Habari Rafiki, karibu kwenye makala ya leo ambayo tunaendelea na uchambuzi wa sheria ya wanyamapori ya mwaka 2009. Leo tunaendelea na Sehemu ya 13 ya sheria hii, ambayo inazungumzia Spishi zinazolindwa au zilizohifadhiwa na Masharti ya Kimataifa au wajibu wa kimataifa. Hii ni sehemu muhimu sana ya sheria inayotoa nafasi kwa nchi wanachama walio saini au kukubali kushirikiana na nchi nyingine kwenye uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori. Karibu twende pamoja ndani ya sheria hii tukianzia kifungu cha 94.

94.-(1) Waziri baada ya kupata mapendekezo kutoka kwa Mkurugenzi, anaweza kutoa taarifa kwenye Gazeti la serikali, kutangaza spishi yoyote ya wanyamapori kama spishi wanaolindwa au wanaohifadhiwa chini ya Sheria hii. Ufafanuzi hapa ni kwamba Waziri mwenye dhamana na Mkurugenzi wa wanyamapori wanaweza kuafikiana baada ya kupokea mapendekezo kutangaza aina ya mnyama, jamii au spishi za wanyamapori kuwa spishi zinazolindwa au zinazohifadhiwa chini ya sheria hii.

(2) Spishi zozote za wanyamapori ambazo zimepatikana, au zilikuwa zinahama kwenda, au kupitia Tanzania ambazo zinalindwa chini ya mikataba au makubaliano yoyote ya kimataifa ambayo serikali ni mwanachama atatakiwa kuchukuliwa au kukubaliwa kwa hadhi ya spishi anayelindwa chini ya sheria hii. Ufafanuzi hapa ni kwamba mnyama yoyote ambaye ametangazwa kuwa analindwa au ni mnyama anayehifadhiwa, endapo atapatikana sehemu yoyote au alikuwa anahama, sheria hii inamtambua mnyama huyo kama mnyama anayelindwa sawa na makubaliano ya kimataifa ambayo nchi imeyakubali na kutia saini.

(3) Waziri anaweza, kushauriana na Waziri anayehusika na mazingira, mifugo, kilimo, na mamlaka nyingine, kutoa taarifa kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali, kuandaa hifadhi au ulinzi wa makazi ya wanyama yanayovuka mipaka, uoto na mifumo ya ikologia. Ufafanuzi kwe ye kipengele hiki ni kwamba Waziri anatakiwa kuwa na ushirikiano wa karibu na Waziri wa anayehusika na Mazingira, mifugo, kilimo ili kwa pamoja washirikiane mambo ya msingi ya uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori, maeneo, makazi na mipaka. Endepo watashirikiana kwa karibu na kwa juhudi ili kuweka mambo sawa itaepusha migogoro mingi sana kati wakulima na wafugaji, au wafugaji na watu wa hifadhi au wakulima na watu wa hifadhi za wanyamapori

(4) Pale ambapo Jamhuri ya Muungano ni mwanachama wa makubaliano yanayohusiana na usimamizi wa wanyamapori na makazi yake, Waziri baada ya kushauriana na mamlaka husika atafanya yafuatayo-

(a)kuanzisha na kuandaa mapendekezo au shauri la kisheria kwa kusudi la utekelezaji wa makubaliano au mikataba; na

(b)kuangalia njia sahihi na za lazima kwa ajili ya utekelezaji wa makubaliano.

(5) Pale ambapo Serikali imejihusisha kwenye majadiliano na mikataba ya kimataifa kwenye mambo yanayohusiana na uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori na makazi yake, Waziri atawasiliana na Waziri anayehusika na Mazingira, kiini cha makubaliano hayo na kupitia madhara yoyote yanayoweza kutokea kutokana na athari za mazingira baada ya hapo atapeleka uthibitisho huo kwenye mkutano mkuu wa bunge kwa majadiliano zaidi. Ufafanuzi hapa ni kwamba endapo serikali itajihusisha na mikataba na makubaliano yoyote ya kimataifa kuhusu uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori na makazi yake, Waziri wa Maliasili na utalii kabla ya kuwasilisha uthibitisho huo kwenye mkutano mkuu wa bunge, anatakiwa kuwasiliana na Waziri anayehusika na mazigira ili waweze kuangalia na kuyapitia makubaliano hayo, kama yanaweza kuwa na athari kwa mazingira.

(6) Mkurugenzi ataendelea kurejesta mikataba na makubalianao yote yanayohusiana na uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori na makazi yake ambayo Jamhuri ya Muungano ni mwanachama. Ufafanuzi hapa ni kwamba kwenye makubaliano na mikataba yote ambayo Serikali ya Jamhuri ya Muungano ni mwanachama au mshirika itaendelea kuwepo na Mkurugenzi ndiye atakayekuwa anafuatilia na kuhakikisha inaendelea kuwepo.

(7) Waziri atahakikisha kwamba hifadhi za Taifa Tanzania na Hifadhi ya Mamlaka ya Eneo la Ngorongoro na taasisi nyingine zinazohusika, kuchangia kifedha kwenye utekelezaji wa mikataba ya kimataifa na ya kimkoa kuhusiana na wanyamapori na makazi yake ambayo Jamhuri ya Muungano ni mwanachama. Ufafanuzi hapa ni kwamba, Hifadhi za Taifa yani TANAPA, na Hifadhi ya eneo la Ngorongoro wanatakiwa kuchangia kiasi cha fedha kwenye utekelezaji wa mikataba ya kimataifa ya uhifadhi wa wanyamapori na makazi yao.

Hii ndio sehemu muhimu ya sheria inayoelezea mikataba na spishi za wanyamapori wanao vuka mipaka na kwenda nchi nyingine. Ifahamike kwamba wanyamapori hawajui mipaka ya maeneo yao wanayotakiwa kuishi na kuzaliana, aidha hawajui mipaka ya hifadhi za taifa. Hivyo ni muhimu kwa sisi kuelewa mambo haya ili tuweze kushirikiana na sekta husika kuhakikisha wanyamapori na maliasili zetu zinaendelea kuwepo na kuwanufaisha wengi wa sasa na wa kizazi kiacho.

Mwisho, nakushukuru kwa kusoma makala hii, naamini kwa pamoja tutaifanya Tanzania yetu kuwa sehemu salama kabisa kwa wanyamapori na viumbe hai wengine kuishi na kuendelea kuwepo kwa vizazi vingi vijavyo.

Ahasante sana!

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 248 681/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania