Historia ya uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yake imeandikwa sana kuanzia kipindi cha ukoloni ambapo Tanganyika ilikuwa  ikitawaliwa na mjerumani  na baadaye mwingereza. Katika kipindi hiki ndipo sheria za uhifadhi zilianza kutungwa kwa lengo la kuhifadhi wanyamapori kwa mustakbali wa wakati huo na baadae.

Swali ni  namna gani jamii za kiafrika ziliweza kuhifadhi rasimali zake hususani wanyamapori katika kipindi aambapo hapakuwa  na sheria yeyote, na je ni kwanini kwa sasa wanyamapori na mazingira yao yamekuwa hatarini licha ya uwepo wa sheria za  uhifadhi pamoja na elimu ya uhifadhi kutolewa pasi kuwa na kikomo?.

Mpendwa msomaji makala hii imejibu maswali haya kwa kutumia mfano wa  namna kabila la Wahaya nchini Tanzania lilivyoweza kuwahifadhi na kuwalinda wanyamapori na mazingira yao kwa kutumia mila na desturi.

Kwa utangulizi, kabila la Wahaya ni miongoni mwa makabila maarufu nchini Tanzania,  linapatikana Kaskazini Magharibi mwa nchi ya Tanzania katika Mkoa wa Kagera. Ambatana nami tukajifunze namna kabila hili lilivyoweza kufanya  uhifadhi wa wanyamapori na mazingira hususani kabla ya ujio wa sheria za uhifadhi ikiwa tu ni mfano wa jinsi mila za kiafrika zilivyotumika katika uhifadhi. Yafuatayo ni baadhi ya mambo ambayo yaliwasaidia Wahaya kutunza mazingira na wanyamapori;

Katazo la kuwaaua au kuwasumbua wanyama waliodhaniwa kutokuwa na madhara: katika jamii ya Wahaya ipo imani ya kuwa ukiwaua au kuwabugudhi wanyama ambao hawana madhara na pengine sio kitoweo kwa tamaduni zao basi wewe ni mchawi. Hivyo kila mzazi alijitahidi kuwafunza watoto kuzingatia suala hili ili wanafamilia wasiitwe wachawi, na hata ilipotokea watoto wakahidi wakawaua au kuwasumbua wanyama basi aliadhibiwa kisawasawa. Katazo hili lilisaidia sana kuwahifadhi wanyama wadogo kama vile mijusi, vyura, vinyonga na   Imani hii bado inaendelea kuaminiwa na watu wengi huko uhayani hadi sasa.

Mfumo wa kuwa na myama wa koo: katika jamii ya Wahaya huwa kuna mfumo wa koo ambapo ukoo mmoja huhusisha familia nyingi zenye uhusiano kutoka enzi za mababu. Mara nyingine koo hizi huwa kubwa sana kiasi cha kutofahamiana ila wakionana na kujitambulisha kwa koo hizo basi huwa ni ndugu kabisa. Koo hizi zilitumika katika kudhibiti uvunaji wa wanyama kwa kila ukoo kuwa na mnyama ambaye aliitwa mnyama wa ukoo. Mnyama huyo aliheshimiwa na wana ukoo na hawakuwa tayari kumjeruhi wala kumuua mnyama huo. Wanyama waliopewa hadhi ni baadhi ya nyoka, ndege pamoja na mamalia. Ilikuwa ni kawaida kwa familia kumuona nyoka anayedhaniwa kuwa wa ukoo huo wakampisha apite wakiamini kuwa alikuja kukagua familia na kutokana na kuwa walikuwa na maarifa ya utambuzi wa wanyama, mara nyingi nyoka waliopewa hadhi hiyo walikuwa ni wale wasio na sumu kwa binadamu. Sambamba na hilo kila koo ilizuiliwa kula aina fulani ya myama au kundi, hali iliyopunguza uvunaji wa myama huyo. Kwa mfano upo Ukoo wa Abasingo, hawa hawakuruhusiwa kabisa kula samaki na mwanaukoo alipokula alidhurika mfano ngozi kubanduka mithiri ya aleji (allergy). Mpaka sasa wanaukoo wengi wa Abasingo  hawatumii samaki.

Ndege huyu hutambulika kama ndege wa ukoo wa Abazigaba, katika kabila la Wahaya.

 

Mfumo wa kilimo mseto (agroforestry); kilimo mseto ni aina ya kilimo ambacho huchanganya mimea ya aina mbalimbali, mfano miti, mazao ya jamii ya kunde nakadhalika. Kwa muda mrefu kabila la wahaya walikuwa na aina hii ya kilimo ambapo wao hupendelea kuwa na mashamba yanayozunguka nyumba zao yakiwa na migomba, miti, mahindi, maharage, mihogo na mimea mingine. Uwepo wa kilimo mseto uliweka mazimngira rafiki kwa makundi mbalimbali ya wanyama ambao waliweza kupata hifadhi na mahitaji hayo kutoka katika mashamba hayo. Sambamba na hilo, Wahaya waliamini katika uwepo wa baadhi ya wanyama katika mashamba yao ilisaidia kuongeza mavuno, mfano waliamini kuwa ndege jamii ya Starling husaidia kuongeza mavuno katika mashamba ya migomba hivyo wasingeweza kuwadhuru ndege hao na hata walipokuta viota, mayai au vitoto vya ndege hao walivihifadhi vizuri katika hali ambayo haikuhatarisha maisha ya ndge hao.

Miiko yenye mlengo wa kihifadhi: kabila la Wahaya lilikuwa na miiko ambayo ukiingalia kwa jicho la kihifadhi utaona kabisa ilichochea uhifadhi wa mazingira. Kwa mfano; Katazo la kuoshea vyombo kwenye chemichemi au vyanzo cha maji: maeneo mengi ya uhayani yalitegemea sana maji ya kwenye chemichemi hususani katika kipindi ambavyo mvua hazikunyesha. Uchotaji wa maji katika chemichemi ulimuitaji mchotaji kuzingatia usafi, kwa mfano haikuruhusiwa kabisa kwenda kuchoka maji ukiwa na chombo kichafu. Na iliaminika kuwa ukienda na chanzo kichafu utawakaribisha nyoka wa majini na wangeweza kukausha maji katika chemichemi. Imani hii ilisaidia kuhifadhi vyanzo vya maji na viumbe maji ambao walikuwa katika chemichemi hizo kwa kudhibiti uchafuzi wa makusudi.

Aidha, nipende kukumbusha baadhi ya sababu ambazo zinaathiri uhifadhi wa wanyamapori katika zama hizi licha ya uwepo wa sharia za uhifadhi wa awanyamapori na mazingira. Sababu hizo ni:

  • Kushamiri kwa vitendo vya ujangili sambamba na ukuaji wa teknolojia za uwindaji.
  • Ongezeko la idadi ya watu ambalo huongezeka msukumo wa matumizi wa rasimali, kuvamia makazi ya wanyapori na kuchochea shughuli za binadamu ambazo huathiri mifumo ya ikolojia.
  • Mabadiliko ya hali ya hewa kutoka na kushamairi kwa shughuli za binadamu.
  • Kusambaa na kuenea kwa viumbe vamizi.

Hitimisho:

Mpendwa msomaji wa makala zetu, zipo mila na desturi mbalimbali ambazo ni chanya kwa uhifadhi wa wanyapori na mazingira yao, hivyo hatuna budi kizidumisha. Pia, ni vema tushiriki katika mambo yanaoweza kusaidia uhifadhi kama vile kupanda miti, kudhibiti uzalishaji wa taka, na kupiga vita ujangili na uvamizi wa makazi ya wanyapori kwaajili ya kutunza tunu pekee na wanyamapori na mazingira tuliyojaliwa na Mwenyezi Mungu.

 

Makala hii Imeandaliwa na:  Lucia Romward Reveliani luciaromward@gmail.com