Sehemu yoyote ambapo kuna migogoro sugu isiyoisha, mara nyingi migogoro na vita hutengeneza fursa nyingi ya vitendo vya ujangili na uvunjaji wa sheria kuendelea. Migogoro na vita kutoelewana na kukosekana kwa utulivu kwenye nchi au sehemu fulani kunachangia sana kuendelea kwa vitendo vingi viovu, siasa za nchi na hali ya uchumi vina nafasi kubwa sana kwenye usalama wa maliasili na utajiri wa nchi husika. Matendo maovu huwa yanashamiri sana kipindi ambacho kunakuwa na vurugu, vita hasa vita vya wenyewe kwa wenyewe, ubaguzi, ukandamizaji na ruhwa iliyokithiri kwenye sehemu nyeti kama mahakama na polisi vinachangia sana uharibifu na kukosekana kwa usalama kwenye maliasili nyingi hasa wanyamapori na madini.

Nina mifano mingi sana ya nchi ambazo hazina utulivu wala amani zimeathirika sana na uharibifu wa mazingira yao ya kuishi lakini pia uharibifu kwa maliasili za nchi. Kuna siku nilikua naangalia filamu inayooelezea hifadhi ya taifa ya Virunga iliyopo nchini kongo, walikuwa kwa wanaelezea namna vita hasa vita vya wenyewe kwa wenyewe zinzvyozorotesha juhudi za uhifadhi, katika maelezo inaonyesha kiwango cha juu kabisa cha ujangili kwenye nchi ya DRC Kongo ni kipindi cha vita. Niliona kipindi cha vita majingili wameingia kwenye hifadhi za wanyama na wameamua kukaa huko na kujenga vbanda kama ni eneo la Kijiji chao. Nimeona watu na wanyama wanavyohangaika na kutafuta utulivu wa kuishi maisha yao, wengi walipoteza maisha kipindi hiki, askari wengi sana wa wanyamapori waliuwawa sana kutokana na vita kwenye nchi yao hasa kwenye maeneo ya rasilimali muhimu na adimu.

Kutokana  na ripoti ya “Africa’s White Gold of Jihad: al-Shabaab and Conflict Ivory” ambayo niliisoma inayoelezea maswala ya uagidi na ujangili ambapo kundi la al-shabaabu walikuwa wanajihusisha na biashara hii ya kuuza meno ya tembo na kusafirisha kwenda nchi nyingine. Ripoti hiyo inaeleza kwa kina namna ugaidi na biashara ya meno ya tembo inavyofanikiwa na kutekelezwa katika pembe ya Afrika mashariki. Katika ripoti hiyo ya uchunguzi inaonyesha kuwa vikundi vya kigaidi kama al-shabaabu walikuwa wanahitaji fedha kwa ajili ya shughuli zao za kila siku kama vile kuwalipa askari wao na kuendesha maisha yao. Katika ripoti hiyo hawaonyeshi kuwa kundi hili la kigaidi linategemea sana biashara hii lakini liliamua kuingia kwenye biashara hii kutokana na hali ya kisiasa za nchi husika na jinsi ambavyo ilikuwa ni rahisi na inawezekana kiifanya biashara hii kwa pande wao. Mfano nchi ya Somalia ambapo ndio kitovu cha makundi haya ya ugaidi nchi hiyo ambayo haina amani kwa muda mrefu imekua ndio sehemu za kuuzia na kutoroshea meno ya tembo. Hii ni kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Vilevile tafiti na uzoefu unaonyesha nchi za Afrika magharibi ambako kuna vita na migogoro mingi ya kisiasa kuna uharibifu mkubwa sana wa maisha ya watu na maliasili za nchi. Kutokana na kutokuwa na utulivu katika nchi husika imepelekea kuwepo kwa ujangili na vitendo vingi viovu kwenye maliasili na viumbe hai. Kwa mujibu wa ripoti ya ujangili inayohusisha makundi ya kigaidi na biashara haramu ya meno ya tembo inaonyesha kuwa vikundi hivi vya kigaidi vinatumiwa na wafanyabiashara na watu wanaohitaji meno ya tembo kwa ajili ya shughuli zao, pia inaonyesha kuwa nchi ambazo huitaji zaidi meno ya tembo ni nchi za Asia na Marekani kidogo, nchi kama China ndio muhusika mkuu wa biashara hii ambayo inatekelezwa kwa gharama kubwa sana.

Jambo hii linanipa kufikiri sana juu ya hali za kisiasa za nchi nyingi kuendelea kuzorota na kutokuwa na mwafaka wa kudumu ni kutokana na baadhi ya vikundi au mataifa mengine kuhusika kwa siri kupenyeza ajenda zao za siri ili kuwe na vita na wao waanze kuvamia na kupora rasilimali za nchi, ndio maana kuna vikundi vingi sana vya kiasi, au vikundi ambavyo vimeasi serikali na mamlaka ya nchi husika kama vile M23, Lord resistant Army, vipo vingi ambavyo huishi na kuendesha mapigano msituni. Vikundi kama hivi ni hatari sana kwa sababu havina nia njema na pia inawezekana vinatumiwa na mataifa mengine kwa maslahi yao binafsi, jambo jingine sehemu ambazo kuna rasilimali nyingi kama vile madini, mafuta, gesi na maliasili nyingi muhimu kama wanyamapori huwa kunakuwa na migogoro kwa mfano kama nchi ya DRC Kongo, na nchi nyingi za Afrika Magharibi kama vile Nigeria kumekuwa na makundi mengi ya waasi na kigaidi. Vikundi hivi ambavyo huondoa utulivu kwenye nchi vinakuwa na ajenda nyingine ambayo ni kumiliki na kutumia mailasili muhimu za nchi hiyo. Kwasababu wanaamini wanathulumiwa basi huwa wanaamua kutumia vita na matendo mengine yanayotishia usalama wa binadamu na viumbe hai wengine ili kupora na kufanya ujangili kwenye maliasili za nchi.

Afrika tunatakiwa kuwa makini sana kwenye mambo kama haya, tusiruhusu hata kidogo migogoro na kutoelewana kushamiri kwenye nchi zetu. Jambo linaweza kuanza kidogo kidogo kama migogoro ya kawaida ya ardhi, au migogoro ya wakulima na wafugaji, au migogoro ya wafugaji na mamlaka za hifadhi za wanyamapori au hata migogoro ya kisiasa, baina ya vyama vya siasa. Baadaye unaona migogoro hiyo haiishi na inaendelea kuwa sugu, baadaye unaanza kuona mapigano, wanaanza kutafuta silaha kali, hapo ndipo mwanzo wa kuingia kwa makundi mengine kutoka sehemu mbali mbali na wengine wataanza kutafuta msaada na hapa ndipo nchi inaanza kuhangaika kuzuia na kutatua migogoro hiyo, wakati huo kuna watu wanaendelea na ajenda zao nyingine za siri hasa kwenye maliasili zetu.

Naamini serikali za nchi zetu zinafahamu jambo hili, na zimejipanga kuzuia kabisa hali ya namna hii isiendelee kwenye maliasili zetu. Nchi zetu zinatakiwa kuwa na siasa za haki na usawa ili kuzuia kabisa hali ya vurugu za kisiasa ambazo huja na mambo mengi yanayotishia usalama wa maisha ya watu na usalama wa maliasili zetu. Tujifunze kwa nchi zetu za jirani, hali ya kisiasa ya nchi inaweza kusababisha ulinzi na uaslama wa maisha ya watu na wanyama au inaweza kupelekea uharibifu wa maisha ya watu na viumbe hai wengine. Hivyo tusiruhusu kabisa migogoro kutawala na kuendelea kwenye nchi yetu, migogoro yote inatakiwa itafutiwe ufumbuzi mapema ili hali ya amani iendelee na watu wafanye shughuli zao kwa uhuru na amani.

Kipekee naipongeza serikali ya Tanzania kwa kusimamia amani na kuzuia migogoro mingi ambayo inaweza kuwa na faida kwa watu wengine na ikawa hasara kwenye maisha yetu. Pia nawapongeza watanzania wote kwa kuwa watulivu na kutii sheria, jambo hili sio tu linaleta utulivu na maendeleo kwenye maisha yetu bali hata kwenye maisha ya mamilioni ya wanyama, ndege, wadudu, na hata mimea. Tuendelee kuweka juhudi kubwa kufanya kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano ili kwa pamoja tuwe walinzi wa nchi yetu na maliasili zetu.

Asante sana msomaji wangu, naamini umepata uelewa wa jambo hili na utafanyia kazi uliyojifunza kwenye makala hii. Endelea kuwashrikikisha wengine maarifa haya uliyojifunza hapa. Kila la kheri, nakutakia maandalizi mazuri ya sikukuu na mwisho wa mwaka, karibu tuendelee kujifunza kwa pamoja kwenye makala ijayo.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania