Habari za siku kidogo ndugu msomaji wa makala hizi za wanyamapori. Ni matumaini yangu umzima wa afya na nakupongeza sana kwa kufanikiwa kufika mwaka mpya wa 2018 huku ukiwa na afya nzuri na kama afya yako haijakaa vizuri basi hunabudi kuwahi hospitali ili kupata uchunguzi yakinifu wa afya yako. Basi kama ilivyo kawaida ya darasa letu hili huru ambalo huwa tunajifunza mambo machache kuhusu wanyamapori na mazingira yao bila kusahau uelekeo wa wanyama hawa kwa ujumla hususani hapa nchini kwetu Tanzania.

Katika mfululizo wa makala za hivi karibuni nimeona ni vyema kuwaelezea kwanza wanyama wanaopatikana kwenye kundi la wanyama jamii ya swala kwani kundi hili lina spishi nyingi sana. Leo tena tutapata kumjua swala mwingine ambae sio maarufu sana kwenye macho na fikra za watu wengi sana ila ni mnyama muhimu sana si tu kwa kigezo cha uchumi bali pia mchango wake katika usawa wa mazingira hususani ikolojia.

Bila kupoteza muda leo tutamjua mnyama ajulikanae kama “CHOROA” ambae kwa lugha ya kigeni (kingereza) hujulikana kama “ORYX”

Sasa kabla sijaendelea na uchambuzi ningependa ndugu msomaji ufahamu kwamba wanyama hawa (CHOROA) wapo wa aina mbali mbali na kuna takribani spishi 4 za choroa.

1.Choroa Kitara

2.Choroa wa Uarabuni

3.Gemsbok na

4.Choroa wa Afrika Mashariki.

Choroa hawa wa Afrika ya mashariki nao wamegawanyika katika makundi makuu mawili ambayo ni

(a)Choroa masikio pindo na

(b)Choroa beisa.

Choroa masikio pindo wanapatikana nchini Kenya na maeneo ya kati nchini Tanzania huku Choroa beisa wanapatikana zaidi chini Ethiopia, Somalia na baadhi ya maeneo ya kaskazini mashariki mwa Kenya na Uganda. Hivyo kwa ufahari na kujivunia tulichinacho leo hapa nitamzungumzia “Choroa Masikio Pindo”

UTANGULIZI

Kama nilivokwisha tangulia kusema hapo juu, choroa hawa wanapatikana nchi mbili tu nazo ni Tanzania na Kenya. Wanyama hawa wanahitaji uangalizi mkubwa sana kwani kuna baadhi ya nchi tayari wanyama hawa wamekwisha toweka kabisa.

Sasa tuzame ndani zaidi ili kuwajua choroa hawa hasa tukiangalizia sifa na tabia zao, mazingira wanayoishi, chakula, kuzaliana hali kadhalika uhifadhi na uelekeo wa wanyama hawa kutokana na Tafiti mbalimbali zilizofanywa kuhusu choroa hawa.

SIFA NA TABIA ZA CHOROA

Wana mili mikubwa na pembe ndefu sana zilizo chongoka mithili ya mikuki ambazo pia hutumika kama silaha wakati wa kujihami au kipindi wanapokaribia kuzaliana hasa kwa madume wanapo hitaji kuanzisha himaya ndhidi ya madume wengine.

Wana mashingo manene kama ya farasi yenye manyoa mengi na mafupi.

Wana masikio marefu yaliyo chongoka na kuonekana na upindo maeneo yakati huku masikio hayo yakiwa na manyoa mengi sehemu za nchani huku wakiwa na sura nyeupe zenye maumbo ya pembe tatu na mistari myeusi.

Miili yao ina rangi ya kahawia huku ikiwa na mistari myeusi maeneo ya chini ubavuni, usini na sehemu ya juu kwenye miguu ya mbele. Ukiwachunguza vizuri utaona pia mstari mweusi unaoanzia sehemu ya juu ya shingo na kushuka sehemu ya kifuani katikati ya miguu ya mbele.

Mistari myeusi hii ya usoni haijaungana kama ilivyo ya ubavuni na sehemu ya juu ya miguu ya mbele, hivyo kwa wengi wao huwa wana mistari myeupe inayotokea sehemu za juu ya macho kuelekea sehemu ya pua.

Wote madume na majike wana pembe zenye miduara ambazo huwa na urefu wa hadi nchi 30. Pembe za majike huwa ni ndefu na nyembamba kidogo kuliko za madume.

Tabia za kijamaa kwa wanyama hawa huwa ni tofauti tofauti sana kwani kuna ambao huishi kwa himaya na wengine huishi bila kuanzisha himaya. Kwa wale wanaoishi kwa himaya basi huweka alama kwenye himaya zao kupitia kinyesi.

Kwa ambao wanaishi bila himaya kundi moja huwa na wanyama 10 – 40 japo kuna wakati kundi hili linaweza kukua na kufikia hadi wanyama 200 katika kundi moja.

Ngazi za utawala kwenye kundi huzingatia umri na ukubwa wa mwili. Mara nyingi makundi huongozwa na madume wenye umri mkubwa na wenye mili mikubwa zaidi. Kundi la choroa huwa na eneo kubwa sana na hutembea polepole wakati wa kula ila wakati mwingine huonekana wakikimbia kidogo kidogo.

Wana uwezo mkubwa sana wa kunusa, na hali hii inawasaidia wanyama hawa kuhisi au kutambua maeneo ambayo mvua zinanyesha kisha kiongozi wa kundi huwaongoza wenzake wote kuelekea maeneo hayo yenye mvua kwani huwa na majani ya kutosha. Na mara nyingi kundi huwa lina hama maeneo tofauti tofauti kutokana na majira ya mwaka.

Wana mikia mirefu ambayo ina manyoa mengi na meusi sehemu ya nchani.

UREFU, KIMO NA UZITO

Urefu=huwa na urefu wa nchi 60 – 67 kuanzia kichwani mpaka kiwiliwili huku mkia ukifikia urefu wa nchi 18 – 20.

Kimo=kimo cha wanyama hawa huwa ni nchi 43 – 47

Uzito=huwa kuna utofauti kidogo kati ya uzito wa dume na jike. Dume huwa na uzito mkubwa kidogo kuliko jike. Dume huwa na uzito wa kilogramu 170 – 210 huku jike akiwa na uzito wa kilogramu 140 – 185.

MAZINGIRA

Wanyama hawa hupendelea sana maeneo yenye jangwa au nusu jangwa. Wana uwezo wa kukabiliana na mazingira yenye joto sana ukilinganisha na wanyama jami ya swala wengine.

CHAKULA

Choroa hawa ni wanyama walao majani kama walivyo swala wengine. Mara nyingi hupendelea kula wakati wa asubuhi mapema sana na majira ya jioni na wakati mwingine kipindi cha usiku na wakati mwingine wakati wa majira ya mwezi.

KUZALIANA

Wanyama hawa hawana muda maalumu wa kuzaliana, japo mara nyingi huwa wana zaliana kuanzia kipindi cha mwezi wa 12 – 4.

Jike hubeba mimba kwa muda wa miezi 8 – 9 na huzaa mtoto mmoja tu. Mtoto huzaliwa akiwa na uzito wa takribani kilogramu 10. Mtoto hufichwa na mama katika mazingira salama mara tu baada ya kuzaliwa na hukaa hao kwa wiki 2 – 3 kisha mama huwa anakuja kumuangalia mara mbili hadi mara nne kwa siku ili kumnyonyesha.

Watoto huzaliwa na rangi ya kahawia na mistari katika mili yao huanza kuonekana pale wanapoanza kufikisha umri wa kujiunga na kundi la kina mama na choroa wengine. Mara tu baada ya kuzaa jike huwa ana pevusha yai baada ya muda mfupi tu na kumfanya jike awe na uwezo wa kuzaa mtoto kila baada ya miezi tisa.  Watoto hufikia uwezo kuzaliana mara wakishapo umri wa miezi 18 – 24.

Kama mazingira ni mazuri na chakula kinapatikana vizuri wanyama hawa wana uwezo wa kuishi hadi miaka 20 katika mazingira yao halisia japo ukame na changamoto nyingine vinaweza kupunguza umri wa kuishi kwa wanyama hawa.

UHIFADHI

Idadi ya wanyama hawa inapungua kwa kasi sana kutokana na changamoto mbalimbali wanazopata wanyama hawa. Tusipokuwa makini tunaweza kuwapoteza kabisa wanyama hawa katika hifadhi zetu za taifa kwani tumeona baadhi ya nchi za Kaskazini mwa Afrika wayama hawa wametoweka kabisa katika maeneo ya hifadhi zao na kubaki wachache katika bustani za ufugaji wa wanyama.

Choroa ni swala ambae anaongoza kuwa hatarini kutoweka katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kutokana na changamoto ambazo tutazielezea katika kipengele kinacho fuata. Hivyo tunaona kabisa inahitajika jitihada kubwa sana kunusuru maisha ya wanyama hawa hasa hapa nchini.

CHANGAMOTO NA TISHIO KWA WANYAMA HAWA

Maadui wa choroa katika mazingira yao alisia ni simba, mbwa mwitu na fisi.

Mbali na maadui hawa asilia ambao wana umuhimu mkubwa sana kwenye ikolojia ya Wanyama, bado kuna adui mkubwa sana ambae yupo nje ya mazingira ya wanyama hawa ambae ni binaadamu. Binaadamu ni adui mkubwa sana kwa wanyama hawa hasa kutokana na matendo yake dhidi ya choroa.

Changamoto kubwa sana kwa wanyama hawa ni ujangili ulio kithiri kwenye maeneo ya hifadhi zetu za taifa. Watu wamekuwa waki wawinda wanyama hawa kwa kasi kubwa sana kitu ambacho kinatia hofu kwani tumeona hapo juu kuwa wanyama hawa ndio wanaongoza kwa kuwa hatarini kutoweka katika wanyama jamii ya swala hifadhini Serengeti.

Uingizwaji wa mifugo katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori nalo ni tatizo kubwa sana kwa choroa kwani wanapata changamoto sana hasa kwa upande wa chakula. Chakula chao kimekuwa kikiliwa sana na mifugo na kusababisha wanyma hawa kupata chakula kidogo sana hali ambayo huwafanya choroa kuwa dhaifu na hata kuuwawa kirahisi na maadui zao.

Ukame ambao husababishwa hasa na shughuli za kibinaadamu na makundi mkubwa wa mifugo katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori. Hali hii imesababisha wanyama hawa kuhama baadhi ya maeneo kutokana na kuongezeka kwa ukame kwenye maeneo yao asilia.

NINI KIFANYIKE KUWANUSURU CHOROA WETU HAPA NCHINI

Jambo lakwanza kabisa ni kuongeza idadi ya askari wa wanyamapori katika hifadhi za taifa na mapori ya akiba hali kadhalika katika maeneo ya hifadhi za jamii za wanyamapori. Hili litasaidia kuongeza uimara wa doria katika maeneo haya na kupungua tatizo la ujangili kitu ambacho kinapelekea kupungua sana kwa idadi ya choroa. Askari waadilifu na wenye moyo wa kujitolea ni muhimu sana kwani watafanya kazi kwa kujitoa ili kunusuru rasilimali zetu hizi badala ya wao kuwa ndo wachochezi wa vitendo vya ujangili.

Jamii ishirikishwe kwa ukaribu zaidi katika shughuli za uhifadhi wa wanyamapori na kujua kinachoendelea katika shughuli nzima za uhifadhi wa wanyama hawa. Tusiishie tu kwa jamii ambazo zinazunguka maeneo ya hifadhi za wanyamapori bali hata kwa jamii za mijini kwani ni dhahiri kwamba majangili wanapouwa wanyama basi hufanya biashara na watu wa mjini. Hivyo kama tutaweza kuwashirikisha na watu wa mijini pia kuhusu umuhimu wa kuwatunza wanyama hawa basi biashara hii haramu ya wanyamapori itapungua.

Serikali kupitia wizara ya elimu ijitahidi kuanzisha mitaala ya masomo ya maliasili kwa wanafunzi kuanzia ngazi ya shule ya msingi hadi sekondari ili kuwafanya watoto hawa kuwa na utambuzi na uchungu wa kuhifadhi wanyama hawa. Ni dhahiri kwamba mtoto anapokuwa na elimu ya maliasili kuanzia utotoni atakuja kuwa balozi mzuri sana hapo baadae kwani anakuwa na utambuzi nakujua thamani ya wanyama hawa.

Wizara ya maliasili na utalii kwa kushirikiana na wizara ya mifugo hali kadhalika wizara ya mazingira kwa pamoja wizara hizi zipambane na tatizo la uingizwaji wa mifugo katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori na uharibifu wa mazingira. Tumeona hapo juu miongoni mwa matatizo yawakumbayo choroa ni pamoja na uingizwaji wa mifugo kwenye hifadhi za taifa na uharibifu wa mazingira kitu ambacho kinasababisha ukame nakufanya wanyama hawa kuhama mazingira yao.

HITIMISHO

Kamwe huwezi jua thamani ya kile ulichonacho hadi pale kitakapo toweka. Kuna baadhi ya nchi hadi leo wanajuta na wanatamani kuwarudisha wanyama hawa lakini hawana uwezo tena hasa kutokana na kutokuwepo kwa mahitaji ya wanyama hawa ili waweze kuishi bila shida. Basi nasi hatuna budi kupambana ili kuwafanya wanyama hawa waendelee kuwepo hapa nchini kwa kizazi cha sasa na cha hapo baadae.

Napenda kumpongeza waziri wa maliasili na utalii Dr.Kingwangalla kwa jitihada kubwa anazo zifanya kwani kwa muda mfupi aliongia ameonesha nuru kubwa sana na kuudhihirishia umma kuwa hakuna kinacho shindikana kama kwa pamoja tutaamua kulinda maliasili zetu.

Pongezi za dhati sana kwa mamlaka mbali mbali ambazo kwa pamoja zinashirikiana kusimamia uhifadhi wa wanyama hawa hasa TANAPA, NCAA na TAWA kwa kazi kubwa sana mnayoifanya kutunza wanyama hawa kwani bila kazi kubwa mnayo ifanya tusingekuwa na wanyama hawa katika hifadhi zetu mbali mbali za wanyamapori.

MWISHO

Kwa mengi zaidi kuhusu wanyamapori au maelekezo na mchango wowote kuhusu makala hizi wasiliana na mwandishi wa Makala hii kupitia

 

Sadick Omary

Simu= 0714116963 / 0765057969 / 0785813286

Email= swideeq.so@gmail.com

Au tembelea= www.mtaalamu.net/wildlifetanzania

……”I’M THE METALLIC LEGEND”….