Habari Rafiki, karibu kwenye makala yetu ya leo, jana niliandika jinsi ambavyo jamii zetu zinavyochangia kwa kiasi kikubwa kukua na kuenea kwa ujangili, nilieleza sababu na chimbuko kubwa la ujangili kwenye jamii ambazo zinzishi kando kando ya hifadhi za wanyamapori. Leo nitaelezea kidogo kipengele ambacho nilikiacha kuhuhu ujangili wa wanyamapori ili tuelewe jinsi ambavyo wanyamapori wanatishiwa maisha yao na makazi yao kutokana na mila, desturi ,visasi na tamaduni zilizopitwa na wakati kwenye baadhi ya jamii za kifugaji. Hii ni jambo ambalo nimejionea mwenyewe kwenye maeneo ya kazi zangu, hivyo ni jambo la uzoefu wa kuishi na jamii hizi ndio nilipojifunza na kujionea mambo haya niliyodhani yalikuwa yamekwisha.
Ili mwanaume athaminike na kuwa na sauti kwenye jamii za kifugaji lazima upitie kwenye majaribio na hatua nyingi za hatari kwenye maisha yako moja wapo ikiwa ni uuwaji wa wanyamapori wakubwa na wakali kama vile simba au tembo. Jamii hizi ambazo huendeleza tamaduni hizi kwa kipindi maalumu ili kuonyesha kwamba wao ndio wanaume na kwamba wanaweza kuzilinda familia zao kwa ujasiri mkubwa. Tamaduni za aina hii zinachangia sana kwenye uuwaji na uharibifu wa wanyamapori kwenye hifadhi zetu. Kwa mfano imefikia kipindi kijana wa Kimasai au kimang’ati anataka kuoa unakuta ni lazima akauwe simba au tembo na arudi na kipande au sehemu ya mnyama huyo na kuonyesha jamii yake kwamba ameua myamaa huyo, ndipo atakapo kubaliwa kuoa na kupewa mifugo na jamii yake.
Kwenye mauaji ya wanyamapori kutokana na sababu za kisasi hii mara nyingi ni kutokana na wanyama hawa kusababisha hasara kwa wafugaji, mfano unakuta simba au fisi amevamia boma la mfugaji na kua, mbuzi, ng’ombe au kondoo, hivyo mfugaji hukasirika na kuamua kutafuta suluhisho la mifugo yake kutovamiwa na wanyamapori tena. Hivyo mfugaji aliyevamiwa mifugo yake hukusanya vijana na wafugaji wenzake na kwenda porini kumwinda mnyama huyo aliyesababisha hasara ya mifugo, watamwinda hadi wamwone na wamuue. Na baya zaidi endapo watakuta mnyama mwingine tofauti na yule aliyeua watamwua bila hata kuangalia, hata wakiona vitoto vya simba au fisi wataviuwa bila huruma, hii yote ni kulipiza kisasi kwa mauwaji ya mifugo ya mfugaji huyu.
Kutokana na mambo hayo imepelekea vifo vingi sana vya wanyama hawa wanaokula nyama kama simba, fisi, chui na hata mbwa mwitu kwenye maeneo ya hifadhi ya wanyamapori. Na kama unavyojua wafugaji hupenda kuishi na mifugo yao kwenye maeneo haya yaliyo karibu na hifadhi ya wanyamapori kwa sababu ya malisho na maji, maeneo hayo ambayo yapo karibu na makazi ya simba na wanyamapori wengine, hivyo uvamizi wa mara kwa mara unakuwepo kwa mifugo ya wafugaji. Kitu kingine kibaya zaidi kinachofanywa na hawa wafugaji wenye hasira baada ya mifugo yao kuuliwa huwa wanatabia ya kuweka sumu kwenye mzoga wa ng’ombe au mbuzi aliyeuliwa na simba au fisi na kuuacha huko porini, endapo simba au fisi atakaporudi kula mzoga ule anakufa hapo hapo. Na kama unavyo jua wanyama wengi wanaokula mizoga watakapouona mzoga huo wataula na hapo kupelekea vifo vya maelfu ya wanyamapori na ndege wanaokula mizoga kama tumbusi.
Kuna baadhi ya maeneo mambo haya yamepungua na kuisha kabisa kutokana na juhudi za serikali na mashirika ya uhifadhi wa wanyamapori. Kinachowasumbua wafugaji wengi ni kukosa elimu na uelewa wa mambo ya wanyamapori na faida wanazoweza kuzipata kwa uwepo wa wanyamapori kwenye maeneo yao. Kwa eneo la hifadhi ya wanyamapori la Ruaha, jamii imepata mwamko na sasa wanaanza kuelewa taratibu na wengi wameacha kuwinda kwa sababu za kitamaduni hasa wamasai wengi wao wameacha, wamang’ati nao wapo mbioni kuachana na mambo hayo ya kitamaduni zilizopitwa na wakati, sasa wengi wao wanakwenda shule wengi wao wanashirikiana na jamii na watu wengine kwenye shuguli za uhifadhi na maendeleo. Bila hiana hii ni kazi kubwa iliyofanywa na mradi wa utafiti wa wanyama wanaokula nyama unaojulikana kama “Ruaha Carnivore Project”. Pia juhudi za wadau wengine wamechangia sana kwenye jambo hili ili kupunguza mauaji ya wanyamapori kwa sababu za kitamaduni na sababu za visasi.
Kazi kubwa bado inahitajika kufanyika ili kuwasaidia wafugaji kutulia sehemu moja ili waweze kupata huduma muhimu kama elimu, endapo wafugaji watatulia na kuacha kuhama hama basi itakua rahisi kutoa elimu na kushirikiana nao kwenye uhifadhi, hili ni jambo linalohitaji muda na umakini mkubwa ili lifanyike vizuri na kwa weledi, naamini njia sahihi ya kutokomeza mauaji ya wanyamapori kwa njia ya kitamaduni na visasi ni elimu na faida za moja kwa moja kwa jamii hizi.
Ahsante sana kwa kusoama makala hii,
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 248 681/+255 742 092 569