Habari mpendwa msomaji wa Makala za wanyamapori, karibu katika Makala ya leo inayohusu  mimea vamizi katika hifadhi za nchini Tanzania. Taarifa mbalimbali zimeonesha kuna aina tofauti za mimea vamizi katika hifadhi za nchini Tanzania. Uwepo wa mimea vamizi umeathiri shughuli mbalimbali zinazofanyika katika hifadhi hizi.

 Chanzo cha picha hii ni tovuti ya africanccf.org

Data zilizopo zinaonyesha kuwa hifadhi ya Ngorongoro ndiyo hifadhi iliyoathirika zaidi kwa kuwa na spishi nyingi , ikifuatiwa na hifadhi ya Taifa ya Serengeti na hifadhi yenye spishi chache zaidi ni Msitu wa Akiba wa Amani (NISSAP, 2019.)

NINI MAANA YA MIMEA VAMIZI

Mimea vamizi ni mimea ambayo huingia katika mazingira mapya na kuanza kukua kwa kasi ,kuchukua nafasi kubwa na kuzidisha idadi yao kwa kiwango cha juu sana. Mara nyingi mimea hii hushindana na mimea asili ya eneo hilo hivyo husababisha kuvuruga usawa wa mazingira na kubadili mifumo ya kiikolojia ya eneo husika.

Mimea vamizi imekuwa ni tatizo kubwa sana katika hifadhi za hapa nchini Tanzania na pia katika nchi nyingine, kwani inasababisha kuharibu mifumo ya mazingira ya hifadhi zetu .

NINI KINAFANYA MMEA UWE VAMIZI.

Mimea vamizi ni aina yeyote ya mmea ambao haupatikani kiasili katika eneo, lakini inaweza kustawi na kusambaza katika mfumo mpya wa ikolojia. Sio lazima mimea hii vamizi iwe ni kutoka katika nchi za nje lakini ili mmea kuwa vamizi unatakiwa uwe na sifa zifuatazo.

Ukuaji wa haraka; Kwa kawaida mimea vamizi hukua haraka sana ,huku ikishindana na mimea ya asili ya eneo hilo kupata rasilimali kama jua, maji na virutubisho vingine.

Uwezo wa kuzaliana kwa wingi; Mimea vamizi hutoa idadi kubwa sana yaa mbegu hivyo kusababisha kuwe na idadi kubwa sana ya mimea inayoenea kwa kasi kubwa.

Uvumilivu wa hali tofauti; Mara nyingi mimea hii ina uwezo wa kukua na kustawi katika mazingira tofauti na hali tofauti hivyo huvumilia sana hali mbalimbali .

Uwezo wa kutumia sumu; Baadhi ya mimea vamizi hutoa kemikali iitwayo alelopati (allelopathic) ambayo huzuia ukuaji wa mimea mingine na pia kemikali hizo huwa ni mbaya kwa wanyama mbalimbali hivyo mara nyingi mimea vamizi huwa hailiwi na wanyamapori.

Kutokuwa na maadui wa asilia; Mimea vamizi mara nyingi haina wadudu wa asili au magonjwa yanayowakabili hivyo idadi yao hubaki sawa.

NJIA AMBAZO MIMEA VAMIZI HUINGIA KATIKA HIFADHI.

Shughuli za Binadamu: Shughuli za binadamu ni njia kuu ambayo mimea vamizi huingizwa katika maeneo ya hifadhi. Shughuli hizi zinaweza kujumuisha utalii, kilimo, ujenzi, na maendeleo. Mbegu za mimea vamizi zinaweza kusafirishwa kwa bahati mbaya kwenye magari, vifaa, au nguo.

Usambazaji wa Asili: Baadhi ya mimea vamizi ina njia za kusambaza kiasili, kama vile mbegu zinazosambazwa na upepo au matunda ambayo wanyama hula na kisha kusambaza. Mimea hii inaweza kuingia katika maeneo ya hifadhi kwa njia za asili.

 Usambazaji unaofanywa na Wanyama: Wanyama wanaweza kuchangia katika kusambaza mimea vamizi. Ndege, wanyama wa porini, au wanyama wengine wanaweza kubeba mbegu kwenye manyoya yao, au kwenye mfumo wao wa mmengenyo, na kuzisambaza katika maeneo mapya ya hifadhi.

Mito na Maziwa: Mito na maziwa yanaweza kusafirisha mbegu za mimea vamizi chini ya maji, ikiruhusu kuingia katika maeneo ya hifadhi yanayopatikana karibu na vyanzo vya maji. Pia matawi au mmea wenyewe unaweza kusombwa na maji na kuingiza mimea vamizi katika hifadhi.

Picha hii inaonyesha mimea vamizi imetanda katika ziwa: chanzo cha picha hii ni BBC

MADHARA YA MIMEA VAMIZI KATIKA HIFADHI.

Kupunguza Utajiri wa Mimea Asilia: Mimea vamizi hushindana na mimea ya asili kwa rasilimali kama maji, virutubisho, na nafasi. Hii inaweza kusababisha kupungua kwa utajiri wa mimea ya asili na kuhatarisha spishi za mimea za asili.

Picha hii inaonyesha mimea vamizi imetanda katika hifadhi hivyo kupunguza utajiri wa mimea asilia: chanzo cha picha hii ni Africa Press Arabic.

Kupunguza spishi: Kwa kushindana na mimea ya asili, mimea vamizi zinaweza kusababisha upotevu wa utofauti wa spishi za mimea na kuathiri viumbe hai wanaotegemea mimea hiyo.

Kuvuruga Mfumo wa Ikolojia: Mimea vamizi inaweza kubadilisha muundo na utendaji wa mfumo wa ikolojia kwa kubadilisha mfumo wa kikazi, mzunguko wa maji, na uhusiano wa viumbe hai.

Kupunguza chakula na makazi ya  Wanyama:  Kwa kuharibu mimea ya asili ambayo wanyama wa porini wanategemea kwa chakula au makazi, mimea vamizi inaweza kuathiri spishi za wanyama wa porini na kusababisha upungufu wa chakula na makazI

Picha hii inaonyesha mimea vamizi imetanda katika Hifadhi ya Serengeti hivyo kupunguza makazi na chakula cha wanyamapori : chanzo cha picha hii ni Proud Africa Safari.

Kupunguza Thamani ya Utalii: Maeneo ya hifadhi ya asili nchini Tanzania yanategemewa kwa utalii. Kuingia kwa mimea vamizi kunaharibu uzuri wa asili wa maeneo haya na kuharibu thamani ya utalii.

Picha hii inaonyesha mimea vamizi imetanda katika eneo la hifadhi la Ngorongoro: chanzo cha picha hii ni tovuti ya istock.org

Kuathiri Uchumi: Kwa sababu ya madhara kwa utalii, kilimo, na maisha ya binadamu, mimea vamizi inaweza kuathiri uchumi wa maeneo ya hifadhi na jamii zinazoishi karibu na hifadhi.

MIFANO YA MIMEA VAMIZI

Baadhi ya mimea vamizi inayopatikana katika hifadhi zetu ni pamoja na Mkonge wa India (Lantana camara), Mnafu (Chromolaena odorata), Mkia wa Punda (Lantana trifolia),  Mbaruti (Parthenium hysterophorus), Kikarakara (Prosopis juliflora) na  Guternibergia cordifolia.

MBINU ZINAZOTUMIKA KUONDOA MIMEA VAMIZI

Mbinu za kibioljia; Mbinu hii inahusisha kutumia wadudu au vimelea ambavyo huweka katika eneo ambalo limeathiriwa na mimea vamizi hivyo wadudu hawa hushambulia mimea vamizi na kupunguza idadi yao

Picha hii inaonyesha wadudu wamewekwa katika mmea vamizi ili waushambulie mmea huu: chanzo cha picha hii ni tovuti ya cibi.org

Mbinu ya kemikali; Kemikali mbalimbali za kibiolojia hupuliziwa sehemu ambapo kuna mimea vamizi hivyo baada ya muda mimea hii hufa, kemikali hizi huwa zimetengenezwa maalum kwa ajili ya kuua mimea vamizi hivyo huwa na madhara kidogo katika mazingira.

Picha hii inaonyesha wataalam wakipuliza kemikali katika mimea vamizi: chanzo cha picha hii ni tovuti ya africanccf.org

Mbinu ya kung’oa au kufyeka; Baadhi ya mimea vamizi huondolewa kwa njia ya kungolewa mpaka mzizi ili kuzuia zisiote tena au kufyeka ambapo huondoa shina lakini mzizi hubaki ndani hivyo baada ya muda mimea hii huanza tena kuota. Njia hii ndiyo njia salama na haina madhara kwa mazingira au viumbe wengine.

Picha hii inaonyesha wahifadhi katika eneo la Ngorongoro wakifyeka mimea vamizi: chanzo cha picha hii ni ngorongorocratertanzania.org

Mbinu ya kuchoma moto; Baadhi ya mimea vamizi huthibitiwa kwa kuichoma moto mpaka iteketee

Picha hii inaonyesha wahifadhi katika eneo la Ngorongoro wakichoma mimea vamizi: chanzo cha picha hii ni ngorongorocratertanzania.org

 JINSI AMBAVYO JAMII INASHIRIKISHWA KATIKA KUONDOA/KUZUIA UENEAJI WA MIMEA VAMIZI.

Mpendwa msomaji wa makala hii tukumbuke kuwa uhifadhi nchini Tanzania unategemea sana ushiriki wa wananchi wanaoishi katika vijiji Jirani na hifadhi hivyo jamii hizi hushirikishwa katika kuzuia ueneaji wa mimea hii vamizi kwa kupitia njia zifuatazo.

Kupitia elimu; Mamlaka za hifadhi mbalimbali zinatoa elimu kwa jamii za Jirani kuhusiana na madhara ya mimea vamizi na njia mbalimbali za kuzuia ueneaji wa mimea hii. Hii inasaidia sana katika kupunguza ueneaji wa mimea hii nje ya hifadhi na ndani ya maeneo ya hifadhi.

Kupitia vikundi vya kujitolea; Vikundi mbalimbali vya kujitolea kutoka katika jamii ziishizo Jirani na hifadhi huundwa ambavyo hushirikiana na hifadhi katika shughuli mbalimbali za kuzuia na kudhibiti ueneaji wa mimea vamizi.

Picha hii inaonyesha wananchi katika eneo la Ngorongoro wakifyeka mimea vamizi: chanzo cha picha hii ni ngorongorocratertanzania.org

Kushirikisha jamii  kushiriki katika mipango ya udhibiti wa mimea vamizI; Jamii zimekuwa zikishirikishwa katika mikutano na vikao vinavyohusisha mipango na mikakati ya hifadhi juu ya udhibiti wa mimea vamizi, hivyo wanapata nafasi ya kutoa maoni Pamoja na ushauri wao juu ya uelewa na njia mbalimbali wanazoona zinaweza kusaidia kudhibiti ueneaji wa mimea vamizi.

CHANGAMOTO ZA UONDOAJI NA UDHIBITI WA MIMEA VAMIZI KATIKA HIFADHI.

Baadhi ya changamoto zinazikabili hifadhi mbalimbali juu ya udhibiti wa mimea vamizi ni zifuatazo.

UFINYU WA RASILIMALI FEDHA; Uondoaji wa mimea vamizi unahitaji matumizi makubwa ya fedha kwa ajili ya kununua vifaa vya kuondolea mimea hii,kulipa watu wanaotumia vifaa hivi na pia kulipa wasimamizi wa shughuli hizi za uondoaji hivyo ufinyu wa pesa za kufanikisha shughuli hii unaleta changamoto kubwa katika kufikia malengo ya kuondoa mimea vamizi katika hifadhi.

Upungufu/ukosefu wa vifaa maalumu kwa ajili ya kutambua na kuondoa ,mimea vamizi; Vifaa maalumu vinahitajika ambavyo vitatumika katika ukaguzi wa mizigo na vifaa  mbalimbali vinavyoingia katika hifadhi ,pia kuna upungufu/ukosefu wa vifaa maalumu ambavyo vitatumika katika kuondoa kabisa mimea vamizi ili isijirudie.

Mabadiliko ya hali ya hewa; Mabadiliko ya hali ya hewa pia ni changamoto katika udhibiti wa mimea hii kwani mabadiliko ya hali ya hewa yanasaidia au yanachangia katika kuongezeka kwa ueneaji wa mimea vamizi katika maeneo mapya na pia yanazuia ukuaji na ueneaji mzuri wa mimea asilia

Upungufu wa elimu na uelewa wa kina ; Pia kuna changamoto ya upungufu wa uelewa na elimu ya kina kuhusu aina mbalimbali za mimea vamizi, madhara yake na jinsi ya kuzuia au kudhibiti mimea hii vamizi.

HITIMISHO

Wananchi wengi hawafahamu mimea vamizi ni ipi na mimea asilia ni ipi hivyo basi Serikali, Mamlaka za hifadhi na Sekta mbalimbali zishirikiane katika kutoa elimu kwa wananchi wajue mimea vamizi ni ipi ili iwe rahisi kupambana nayo.

Makala hii imeandikwa na Monica Mahilane na kuhaririwa na Hillary Mrosso, unaweza kuwasiliana na mwandishi wa makala hii kwa mawasiliano yake hapo chini, karibu sana tufanye kazi pamoja kwenye uhifadhi wa wanyamapori.

ASANTE

Monica Mahilane Mahilanemonica49@gmail.com

0652267935