Ni siku nyingine tena ndugu msomaji wa makala hizi za wanyamapori tunakutana tena darasani angalau kujua machache lakini yenye funzo kubwa kuhusu wanyamapori na mazingira yao lakini pia uelekeo wa wanyama hawa. Basi kama nilivyo kusihi kwenye makala iliyopita leo tena nakukaribisha katika makala nyingine mpya ili ujifunze machache tena kuhusu wanyama. Leo narudi tena kidogo upande wa viumbe wajulikanao kama reptilian (tambaaji). Na hapa leo tutamuangalia NYOKA, lakini kuna nyoka aina nyingi sana duniani. Hivyo tuwe pamoja katika makala hii ili ujue ni nyoka yupi leo tutamsoma kwa undani.

 

UTANGULIZI

Nyoka ni viumbe hai ambao wapo kwenye daraja la reptilian kutokana na uainishaji wa viumbe hai. Viumbe hawa wapo wa jamii nyingi sana, na inakadiriwa kuwa kuna aina takribani elfu tatu ( 3,000) za nyoka duniani. Licha ya kuwepo aina nyingi za nyoka duniani ila ni jumla ya aina 375 tu ya nyoka ndio nyoka wenye sumu ambapo ni sawa na asilimia 12.5%. Ukweli ni kwamba jamii nyingi za nyoka ambazo zinaishi karibu na binaadamu huwa ni nyoka ambao hawana sumu ya kusababisha kifo pale anapo muuma binaadamu.

Na huwa ni ngumu sana kwa nyoka kumuuma binaadamu kama nyoka huyo hana hofu ya kuuwawa au kupata mshtuko wa hatari. Hatua ya kwanza kabisa ya nyoka huwa anakimbia pale anapohisi kuwa kuna hatari, ila inaposhindikana na anapohisi hakuna namna ya kukimbia basi nyoka  hapo hulazimika kujiandaa kwa ajili ya kuuma.

Sasa kutokana na kuwepo kwa aina nyingi za nyoka ni vyema tukachagua aina moja ili tumsome hapa. Na bila kupoteza muda leo tutamsoma nyoka ajulikanae kwa jina la KOBOKO.

Lakini koboko hawa wapo wa aina mbili ambao na koboko mweusi na koboko wa kijani. Sasa hapa nitamzungumzia KOBOKO MWEUSI

SIFA NA TABIA ZA KOBOKO MWEUSU

1.Ndiyo nyoka mrefu kuliko nyoka wote miongoni mwa nyoka wenye sumu wapatikanao barani Afrika.

2.Ni nyoka mwenye sumu kali zaidi na anachukuliwa kuwa nyoka wa pili duniani katika nyoka wenye sumu kali. Anapo kuuma ukikosa huduma ya kwanza nza ndani ya dakika ishirini basi unaweza poteza maisha.

3.Koboko mweusi ni nyoka mwenye uwezo wa kukimbia kwa kasi kuliko nyoka wote duniani na ana uwezo wa kukimbia hadi kilometa ishirini kwa saa (20km/saa)

4.Ni nyoka mwenye hasira sana na mwenye uwezo wa kuuma ndani ya sekunde chache pale tu anapo hisi kuna hatari.

5.Koboko weusi wana rangi ya kijivu au wakati mwingine rangi ya kahawia nah ii hutokana na mazingira anayoishi ndio huendana na rangi ya mwili ili kumfanya asionekane kwa urahisi zaidi.

 

6.Anapo kuwa anakimbia au kupata hasira, nyoka huyu ana uwezo wa kuinua moja ya tatu ( 1/3 ) ya mwili wake. Hii inashangaza sana hasa unapo muangalia unaweza ukasema kuna kitu kina mwinua nyoka huyu ila kumbe ni uwezo wake tu.

7.Ni nyoka ambao wana weza kuuma mara nyingi zaidi tena ka muda mfu na pale wanapouma basi hutoa kiwango kikubwa sana cha sumu.

Kutokana na uwezo mkubwa wa nyoka huyu kukimbia, tabia zake nyingi sana bado hazijaweza kugundulika. Ila utafifiti bado unaendelea ili kujifunza mengi hasa tabia za nyoka huyu hatari duniani.

MUHIMU KUJUA

Jina koboko mweusi halitokani na rangi ya ngozi yake na wengi huchanganya sana hapa. Nyoka huyu kama nilivo eleza hapo juu hana rangi nyeusi kabisa. Jina koboko mweusi lina tokana na kuwepo kwa rangi nyeusi ndani ya mdomo ambayo huwa tofautisha nyoka hawa na nyoka wengine.

Watu wengi huamini nyoka huyu kuwa ni shetani kutokana na rangi hii iliyopo ndani yam domo wake.

UREFU NA UZITO

Urefu= Nyoka hawa wa uwezo wa kurefuka hadi kufikia urefu wa futi 14

UZITO=Koboko mweusi mkubwa anauweo wa kufikia hadi kilogramu 1.6kg

MAZINGIRA NA MAENEO APATIKANAYO KOBOKO MWEUSI

Koboko weusi ni nyoka wenye uwezo wa kuishi katika mazingira mbalimbali endapo tu mahitaji yao yanapatikana katika mazingira hayo. Wana uwezo wa kuishi kwenye misitu, vichaka, maeneo yenye mabwawa ya maji lakini pia hata maeneo ya Savana.

Nyoka hawa wanapamua kuishi sehemu huwa ni vigumu sana kuwatoa kwani huchukulia sehemu hiyo kama eneo salama lenye manufaa kwao kuishisiku zote na watahama tu endapo mazingira yata haribiwa kwa kiasi kikubwa.

Nyoka hawa wanapatikana karibu nchi 20 barani Afrika, Tanzania tukiwemo miongoni mwa nchi hizo. Kumbuka kuwa nyuka hawa hawapatikani sehemu nyingine zaidi ya bara la Afrika.

CHAKULA

Mara nyingi nyoka hawa wamekuwa wakionekana sana juu kwenye miti na hii ni kwa sababu wanapata chakula sana hasa juu ya miti. Kinacho wasaidia sana ni kutokana na rangi ya ngozi zao kufanana na miti wanayo kaa hivyo inakuwa ni vigumu kuonekana.

Anapo muuma mnyama mfano panya basi huakikisha hamuachii huku akiendelea kutoa sumu mpaka ahakikishe panya yule hawezi kutembea tena. Ndipo hapo ata muachia na kuanza kummeza polepole mpaka ammalize. Hupendelea sana kula panya na ndege.

KUZALIANA

Nyoka hawa mara nyigi hupandana msimu wa kipupwe au kiangazi na hii ni kwasababu huwa wana hitaji joto la kutosha katika kipindi hiki.  Dume huenda maeneo apatikanayo jike na kabla ya kupandana huwa wana pigana sana mpaka kufikia hatua hasira zao na hali ya miili kulingana baada ya hapo sasa huweza kupandana.

Mara nyingi jike huchagua ni dume yupi wa kupandana nae kwani kuna wakati dume hufukuzwa kabisa katika eneo hilo. Mara baada ya kupandana kuna baadhi ya majike huwa ruhusu madume kukaa nao pamoja kwa muda mfupi lakini wengine huwa wana wafukuza na huwa wana hasira sana kipindi hiki.

Jike hutaga mayai 10 – 25 na hutafuta sehemu yenye majani ambapo kuna joto linaloweza kuruhusu mayai kutotolewa. Mara tu baada ya kutaga jike huondoka kwani huwa hawana tabia ya kutamia mayai na hapo mayai hubaki yenyewe sehemu iliyo jificha. Mayai huchukua muda wa takribani siku 80 – 90 ( makadirio ya miezi 2 – 3) na baaada ya hapo watoto hutoka wenyewe kwenye mayai.

Watoto hutoka wakiwa wamekamilika lakini wengi wao hufa mapema ama kwa maadui au kushindwa kupata chakula vizuri. Hii ni kwa sababu wanakuwa bado hawa jawa na uwezo wa kutafuta chakula wenyewe na huwa hawana msada wowote toka kwa mama kama ilivyo kwa baadhi ya viumbe wengine.  Watoto hutotolewa wakiwa na urefu wa sentimita  51sm na baada ya mwaka mmoja huwa wamefikia urehu wa hadi mita 2m. Ni watoto wachache sana ndio hukua hadi kufikia umri wa kuweza kuzaliana.

SUMU

Kama nilivyo tangulia kusema hapo juu nyoka hawa ni miongoni mwa nyoka hatari sana duiani na ni nyika ambae anashikilia nafasi ya pili kwa kuwa hatari duniani. Kama wewe ni mfuatiliaji mzuri wa makala zangu nimewahi elezea aina za sumu zipatikanazo kwa nyoka wakati namuelezea kifutu msitu. Nitazirudia kwa faida yako ndugu msomaji.

Sumu za nyoka zipo za aina nne,

( a )Sumu inayo shambulia mfumo wa seli za neva ( Neurotoxin)

( b )Sumu inayo shambulia misuli/nyama ( Cytotoxin ) na

( c )Sumu inayo shambulia mfumo wa damu ( Hemotoxin )

( d )Sumu inayo shambulia ufanyaji kazi wa moyo ( Cardiotoxin )

Sasa sumu aliyo nayo koboko mweusi ni aina ya Neurotoxin ambayo anapo kugonga tu huathiri sana mfumo wa usafirishaji taarifa ndani ya mwili. Sumu hii hupelekea kupooza kwa mwili ndani ya muda mfupi na endapo utakosa huduma ya kwanza ya hospitalini ndani ya dakika 2- – 30 basi mtu anaweza kupoteza maisha.

Utafiti unaonesha kuwa nyoka huyu anapo uma basi hutoa kiasi cha sumu kinacho fikia miligramu 100mg – 120mg wakati mwingine huweza kufika mpaka miligramu 400mg. Huku kiasi cha miligramu 10mg – 15mg kinaweza sababisha kifo kwa mtu mzima.

DALILI ZA SUMU YA KOBOKO MWEUSI

Dalili za sumu hii ni maumivu sehemu iliyo umwa, kuanza kupoteza fahamu , macho kufumba, kutoka jasho, kutoka mate mdomoni na misuli kushindwa kufanya kazi ( hasa ulimi na mdomo), hli hii hupelekea kushindwa kupumua vizuri na mpaka mwisho mtu ana pooza ka muda mfupi tu.

Hasa kinacho muuwa mtu zaidi ni kushindwa kupumua kwasababu misuli inayo husika na upumuaji inakuwa imeathirika hivyo inakuwa ni vigumu kwa mtu kuvuta hewa hatimae anakufa.

Hivyo tunashauriwa mtu anapo umwa na nyoka basi awahishwe hopitali haraka sana ili kuokoa maisha yake kabla sumu haija samba zaidi mwilini na kuleta athari kubwa.

ADUI NA TISHIO KWA KOBOKO MWEUSI

Kwa uhalisia nyoka hawa wana maadui wachache sana kitu ambacho hakiwezi tishia uwepo wao katika mazingira wanayoishi. Adui wa nyoka hawa ni wanyama jamii ya Nguchiro, Nyegere na baadhi ya ndege wakiwemo Karani na Tai.

Ila tishio kubwa kwa nyoka hawa ni uharibifu wa mazingira utokanao na shughuli za kibinaadamu mfano ukataji miti na uchomaji misitu umepelekea sana nyoka hawa kuhama baadhi ya maeneo. Japo takwimu zinaonesha kuwa idadi ya nyoka hawa ipo vizuri kwani hawajapungua kabisa.

HITIMISHO

Nyoka huyu ni nyoka hatari sana kwani ana uwezo wakushambulia hata watu 10 kwa muda mfupi sana. Ina shauriwa kuwa unapo hisi au kumuona nyoka huyu mahali fulani basi hakikisha husogei mazingira hayo kwani ni nyoka mwenye hasira sana. Anaweza dhani unamfuatilia ili umuuwe na anapo hisi hivyo huwa na hasira sana na huanza kukufuata kasha kukuuma.

Hinyo tahadhari ni muhimu sana kabla ya kukumbwa na adha ya sumu kali itokanayo na nyoka huyu hatari sana.

AHSANTE SANA.

Endelea kufuatilia makala zijazo ili uweze kujifunza mengi zaidi kuhusu wanyamapori na faida zao kwani ni rasilimali zetu wote kwa pamoja.

Kwa mengi zaidi kuhusu wanyamapori, ushauri na maswali wasiliana na mwandishi kupitia

Sadick Omary

Simu= 0714 116963 / 0765 057969 / 0785 813286

Email= swideeq.so@gmail.com

Au tembelea= www.mtaalamu.net/wildlifetanzania

” I’M THE METALLIC LEGEND”