Tunapoadhimisha Siku ya Tembo Duniani tarehe 12 Agosti, 2024 ni wakati mwafaka wa kuangazia kipengele cha kushangaza cha jamii ya tembo ambacho kinafanana na jamii za kibinadamu, nguvu na uongozi wa tembo wa kike, wanaojulikana kama mama wakuu (matriarchs).
Viongozi hawa wenye busara na uzoefu mkubwa wanaongoza makundi yao kukabiliana na changamoto za porini, kama ambavyo wanawake wanaongoza jamii zao kwenye Nyanja mbali mbali ya maisha kama vile malezi, masuala ya uchumi, siasa na uongozi.Fahamu Machache Kuhusu Tembo, Mnyama Mkubwa Zaidi Ardhini
Picha ya Tembo akiwa na mtoto wake, katika eneo la Amboseli, picha kutoka Trust for Elephants
Jukumu la Mama Wakuu katika Makundi ya Tembo
Katika makundi ya tembo, uongozi uko mikononi mwa mama mkuu ambaye ni tembo jike mwenye umri mkubwa na mwenye uzoefu zaidi. Hekima yake inayotokana na miaka ya uzoefu, ni muhimu kwa maisha ya kundi. Mama mkuu anaongoza kundi lake kwenye vyanzo vya maji wakati wa ukame, anazifahamu mbinu za kupita katika maeneo hatarishi, na hufanya maamuzi yanayohakikisha usalama wa familia yake.
Picha ya kundi la tembo wakiwa katika maeneo yao asilia. Picha hii ni kutoka katika eneo la Amboseli, Trust for Elephants
Maarifa yake ya mandhari, vyanzo vya maji, na maeneo salama ya kulisha yanarithishwa kutoka kizazi hadi kizazi, kuhakikisha mwendelezo wa kundi. Nafasi ya tembo jike katika kuongoza makundi ya tembo imeelezwa zaidi katika chapisho maarufu sana linaloitwa Leadership in elephants: The adaptive value of age.” Proceedings of the Royal Society B: Biological Sciences
Mama wakuu wanalea na kulinda watoto, kuwafundisha mbinu za kuishi, na kudumisha mshikamano wa kundi. Uongozi huu wa wanawake ni ushahidi wa nguvu, uvumilivu, na hekima ya wanawake katika ulimwengu wa wanyama na pia katika jamii za kibinadamu. Jinfunze zaidi tabia za tembo, Fahamu zaidi tabia za tembo zinavyoshabihiana na tabia za binadamu Tabia Kumi (10) Za Tembo Zinazofanana Na Tabia Za Binadamu
Nguvu ya Wanawake katika Jamii za Kibinadamu
Kama ambavyo mama wakuu wanaongoza makundi ya Tembo, wanawake wana jukumu muhimu katika jamii zao. Katika tamaduni nyingi, wanawake ndio wahudumu wakuu wa familia zao na walinzi wa rasilimali za familia. Ushiriki wao katika michakato ya kufanya maamuzi, hususani katika uhifadhi, umeonekana kuwa na matokeo bora zaidi na endelevu.
Mathalani, kwa nyakati tofauti Wizara ya Maliasili na utalii Nchini Tanzania imekuwa ikiongozwa na wanawake ambao wanaleta matokeo Chanya, miongoni mwao ni Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana na Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki ambaye ndiye Waziri kwa sasa.
Si hivyo tu, kubwa zaidi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni mwanamke amekuwa balozi namba moja wa uhifadhi wa wanyapori na mazingira yao nchini. Ni dhairi kuwa uhifadhi unamtegemea mwanamke. Pamoja na hayo, hatuwezi kusahau mchango wake mkubwa katika uhifadhi na kukuza utalii hapa nchini kupitia kampeni maarufu duniani ya Royal Tour ambayo imekua chachu ya kukuza utalii hapa nchini. Jinfunze zaidi hapa, makala kuhusu wanawake na nafasi yao katika uhifadhi Siku ya Wanawake Duniani, Nafasi ya Wanawake Kwenye Uhifadhi wa Maliasili
Wanawake huleta mitazamo ya kipekee katika uhifadhi. Mara nyingi wanaelewa zaidi mahitaji ya jamii zao na mazingira, na ushiriki wao unahakikisha kuwa juhudi za uhifadhi ni jumuishi na zinazingatia ustawi wa watu. Hapa Nchini Tanzania, ambako tembo wanakabiliwa na changamoto lukuki, wanawake wanao wajibu wa kuchukua nafasi za uongozi katika uhifadhi, kuongoza miradi inayolinda wanyamapori huku pia wakiimarisha jamii zao.
Jukumu la Women in Conservation Organization
Women in Conservation Organization ni mfano bora wa uwezo wa wanawake katika usimamizi wa mazingira. Shirika hili lililoko nchini Tanzania, lina mlengo wa kuhamasisha uhifadhi wa bioanuwai ya nchi ikiwemo wanyama kama tembo huku likiamini katika dhana ya ushiriki wa mwanamke katika uhifadhi. Kwa kufanya tafiti za kijamii na kiikolojia sambamba na kutoa elimu, shirika hili linasaidia jamii kwa ujumla kukuza ujuzi wanaohitaji ili kuongoza juhudi za uhifadhi.s
Hitimisho
Katika Siku hii ya Tembo Duniani, hebu tuwapongeze mama wakuu wa savannah na wanawake kwa hekima, ujasiri, na huruma. Nguvu ya tembo wa kike ni ukumbusho wa nguvu iliyopo katika jamii na uongozi. Kwa kuunga mkono mashirika kama Women in Conservation Organization, tunaweza kuhakikisha kuwa mama wakuu wa porini na wanawake katika jamii zetu wanaendelea kutuongoza kuelekea ulimwengu endelevu na wenye usawa zaidi.
Pamoja, tunaweza kuunda mustakabali ambamo hekima ya mama wakuu na uongozi wa wanawake unafanya kazi kwa pamoja kulinda dunia yetu na wanyamapori wake wa ajabu.
Makala hii imeandaliwa na:
Lucia Romward na Eva Ayoro (Waasisi wa Women in Conservation Organization)
Email; savenature@wicotz.org, phone: +255747419204/+255743927610.