamba dume mmoja huishi na jike wake mpaka nwisho wa maisha yao. Dume hawezi kuwa na jike zaidi ya mmoja hali kadhalika jike hawezi kuwa na dume zaidi ya mmoja. Kabla ya kupandana kwa pamoja dume na jike huwa wanacheza ili kuvutiana na wakati mwingine michezo ya kukimbizana ardhini yote hii ni kumfanya kila mmoja kuwa tayari kwa tendo la kupandana ili waweze kuendeleza kizazi chao kupitia kuzaliana.
Hujenga viota kwenye miti jamii ya michingoma, viota hivi hupendelea kujenga kwenye miti yenye urefu wa wastani wa mita 5-7. Kwa pamoja dume na jike hutembelea eneo la kiota kwa muda usiozidi nusu mwaka kabla ya jike kuanza kutaga mayai. Kiota huwa na upana wa takribani mita 2.5 na kimo cha futi moja kwenda chini huku kikiwa na vijiti ambavyo ni bapa sehemu ya chini.
Jike hutaga kuamzia yai 1 – 3 na kila yai moja hutagwa kwa tofauti ya siklu 2- 3. Mayai hutamiwa kwa muda wa siku 42-50 na jukumu la kutamia huwa wana shirikiana wote dume na jike japo jike ndio hutumia muda mwingi kutamia mayai kuliko dume. Katika kipindi chote cha kutamia mayai kazi ya kutafuta chakula huwa ni ya dume. Hivyo dume hulazimika kutafuta chakula na kumletea jike katika kiota.
Mayai hutotolewa kwa mpangilio kutokana na yalivyo tagwa. Yai lililo tangulia kutagwa hutotolewa mapema kuliko mengine na mtiririko huo huenda mpaka yai la mwisho. Mara baada ya kutotoa uangalizi wa vifaranga huongezeka baina ya jike na dume na wote kwa pamoja huwa na jukumu la kuwalisha watoto. Watoto wa karani tamba huwa na ngozi yenye rangi ya njano usoni na kwenye manyoa. Watoto huanza kupigiza mabawa wafikishapo siku 60 na kuanza kuruka baada ya siku 80 japo huwa wanakaa kwenye kiota kwa muda mrefu. Na katika kipindi hiki jike na dume huenda na watoto katika mawindo ili kuwafundisha jinsi ya kuwinda. Tofauti na ndege wengine walao nyama, Karani tamba anasemekana ndio ndege mwenye uwezo wa kukuza mtoto zaidi ya mmoja kwa uhakika zaidi.
Karani tamba ana uwezo wa kuishi wastani wa miaka 10 – 15 awapo katika mazingira yake asili japo kama anafugwa kwenye bustani za wanyamapori basi huweza kufikisha hadi miaka 19.
UHIFADHI
Dhima kubwa ya makala hizi za wanyamapori hubebwa kwenye kipengele hiki hivyo huwa nasisitiza sana endapo unasoma makala hizi basi kipengele hiki ni cha kukitilia mkazo sana. Kwni hapa ndipo utaweza kujua ni nini uelekeo wa mnyama husika hali kadhalika kujua takwimu kuhusu mnyama anae elezewa katika makala husika.
Kutokana na kanuni za maumbile asili na rasilimali asili za Afrika, Karani tamba alitajwa kuwa miongoni mwa ndege wanao takiwa kulindwa mwaka 1968. Kutokana utafiti na takwimu zilizo tolewa na shirika la umoja wa mataifa linalo shughulika na uhifadhi wa maumbile asili duniani Internationa Union for Conservation of Nature-IUCN za mwala 2016 idadi ya ndege hawa hasa wakubwa ni kati ya 6,700 – 67,000 na idadi hii inaonekana kupungua siku hadi siku.
Hali hii imepelekea ndege hawa kuwekwa kwenye kundi la viumbe hai ambao kama hali ikiendelea kuwa hivi basi wataingia kwenye kundi la viumbe walio hatarini kutoweka duniani. Zipo changamoto nyingi sana ambazo zinasababisha kupungua kwa idadi ya ndege hawa katika mazingira yao ambazo kwa asilimia kubwa zinasababishwa na shughuli za kibinadamu. Kipengele kijacho kina elezea changamoto zinazo wakumba ndege hawa.
MAADUI NA CHANGAMOTO KWA KARANI TAMBA
Karani tamba mkubwa hana adui asilia japo mayai na watoto wa ndege hawa hukubwa na changamoto ya maadui wengi sana. Miongoni mwa maadui wa mayai na vifaranga wa karani tamba ni kunguru, bundi, mbizi wa nyika na mwewe.
Mbali na maadui hao asilia wa mayai na vifaranga wa karani tamba zipo changamoto ambazo zinatishia maisha ya ndege hawa, nazo ni kama ifuatavyo.
- Makazi na maendeleo ya kibiashara; Kutokana na utafutaji wa maeneo ya kuishi na upanuzi wa maeneo ya biashara, mazingira ya ndege hawa yamekuwa yakiharibiwa sana na kusababisha wahame kwenye maeneo ya asilia kitu ambacho kinapelekea wengine kufa hasa kipindi wanapo tafuta makazi mapya kwa ajili ya kuendeleza maisha yao.
- Shughuli za kilimo; Ufugaji holela na uanzishwaji wa ranchi maeneo mbali mbali vimekuwa ni tatizo kubwa linalo pelekea ndege hawa kutoweka baadhi ya maeneo. Hali kadhalika upanuzi wa mashamba kwa ajili ya kilimo umepelekea kuharibiwa kwa mazingira ya karani tamba.
- Upungufu wa chakula; Kutokana na uwindaji na ukamataji wa viumbe wadogo wadogo mfano wa jamii ya panya kumepelekea changamoto ya chakula kwa ndege hawa kitu ambacho kinafanya wahame kwenda sehemu nyingine.
- Moto; Kumekuwa na changamoto ya myoto katika maeneo mengi sana hasa inayozuka tu bila kuwa na uangalizi. Hali hii inasababisha mazingira ya karani tamba kuharibiwa na hata kuuwa vifaranga wa ndege hawa au kuharibu mayai.
- Mabadiliko ya hali ya hewa; Maendeleo ya shughuli za kibinaadamu hususani maendeleo ya viwanda yamepelekea manadiliko ya hali ya hewa kwa kiasi kikubwa sana duniani hata baadhi ya maeneo kukumbwa na ukame. Hali hii imesababisha mazingira hasa mazalia ya ndege hawa kupotea kabisa baadhi ya maeneo na kusababisha ndege hawa washindwe kuzaliana.
NINI KIFANYIKE ILI KUNUSURU NDEGE HAWA HUSUSANI HAPA NCHINI TANZANIA
Shughuli zote zinazo husisha maendeleo ya makazi zizingatie mipango miji na upembuzi yakinifu wa viumbe hai watakao athirika kutokana uanzishwaji wa makazi katika eneo hilo bila kusahau pia nafasi au mchango wa viumbe hao katika pato la taifa letu hasa kupitia sekta ya utalii. Hali kadhalika maendeleo ya kibiashara yazingatie sera ya uhifadhi wa wanyamapori ili kuepuka kuwapoteza ndege hawa.
Serikali ipambane dhidi ya ufugaji holela na uanzishwaji wa ranchi bila kufanya utafiti katika maeneo yanayo pendekezwa kuanzishwa ranchi hizo. Kuna baadhi ya maeneo unakuta ni mazingira mazuri kwa ajili ya kuzaliana ndege hawa lakini kwasababu hakuna utafiti unao fanyika basi inapelekea watu kujichukulia maamuzi tu na kuanzisha miradi ya ranchi au kugeuza sehemu hiyo kuwa sehemu ya malisho kitu ambacho kina sababisha upatikanaji duni wa chakula kwa ndege hawa.
Tafiti mbali mbali ziendelee kufanyika ili kubaini idadi ya ndege hawa hapa nchini. Kwa kufanya hivi niwazi kabisa tutaweza kujua ni maeneo gani yana uharibifu mkubwa wa mazingira unao pelekea ndege hawa kupungua na hatimae kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo ili tuendelee kuwa na idadi kubwa ya karani tamba katika maeneo ambayo yanaonekana kuwa ni tishio kutoweka kwa karani tamba. Utafiti huu unatakiwa kwenda sambamba na ufuatiliaji kwasababu kama tutapata takwimu tu kasha kuziacha bila kufatilia tutakuwa hatujafanya kitu na hali ya kupungua kwa ndege hawa itaendelea kuwepo.
Baadhi ya maeneo inaonekana ndege hawa wamekuwa wakiwindwa na kusafirishwa kwenye mataifa mbali mbali. Kutokana na taarifa hizi serikali kupitia mamlaka mbali mbali hasa zinazo husika na usimamizi wa wanyamapori na sekta ya biashara ni lazima ifanye ufuatiliaji na usimamizi mzuri wa kukagua rasilimali zetu zinazo safirishwa kwenda nje ya nchi ili kunusuru athari zitakazo jitokeza hapo baadae kutokana na biashara haramu ya wanyamapori.
Kupambana na moto unao zuka hasa katika maeneo ya misitu au maeneo tengefu ya hifadhi za wanyamapori. Kwa kufanya hivyo niwazi itasaidia kutunza mazingira ya ndege hawa kwani tumeona moto unaozuka misituni umekuwa ni changamoto kubwa kwa ndege hawa. Sambamba na hilo mabadiliko ya hali ya hewa ambayo ni ngumu kuyazuia sisi kama taifa peke yetu inabidi kuhusisha mataifa makubwa na mamlaka kubwa za usimamizi wa maliasili mfano WWF ili kupata njia stahiki katika kutatua tatizo hili.
Utoaji wa elimu ya uhifadhi kwa jamii ni jambo muhimu sana ili kuwafanya wana jamii kuwa mabalozi wakubwa hasa kwa kupata taarifa mbali mbali zinazo husu mambo yanayo endelea nje ya maeneo ya hifadhi za wanyamapori. Wananchi wakifahamishwa juu ya umuhimu wa kuwepo kwa ndege hawa niwazi hawatokubali kuona watu wakifanya ufisadi au kiashiria chochote kinacho ashiria tatizo kwa karani tamba tuliyo jaaliwa hapa nchini.
HITIMISHO
Karani tamba ni miongoni mwa vivutio vikubwa vinavyo wavutia watalii kuja hapa nchini ili kuwaona hasa katika hifadhi zetu mbali mbali za wanyamapori na kusababisha nchi yetu iweze kuingiza fedha nyingi za kigeni kupitia sekta ya utalii. Hivyo ni jukumu la kila mmoja wetu kwa jitihada za dhati kupambana na kuhakikisha tunaendelea kuwa na ndege hawa hapa nchini kwani sio jukumu la mamlaka zinazo simamia uhifadhi wa wanyamapori pekee.
Pongezi nyingi na za dhati ziende kwa mamlaka zote zinazo husika na uhifadhi wa wanyamapori hapa nchini ambazo ni TANAPA, TAWA na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kwa kazi kubwa sana wanazo fanya kuhifadhi maliasili zetu hasa wanyamapori na kuhakikisha mazingira ya wanyama hao yanaendelea kuwa asilia kama yalivyo kuwa hapo zamani. Bila kuwasahau mamlaka ya hifadhi za misitu TFS nao kwa kazi kubwa ya uhifadhi wa misitu kwani ni sehemu kubwa pia ambayo inasaidia kutoa mazingira sahihi na tulivu kwa ajili ya kuzaliana kwa wanyama mbali mbali.
Ulinzi na uhifadhi wa wanyamapori wetu unaanza na mimi na wewe, kamwe tusifumbie macho vitendo vyote vya kiovu vinavyo pelekea taifa letu kupata hasara kwa manufaa ya watu wachache ambao hawana huruma na uchumi wa nchi yetu. Tuyataje maovu yao ili kuinusuru nchi yetu na wabadhilifu hao
MWISHO
Kwa mengi zaidi kuhusu wanyamapori hali kadhalika ushauri kuihusu makala hizi usisite kuwasiliana nami kupitia mawasiliano yafuatayo;
Sadick Omary Hamisi
Simu – 0714116963/0765057969
E-mail – swideeq.so@gmail.com
Au tembelea tovutu yetu ya www.mtaalamu.net/wildlifetanzania
I`M THE METALLIC LEGEND.