Huu ni mfululizo wa makala ambazo naendelea kukuletea kuhusu viumbe jamii ya nyoka kama nilivyokwisha kukuelezea katika makala iliyopita kuwa tutaanza kuwachambua nyoka hususani kwa nyoka wapatikanao katika nchi za Afrika Mashariki. Hivyo nikusihi kuendelea kufuatilia mtiririko wa makala hizi ili uweze kujifunza mambo mengi sana kuhusu nyoka. Katika makala ya leo nakusogezea kundi la nyoka lijulikanalo kama SWILA (COBRA). Kundi hili lina nyoka hatari sana ambao wanaweza kusababisha madhara au kumfanya mtu kupoteza maisha ndani ya muda mfupi mara tu baada ya kuumwa na nyoka hawa. Kufahamu makala iliyopita yenye mwendelezo Kila Kitu Unachopaswa Kujua Kuhusu Reptilia

Takribani spishi tisa za swila zinapatikana barani Afrika huku zaidi ya spishi tano wanapatikana katika nchi za Afrika Mashariki. Unaweza kuona ni kwa jinsi gani nyoka hawa ni wengi hapa Afrika Mashariki. Katika makala hii ya leo nitakupa elimu juu ya swila ajulikanae kama “SWILA MSITU” yaani “FOREST COBRA”. Jina lake la kisayansi ni Naja melanoleuca. Hivyo nakusihi ndugu msomaji kuwa nami mwanzo mpaka mwisho wa makala hii kwani utajifunza mambo mengi sana kuhusu nyoka huyu kuanzia namna ya kumtofautisha na nyoka au swila wengine, mazingira yake, sumu na hata namna ya kuwakwepa nyoka hawa katika mazingira yetu.

Swila Msitu

Swila hawa ni miongoni mwa nyoka hatari wapatikanao katika kundi la nyoka jamii ya swila. Wana sumu ambayo inaweza kusababisha kifo ndani ya muda mfupi tu kama mtu hatopata matibabu kwa muda sahihi. Katika hali isiyo ya kawaida, nyoka hawa sio wakorofi na hushambulia pale wanapo hisi kuna hatari au wanapo shambuliwa. Moja kati ya changamoto kubwa wanazo pitia nyoka wote ni hali tu ya kutopendwa na binaadamu, lakini viumbe hawa huwa hawana tabia ya kumshambulia binaadamu kama hawajachokozwa. Sasa moja kwa moja tukamjue kiundani swila msitu kwa kuangazia namna ya kumtambua na tabia zake kwa ujumla.

Namna ya kuwatambua Swila Msitu

Wana miili mikubwa na minene, kichwa kikubwa, macho makubwa meusi na mboni za duara.

Wana miili ya duara, mikia yenye myembamba yenye urefu wa wastani ambao unakadiriwa kuwa asilimia 15-20 ya urefu wa miili yao.

Swila hawa wana aina tatu za mpangilio wa rangi katika kuwatambua.

(1) Kwa ambao wapatikana kwenye misitu au kando kando ya misitu huwa wana rangi nyeusi inayo ng’aa, kidevu, shingoni na sehemu ya mbele ya tumbo wana rangi ya krimu huku wakiwa na mistari minene myeusi na madoa madoa.

Sehemu ya pembeni kichwani wana alama ya mistari myeupe na myeusi ambayo imefika mpaka sehemu ya mdomoni.

(2) Aina ya pili ya rangi kwenye utambuzi wa swila hawa hasa kwa wanaopatikana pwani ya Afrika mashariki na maeneo ya Zambia ni rangi ya kahawai au kahawai iliyo changanyikana na nyeusi sehemu ya juu, sehemu ya chini wana rangi ya kupauka, tumboni wana rangi ya njano au krimu, madoa makubwa yenye rangi ya kahawai au nyeusi.

(3) Aina ya rangi ya mwisho ni mistari yenye rangi ya njano na nyeusi hasa kwa swila msitu wapatikanao magharibi mwa Afrika.

Wana magamba laini yenye kung’aa ambayo yamejipangilia kwa safu 19 sehemu ya kati kati ya mwili (kwa wapatikanao mashariki mwa Tanzania bara na Zanzibar safu hizi zinaweza kuwa mpaka 17), sehemu ya tumboni safu hizi za magamba ni kati ya 197-226 na 55-74 sehemu ya nyuma.

Swila msitu wakubwa wana urefu wa mita zisizo zidi 2.7 ambapo ni  wastani kati ya mita 1.4-2.2. Wanapo totolewa toka kwenye mayai huwa na urefu wa sentimita 25-40.

Picha ya Swila Msitu akiiinua kichwa chake . Picha imetolewa Wikipedia

Tabia za Swila Msitu

Nyoka hawa wanapendelea maeneo ya nchi kavu mara nyingi aridhini lakini wana uwezo wa kupanda juu ya miti pia. Tafiti zinaonesha wana uwezo wa kupanda miti mpaka urefu wa mita 10.

Wana uwezo wa kujongea kwa haraka zaidi na pia ni wazuri sana kwenye kuogelea. Kwenye baadhi ya maeneo nyoka hawa huingia kwenye maji na hupendelea sana kula samaki kitu ambacho husababisha nyoka hawa kuonekana kama maisha yao nusu huishio nchi kavu na nusu nyingine ni kwenye maji.

Hufanya shughuli za uwindaji mchana na usiku. Kwa mchana mara nyingi huwinda maeneo ya misituni ambapo hakuna watu wengi, lakini usiku hupendelea kuja kuwinda mpaka maeneo ya makazi ya watu. Wanapotaka kupumzika hukimbilia kwenye mashimo, kando kando ya mito, matundu ya viota vya ndege lakini pia hata kwenye magogo au miti yenye uwazi ndani.

Wanapo hisi hatari au kukasirika, huwa wanainuka kimo cha wastani na kutunisha mbavu/mifupa iliyopo shingoni kama swila wengine na kumfanya shingo yake ionekane kubwa zaidi mara inapo tanuka.

Wana uwezo wa kugonga kwa haraka sana hata kwa umbali kidogo. Hawa ni nyoka ambao wanapoona hawana sehemu ya kukimbilia au kutoroka basi nao hujongea mbele na kuanza kushambulia. Wanasemekana ni miongoni mwa nyoka hatari sana linapokija suala la kushambulia wakihisi hawana uwezo wa kukimbia. Makala nyingine kuhusu nyoka unaweza kuisoma hapa Mfahamu Nyoka Mpole Na Hatari Zaidi Duniani.

Je Wajua?

Nyoka ambae anashikilia rekodi ya kuishi miaka mingi zaidi duniani ni swila msitu ambae aliishi miaka 28 katika bustani ya uhifadhi wa nyoka.

Maeneo wapatikanayo Swila msitu hapa Afrika Mashariki

Kama nilivyo eleza hapo juu, nyoka hawa wanapatikana nchi nyingi barani Afrika na wanapatikana nchi zote pia za Afrika mashariki. Hapa nchini swila hawa wanapatikana sana maeneo ya kusini mwa Usambara kuelekea mpaka pwani tambarare mto Ruvuma, Zanzibar (hasa Unguja na sio Pemba) na kisiwani Mafia. Kwa upande wa Kusini Magharibi mwa Tanzania wanapatikana zeidi maeneo ya ziwa Tanganyika, rasi ya Mahale, visiwa vya Rubondo na Ukerewe na Mwanza.  Lakini pia tafiti zinaonesha nyoka hawa wanapatikana kwa wingi zaidi maeneo ya kusini kwenye fukwe za ziwa Victoria.

Chakula

Swila hawa wanakula aina mbali mbali za viumbe kuanzia amfibia, samaki, mijusi, nyoka wadogo na mamalia wadogo wadogo kama panya.

Kuzaliana

Jike hutaga mayai kati ya 15-26 yenye ukubwa wa sentimta 3 X 6. Mayai haya hutamiwa kwa muda wa miezi miwili na baada ya hapo Watoto hujitafutia chakula wenyewe bila kutegemea malezi ya mama au baba.

Sumu

Swila hawa wana sumu ambayo ni hatari sana. Sumu ambayo hushambulia mfumo wa neva kitu ambacho kama mtu hatopata tiba haraka anaweza kupoteza maisha. Nyoka hawa wana uwezo wa kutoa miligramu 500 kwa mara moja sumu ambayo ni nyingi sana yenye uwezo wa kusambaa mwilini kwa haraka sana. Soma zaidi makala hii Mfahamu Nyoka Hatari Zaidi Duniani, Ana Uwezo Mkubwa Sana Wa Kuua Anapouma

Miongoni mwa dalili za mtu alie umwa na swila hawa ni maumivu makali sehemu ya jeraha, kichefuchefu, kutapika, kuharisha, mapigo ya moyo kwenda mbio, msukumo mdogo wa damu, kuanza kutoona vizuri, kutoka jasho sana, kushindwa kupumua na hata kupelekea mtu kupooza kwasababu sumu hii huathiri mfumo wa neva. Unaweza kusoma makala hii kufahamu mengi zaidi Mambo Usiyoyajua Kuhusu Tofauti Zilizopo Kati Ya Nyoka Aina Ya Cobra(Fira/Swila) Na Black Mamba(Koboko)

Nchini Ghana kuna mtoto aliumwa na nyoka huyu na alipoteza maisha baada ya dakika 20 tu. Hii ni kwasababu walichelewa kumpeleka hospitali ili kupata huduma kwa haraka zaidi.

Mwisho

Makala hii imehaririwa na Hillary Mrosso. Unapo maliza kusoma makala hii jiandae kwa makala nyingine ya nyoka jamii ya swila ambayo itakujia tena siku zijazo.

Kwa maswali, ushauri au maoni kuhusu makala hii  usisite kuwasiliana nami,

 

Sadick Omary Hamisi

Simu; 0714116963

Email; swideeq.so@gmail.com

Instagram; wilflife_articles_tanzania

Facebook; Envirocare and wildlife conservation

Tovuti; www.wildlifetanzania.co.tz

………………………..I’M THE METALLIC LEGEND………………….